Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, NINGEJUA



Wwapendwa, hii ni sehemu ya kitabu changu kiitwacho NDOA YANGU, NINGEJUA ambacho kimekuwa kikiuzwa sehemu nyingi ndani na nje ya nchi. Hapa naweka ili kuonesha hali halisi ya maisha ya wanandoa wengi


"NINGEJUA......”


      Ndoto na matumaini ya kila mmoja wetu wakati tulipoufunga ndoa, yalikuwa kuishi maisha yaliyojaa upendo, furaha na amani tele. Na ndizo ndoto za wengi wanaofunga ndoa. Kwamba, maisha yao yawe ya furaha. Lakini mambo yako kinyume kabisa na matarajio hayo. Utafiti ulliopelekea kuandikwa kwa kitabu hiki, umeleta umeleta matokeo ya kusikitisha sana ambapo watu 170 kati ya 200 wanajuta kufunga ndoa na wenzi wao na kama wangejua tabia zao zitakuwa walizonazo sasa, wasingekubali hata kwa bakora! Kadhalika, wanandoa 122 kati ya 200 wanakiri kufunga ndoa na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati na hawakuwa chaguo lao!
“Kama ningejua mume wangu atanitendea haya, nisingekubali kuolewa hata kama ingebidi kufa”  “Kama leo Kanisa litatoa ruhusa ya kuachana, mimi nitakuwa wa kwanza kumpa mke wangu talaka”. Majibu haya yanadhihirisha kuwa wanaume na wanawake wengi wamezichoka ndoa zao kwa namna isiyotarajiwa. Hawana hamu na wenzi wao na wangependa hata pengine, Mwenyezi Mungu afanye miujiza itakayosaidia kuachana nao haijalishi ikiwa ni kwa njia ya kifo! Ndoa zimetawaliwa na vilio na majuto kama ilivyodhihirika wakati wa utafiti uliopelekea kuandikwa kwa kitabu hiki.

