WAPENDWA, nawaletea uhakiki wa kitabu cha NDOA YANGU, NINGEJUA kama ulivyofanywa na Padri Privatus Karugendo na kuchapwa katika gazeti la Tanzania Daima hivi karibuni.
UHAKIKI
WA KITABU: NDOA YANGU “NINGEJUA.....!”
- Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu
kinachohahikiwa hapa ni NDOA YANGU ‘Ningejua...!’, Kimeandikwa na Charles B
Misango. Kitabu hiki kina namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani
(ISBN): 9987 433 022. Kitabu kina kurasa 109 . Na anayekihakiki sasa hivi
katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Kitabu hiki kinaitwa Ndoa
Yangu Ningejua...! Haina maana kwamba
mwandishi anaandika juu ya ndoa yake, bali kwa vile ameamua kuandika juu ya
ndoa anataka kila mtu aichunguze ndoa yake na yeye akiwemo. Kwa maoni ya
mwandishi kama angeandika “Ndoa yako” au “Ndoa zenu” ingekuwa sawa na
kuwanyoshea wengine kidole kana kwamba ndoa yake haina changamoto zozote zile.
Ni Ndoa yangu... tunaiboresha vipi? Au tuseme: Ndoa yangu, Ningejua.... ningeiboresha au ningefanya chaguo zuri? Au
ningezingatia maadili na busara ya kuiongoza ndoa; kuwaunganisha watu wawili ni
kazi kubwa ambayo bila uvumilivu na kuchukuliana ni muungano wenye mashaka!
Lengo kubwa la mwandishi ni
kumwalika kila mwenye ndoa kuichunguza ndoa yake na kutafakari kwa kulinganisha
na yale anayoyaandika mwandishi katika kitabu hiki. Msukumo wa kuandika kitabu
hiki umetokana na ukweli kwamba siku za hivi karibu na hasa kwenye Jiji la Dar-es-Salaam,
ndoa nyingi zinafungwa na sherehe kubwa zinafanyika kwenye kumbi mbali mbali,
na jinsi ndoa nyingi zinavyofungwa kwa mbwe mbwe ndivyo ndoa hizo zinavyovunjika
na nyingine zinakuwa na changamoto, vurugu na migogoro nyingi baina ya familia
za bwana harusi na bibi harusi.
Kosa liko wapi? Kwa nini
hakuna amani kwenye ndoa? Tumekosea wapi
kama jamii? Haya ndiyo maswali ambayo mwandishi anajaribu kuyajibu baada ya
kufanya utafiti wake na kuwahoji watu mbali mbali wenye ndoa.
Mwandishi wa kitabu hiki
ambaye pia ameoa, maana kwenye shukrani anasema hivi: “ Shukrani za pekee
zimwendee MKE WANGU ambaye kwa maisha yake, amenisaidia pasipo yeye mwenyewe
kujua, jinsi maisha ya ndoa yanavyoweza kubadilika kutoka namna mmoja hadi
nyingine na njia ya kukabiliana nayo”. Kwa wengi mwandishi huyu anajulikana
kama MC Kibonge, ingawa ni mwembamba kwa maana ya neno hilo – labda kwa vile
mambo yake ni ya “Ubonge bonge” kama alivyoandika kitabu hiki juu ya ndoa. Huyu
ni mwandishi aliyebobea na kwa wale wanaosoma gazeti la Tanzania Daima watakuwa
wanakutana safu yake ya Nani anajali..., Alifanya kazi kwenye gazeti la
Kiongozi na sasa ni mmoja wa wahariri wa gazeti la kila siku la Tanzania Daima.
III. Mazingira
yanayokizunguka kitabu
Nitafanya uhakiki wa kitabu
hiki, lakini kwanza kwa kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki.
Mwandishi alifanya utafiti juu ya maisha ya ndoa na dodoso lake lilikuwa na
maswali kwa wenye ndoa, matokeo yake ndio yalimsukuma kuandika kitabu hiki.
