Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

HABARI NZITO




OPERESHENI UJANGILI YAZIDI KUPINGWA


WAKILI wa kujitegemea, Alloyce Komba wa Kituo cha Uwakili cha Haki Kwanza, amesema vitendo vya kutokomeza majangili vilifanyika kinyume cha katiba ya nchi ibara ya 15(1).
Alisema ibara hiyo inataka kila mtu kuwa na uhuru wa kuishi, lakini operesheni hiyo ilikiuka haki ya kutoteswa na kudhalilishwa, inayokataza mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama na kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Komba alisema kuwa anaishangaa serikali kutumia wanajeshi katika operesheni hiyo wakati hawana utaalamu wa kuhoji.
Kwamba matokeo yake walitengeneza mahabusu zisizo rasmi, kuwaweka watu katika mateso makali ili waweze kukubali makosa mbalimbali waliyotuhumiwa nayo kuhusu ujangili.
Alisema anao ushahidi kutoka kwa mmoja ya wateja wake, Ali Gedi (65), ambaye alikamatwa Kijiji cha Pawaga mkoani Iringa akiwa katika shughuli zake na kujumuishwa na watuhumiwa wengine 30 kisha kupelekwa msituni kilometa 100 nje ya mji, sehemu iliyo karibu na kambi ya askari wa wanyama pori wa hifadhi ya Ruaha.
Kwa mujibu wa wakili huyo, baada ya watu hao 30 kufikishwa huko, walifanyiwa vitendo kadhaa na askari wa wanyama pori ikiwa ni pamoja na kuwavua nguo zote, kufungwa pingu mikono na miguu na kuning’inizwa kati ya miti miwili na chini yake uliwashwa moto.
“Walichapwa fimbo wakati wananing’inizwa karibu na moto, kutishwa na kulazimishwa kusema kama wanahusika na ujangili au la, au kama wanamiliki silaha yoyote inayotumika kuua tembo,” alisema.
Alisema pia walitishiwa kuuawa kwa kupigwa risasi wakiendelea kukaidi kukiri kosa, kuwekwa katika mahabusu ndogo yenye msongamano na ambayo sio rasmi kisheria huko porini kama vile walikuwa ni mateka wa vita.
Kutokana na hali hiyo, Komba alisema hata kama Bunge limeunda kamati teule, anaomba pia watetezi wengine wa haki za binadamu nchini waingilie kati kusaidia wananchi walioteswa katika maeneo mbalimbali nchini






DK MVUNGI AVAMIWA AJERUHIWA VIBAYA
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi (61), amevamiwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa kwa mapanga sehemu za kichwani na usoni.
Dk. Mvungi ambaye ni mwanasheria maafuru nchini na mwanachama wa NCCR-Mageuzi, alivamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi saa 6:30 usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake Kibamba, Kata ya Mpiji Majohe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alikolazwa Dk. Mvungi kwa matibabu, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema watu hao kabla ya kuvunja milango ya nyumba walilipua kitu ambacho kilitoa moshi mwingi na cheche kisha kuingia ndani na kuanza kudai wapewe fedha.
Alisema kuwa hatua hiyo ilisababisha Dk. Mvungi kupambana nao bila mafanikio, ndipo wakamjeruhi vibaya kwa kumcharanga mapanga kichwani, usoni na kisha kuondoka na kompyuta mpakato (Laptop) yake, pisto na kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana.
Mbatia alisema majirani na ndugu walifanikiwa kumbeba Dk. Mvungi na kumkimbiza katika Hospitali ya Tumbi mkoani Pwani ambako alipatiwa matibabu ya awali na kisha kuhamishiwa Muhimbili saa 10:00 alfajiri.
Alisema kuwa alipokelewa na kuingizwa katika wodi ya huduma ya dharura na ilipofika saa 4:16 asubuhi gazeti hili lilishuhudi Dk. Mvungi ambaye alikuwa hajitambui akitolewa kwenye chumba hicho na kuingizwa kwenye gari la wagonjwa lenye namba za usajili STK 8767.
Wakati huo, Dk. Mvungi alikuwa akipelekwa katika Hospitali ya Aghakan kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha siti scan kwa ajili ya kuona ameathiriwa vipi katika eneo la kichwa.
Mbatia aliongeza kuwa ndugu na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walifikia uamuzi wa kumpeleka Dk. Mvungi akapimwe kipimo hicho Aghakan na kisha arejeshwe kwa sababu uongozi wa MOI uliwaeleza kuwa mtaalamu anayefahamu kutumia kipimo hicho hakuweza kupatikana mara moja.
Majira ya saa 5:58, Dk. Mvungi alirejeshwa MOI huku akiwa bado anavuja damu maeneo ya puani na kichwani na kisha akaingizwa tena katika chumba cha huduma ya dharura.
Baadaye saa nane mchana alihamishwa katika chumba hicho na kupelekwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
“Jamani Watanzania, Dk. Mvungi hali yake ni mbaya kama mlivyomuona, kwani tangu alivyopigwa jana saa sita usiku hadi sasa bado anavuja damu…tumeumizwa sana na kitendo hiki na tunaamini serikali inafanya kazi yake ya kubaini ni wakina nani wamefanya unyama huu,” alisema Mbatia.
Shuhuda wa tukio hilo, ambaye ni dereva wa Dk. Mvungi, alisema kuwa wahalifu hao walikuwa wakisema wanahitaji fedha ila walimpiga sana na mapanga na kwamba ndiye aliyembeba kumkimbiza Tumbi na baadaye Muhimbili.
Mke wa Dk. Mvungi, Anna Mvungi, alisema watu hao walipoingia ndani walitembeza mapanga huku wakimtaka asiwatazame usoni.
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliofika kumjulia hali Dk. Mvungi ni pamoja na Prof. Paramaganda Kabudi, Joseph Butiku na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Prof. Costa Mahalu na wahadhiri wengine