1. KAMA UNGEJUA MUMEO ATAKUWA NA TABIA ALIYONAYO SASA UNGEKUBALI
     AKUOE?    (a) Ningekubali    (b) Nisingekubali

Katika swali hili, wanawake 93 kati ya 100 waliofunga ndoa ya Kanisa, walisema kuwa wasingekubali kuolewa. Watano walisema wangekubali, wakati wawili waliobaki walisema kuolewa ama kutoolewa kwao yote yalikuwa sawa. Kwa upande wao kuolewa ama kutoolewa haikuwa tija. Lakini hata wale watano waliokubali walipotakiwa waseme msingi wa kukubali kwao, baadhi ya majibu yao yalisikitisha. Watatu kati yao walisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwa waume zao wanawapenda na ni waaminifu na wakweli katika ndoa zao. “Nathubutu kusema kuwa tangu niolewe, mume wangu hajawahi kuwa na mwanamke mwingine. Najua nyendo zake na hanifichi kwa jambo lolote analopanga kufanya ama hata linalomkwaza” anasema mama mmoja kati ya hao. Kadhalika, mwingine anasema anajua mume wake anampenda sana na hajawahi kumtendea jambo lolote la kikatili, hata kule kumsonya tu. “Ninapohisi nimemkosea, hunyamaza na hasira yake ikiisha ndipo huniita na kuniambia kosa langu kwa upole na heshima tena tukiwa wawili tu chumbani. Kwa kweli nampenda sana mume wangu na najivuna kwamba mimi ni mmoja wa wanawake waliobarikiwa kupata mume bora kabisa duniani”
Mmoja anasema, pamoja na mumewe kuwa mlevi, lakini anampenda kwa sababu hampigi wala kufanya fujo alewapo. Anatunza familia ingawa kama angeacha pombe, wangekuwa na maendeleo makubwa. Wa mwisho ndio alitia fora. Yeye alisema anafurahia kuishi na mume wake kwa sababu kila asemacho ama atakacho anatimiziwa bila usumbufu. "Hata nikimwambia naenda kulala kwetu anakubali. Yaani hana shida ingawa watu wanadai eti nimemlisha limbwata, yote naona heri” Lakini anakubali kwamba kama angekuwa anamkatalia mambo anayomuomba, ama kumfanyia vituko vya aina yoyote ile hasa kumpiga, angeshafungasha virago muda mrefu!
“Kwa kweli kama kungekuwa na utaratibu wa kila baada ya miaka fulani mtu unarudi tena kanisani na unapewa nafasi ya kuamua upya, naapa hata kwa sumu nisingekubali kuishi na mwanaume huyu” anasema mama mmoja katika majibu yake. Mwingine anasema hata ikitokea mumewe anafariki na ajitokeze mwanaume atake kumwoa, hatakubali kuingia tena katika ndoa, labda awe maiti.
Wanawake hawa wanakiri kuteswa kwa namna nyingi na waume zao na wengine wamepata vilema vya maisha kutokana na kipigo. “Mume wangu amekuwa mlevi na mara nyingi hunigeuza gunia kwa kipigo. Sura yangu imejaa makovu shauri ya kipigo. Sioni maana ya ndoa wala ule upendo niliotarajia kuupata, sijauona zaidi ya mateso. Kama maana ya ndoa ndio hii, mie nimeshindwa” anasema mama mwingine katika majibu yake.
Wengine walisema waume zao wamewageuzwa kama wafanyakazi wa ndani. Hawathaminiwi, hawana kauli, waume zao wanalala nje wanavyotaka na wengine wamediriki kuoa wanawake wengine kinyume kabisa na sheria za ndoa. Yote hayo, mume anayafanya kwa jeuri tu ya kwamba yeye ni mwanaume na hakuna wa kumuuliza.
“Binafsi sijielewi kama mimi ni mke halali ama dada wa kazi. Nina mwaka wa nne sijakutana kimwili na mume wangu. Kila ninapomdadisi, anasingizia ugonjwa ambao hajawahi kuniambia anaumwa nini. Nikija juu anafoka na kusema kama nashindwa kuishi bila kushiriki naye tendo la ndoa, nitafute wanaume wengine. Lakini anafanya hivi kwa sababu amepata msichana mdogo anayemchanganya akili” anasema mama mwingine. Sababu nyingine, ni tabia ya wanaume kutowajali wake zao kiasi kuwa hawajali afya wala uzima wao hata wanapougua.
“Mimi hanijali hata nikiugua. Wakati fulani aliwahi kumleta hapa nyumbani hawara yake huku mimi mwenyewe nikiwa hoi kitandani kwa ugonjwa. Kesho yake wakabebana na huyo mtu wake wakaenda kuishi kwingine. Kama sio ndugu zangu kunichukua na kuniuguza, labda ningeshakufa. Hapa nimerudi baada ya wanangu kuniomba sana kwa sababu walikuwa wanaishi maisha ya shida sana.” Hili ni jibu la mama mwingine aliyeshiriki katika kujibu maswali haya. Maneno haya na mengine mengi yaliyotolewa na wanawake hawa, yanathibitisha kuwa wanawake wengi walioolewa wanaishi katika mazingira magumu ya ndoa.

TAFAKARI YA MSOMAJI;

Katika ndoa yangu, ninaishi na mume wangu kwa upendo ama kwa shinikizo?