Nina imani kama angekutana na majibu chanya, asingeweza kupoteza muda wake
kuandika kitabu hiki. Kwa ufupi tu, tutayaangalia baadhi ya maswali:
Swali la kwanza kwa wanawake:
Kama ungejua Mumeo atakuwa na tabia alizonazo sasa ungekubali akuoe? Jibu
lilikuwa ni ama Ningekubali au Nisingekubali.
Wanawake 93 kati ya 100 waliofunga ndoa ya kanisa, walisema kuwa
wasingekubali kuolewa. Watano walisema wangekubali, wakati wawili waliobaki
walisema kuolewa ama kutoolewa kwao yote sawa. Lakini hata wale watano
waliokubali walipotakiwa waseme msingi wa kukubali kwao, baadhi ya majibu yao
yalisitisha. Watatu kati yao walisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwa waume
zao wanawapenda na ni waaminifu na wa kweli kati ndoa zao.
Swali hilo hilo waliulizwa wanaume,
na majibu hayakuwa tofauti sana, maana wanaume 79 kati ya 100 walihojiwa
walisema wasingekubali kuwaoa wanawake hao kama wangefahamu tabia zao, ni 12 tu
ndio waliosema wangekubali kuwaoa.
Swali la pili kwa wanandoa
lilikuwa: Je, Umeoa/kuolewa na Mtu uliyemtaka; Ni chaguo lako halisi. Hapa jibu
lilitakiwa Ndiyo au hapana. Ukweli uliojitokeza ni kwamba wengi wamefunga ndoa
na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati. Wanaume 49 kati ya 100 yalisema
walifunga ndoa na watu ambao hawakuwataka na wanawake 73 walisema waliolewa na
wanaume ambao hawakuwa chaguo lao. Kwa lugha nyingine ,ndoa 120 kati ya 200
zilifungwa pasipo hiari wala upendo wa dhati wa wanandoa wenyewe.
Utafiti huu umebaini sababu
nyingi za kuwalazimisha watu kuolewa bila upendo wa kweli, na sababu hizo ni
kama vile Kukosa uaminifu wakati uchumba, Kupata ujauzito bila kutarajia na
kulazimika kuolewa na huyo aliyekupatia ujauzito na wakati mwingine
kulazimishwa na wazazi.
Matatizo katika ndoa yanasababisha
ndoa kuvunjika, lakini wakati mwingine ndoa inaendelea hivyo hivyo kwa
matatizo. Mtafiti alichunguza na hili pia kutaka kujua: Sababu gani zinakufanya Uendelee kuishi na
Mkeo/Mumeo hadi sasa? Ni watoto? Ni kwa vile ndoa ya kidini? Ni kuogopa laana
za wazazi? Ni kuvumilia, Ni upendo? Au ni kuishi kwa mazoea?
Wanawake 9 katika ya 100
waliohojiwa walisema wanaishi kwenye ndoa hata kama ina matatizo kwa sababu ya
upendo kwa waume zao. Na 4 kati ya hao wanasema pamoja na ukatili wanaoupata
katika ndoa zao bado wanaendelea kuwapenda waume zao. Wanawake 86 katika 100
walihojiwa walisema wanaendelea kuishi kwenye ndoa kwa sababu ya watoto wao. Ni
wanawake 3 tu kati ya 100 walihojiwa waliosema wanaogopa laana ya wazazi wao.
Kwa upande wa wanaume ni
kwamba 16 kati ya 100 aliohojiwa walisema pamoja na matatizo kwenye ndoa
wanawapenda wake zao na wala hawajuti kuwaoa. Na wanaume 51 walisema ni kwa
vile ni ndoa ya kanisa ndio maana wanaendelea kuvumilia matatizo kwenye ndoa
zao na wanaume 24 walisema wanavumilia kwa sababu ya watoto. Waliobaki, ingawa
majibu hayakufanana sana, lakini maana halisi
ni kwamba kwao kuishi kwenye ndoa au kutokuwa na ndoa ni sawa sawa,
wanaishi kwa mazoea tu!
