Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

WASOMI WAMCHACHAMALIA MWIGULU NCHEMBA WA CCM


WASOMI mbalimbali wameinesha kushangazwa kwao na tabia ya  Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha mapinduzi(CCM) Bara,  kutumika kama Mkuu wa Upelezi wa Makosa ya Jinai(DCI) na Mwendesha Mashataka Mkuu(DPP) ambako amekuwa  akitoa maneno na video mbalimbali kama njia mojawapo ya kutaka kuhalalisha matukio yaliyofanywa na wanachama wa upinzani.
Hayo yalisemwa jana na Mhadhiri wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Onesmo Kyauke, wakati alipokuwa akichokoza mada kwenye kongamano la kuangalia mustakabali wa nchi, lililoandaliwa na Wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDASA).
Akitolea mfano wa matukio ambayo Nchemba amekuwa akiyafanya ni pamoja na lile la kuonesha ushiriki wa kupanga tukio la ugaidi la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Wilfred Lwakatare.
Tukio lingine Kyauke alisema ni la wakati wa kampeni za uchaguzi wa udiwani Jijini Arusha, ambako kiongozi huyo aliwataka wananchi wa Jiji hilo kutochagua madiwani wa Chadema kwa kuwa ni chama cha ugaidi kwa madai kwamba ndio waliohusika kummwagia tindikali kijana wa Igunga.
Kutokana na matamshi hayo, Mhadhiri  huyu alisema baadhi ya wanachama wa Chadema waliweza kukamatwa kama njia mojawapo ya kuisaidia polisi jambo linalowafanya kama wasomi kujiuliza kuwa Mwigulu siku hizi kawa DCI au DDP?
Akizungumzia kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, alisema ndilo limekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani kwa kupoka haki ya kikatiba ya wananchi kuandamana na kufanya mikutano huku akitolea mfano wa mauaji waliyoyafaya ya Mwandishi wa habari Daudi Mwangosi Kijijini Nyororo Mkoani Iringa  wakati wa kuzindua matawi ya Chadema.
Katika mauaji hayo, alisema ushahidi wa wazi umeonesha namna gani Plisi walivyoshiriki na tume zote zilizoundwa zikaelekezea kidole Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa na Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi leo zaidi ya polisi mwenye cheo kidogo akitolewa kafara huku mkubwa wake akiendelea kupandishwa cheo.
Pia alisema kumekuwepo na upendeleo wa Jeshi hilo wa kutetea chama tawala ikiwemo enzi za Mahita kudai kuwashilikilia wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na majambia ambako hadi leo wamekosa uthibitisho ambako kutokana na uongo huo wameshindwa kumchukulia hatua kiongozi huyo.
Katika mapendekezo yake, Kyauke aliitaka  Polisi kubadili mfumo wake wa kufanya kazi, Waziri Nchimbi aeleze ni kwa nini Tanzania ni dhambi kuandamana, Waziri Mkuu kufuta kauli yake ya kutaka wanachi kupigwa tu na Jeshi hilo na wanasaiasa kubadilika katika kufanya siasa zao ambalo wengi wa sasa hivi wamekuwa wakitanguliza matusi katika kueneza propaganda zao.
Kwa upande wake Benadetha  Kilya, ambaye ni Mtaalam wa Sayansi ya Siasa  na Utawala kwa Umma, alisema mpaka sasa bado kiini cha uvunjifu wa amani hakijagundulika na badala yake pande zote zimekuwa zikirushiana mpira ikiwemo Serikali, wananchi na wanasiasa.
Kilya alizitaja sababu zinazochangia matukio hayo kuwa ni pamoja na hali ya upinzani kuja juu hivyo chama tawala  kinajihami kutokana na mabadiliko hayo, nyingine ni kuongezeka kwa kiwango cha umasikini na mfumo wa kiliberali  ambao umechangia matabaka, uhuru wa kutoa maoni tofauti na enzi za ujamaa.
Ayoub  Rioba, Mhadhiri wa Chuo cha Uandishi wa habari katika masomo ya Habari na Mawasiliano kwa Umma, alisema suala la amani sio la kuombewa bali ni la kisayansi zaidi  na kudai kwamba wanasiasa wamekuwa wakijidanganya pale wanapowahimiza watu kuliombea taifa hili amani.
Pia Rioba alikanusha kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikichangia kuharibu amani na badala yake alivifananisha vyombo hivyo na bunduki ambako kama isipotumiwa kamwe haiwezi kuharibu amani.
Akifafanua hili alisema vyombo vya habari vitaharibu amani endapo tu wanasiasa watavitumia na kuitaka jamii ielewe kwamba vyombo hivyo  vina dhima kubwa kama mlinzi wa Taifa na ndio maana wakati mwingine vinapendekezwa kuwa NGO’s ili viweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi.
Wito wake kwa vyombo vya habari, Rioba alivitaka kujua histiroa ya nchi   kuanzia enzi za utumwa, kujua dhima  ya vyombo vya habari, sheria za vyama vingi, kujua katiba za vyama kuwa karibu na wananchi na kuepuka kuwa mashabiki wa migogoro.