2.   KAMA UNGEJUA MKEO ATAKUWA NA TABIA ALIYO NAYO SASA, UNGEKUBALI
KUMUOA? (a) Ningekubali  (b) Nisingekubali

      Katika swali hili, wanaume 79 walisema wasingekubali! Wanaume 12 walisema wangekubali. Ungetegemea kuwa akina mama ndio wanaoishi maisha magumu katika ndoa, lakini kwa majibu haya ni dhahiri kuwa akina baba wengi nao wana machungu makubwa ndani ya ndoa zao. Katika majibu yake, mwanaume mmoja alisema kuwa, anajuta kuoa mwanamake aliye naye kwa sababu amekuwa na maisha magumu sana tangu wawe pamoja. Mkewe amesababisha akorofishane na ndugu zake wote. “Hataki kabisa kuona ndugu zangu wakija nyumbani kwangu wakiwemo wazazi wangu. Wanapofika huanzisha vurugu na ugomvi wa makusudi na hufikia kiwango cha kuwasimanga na kuwatukana wazazi wangu bila aibu”
Wanaume waliochoka ndoa zao wamesema kuwa wake zao sio waaminifu kwa vile wamegundua wana wanaume wengine nje ya ndoa na wengine wanaendekeza ushirikina kwa nia ya kuwafanya waume zao watulie nyumbani. Mmoja anasema kama isingekuwa maombi ya waamini wenzake, angeshapoteza maisha. “Mke wangu aliniwekea dawa kwenye chakula ili niwe namtii kila asemacho. Dawa hii nasikia alipewa na mganga mmoja huko Bagamoyo. Matokeo ya dawa ile ilinifanya nipooze upande mmoja wa mwili wangu na niliteseka sana na maradhi hayo hadi pale watu wa kanisani kwangu walipokuja kuniombea na kisha kunipeleka  katika mikutano ya Kanisa hadi nilipopona”
 Wengine wamelalamikia tabia ya dharau, matusi na umbea zinazofanywa na wake zao. “Nimekwisha hama zaidi ya nyumba sita hapa mjini kwa ajili ya tabia za umbeya wa mke wangu. Kila wiki vikao vya kusutwa na kupigwa faini. Yaani ni aibu juu ya aibu” wakati huyu anasema hivi, mwingine alieleza kwamba, mke wake hatulii na anabadilisha wanauame kama nguo. “Kibaya sana anaweza kutembea hata na marafiki zangu. Ameshafumaniwa mara mbili nikalazimika kuomba uhamisho toka Iringa kuja hapa ili kuepuka aibu, lakini hata huku mambo yamekuwa yale yale’


  
 TAFAKARI KWA MSOMAJI.

    Ninaishi kwa amani na mke wangu ama kwa hakika nimemchoka na hata natamani kuoa mke mwingine?


3.  JE, UMEOA/KUOLEWA NA MTU ULIYEMTAKA; NI CHAGUO LAKO HALISI?
  (a) Ndiyo (b) Hapana

Katika majibu ya swali hili, wengi wamekiri kufunga ndoa na watu ambao kwa kweli hawakuwapenda kwa dhati na hawakuwa chaguo lao. Katika kundi hili, wanawake wanaonekana kuathirika zaidi. Wanaume 49 walisema walifunga ndoa na wanawake ambao hawakupanga kuwaoa. Nao wanawake 73 walisema waliolewa na wanaume ambao hawakuwa chaguo lao. Kwa lugha nyingine, ndoa 122 kati ya 200 zilifungwa pasipo hiyari wala upendo wa dhati wa wanandoa wenyewe. Je, hali hii imetokana na nini?
Zipo sababu nyingi zilizosababisha hali hii kama wahusika wenyewe walivyojibu katika maswali haya. Ingefaa tuziangalie kwa uchache tu zile zilizobeba uzito mkubwa zaidi.

(A) KUKOSA UAMINIFU WAKATI WA UCHUMBA

      Mwanamke mmoja anasema hivi katika jibu lake;- “Huyu hakuwa mchumba wangu, ila nilikuwa naye kama rafiki wa kutoka naye mara moja moja. Bahati mbaya wambeya walimpelekea taarifa mchumba wangu ambaye aliweka mtego na siku moja akaninasa. Sikuwa na jinsi zaidi ya kumlazimisha huyu anioe ingawa ilichukua muda mrefu kukubali. Kwa kweli ni mimi ndiye ninayeonesha kumpenda wakati yeye, wala hajali kitu chochote kwangu”
Jibu lake liliungwa mkono na wanandoa wengi. Hii inaonesha kuwa udanganyifu na ukosefu wa uaminifu wakati wa uchumba ni mkubwa. Wachumba wengi wanaendeleza tabia ya kuwa na marafiki wengine wanaoshirikiana nao hata kufanya ngono. “Unajua kwa sisi wanawake huwezi kuamini kuwa huyu uliye naye atakuoa kweli kwa sababu wengi wanakwambai wanakupenda lakini baada ya muda wanakuacha. Kwa jinsi hiyo, unalazimika kuwa na mtu mwingine wa akiba ili huyu wa sasa akikutupa upate pa kukimbilia”. Maneno haya ya kujitetea yanatia simanzi na kuonesha kuwa chanzo ni kikubwa cha matatizo yanayozuka hata baada ya ndoa.

 (B)  KUPATA UJAUZITO.