Swali jingine la utafiti
lilikuwa: Nini chanzo kikubwa cha matatizo katika ndoa? Je ni kwa kutokuwa na kipato kizuri pande zote mbili? Au ni
wazazi wa pande zote mbili au ni mtu binafsi ndani ya ndoa yake au ni umasikini
na kumuasi Mungu?
Wanawake 33 kati ya 100
walihojiwa walisema chanzo cha matatizo katika ndoa ni kipato kizuri cha waume
zao kinachowafanya wawe na “jeuri” ya kutumia fedha katika starehe na kuiacha
familia ikiteseka. Wanawake sita, walisema chanzo ni wazazi wao na 14 walisema
chanzo ni wakwe zao. Wanawake saba, walisema marafiki wao wa kike ndio
wanasababisha matatizo katika ndoa zao. Kwa bahati mbaya, hakuna mwanandoa
aliyekubali kwamba yeye binafsi amechangia kuleta matatizo katika ndoa yake,
kila mmoja anajaribu kutafuta mchawi nje ya ndoa.
Kwa upande wa wanaume, 13
kati ya 100 aliohojiwa walisema chanzo ni kipato kidogo, hii inasababisha
wanawake kuwadharau na vurugu inaanzia hapo. Na wanaume 14 walisema shinikizo
la wazazi na hasa mwanamke akichelewa kuzaa ndo chanzo cha vurugu. Katika
majibu yote hakuna mwanandoa aliyesema kuwa chanzo cha matatizo ni kuwa mbali
na Mungu. Wote wanafikiri wakienda kwenye ibada mara kwa mara wanakuwa karibu
na Mungu, hawaangalii ukaribu wa Mungu na maisha yao ya siku kwa siku kwenye
ndoa zao.
Swali la kizushi, ni kwamba
kama talaka ingeruhusiwa mambo yangekuwa vipi? Kusema kweli asilimia 70,
wangeomba talaka na kuachana na ndoa zao. Na hili linaonyeshwa na ukweli kwamba
wanaume 78 katika ya 100 walihojiwa walikubali kuwa na mahusiano ya kingono nje
ya ndoa zao, na wanawake 62 pia walikubali kutembea nje ya ndoa zao.
Pia kuna utata wa watoto. Kwa
vile siku hizi mtu anaweza kupima DNA, kuna mshangao mkubwa wa kujitokeza;
inasemekana kwamba asilimia kubwa ni watoto wa kubambikizwa; wanaume wengi
wamekuwa wakiwatunza watoto ambao si wao; ni watoto wa nje. Lakini mtafiti
alipoulizia wanaume kuwa na watoto nje ya ndoa asilimia 12, walikubali kuwa na
watoto nje ndoa. Na fumbo kubwa linabaki watoto wengi kuwa na baba tofauti na
wale wanaojulikana rasmi.
Mazingira yanayokizunguka
kitabu hiki ni utata katika ndoa, vurugu na magomvi hadi ndoa kuvunjika. Ni
kwamba ndoa nyingi hazina amani na hasa ndoa zinazofungwa siku za hivi karibuni
hazidumu. Tatizo liko wapi? Tufuatane na mwandishi wa kitabu kuona majibu.
IV. Muhtasari wa Kitabu
Kitabu hiki kina sura sita,
baada ya kutanguliwa na dibaji, shukrani na utangulizi. Dibaji ya kitabu hiki
imeandikwa na mheshimiwa Msgr. Padri Deogratias H. Mbiku wa jimbo katoliki la Dar-es-Salaam.
Ina maana hiki si kitabu cha mzaha, maana padri huyu ni mgongwe katika Kanisa
Katoliki, msomi na mtu anayeheshimika katika jamii. Kukubali kuandika dibaji,
ina maana alikisoma kitabu na kuona kinafaa kwenye jamii yetu.