WABUNGE KUZIBWA MIDOMO



WABUNGE wanaotumia nyaraka za siri za serikali, Bunge au taasisi yoyote ya umma kulipua mabomu mbalimbali ndani na nje ya Bunge, kuanzia sasa 'watakiona cha moto' iwapo watakutwa nazo.
Mbali na nyaraka hizo, pia watakumbana na kibano iwapo watazomea au kufanya vurugu zitakazosababisha kuahirishwa kwa shughuli za Bunge.
Vibano hivyo vinatokana na mwongozo wa kanuni za maadili ya wabunge ambazo zinatarajiwa kupitishwa wakati wowote kuanzia sasa.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa mbunge atakayekutwa na nyaraka za siri zinazohusu utendaji wa serikali bila kibali cha mamlaka husika, atahesabika ametenda kosa na atachukuliwa hatua.
Chanzo kimoja kimelidokeza gazeti hili kuwa kanuni hizo zinamzuia mbunge kutumia taarifa zozote atakazozipata kwa wadhifa wake wakati akitekeleza shughuli za Bunge au kamati kwa ajili ya kujinufaisha, kujipatia fedha au kujipatia umaarufu.
Pia inaelezwa kuwa mbunge haruhusiwi kutoa taarifa zozote za siri za Bunge anazozifahamu bila idhini ya mamlaka husika.
Tanzania Daima limeelezwa kuwa kanuni hizo zinakataza mbunge kumtuhumu mwenzake kwa jambo lolote bila ya kuwa na ushahidi.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima, wamebainisha kuwa kanuni za maadili hayo zinalenga kuwaziba midomo wanaonekana kutumia nyaraka mbalimbali kuibua madudu yanayofanywa na serikali, taasisi au idara zilizopo chini yake.
Waliongeza kuwa kanuni hizo zina lengo la kurejesha nyuma dhana ya Bunge kuisimamia serikali, na badala yake zinajenga mazingira ya serikali kulimeza Bunge.
Walibainisha kuwa mwongozo wa kanuni za maadili ya wabunge utaisaidia serikali iendelee na madudu yake ambayo katika siku za hivi karibuni yamekuwa yakianikwa bungeni na wabunge mbalimbali.
“Bunge linataka kuingia kwenye historia mbaya, yaani linajipa kazi ya kulinda uovu wa serikali, hii ni aibu sana. Sisi hatutakubali kupitisha mambo haya, tunasubiri siku ya kuyajadili,” alisema mmoja wa wabunge.
Chanzo kingine pia kimedokeza kuwa kanuni za maadili ya wabunge pia zinawazuia wabunge kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji, unyanyasaji wa kijinsia baina yao au vitakavyowashushia hadhi katika jamii.
Tanzania Daima, limedokezwa kuwa wabunge hawataruhusiwa kujishirikisha na watu au vyombo binafsi kwa ajili ya kujipatia maslahi ya kifedha au mali yoyote inayoweza kuathiri utendaji wa kazi za Bunge.
 Inasemekana baadhi ya mambo yaliyomo kwenye kanuni hizo ni yale yanayotajwa kwenye sheria za nchi, ikiwemo viongozi na watumishi wa umma kutoa tamko la mali walizonazo.
Jingine linalodaiwa kuwemo kwenye kanuni hizo ni mbunge anapaswa kuepuka mgongano wa maslahi, vitendo vya rushwa, kutokuwa na ubinafsi na kutopokea au kutoa zawadi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
 Kanuni hizo zinadaiwa kumlazimisha mbunge kuweka wazi umiliki wa hisa kwenye kampuni, taasisi au asasi yoyote inayosimamiwa na kamati za Bunge.
Mbunge huyo pia atatakiwa kutoa taarifa kwa spika ili asipangwe kwenye kamati zinazosimamia taasisi hizo lengo likiwa ni kuepusha mgongano wa kimaslahi.
Pia kanuni hizo zinamtaka mbunge kushirikiana vyema na watumishi wa Ofisi ya Bunge, taasisi za umma, waandishi wa habari, asasi zinazojitegemea na makundi mbalimbali kwenye jamii.
Kanuni hizo pia zinaweka wazi kwamba uamuzi wowote ya vikao vya kamati ya uongozi utatolewa hadharani na spika au afisa yeyote wa Bunge kwa idhini ya spika.
Tanzania Daima lilizungumza na Naibu Spika Job Ndugai, juu ya kanuni hizo ambazo alisema bado hazijafikishwa bungeni kwa uamuzi, lakini anazikaribisha kwa mikono miwili.
Ndugai alisema amefurahishwa na kipengele kinachomtaka mbunge kuweka wazi umiliki wa hisa kwenye kampuni, taasisi au asasi yoyote inayosimamiwa na kamati za Bunge.
“Hizo kanuni zitatusaidia sana kwani kuna baadhi ya wabunge wamekuwa wakizizungumzia kampuni fulani kwa ubaya au mema, lakini kumbe wanamiliki hisa, sasa tutawatambua,” alisema.
Ndugai aliongeza kanuni hizo zikifikishwa bungeni zitajadiliwa kwa kina kama kuna vitu vya kuongeza au kupunguza na baadae zitapitishwa na kuanza kutumika rasmi.