Wanaume waliojibu swali hili, walisema walilazimika kufunga ndoa na wake zao baada ya kuwapa ujauzito. “Sikupanga kuwa na mke huyu. Nilimwoa baada ya kulazimishwa na wazazi hasa pale alipopata ujauzito na wazazi wake wakatishia kunipeleka mahakamani kama nisingemwoa. Kwa kuwa niliogopa kuipa familia yangu na mimi mwenyewe fedheha, niliamua kumuoa” anasema mwanandoa mmoja. Sababu hii ilitolewa pia na wanawake ambao walisema hawakuwa na namna ya kukwepa kuolewa na wanaume wa sasa baada ya kupata mimba “isiyotarajiwa” na hivyo kukubali kuolewa.”Mimi nilikataliwa na mchumba wangu niliyempenda sana baada ya kugundua kuwa nimepata ujauzito wa mtu mwingine. Yeye kwa sasa ameoa, lakini kwa kweli nilimpenda mwanaume yule na bado nampenda hata sasa” anakiri mama mmoja katika majibu yake. Ni wazi kuwa wengi wetu tumefunga ndoa katika namna ambayo hatukuwa tumepanga.

(B)  KULAZIMISHWA NA WAZAZI.

Baadhi ya wanandoa walisema kuwa, walilazimika kuoana kwa sababu ya shinikizo la wazazi. Mmoja alisema alimwoa mkewe baada ya wazazi wake kumkataa mchumba aliyemchagua kwa vile hawakutaka kuletewa mwanamke asiye wa kabila lao. “Nami kwa sababu sikutaka kuwakorofisha wazazi wangu, na kwa vile pia jamii yetu inaheshimu sana wazee na kama njia ya kukwepa laana, niliwakubalia wanipe huyu mke niliye naye.
Ni kweli kwamba wazazi wanao wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata wenzi wema. Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira kinaeleza wajibu wa wazazi kuwapatia vijana wao wenzi wao wa ndoa..‘ikiwa una watoto uwarudi, bali uwapatie wake zao wakati wa ujana wao. Umwoze binti yako, nawe utakuwa umemaliza jambo kubwa; tena umpe mtu mwenye ufahamu’ (YBS. 7:23,25)
     Pamoja na haki hii ya wazazi, ingelikuwa busara sana jambo hili likafanyika kwa umakini na busara na kuwapa watoto wao haki na ruksa ya kuchagua mke ama mume anayemwona ni mwema kwake, hata kama wazazi wanaona kuwa huyo ni masikini ama hataweza kuwasaidia kwa kipato. “Usijinyime mke aliye mwema mwenye akili, kwa maana neema yake hupita dhahabu (YBS. 7:19)
Wazazi wengi huenda waliangalia mambo yasiyokuwa na tija. Matokeo yake hayakuwa kama walivyotegemea. Binti yao hakai kwa amani, kila siku masimango na manyanyaso kutoka kwa mume. Anaishi kwa mateso na sononeko la moyo. Badala ya kuwapenda wazazi wake, anawachukia kwa sababu wamemwingiza katika janga. Hata anapolazimika kufikisha kilio chake kwa wazazi, hakuna linalofanyika kwa sababu wazazi hawana “jeuri’ ya kumsema mkwe wao kwa lolote. Mali walizopewa zimewafumba mdomo; hawana kauli tena. Ni kama walimuuza binti yao na sasa ni uamuzi wa mnunuzi kuamua atumieje bidhaa aliyonunua. Kumbe wazazi walitakiwa kuwapatia watoto wao wenza wenye sifa za wema, akili na neema na sio fedha, mali ama umaarufu.
Utafiti umeonesha kuwa wanandoa walioshindwa kuoana kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, bado wanaendelea na uhusiano wa kingono na hawajisikii kosa lolote kufanya hivyo. Wanaishi na wenzao wa ndoa kama kinga ama hifadhi tu, lakini akili na mioyo yao iko kwa wale waliowapenda. Katika uhusiano kama huo, watu hawa huweza kufanya mambo ya aibu kubwa bila woga wowote. Mwanandoa mmoja alikiri kufanya ngono na mwanaume aliyempenda kwa dhati na katika kudhihirisha upendo huo, ameshika mimba ya bwana huyo wa nje na hajali kama mumewe wa ndoa atajua. “Siogopi kitu na hilo libwana lenyewe (hapa akimaanisha mumewe wa ndoa!), likijua ndio itakuwa nafuu yangu maana atanifukuza na nitakuwa nimepata uhuru wa kwenda kuishi na kipenzi changu” anasema mwanamke huyo. Mwingine alisema kuwa anafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa anavunja ndoa yake na ya yule mwanaume ampendaye, ili waje kuishi pamoja. Katika hali kama hii, kuishi na mwanandoa asiyekuwa chaguo lako, ni sawa na kuishi jela. Kama sio kwa sala na msaada wa Mungu, ndoa ya aina hii imekufa na daima haiishi ugomvi na visirani vya kila namna.
Mwanaume mmoja, anakiri kuoa mke anayejua kuwa hampendi. Alifanikiwa kumwoa mkewe baada ya kuwashawishi wazazi wa binti kwa kutumia uwezo wake wa kipesa. Lakini pamoja na kumfanyia kila aina ya jema, kumnunulia hadi gari, lakini mkewe hana mapenzi kwake. “Ni kweli mke wangu hanipendi, ingawa namfanyia kila jema. Nimejaribu kumwonya hadi kwenda kwa wazazi wake, lakini amesema wazi kuwa anayempenda ni mwanaume mwingine” kadhalika, mwanaume huyu anasema kuwa alijaribu kumtafuta huyo mwanaume anayemzuzua mkewe, lakini wazee walimshauri aachane na jambo hilo baada ya kujua kuwa alioa mahali asipopendwa akidhani kuwa fedha yaweza kununua upendo.