Katika dibaji, padri Mbiku,
anasema hivi: “Katika nyanja za dini, jamii, Serikali na siasa, ndoa ni muhimu sana; kwa sababu bila kuwa na ndoa
nzuri na imara, dini, jamii, Serikali na hata siasa zitalegalega na kukosa
maadili mema, haki na amani miongoni mwa watu...”Juu ya mwandishi anasema “Mwandishi
wa kitabu hiki anazungumzia kwa undani na ufasaha sababu za kuvunjika kwa ndoa:
sababu za msingi ni ubinafsi, kukosa maandalizi ya kina; binadamu wenzetu; na
ibilisi... Lakini mwandishi haachii uchambuzi wake kwenye sababu tu, bali pia
anatoa ushauri na rai kuhusu nini kifanyike ili kuboresha ndoa. Hatimaye,
anaongelea wajibu wa Kanisa katika kuzishughulikia ndoa ili ziwe msingi imara
kwa jamii, dini, Serikali na hata siasa”
Utangulizi, umeandikwa na
mwandishi mwenyewe. Hapa anajaribu kuelezea kwa undani juu ya kichwa cha kitabu
kuitwa “Ndoa yangu”. Hakutaka kusema ndoa yako au ndoa yenu, kwa maana kwamba
anapozungumzia maisha ya ndoa kwa vilele na yeye anayaishi maisha hao, hawezi
kujiweka kando. Lakini pia anaposema ndoa yangu haina maana kwamba anaongelea
ndoa yake mwenyewe. Anataka kila mtu atakapokuwa anakisoma kitabu hicho, aseme
“Ndoa yangu, ningejua...”
Sura ya kwanza ya kitabu hiki
ni Ningejua. Kwa kiasi kikubwa sura hii mwandishi anatoa mrejesho wa utafiti
alioufanya juu ya ndoa. Mrejesho wa jumla ni kwamba kati ya watu 200,
waliohojiwa, 170 wanajuta kufunga ndoa na wenzio, kama wangejua tabia zao
mapema, wangefanya uamuzi mwingine. Kadhalika 122 kati ya 200 waliohojiwa
wanakiri kufunga ndoa na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati na hawakuwa changuo
lao.
Katika sura hii ya kwanza,
kutokana na maswali ya dodoso: Kama ungejua mumeo atakuwa na tabia alizonazo
sasa ungekubali akuoe, Kama ungejua mkeo atakuwa na tabia alizo nazo sasa,
ungekubali kumuoa? Mmeo/Mkeo ni chaguo lako halisi? Tunaona kwamba asilimia
kubwa katika ndoa wanaangukia mikononi mwa watu ambao hawakuwatarajia.
Mwandishi anatoa asilimia kuonyesha
jambo hili. Na sababu kubwa zikiwa ni kulazimishwa na wazazi, kukosa uaminifu
wakati wa uchumba, kupata ujauzito kabla ya ndoa na mambo mengine kama kufuata
mali na cheo cha mtu.
Pamoja na ndoa kuwa na
matatizo bado watu wanaendelea kuishi kwenye ndoa hizo. Asilimia kubwa ya
wanawake walihojiwa walisema wanavumilia magumu ya ndoa kwa sababu ya watoto.
Si upendo na wala si shinikizo la dini, bali nia watoto. Na asilimia kubwa ya
wanaume wanavumilia machungu ya ndoa kwa shinikizo la dini.
Pia kwenye utafiti huu,
mwandishi naweka wazi kwamba wanandoa wengi wanatembea nje ya ndoa na kuzaa
watoto nje ya ndoa zao. Asilimia kubwa wanalifanya suala la watoto wa nje ya
ndoa kuwa ni la siri na wengine wanalifichua kwa wenzao wa ndoa. Wanaume
wanaongoza kuwa na namba kubwa ya watoto wa nje ya ndoa.
Sura ya pili ni swali: Nilikosea wapi?
Katika sura hii mwandishi
anajaribu kuangalia sababu zinazopelekea
watu kuangukia kwenye chaguo baya na kujiingiza kwenye matatizo ya ndoa.
Kosa la kwanza ni: Hatukujijua! Ni muhimu
mtu kujijua yeye ni nani na aliumbwa kwa ajili gani. Ili mtu afanye uchaguzi
mzuri na kumpata mwenzi wa maisha ni vyema, ajijue kwanza. Kwa kujiua, anaweza
akawajua na wengine na hatima kumjua ni mtu gani anaweza kuwa mwenzi wa maisha.