Vile vile aliwataka wanahabari kuwa makini katika kutoa fursa kwa pande zote mbili zenye migogorokuwa na tabia ya kuuliza maswali ya kutafuta suluhu badala ya kuchochea na kuchimba na kuchunguza zaidi kuhusu kiini cha mgogoro badala ya kudandia hoja.

Akichangia hoja katika mdahalo huo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Slaa alisema mchawi wa hayo yote ni serikali, huku akinukuu ripoti ya tume ya haki na utawala bora iliyomtuhumu aliyekuwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na Msajili wa vyama vya siasa. Dk Slaa alisema Amani sio suala la kuhubiriwa au kujadiliwa, amani ni matokeo ya utekelezaji wa haki mbalimbali.
Dk Slaa pia alilalamikia vitendo vya ukatili vilivyofanywa Mtwara na vyombo vya dola dhidi ya wananchi, huku akimnyooshea kidole Brigedia Elia Athanasi aliyekuwa amemwakilisha Mkuu wa majeshi, Dk Slaa alisema “jeshi letu lilikuwa linaheshimika sana, lakini siku za hivi karibuni linaelekea kupoteza heshima yake kwa jamii, tukirejea mfano katika uchaguzi Mkuu uliopita ambapo mnadhimu wa jeshi Abdulrahman Shimbo alivyotoa kauli yenye utata, jeshi linaingiaje kwenye siasa wakati suala la uchaguzi ni suala la kiraia? Alihoji Dk Slaa
Hoja ya Dk Slaa kuhusu utendaji wa jeshi la wananchi Mkoani Mtwara ilipingwa kwa haraka na Brigedia Athanasi akisema “naomba kuweka wazi kuwa jeshi letu lipo Mtwara, lina adabu na vitendo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa ni vya propaganda tu kama alivyosema Dk Slaa”.
Licha ya Mwanajeshi  huyo kujitetea, mchangiaji aliyefuata alikuwa ni Julisu Mtatiro, Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyethibitisha kuwa wanajeshi wanabaka na walitenda vitendo vya kikatili dhidi ya raia na viongozi wa CUF akiwemo Mkurugenzi wa Chama hicho kutoka makao makuu Shaweji Mketo.
NCCR WAJITETEA.
Akichangia mjadala huo, Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi alisema kwanza Chama chake hakipo tayari kufanya maandamano, na kwamba Chama chake kimeamua kupambana kwa nguvu ya hoja, na wataendelea kutumia nguvu ya hoja kama walivyomtuma Mbatia akapeleka hoja ya Elimu Bungeni na wakaungwa mkono na watanzania wengi.
Akihitimisha kongamano hilo la Amani, Wazri wa Mambo ya ndani Dk Emmanuel Nchimbi alisema kuwa kati ya mambo ambayo  yanayompa changamoto ni amani ya nchi hii. Alisema kuwa tulirithi nchi ikiwa na amani, hivyo tuna deni la kurithisha nchi hii ikiwa ya amani katika kizazi kijacho.
Dk Nchimbi alikemea suala la udini, akitahadharisha watanzania kuwa wasiingie katika vurugu na wasikubali kugawanywa kwa sababu ya dini zao. “Tukiingia katika vurugu za dini hatutapona, Wakristo na waislam wote tukatae kugawanywa kwa kutumia misingi ya udini kwa manufaa ya Tanzania ya sasa na kizazi kijacho.
Kwa upande wa siasa, Waziri Nchimbi, huku akimtambua Katibu Mkuu wa Chadema Dk Slaa, alisema wanasiasa wote wana wajibu wa kuwatumikia wananchi, “Suala la amani sio suala la chama cha Mapinduzi peke yake, ni suala la wanasiasa wote wa Chama tawala na wapinzani kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma, na kuvumiliana kisiasa ndio kunaleta amani.
Kuhusu vyombo vya dola kutumika vibaya Dk Nchimbi aliwatetea polisi, na kusema kuwa kuna sehemu ambazo pia polisi wanakosea na wanawajibishwa, huku akitaja takwimu za askari waliowajibishwa kwa mwaka 2012 kuwa Askari 106 wamefukuzwa kazi, Maafisa 6 wa polisi wamesimamishwa na 95 walifukuzwa Chuo cha Polisi kilichopo Moshi waliojiunga kinyume cha utaratibu. Dk Nchimbi alikwepa kuzungumzia suala la mauaji ya Arusha, Morogoro na Iringa ambapo wakati wa mjadala yalijitokeza sana kuhoji uadilifu wa polisi, hasa aliyekuwa  kamanda wa Polisi wa mkoa wa Iringa aliyevunja sheria na kusababisha kifo cha Mwandishi wa habari Daud Mwangosi