TAFAKARI KWA MSOMAJI.

Hivi nimefunga ndoa na mtu niliyemchagua kweli ama nililazimishwa? Ukatili gani ninamtendea mwenzangu kama njia ya kumwonesha kuwa simpendi? Je, bado ninaendelea na mahusiano ya kingono na yule niliyezuiwa kuishi naye katika ndoa? je, mimi kama mzazi, nilishinikiza mwanangu afunge ndoa aliyo nayo kwa sasa? Je matokeo ya mgogoro ndani ya ndoa ya wanangu haukusababishwa na mimi mwenyewe kama mzazi?


4.   SABABU GANI ZINAKUFANYA UENDELEE KUISHI NA MKEO/MUMEO HADI SASA?
  (a) Watoto  (b) Sababu ndoa ya Kikristo haina talaka  (c) Wazazi watanilaani                      
  (d) Navumilia (e) Bado nampenda (f) Tunaishi kwa mazoea          

      Wanawake 9 walisema bado wanawapenda waume zao. Katika jibu hili, wanawake 4 wameongezeka na kudai kuwa licha ya mateso makubwa wanayopata, lakini wanawapenda sana waume zao japo wanalipwa ukatili. Wanawake 86 walisema wanaishi tu kwa ajili ya watoto. Wanasema wakiondoka watakaoteseka ni watoto na wasingependa walelewe na mama wa kambo. Juu ya amri ya kanisa, hakuna aliyeona kama ni sababu. 3 walisema wanaogopa laana ya wazazi "Kwetu ukiachwa na mumeo, hupokelewi hata kama una haki" anasema mmoja wao. Kwa lugha nyingine wanaishi kwa uvumilivu tu na sio kwa mapenzi. Wanawake wawili walisema wanaishi na waume zao kwa sababu wameshazoea. "Kila mwanaume ana matatizo yake. Bora zimwi likujualo..." ndilo hitimisho la jibu lao. Nao wanaume, 16 walisema wanawapenda wake zao na wala hawajuti kuoa. 51 wakasema ni kwa sababu ya ndoa ya Kanisa. Wanaume 24 wakasema ni kwa sababu ya watoto. Waliobaki, ingawa majibu hayakufanana sana, lakini maana halisi waliokusudia ni kuwa wawepo ama wasiwepo hawaoni tofauti yoyote. Wanaishi kwa mazoea!

     TAFAKARI KWA MSOMAJI;

           Kwa nini naendelea kuishi na huyu mwenzangu. Ni kwa sababu ya watoto? Sina pa kwenda ama  naogopa kutengwa na Kanisa langu na hivyo kukosa huduma za kiroho? Ni kweli kwamba naishi na huyu mwenzangu kwa sababu nampenda japo yeye hanipendi?