WAZIRI MKUU AMEDHIHIRISHA KWAMBA WATETEZI WA HAKI ZA WAFUGAJI WALIKUWA SAHIHI KATIKA KUPINGA UMEGAJI WA KILOMITA ZA MRABA 1500 LOLIONDO.

Katika ziara yake ya hivi karibuni mjini Loliondo Waziri Mkuu  Mh. Mizengo Peter Pinda amewaambia wananchi kuwa mpango wa kuwaondoa Wanaloliondo katika maeneo yao ya malisho kwa kumega eneo lenye kilomita  mraba 1500  haukuwa sahihi na pia ni sawa na kuwanyang’anya wananchi ardhi yao.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu  ambao ulishiriki kuwaongoza watetezi wa haki za wafugaji  na viongozi wa jamii toka Loliondo kuhusu njia sahihi na salama  za kutumia kudai haki zao,  una kila sababu ya kumpongeza Mh Pinda kwa uamuzi wake wa kwenda Loliondo na kuridhika kwamba  kitendo cha serikali kupinga mpango huo kimezingatia busara na mazingira halisi ya Loliondo.

Mpango huo ulipingwa vikali na watetezi wa haki za wafugaji  hapa nchini,  lakini viongozi mbali mbali wa serikali waliibuka na kuwatishia wanaharakati hao kwa kuwaita kwamba ni Wakenya, wachochezi, wakala wa nchi za magharibi nk.  Mathalan Waziri Hamis Kagasheki alinukuliwa mara kadhaa akiwa Bungeni na nje ya Bunge akisema kuwa  kuna asasi za kiraia  nyingi ambazo ndiyo zinawachochea wananchi wa Loliondo ili kupinga mpango wa kuchukua ardhi hiyo.

Aidha Kagasheki alienda mbali na kutishia kuwa atawashughulikia wote waliokuwa wanapinga mpango huo. Kwa upande mwingine Jitihada za viongozi wa jamii  na watetezi toka Loliondo kuonana na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, mabalozi, wawaikilishi wa jumuiaya ya kimataifa na wabunge ulioratibiwa na Mtandao huu na mashirika ya kifugaji mkoani Arusha na Loliondo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuokoa ardhi ya wafugaji.