Hakimu ashinda kesi ya rushwa

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Ilala, jijini Dar es Salaam, imemwachia huru Hakimu wa mahakama hiyo, Pamela Kalala, aliyekuwa akikabiliwa na makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa ya sh 100,000 kwa njia ya simu.
Uamuzi huo ulitolewa jana asubuhi na Hakimu Mkazi, Alocye Katemana, ambaye alisema kwa mujibu wa vielelezo na ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa  Jamhuri katika kesi hiyo, mahakama yake imeona upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yake.
Hakimu Katemana alisema kwa mujibu wa hati ya mashtaka inaonesha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, walidai kuwa Kalala aliomba na kupokea rushwa kutoka kwa Josephine Wage, ambaye ni mke wa mshitakiwa, Abubakar Mzirai ambapo Kalala alikuwa akisikiliza kesi ya jinai inayomkabili Mzirai ili amfutie kesi.
‘Lakini mimi nimeyasoma malalamiko yaliyoandikwa na Joseph kuhusu Kalala na nimebaini katika malalamiko yake, Josephine alikuwa akilalalamika kuwa Hakimu Kalala alipomfutia dhamana mumewe (Mzirai), hakutaja sababu,” alisema.
Alisema kuwa Josephine alilalamikia mwenendo wa kesi lakini hakuna mahala popote alipolalamika kuwa Kalala alimuomba au kumpatia rushwa.
Alisema kuwa alibaini ni kweli Hakimu Kalala alishindwa kuandika sababu za kumfutia dhamana mshitakiwa licha ya sababu hiyo kutoweza kuishawishi mahakama hiyo imuone mshitakiwa ana kesi ya kujibu.
“Na kwa sababu hiyo mahakama hii inamuachilia huru kwa vile upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo ya rushwa dhidi ya Hakimu Kalala,” alisema Katemana.
 Awali ilidaiwa na Wakili wa Serikali, Kasamala kwamba Pamela akiwa mwajiriwa wa Mahakama, kama Hakimu Mkazi na wakala wa sheria ya Takukuru, alikiuka kifungu namba 11 cha sheria ya mwaka 2007 kwa kuomba rushwa kutoka kwa Josephine Wage.
Kasamala alidai Pamela alitenda kosa hilo ili kumshawishi kutoa uamuzi wa kumpendelea mumewe. Katika shtaka la pili, Hakimu Mkazi Pamela anadaiwa kuwa Februari 2, mwaka huu, eneo la Manispaa ya Ilala, akiwa na wadhifa huo, alipokea sh 800,000 kutoka kwa Josephine.
Pia anadaiwa kuwa  Februari 6, mwaka huu, katika eneo hilo, alipokea tena sh 100,000 kutoka kwa Josephine.
Hiyo si mara ya kwanza kwa mahakimu kufikishwa mahakamani hapo kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.
Aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Jamila Nzota, alifikishwa katika mahakama hiyo na mwaka 2010 alitiwa hatiani kwa makosa hayo na kufungwa jela miaka mitatu.

Mwisho


No comments:

Post a Comment