5.  JE, WADHANI CHANZO KIKUBWA CHA MATATIZO KATIKA NDOA YAKO NI KIPI?
 (a) Kazi/ kipato kizuri  (b) Wazazi wako (c) Wazazi wake (d) Marafiki (e) Wewe
(f) Umasikini (g) Mmemuasi Mungu

Wanawake 33 walisema chanzo ni kipato kizuri cha waume zao kinachowafanya
wawe na "jeuri" ya kutumia fedha katika starehe na kuiacha familia ikiteseka. Nao wanawake sita (6) walisema chanzo ni wazazi wao ambao huwanyanyasa waume zao kwa vile hawana kipato kikubwa kulingana na kule walikotoka wao. Kwa sababu hiyo mwanaume anatumbukia katika kunywa pombe muda mwingi kama njia ya kupunguza msongo wa mawazo ya kunyanyaswa na wakwe zake. Aidha, wanawake 14 walisema chanzo ni wakwe zao (wazazi wa mume) ambao wengine wanawanyanyasa kwa vile hawajajaliwa kupata mtoto.
   Wanawake saba (7) wanakiri kuwa mashoga (rafiki wa kike) wamechangia sana kuvuruga nyumba zao kwa sababu wengi wao walikuwa ndumilakuwili. Inadaiwa kuwa marafiki hao huweza kukuletea habari za mumeo kuwa na wanawake wengine, kumbe ni huyo huyo anarudi tena kwa mumeo kumweleza eti una wanaume wengine. Matokeo yake kila mmoja anamkasirikia mwenzake, anakuwa jeuri na hata kufanya mambo mabaya kwa kuamini maneno ya mashoga (marafiki). Hakuna aliyekubali kwamba, binafsi amechangia vurugu katika nyumba yake. Kila mmoja ameelekeza kidole kwa wengine kuwa chanzo. Nao wanaume kumi na watatu (13) walisema kuwa chanzo ni kipato kidogo walichonacho hivyo, wake zao kuwadharau. "Mke wangu kabla hajaanza kazi alikuwa na tabia njema kabisa. Hata siku za mwanzo alikuwa akiwahi kurudi na apokeapo mshahara hukimbia nao nyumbani na kunikabidhi wote.pesa zake na zangu tulitunza pamoja na kila kitu tulifanya kwa kushauriana. Lakini Ghafla akabadilika na kuwa mtu tofauti. Mkali, dharau, masimango na hata kulala nje akisingizia eti kuna semina kumbe anatembea na bosi wake" anasema kwa masikitiko makubwa mmoja wa wanaume hao.
     Wanaume kumi na wanne (14) walisema chanzo ni wazazi wao kwa sababu mke hajajaliwa kuzaa. "Wazazi wengi wanapoona siku zaenda na hawaoni dalili za mjukuu, sio rahisi kukubali. Lazima waje juu na hata wewe ukiangalia kwa ule ukweli, inauma maana unahitaji mtoto ili hata ukifa jina libaki" anasema mwanaume mmoja kati ya hawa. Wanaume tisa (9) walisema chanzo ni wakwe zao, yaani wazazi wa mke.. "Unajua mimi nimeoa katika ukoo wa watu wenye nazo (matajiri). Sasa  hilo limekuwa gumu kukubalika kwa wakwe zangu ambao kila siku hawaachi kufanya chokochoko ili tu nimwache mke wangu. Hudiriki kumwita huko kwao na kumlazimisha kukaa hata mwezi bila idhini yangu. Nikilalamika, inakuwa balaa" anasema mmoja wao. Mwingine alijibu huku akionesha ujumbe wa maandishi (sms) ambao ulitoka kwa mama mkwe wake baada ya kuhoji vipi aingilie ndoa yake. Ujumbe huo ulisema hivi:- "hivi wakiitwa wanaume nawe utasimama. Sijui mwanangu kaenda kukuzoa wapi kinyago kama wewe" Katika majibu karibu ya wanandoa wote, hakuna aliayesema kuwa chanzo cha matatizo ni kuwa mbali na Mungu. Wanaona kuwa kwenda kanisani na kushiriki kikamilifu shughuli za kanisa na jumuiya kwatosha kabisa na ni dalili njema ya kuwa karibu na Mungu.

TAFAKARI KWA MSOMAJI.

      Kero na masumbuko yaliyo ndani ya ndoa yangu chanzo kikubwa ni nani? Mimi ama mwenzangu? Je, sio mimi ninayeharibu? Sio wakwe zangu ama wazazi wangu? Sio marafiki zangu wanaonipotosha kwa ulevi na ukahaba? Je, sio kiburi cha pesa nilizo nazo? Ama sio kwa sababu ya ufukara wangu? Ama ni kwa sababu nimemuacha Mungu?

