Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

CHADEMA YAPETA


CHADEMA YAPETA
·       Mahakama yamtosa mbunge wake
CHAMA Cha Mapinduzi, kimepata pigo baada ya Mahakama Kuu Kanda  ya Sumbawanga kutengua matokeo ya ubunge wa Jimbo la Sumbawanga mjini yaliyompa ushindi mgombea wake Aeshi Hilal
Jaji wa mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Betwell Mmila alitengua matokeo ya mbunge huyo baada ya kubaini kuwapo kwa dosari katika ya vipengele kadhaa wakati mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka 2010.
Kati ya hoja 21 zilizowekewa pingamizi na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chadema, Nobert Yamsebo, ni vipengele viwili pekee ambavyo mahakama hiyo imeridhia kuwa na dosari katika uchaguzi huo.
Katika hukumu hiyo ambayo ilichukua zaidi ya saa tatu kusomwa na Jaji huyo, imevitaja vipengele ambavyo vilikuwa na dosari kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mazingira ya rushwa na kutokuwapo kwa mazingira huru katika kampeni kwenye baadhi ya maeneo yaliyopo katika jimbo hilo.
Jaji huyo alibaini kuwa aliyekuwa mgombea wa CCM  Aeshi Hilali alikwenda kwenye kikao cha ndani kilichodaiwa kuitishwa na viongozi wa CCM katika eneo la shule ya Msingi Kantalamba Mazoezi, na  kuwashawishi baadhi ya wapiga kura kwa kuwapa rushwa ya Sh.15,000 watu sita walikuwa kwenye mkutano huo  kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Eneo jingine ambalo lilitajwa kuwa na dosari ni kutokuwapo kwa mazingira huru kwa zoezi la kampeni kwenye vijiji vya Mtimbwa na Kisumba  ambako mgombea wa Chadema alizuiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kufanya kampeni zake baada ya kumfanyia fujo.
Katika hoja ya msingi ya mlalamikaji  aliiomba  Mahakama  kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo,   kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za uchaguzi.
Waliokuwa walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), msimamizi  msaidizi na msimamizi mkuu wa uchaguzi ambao  nao walidaiwa  kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo, mlalamikaji Yamsebo  aliwakilishwa na kampuni ya kisheria ya  Mkumbe  Advocate  and  Company Ltd  ya  mkoani Mbeya ambapo  kwa  upande wa Serikali uliwakilishwa na wanasheria wawili  wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul  Shahidi.
Aiyekuwa mlalamikiwa  aliwakilishwa na jopo  la Mawakili watatu, Juma Nassoro kutoka kampuni ya Nassoro Advocate, Abubakar Salim wa kampuni ya BLC Advocate na Wakili Ileth  Mawalla  kutoka  S. Mawalla , Law  Consultant  and Attorney ya  mjini  Sumbawanga .
Aidha hukumu ya mahakama  hiyo  imemtaka aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Bw. Aeshi Hilali kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Pamoja na hukumu hiyo mahakama hiyo imetoa fursa kwa upande wa Mlalamikiwa kukata rufaa iwapo atakuwa hajaridhika na hukumu iliyotolewa.
Hata hivyo, Wakili Nassoro aliyekuwa akimtetea Aeshi alisema kuwa wanakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo mara baada ya kutathimini mwenendo mzima wa kesi hiyo.
Kwa upande wake, aliyekuwa mlalamika wa kesi hiyo, Yamsebo alisema kilio cha wanyonge kimesikika na mahakama imetenda haki hali ambayo inawafanya wananchi kuendelea kuwa na imani na muhimili huo wa dola.
Katika uchaguzi huo uliotenguliwa,  Aeish alishinda kwa kupata kura 17,328 wakati mgombea wa Chadema , Yamsebo  akipata kura 17132.
Mji walipuka kwa shangwe

Mara baada ya hukumu hiyo, umati mkubwa wa watu uliofurika katika viwanja vya mahakama hiyo, wengi wao wakiaminika kuwa wanachama na mashabiki wa Chadema, ulilipuka kwa shangwe.
Idadi kubwa ya askari polisi waliokuwa wameletwa kwa wingi tangu asubuhi na kutanda kote mahakamani hapo, waliondoka kimya kimya mara baada ya kutolewa kwa hukumu, wakiwaacha mamia ya wananchi wakishangilia.
Shangwe hizo zilizagaa kwa kipindi kifupi na kuenea katika mji na vitongoji vingi vya mjini hapa kiasi cha kusababisha baadhi ya watu kuacha kwa muda shughuli zao na kuungana katika makundi ya watu waliokuwa wakipita mitaani wakionesha alama ya V inayotumiwa na Chadema.
 Mnyika apongeza

Ushindi huo umepongezwa na Mkurugenzi wa habari na Uenezi wa Chadema John Mnyika ambaye alisema miongoni mwa kesi walizokuwa na matumamini nazo ni ya Sumbawangawa Mjini na kwamba haki imetendeka.

Alisema kuwa wanasubiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza jimbo hilo kuwa wazi, ili wajiandae kwenda kuongeza mbunge mwingine wa  chama hicho.


‘CCM ni ya mafisadi’

Na Tamali Vullu

BARAZA Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limesema kuwa mabadiliko ya baraza la mawaziri yanayotarajiwa kufanyika wakati wowote si suluhu ya kupunguza au kumaliza ubadhilifu serikalini kwa madai kuwa ufisadi ni sehemu ya mfumo wa utawala wa CCM.