Kosa la pili ni kwamba:
Hatukujua wito wetu: “ Kila mtu ameletwa duniani kwa sababu maalumu. Hivyo,
si kila mwanaume ama mwanamke alipangiwa maisha ya ndoa kama ambavyo wengi wetu
tunadhani..” (uk wa 19). Ka kutetea hoja hii mwandishi naonyesha historia ya
watu ambao waliishi maisha yao yote bila kuingia kwenye ndoa na wengine
walizaliwa wakiwa matowashi. Ili ndoa iwe ya furaha na amani ni muhimu wanandoa
wakatambua wito wao.
Kosa la tatu: Tulikurupuka! Kwamba
watu wanapotafuta wachumba hawatulii na kuchunguza na kutafakari juu ya
wachumba wao: “ Ni kama tulirukia gari lililokuwa katika mwendo bila ujuzi..”
(Uk wa 22). Mtu anapomtafuta mchumba kwa lengo la kufunga ndo ni lazima
ajipatie muda wa kutosha. Uchumba wa siku moja na ya pili kufunga ndoa ni
hatari kubwa.
Kosa la nne: Hatukuzijua familia za wenzetu: “
Tulitakiwa kujua historia ya maisha ya familia ya wenzetu kikamilifu. Kujua
kama wana maisha ya ajabu kama vile uchawi ama
wapenda ushirikina. Maana kama huyu alizaliwa, akalelelewa katika maisha
ya aina hii, uwezekano wa yeye kushiriki matendo hayo ni mkubwa...” ( Uk wa
26).
Kosa la tano ni: Hatukuwajua wenzetu:
Ni muhimu kumfahamu mwenzako
vizuri kabla ya ndoa. Ni muhimu pa kuwafahamu marafiki zake, kufahamu kama huyu
ni msiri au ni muwazi? Na je mlikutana katika mazingira gani? Ni mazingira ya
kuruhusu mtu kuwa wazi au ni mazingira ambayo yanaweza kuwa ni shinikizo? Je
tulikutana kazini? Tulikutana kanisani au kwenye baa? Kama tulikutana kwenye
baa, kesho na keshokutwa tabia kama hiyo inaweza kujirudia.
Kosa la sita na saba, ni kutojua uzito wa agano.
Maana ndoa ni agano linalowaunga watu
wawili, kwa imani nyingine, hawa wanakuwa kitu kimoja. Si wawili tena bali ni
kitu kimoja. Je wanandoa tunajua uzito huu kabla ya kufunga ndoa? Tunatafakari
juu ya uzito huu kabla ya kufanya uamuzi?
Sura ya tatu ni swali pia: Ndoa yangu ni mpango wa Mungu?
Mwandishi, anataka tutafakari
juu ya ndoa kama mpango wa Mungu. Tunafunga ndoa kujifurahisha au tunafunga
ndoa kuendeleza Mango wa Mwenyezi Mungu wa kupendana na kuzaa kwa lengo la
kuujaza ulimwengu?
Sura ya nne ni swali jingine:
Nani maadui wa ndoa yangu? Katika
utafiti uliofanywa, ambao unajadiliwa kwenye sura ya kwanza. Wanandoa
walipoulizwa swali hili, wote waliwanyoshea wengine kidole, kwamba maadui wa
ndoa zao ni ndugu, wazazi na marafiki. Walishindwa kutaja kwamba adui mkubwa wa
ndoa ni wanandoa wenyewe. Kuna suala la kuendeleza utoto katika ndoa. Mtu
anafunga ndoa lakini anashindwa kuachana na tabia zake za kitoto; hiki ni chanzo
cha matatizo katika ndoa nyingi. Pili kuna suala la kuendeleza ukahaba kwenye
ndoa na hiki ni chanzo cha matatizo mengi kwenye ndoa. Kuna tatizo la kunyimana
tendo la ndoa; likisababishwa na kutembea nje ya ndoa na wakati mwingine
unywaji wa pombe kupindukia. Kuna kauli mbovu kwenye ndoa, ujeuri, majivuno na
kudharauliana.