6.   KAMA LEO KANISA LITARUHUSU TALAKA, JE MTAACHANA?
 (a) Hapana (b) Ndiyo (c) Nitavumilia (d) Sijui

Waweza sasa hata kukisia majibu ya swali hili kwa wanandoa hawa kutokana na majibu ya maswali yaliyotangulia. Unategemea nini ikiwa idadi kubwa ya wanandoa wanaishi bila upendo? Usishangae kusikia kuwa zaidi ya asilimia sabini (70) ya wanandoa hawa walioonesha ujasiri mkubwa wa kuwa tayari KUACHANA!

TAFAKARI KWA MSOMAJI.

      Ikiwa kweli Kanisa litatoa ruhusa ya ndoa, mimi nitachukua uamuzi gani? Ni kweli kwamba sitamtwanga talaka? Moyo wangu una amani ya kuendelea kuishi na huyu mwenzangu?

7.  TANGU UFUNGE NDOA UMEWAHI KUWA NA MWANAUME/MWANAMKE NJE YA NDOA?  (a) Hapana  (b) Ndio

Kwa vile hali ya wanandoa wengi ni ya shida  kama tulivyoona, haishangazi ingawa inasikitisha sana kusikia kuwa asilimia 78 ya wanaume wote mia moja wamekiri kuwa na uhusiano wa kingono na wanawake wengine nje ya ndoa, huku asilimia 62 ya wanawake mia moja wakikubali kujihusisha na ngono nje ya ndoa! Aibu! Aibu! Aibu!

TAFAKARI KWA MSOMAJI;.

Niko mwaminifu kiasi gani kwa ahadi yangu ya ndoa na kwa mwenzangu? Je, ni kweli kwamba sina mtu ninayezini naye? Hivi kama nikijua kuwa mwenzangu ana mtu mwingine nitaumia kiasi gani na nitachukua hatua gani nikiwakuta? Kama inaniuma kwa nini nafanya hivyo?

8.   SABABU GANI ILIYOKUFANYA UWE NA UHUSIANO WA KINGONO NJE YA NDOA?
 (a) Kuchuja kwa mwenzangu (b) Tamaa ya mwili (c)  Marafiki wabaya                                   
(d) Kasoro ya kimaumbile ya mwenzangu (e) Tamaa ya mali
(f) Kukosekana kwa maelewano ndani ya nyumba

Wanaume 9 walisema kuchunja kwa wake zao ndio sababu iliyowafanya watoke nje, wakati wanaume 13, wakadai kuwa ni tamaa ya mwili. Kadhalika wanaume 7 Wanakiri kuwa marafiki zao ndio waliowaambukiza tabia ya kuwa na wanawake nje ya ndoa, na karibu waliobaki katika kundi la wale wenye uhusiano nje ya ndoa wakisema kuwa kukosekana kwa amani ndani ya nyumba kumechangia sana watafute amani ya moyo nje ya ndoa.
Kwa wanawake, kuchuja kwa waume zao na tamaa ya mwili haikuonekana kuwa na maana zaidi kwao, bali marafiki wabaya, tamaa ya mali na kukosekana kwa maelewano ndani ya ndoa ndizo sababu kubwa zilizowafanya watoke nje ya ndoa. Ni wanawake wawili tu kati ya hao waliosema kuwa wamechukua uamuzi wa kuwa na mahusiano nje ya ndoa kutokana na kasoro za kimaumbile za waume zao. Mmoja kati ya wanawake hao wawili, alisema kuwa suala la kutoka nje ya ndoa analijua mume wake na walifikia uamuzi huo, kama njia ya kumsaidia mwanamke. “mume wangu hana nguvu kabisa za kiume baada ya kupata matatizo. Na mimi bado kijana na ingawa namapenda mume wangu, lakini kuna wakati kama mwanadamu nazidiwa na hivyo, najikuta nimetoka nje” anajitetea mwanamke huyo. Jibu hili kwa akili na uwezo wa kufikiri wa mwanadamu ni sahihi kabisa. Ni ukweli kwamba ni kazi kubwa sana kuishi na maisha yako yote ya ndoa katika hali ya 'utawa" wa kulazimishwa. Hata hivyo, hoja hii ni nyepesi sana na haiwezi kuwa kigezo cha kumfanya mwanamke atoke nje ya ndoa.