Aidha,kuvunjwa kwa baraza la mawaziri kwa kuepuka ushauri wa wabunge na kutumia kauli ya Kamati Kuu ya CCM, ni matokeo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kuhofia nguvu ya umma.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari akielezea maazimio ya baraza hilo lililomaliza kikao chake juzi.

Mnyika alieleza kuwa mabadiliko hayo hayataleta mageuzi ya maana kwa kuwa Rais Kikwete bado atateua sehemu kubwa ya mawaziri waliopatikana kifisadi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

“Kauli ya CCM kuwa watawapeleka mahakamani mawaziri na watendaji wote waliohusika  katika ubadhilifu ni siasa tupu, kwani ushahidi upo wazi kuwa mpaka sasa serikali hii hii  chini ya chama hicho hicho haijawapeleka mahakamani mawaziri waliopatikana na kashfa na kulazimika kujiuzulu mwaka 2008 na wameshindwa kuwafukuza kwenye chama.

“Zaidi ya hayo, ipo orodha ndefu ya mafisadi iliyotolewa hadharani mwaka 2007, na mafisadi wakuu hawajagushwa,” alisema.

Alieleza kuwa CCM iliitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu na kutoa tamko juu ya baraza la mawaziri baada ya kusikia kuwa Baraza Kuu la chama hicho linakutana na kuanza maandalizi ya kuunganisha nguvu ya umma kushinikiza mabadiliko ya kiutawala na mfumo.

“…ni wazi kuwa CCM na Rais Jakaya Kikwete wamekubali kufikia hatua hiyo wakihofia nguvu ya umma.

“Baraza Kuu limeazimia kuwataka Watanzania kutambua kuwa kwa muda mrefu sasa baraza la mawaziri limekuwa kielelezo kamili cha mfumo wa ubadhilifu, rushwa na ufisadi katika utawala wa nchi hii chini ya CCM,” alisema Mnyika.

Alisema chama hicho si cha msimu wala matukio na kwamba wanahitaji uwajibikaji mkubwa nchini na kuongeza kuwa oparesheni za chama hicho nchi mzima hazitakwisha.

“Oparesheni zetu zipo pale pale, tunahitaji mabadiliko ya mfumo, kwani kuna uozo mkubwa kwenye safu za uongozi,” alisema Mnyika wataunganisha nguvu ya umma na kujenga chama katika oparesheni hizo.

Hali ya uchumi

Mnyika alisema kuwa baraza hilo limebaini kuwa hali hiyo inasababishwa na uongozi dhaifu wa serikali ya CCM ambayo imeshindwa kudhibiti matumizi mabaya katika serikali na idara zake, na kushindwa kuchochea uzalishaji wa chakula na nishati nchini.

Alisema kuwa Baraza hilo limeuagiza uongozi wa taifa wa Chadema pamoja na wabunge kuwahimiza wananchi kuendelea kuishinikiza serikali kutimiza wajibu wake.

Pamoja na hilo, alisema baraza hilo limewataka wananchi kujiandaa kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi na utawala katika chaguzi zijazo, kwani kikwazo kikubwa cha maendeleo nchini ni CCM inayoendesha serikali kwa mfumo wa rushwa na ufisadi

Mnyika aliongeza kuwa mabadiliko ya kweli nchini yatapatikana kwa kuiondoa CCM madarakani.

mauaji ya wanachama

Baraza hilo limelaani mauaji ya wanachama wake  huku jeshi la polisi likishindwa kuchukua hatua zozote za maana.

“Baraza Kuu limelaani mauaji ya Mwenyekiti wa Kata ya Usa River yaliyotokea Aprili 28 mwaka huu      na pia limeeleza kusikitishwa na jeshi la polisi kwa kushindwa kuchukua hatua za maana dhidi ya watu waliohusika na mauaji ya wanachama wa Chadema ambayo yamekuwa yakitokea tangu uchaguzi mdogo  wa Igunga,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema  baraza hilo limeuagiza uongozi wa chama hicho kuanzisha mchakato wa kulishitaki jeshi la polisi kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Aidha, pamoja na hayo, alisema baraza hilo limeagiza chama kusukuma hoja ya kuwapo kwa uchunguzi huru  dhidi ya matendo ya kidhalimu yanayofanywa na Jeshi la Polisi na kutolea mfano Arusha, Mwanza, Ruvuma Mbeya na Mtwara (Tandahimba).

Uchaguzi ndani ya chama

Mnyika alisema kikao hicho kimepanga uchaguzi ndani ya chama hicho kufanyika kuanzia Juni mwaka huu kwa ngazi ya msingi na kukamilika Oktoba mwakani kwa ngazi ya taifa.

alisema katika kudhibiti rushwa katika uchaguzi huo, baraza kuu limeiagiza Kamati Kuu kuandaa mwongozi wa kudhibiti hali  hiyo, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uadilifu na maadili.

masuala ya kijamii.

Aidha, alisema baraza hilo limeitaka serikali ya CCM kutekeleza tamko la chama hicho kutatua migogoro ya makundi ya kijamii kama wanafunzi, wafanyakazi, wakulima hasa katika masuala ya ardhi na maslahi ya wafanyakazi.

Alisema kuwa mpaka sasa serikali bado hajapandisha mishahara ya wafanyakazi na kusema kuwa hali hiyo ndio inachangia kuwapo kwa migogoro ya mara kwa mara.

“Tunaamini rasilimali na mapato ya nchi yakitumika vizuri yanaweza kutekeleza mambo haya na wafanyakazi wakawa na maslahi bora,” alisema.

No comments:

Post a Comment