Mashirika ya watetezi wa haki yaliyosimama kidete katika kutetea ardhi hii na ambayo pia ni wanachama wa Mtandao ni pamoja na PINGOs Forum, LHRC, TPCF, NGONET, TGNP, PWC Na Haki Ardhi. Mashirika haya yaendelea kutetea haki za Mtanzania popote pale bila kuhofia vitisho au majina mabaya toka kwa baadhi ya watawala wasiopenda kusikia sauti za wanyonge. Tunawashauri watetezi hawa pamoja na wananchi wa Loliondo kuhakikisha makubaliano haya ya Serikali kupitia Waziri Pinda yankuwa katika maandishi na kushuhudiwa na wadau husika kama Wizara ya Ardhi na Maliasili kwa kumbukumbu ya siku za usoni.

Tunapenda kumshukuru Pinda kwa kuubatilisha upotoshaji kama ilivyokuwa ikihubiriwa na baadhi ya viongozi wa serikali kakiwamo Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkuu wa mkoa wa Arusha pamoja na Waziri Kagasheki dhidi ya Wanaharakati. Mtandao huu unaahidi kutoa ushirikiano kwa watetezi wote wa haki za binadamu pindi itakapohitajika kufanya hivyo, na unasisitiza kwamba mara nyinigi watetezi wanasimamia na kutetea haki za wananchi hata kama baadhi ya viongozi wanawatishia na kuwabatiza majina mabaya kama yale yaliyozoeleka kwamba ni wachochezi, wafuasi wa vyama pinzani au mawakala wa nchi za Magharibi.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu

sign.png
…………………………
Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Watetezi Tanzania





MAJAMBAZI WAPORA



Hivi sasa majambazi wamevamia gari moja mali ya kampuni ya tigo ,
wamepasua matairi kwa risasi na kufanikiwa kuiba kiasi fulani cha
hela

Tukio hilo limetokea maeneo ya Morocco karibu na jengo la Airtel
dakika chache zilizopita .


Mtoto azaliwa bila kichwa, kifua

Na Jumbe Ismailly,Singida    

MTOTO wa ajabu  amezaliwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida huku akiwa hana baadhi ya sehemu za mwili wake kuanzia kifuani hadi kichwani.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida,Dk.Joseph Malunda amesema tukio hilo ni la mara ya kwanza katika Hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa daktari huyo mama wa mtoto huyo alikuwa amejifungua watoto wawili pacha wote wa kike wakiwa na miezi saba huku mmoja akiwa na viungo vyote.

Dk.Malunda alidai mama wa watoto hao Amina Bilau baada ya kujifungua mtoto wa kwanza, alifuatia mtoto mwingine ambaye hakuwa na mikono,kifua na kichwa.  

Hata hivyo, mtoto wa kwanza aliweza kuishi kwa saa sita tu na kufariki.

Kutokana na hali hiyo,Dk. Malunda alitumia fursa hiyo kuwashauri akina mama wanapopata ujauzito wasisite kuhudhuria kliniki na kuacha kutumia madawa makali yanayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa watoto ambao wenye upungufu ya viungo.

Akizungumzia tukio hilo, Amina Bilau mkazi wa Kijiji cha Mtamaa katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida alisema wakati wa ujauzito wake yeye aliona tumbo lake likiongezeka, na baada ya kupata matibabu katika zahanati ya Kijiji bila mafanikio na akaamua kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na kisha kujifungua watoto hao.
Baba wa watoto hao, Maulidi Mkuki alisema hata yeye anashangaa kuona mkewe amejifungua mtoto wa aina hiyo wakati  wana watoto wengine watatu waliozaliwa bila matatizo yoyote yale.

‘’Kwa kweli naona ni ajabu kwa mama kujifungua mtoto na ‘mdoli’alisema Mkuki akiwa na masikitiko.
.



…DK Ulimboka aitesa serikali
*Aliyemtuhumu apewa ulinzi mkali
* Kikwete: Ahoji tumtese  kwa lipi?

Hellen Ngoromera na Irene Mark

SIKU chache baada ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, kudaiwa kuhusika kwenye sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, imeelezwa kuwa afisa huyo amewekewa ulinzi mkali.