Ni wazi hatuwezi kukwepa
kabisa ushawishi wa wazazi katika ndoa zetu. Bila uangalifu, uhusiano wa wazazi
unaweza kujenga matatizo makubwa katika ndoa zetu. Ndugu, jamaa na marafiki nao
wanaweza kuleta matatizo makubwa kwenye ndoa. Na la mwisho ambalo watu wengi
wanasahau ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Ndoa, ambayo haina msingi wa dini ni vigumu
kusimama na kustawi. Hayo ndo maoni ya mwandishi juu ya matatizo yanayozikumbwa
ndoa nyingi.
Sura ya tano ni swali pia: Tufanye nini sasa?
Mwandishi anasema: “ Kwa sisi
tulioingia katika ndoa, sasa si wakati
wa kujihukumu wala kuhukumu wengine. Si wakati wa kujua kama tulikuwa na wito
wa ndoa ama hapana. Si wakati wa
kuwashambulia wenzetu kwa mabaya yanayotendeka ama yaliyotendeka siku za
nyuma ndani ya ndoa zetu. Si wakati wa kujua iwapo tulifunga ndoana watu wasio
wetu wala chaguo la Mungu..”. Kwa maoni ya mwandishi, kila wakati ni wakuanza
maisha upya. La msingi ni kumrudia Mwenyezi mungu na kuishi kwa kutekeleza
mpango wake. Na la msingi ni kujuta na kuomba msamaha, kuwaomba wenzetu wa ndoa
msamaha, kuwaomba watoto msamaha na kuiomba jamii nzima msamaha.
Sura ya sita: Wajibu wa kanisa.
Katika sura ya mwisho,
mwandishi analigeukia kanisa na kulibebesha mzingo mkubwa wa kulinda na kutunza
ndoa. Kwa maoni yake ni kwamba Familia ndiyo msingi wa kila kitu. Msingi wa
kanisa, msingi ya jamii. Bila kuwa na ndoa nzuri ni vigumu kuwa na jamii nzuri.
Hivyo kanisa lina wajibu mkubwa kuhakikisha ndoa zinakuwa imara na zinadumu.
V. TATHIMINI YA KITABU.
Nianze kwa kumpongeza Charles
B. Misango, kwa kazi hii nzuri sana aliyoiandika. Kusema kweli kazi hii
inaburudisha, inasikitisha na kufikirisha. Utafiti wake juu ya ndoa, umeweka
ukweli wazi. Na kila atakayekisoma kitabu hiki atakuwa makini kumchangua mwenzi
wa maisha.
Pili, ni maoni ya baadhi ya
watu waliokisoma kitabu hiki:
Fred Jackosn wa Keko Dar-es-Salaam, anasema “ Kama
nisingesoma kitabu hiki na kuamua kufuatilia kwa ukaribu historia ya familia na
ukoo wa mchumba wangu, ningejikuta naishi na mtu aliyebobea uchawi. Kitabu hiki
kimeokoa maisha yangu” (uk wa 109)
Naye Betty wa NMB Makao Makuu
Dar-es-Salaam, anasema: “ Huu ni funuo wa ajabu sana katika maisha yangu ya
ndoa. Kitabu kimenisaidia sana kujua namna gani kudumisha upendo na amani kati
yangu na mume wangu, upi wajibu wangu katika ndoa yangu” (uk 109).
Na Peter Mizambwa wa
Kisarawe, anasema hivi : “ Kama kuna wachumba watakaokisoma kitabu hiki na
kuamua kufuata kile kilichoanikwa, hakika wataamua kuanza upya, maana wengi
tumechumbiana kienyeji kabisa...”(Uk 109)
Kyaruzi-Rc wa Magomeni,
anasema “ Hiki ni kitabu kilichoanika ukweli mtupu wa maisha ya wanandoa wengi.