TAFAKARI KWA MSOMAJI.

      Kwanini ninafanya ngono nje ya ndoa? nani hasa chanzo cha haya. Rafiki zangu? Pombe? Ugonjwa wa mwenzangu na hivyo kushindwa kufanya tendo la ndoa? ujinga wangu? Na tangu nitumbukie katika ujinga huu, nimepata faida gani? Na mwisho wa haya yote ni nini?

9.  JE UNA WATOTO NJE YA NDOA ULIOPATA BAADA YA KUFUNGA NDOA?
   (a) Ndio na mke anajua  (b) Ndio na mke hajui  (c) Ndio na mume hajui
   (d) Ndio mume anajua (e) Tulitoa mimba (f) Sina

Majibu yaliyopatikana katika swali hili yanatisha hata kule kuyataja tu. Wanaume 22 kati ya mia moja walikiri kuwa na watoto nje ya ndoa, ambapo 17 kati yao walisema kuwa wake zao wanajua, na watano wake zao hawajui. Nao wanawake watano walikiri kuzaa nje ya ndoa ambapo mmoja tu alikiri kuwa mumewe anajua, ingawa alimtimua mtoto. Kwa maana nyingine, wanawake hao wamewapachika watoto kwa baba asiyekuwa wao huku wakijua baba halisi wa watoto wao ni nani. Kibaya zaidi, baba wenye watoto halisi hawajui kama wamezaa na mke wa mtu. Mmoja wa wanawake hao amekiri kumjulisha mwanaume wa nje aliyezaa naye juu ya kuwa na mtoto wake. Itakuwaje atakapomhitaji, ni hatari hata kufikiria.
Vurugu kubwa inakuja katika jibu la (e). Wengi wa waliobaki, wanaume kwa wanawake, wamekiri kutoa mimba, wengine zaidi ya moja mara tu walipogundua kuwapa ama kupata mimba nje ya ndoa! Kwa lugha nyepesi ni kwamba WAMEUA! Katika kundi hili, ni wanaume wawili na wanawake watano tu waliosema kuwa hawajawahi kuzaa wala kupata mimba katika mahusiano yao nje ya ndoa.

TAFAKARI KWA MSOMAJI.

      Nina watoto ama mtoto nje ya ndoa? Huyu mtoto ni wa mume wangu kweli ama ni wa fulani? Itakuwaje kama mwenzangu akijua kuwa nimembambikia mtoto asiye wake? Je, itakuwaje kama mwenzangu akijua kuwa nina mtoto na mwanamke wa nje?nitamtambulishaje kwa watu na maisha yake yatakuwaje? Kwa nini hasa nimefikia hatua hii mbaya mbele za Mungu? Kama nilitoa mimba kwa kuogopa watu, mbele ya Mungu nitajitetea vipi kwa kuua kiumbe kisichokuwa na hatia?

10.  MNAPOGOMBANA/PIGANA MASHITAKA YAKO UNAYAPELEKA KWA NANI?
   (a)Wazazi wake (b) Wazazi wangu (c) S/mtaa (d) Kanisani (f) Tunamaliza wenyewe

Asilimia 60 ya wanandoa walisema matatizo yao huyapeleka Kanisani pale tu wanafamilia wanaposhindwa kuyatatua. Asilimia nane ya wanandoa walisema humaliza matatizo yao wenyewe bila kumshirikisha mtu wa nje. Asilimia mbili walisema hupeleka kwa uongozi wa serikali ya mtaa, wakati ni asilimia moja tu ya wanandoa hawa kumshirikisha mshenga katika masuala yao. wengi wa waliobaki, huwashirikisha marafiki ambao kwa uchunguzi huwa wameshiriki kwa namna moja ama nyingine na kuharibika kwa amani ndani ya ndoa.

TAFAKARI KWA MSOMAJI.

      Nani ninamkimbilia ninapokwaruzana na mwenzangu? Wazazi wake? wazazi wangu? Kanisani ama ninasikiliza ushauri wa rafiki zangu ambao mwenzangu anawalaumu kuwa chanzo cha matatizo katika ndoa yangu?

No comments:

Post a Comment