Kitasaidia sana kuamsha akili za wanandoa na kurejesha amani katika ndoa nyingi
zilizosambaratika na hata zisizo na amani. Kimetoa pia ukweli juu ya wajibu wa
Kanisa kuhusiana na malezi ya wanandoa na kitaokoa wengi”
Zainabu Rahab wa Mikocheni,
naye anasema “ Kitabu hiki ni kioo halisi cha kila mwanandoa. Ingefaa kila aliye
katika uchumba akisome kwa makini ili kupata msaada wa Mungu katika safari ya uchumba...” (Uk wa 109).
Tatu, mwandishi wa kitabu
hiki ametuingiza ndani ya tafakuri. Utafiti wake unaonyesha wazi jinsi ndoa
nyingi zilivyokuwa na matatizo. Swali la kujiuliza sote ni je, ndoa ni Mpango
wa Mungu? Je, Mungu alitaka tuishi kwenye kifungo hiki cha ndoa, au mpango wake
ulikuwa ni sisi pia kuishi kama wanyama wengine? Ukiangalia asilimia ya
wanandoa wanao kwenda nje ya ndoa zao, unakuwa na mashaka. Na je mbona Mwenyezi
Mungu, anaendelea kuumba watu wazuri bila kukoma? Mbona hawezi kuviwekea
kizingiti vishawishi ndani ya miili yetu? Yeye si ni Muumba wa vyote?
Vinavyoonekana na visivyoonekana? Je ndoa ni tendo la ndoa au ni zaidi ya hapo?
Mvuto unaokuwepo kati ya Me na Ke, unaweza kufungiwa tu kwenye ndoa? Mbona hata
baada ya mtu kufunga ndoa, bado macho yanaendelea kuona na mvuto unabaki?
Mvuto ni dhambi au kuutukuza
uumbaji wa Mwenyezi Mungu? Kusifia uumbaji wa Mwenyezi Mungu ni dhambi? Na
kusifia mipaka yake ni wapi? Kuona na kuacha? Kuona na kugusa? Au Kuiingia
kwenye ndoa? Na tuiingie na wangapi kwenye ndoa? Ndoa ya mke mmoja na mwaume
mmoja? Mwanaume mmoja wanawake wengi? Au wanawake wengi mme mmoja? Au maisha ya
uhuru bila ndoa, lakini tunatenda tendo la ndoa? Ni upi ni mpango wa Mungu? Ni
changamoto!
Nne, mwandishi ameonyesha
wazi kwamba mara nyingi tunachezea kifungo hiki cha ndoa. Hakuna mafunzo kwa vijana.
Tumepuuzia mafundisho yetu ya jando na unyago kiasi kwamba vijana wetu
wanatenda na kufuata uzoefu wa kila siku bila kuwa na mafunzo ya maisha.
Tano, mwandishi anaonyesha
wazi kwamba ndoa nyingi zina siri kubwa; watoto wa nje na nyumba ndogo. Hata wale
ambao ni watu wa “Mungu” nao wana nyumba ndogo na watoto wa nje. Mungu, apishe
mbali maana kufuatana na utafiti wa kitabu hiki, watu wakiamua kupima DNA, ndoa
nyingi zitasambaratika maana watoto wengi watagundulika ni wa kubambikizwa.
Sita, kitabu hiki kianzishe
mjadala kwenye jamii yetu, ili tutafute mamoja na ushauri wa mwandishi,
jibu la tufanye nini ili ndoa zetu ziwe
imara. Tufanye nini ili tufanye uchaguzi mzuri wakati wa kuwatafuta wenzi wa
maisha.
VI. HITIMISHO.
Kama kawaida yangu, ningependa
kuwashauri watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Ni imani yangu kwamba
watajifunza mengi kutoka kwenye kitabu hiki na hasa utafiti uliofanywa na
mwandishi.
Lakini, pia ningependa
kuwashauri wale wote watakaokisoma kitabu hiki watafute pia na vita bu vya Dr.
Binagwa, juu ya ndoa. Utafiti wa mwandishi wa kitabu hiki unamwandaa msomaji
kuvisoma vitabu vya Dr. Binagwa, ambaye anaandika kwa undani juu ya mahusiano
kwenye ndoa. Maana, haitoshi kutaja kwamba kuna suala la kunyimana tendo la
ndoa, lakini pia kuna maelezo juu ya tendo lenyewe na sababu za kufikia hatua
ya kunyimana.
Dr.Binagwa, anafafanua vizuri
hata juu ya tendo lenyewe. Haitoshi tendo tu, bali kuna namna ya kutenda tendo hilo. Hivyo kuna mengi juu ya ndoa, na
kwa kusoma vitabu hivi, mtu atagundua kwamba ndoa ni kitu kipana ambacho bila
mafunzo ni vigumu kukiishi. Ndoa zinavunjika kwa vile sote tumepuuzia suala la
kufundisha juu ya ndoa. Ni muhimu kurudisha mafundisho ya Jando na Unyago. Pia
ni muhimu kusoma na vitabu vya Jando na Unyago, ambavyo zamani tulivisoma
tukiwa sekondari.
Mwsho ni ushauri kwa
mwandishi, kwamba sasa ana kazi ya kufanya.
Yeye pia ni lazima atafute vitabu vya Dr. Binagwa na kuvisoma na kuona
jinsi vinavyomsaidia kuandika kitabu kingine juu ya ndoa. Hiki sasa ni utafiti.
Tunataka kitabu cha ndoa kutoka kwa mtu wa ndoa kama yeye na ikiwezekana atoe
mifano ya ndoa yake mwenyewe. Kama tunataka kulisaidia taifa letu, na kama
tunakubaliana kwamba taifa imara linajengwa na familia imara ni lazima
mwandishi aonyeshe hili kwa mifano zaidi.
Je watu wawili wanaweza
kuishi ndoa yao na ikawa imara? Au wanaihitaji msaada wa ndugu jamaa na
marafiki? Tendo la ndoa, ni la wawili, lakini maisha mengine yanayoizunguka
ndoa, kama uwazi, kujifunua na kutafuta msaada kwa wengine, kutafuta
ushauri,ndoa na ndoa kusaidiana; kufundishana uvumilivu na kuchukuliana ni
jambo la muhimu sana. Hatimaye ndoa si ya watu wawili, bali ni suala la jamii
nzima. Ndoa ikibaki kwenye kuta za watu wawili, ni vigumu sana ndoa hiyo
kusimama na kudumu.
Na Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
Huu ni lazima ushuhudia usomaji na kila mtu, nipo hapa kuruhusu ulimwengu wote kujua kuhusu mtu aliyeokoa uhusiano wangu na mtu huyu mkuu anaitwa Dr IZOYA. Hakika alifanya kazi nzuri kwangu kwa kumrudisha mpenzi wangu wa zamani ambaye aliniacha na kuahidi kamwe kurudi kwangu tena. Kwa hili, nimekuja kutambua kuwa kutoa maelezo ya Dk IZOYA kwa ulimwengu utafanya mengi mazuri kwa wale walio na nyumba zilizovunja au uhusiano kwa ajili yake ili kukusaidia kurekebisha uhusiano huo uliovunjika au ndoa yako. Unaweza kumfikia kupitia barua pepe yake: drizayaomosolution@gmail.com. Kuwasiliana naye na kuona jinsi tatizo lako litatatuliwa ndani ya 24hours. Pia mtaalamu katika mambo yafuatayo ...
ReplyDelete(1) Unataka kurudi nyuma yako.
(2) Unataka kukuzwa katika ofisi yako.
(3) Unataka wanaume / wanawake kukufuate.
(4) Unataka mtoto.
(5) Wewe ni mjasiriamali na unataka kushinda mikataba
(6) Unataka mume wako awe wako milele
(7) Unahitaji msaada wa kiroho.
(8) Umeshambuliwa na unataka kupona fedha zilizopotea.
(9) Weka talaka
(10) Kualika kwa mila ya fedha
(11) Chagua uchaguzi