Habari za ndani ya Jeshi hilo zinasema kuwa afisa huyo anaishi kwa mashaka kutokana na tuhuma nzito aliyotupiwa, hatua iliyowafanya wakuu wake kumpa walinzi wawili wa kulinda usalama wake wakati huu ambapo uchunguzi unaendelea chini ya tume maalumu iliyoundwa.

“Issue ya Dk. Ulimboka imemweka pabaya afande Msangi, anaishi kwa hofu sana hadi kufikia hatua ya kupewa walindi wawili,” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Hata hivyo, pamoja na kukiri kukiri kusikia tuhuma hizo ambazo amezikana, Msangi ameliambia Tanzania Daima kuwa, yeye hana hofu kwa kuwa anajua hajafanya wala kuhusika kwa namna moja ama nyingine na tukio la Ulimboka.

Alikanusha kupewa ulinzi, ingawa Tanzania Daima lilishuhudia kwa siku mbili  akiwa ameambatana na watu wengine wawili kila alipokwenda, ingawa alikiri kuwa ni askari wake na kwamba hilo ni jambo la kawaida.

Kwa mujibu wa kanuni za kazi za polisi, Kamanda wa Polisi wa mkoa ama wa Kanda Maalum ndiye tu anayepewa ulinzi binafsi, lakini sio mkuu wa upelelezi wa mkoa.

JK Serikali imtese Ulimboka kwa lipi?
Rais Jakaya Kikwete, ameeleza kushangazwa kwake na tuhuma zilizotolewa na baadhi ya madajktari na wana harakati kwamba, inahusika kumteka na kupiga kikatili mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari, Steven Ulimboka.
atika hotuba yake jana kwa watanzania, Kikwete pamoja na kuelezea masikitiko yake makubwa na kuhuzunishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka usiku wa Juni, 26, 2012, alidai kushangazwa na tuhuma kwamba serikali inahusika na ukatili huo, akisema haoni sababu ya msingi ya kufanya hivyo ikizingatiwa kuwa ndiye aliyekuwa kiungo muhimu baina ya serikali na madaktari.
Kikwete alisema ingawa ni ukweli kwamba Dk Ulimboka hakuwa mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano hayo na pia kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, bado ndiye aliyeamuru aachwe aendelee kuwepo maadam madaktari wenzake wamemuamini na anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Aliongeza kuwa kutokana na mwenendo wa mazungumzo ulivyokuwa ukiendelea, hakukuwa na sababu za Serikali kufikia hatua ya kumdhuru Dk. Ulimboka
Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.  Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa” alisema.
Mnyika amkosoa JK
Naye Mbunge wa Ubungo John Mnyika alimtaka Rais Kikwete kuunda chombo huru cha uchunguzi kwa kuwa tayari baadhi ya maafisa wa polisi wanatuhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Mnyika katika waraka wake wa wazi kwa watanzania, amesema kuwa, alitarajia Rais Kikwete angetangaza kuunda tume huru ya uchunguzi au walau angeongeza nguvu katika jopo la uchunguzi lililoundwa kwa kuunda timu ya maafisa waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine kutoka taasisi huru, badala ya kuacha watuhumiwa wajichunguze wenyewe.  


Wafanyakazi kulia ama kucheka leo

Na Martin Malera, Dodoma

NYONGEZA ya mishahara kwa watumishi wa umma itajulikana leo wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani atakapowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/13 bungeni.

Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, aliposoma bajeti ya serikali kwa mwaka 2012/13 Juni 14 mwaka huu, hakuzungumzia moja kwa moja  kuhusu kupanda kwa mishahara ya watumishi wa umma.

Hata hivyo Waziri Mgimwa alitaja nyongeza mpya ya kodi ya mapato kwenye mishahara jambo ambalo linaonyesha kuwapo kwa nyongeza ya mishahara katika Bajeti itakayosomwa leo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (Tucta), Nicolas Mgaya, alisema hatma ya watumishi wa umma kupata nyongeza ya mishahara ama kutoswa imebaki kwa Waziri Kombani.

Mgaya alisema suala la watumishi wa umma kuongezewa mishahara ni madai ya muda mrefu na kwamba bado ana matumaini serikali kupitia kwa Waziri Kombani itatimiza ndoto hiyo ya wafanyakazi.

Mwaka wa fedha uliopita, kambi ya  upinzani ilipendekeza kiwango cha chini cha mihahara kitoke sh. 135,000 ya sasa hadi 315,000 ili watumishi wakabiliane na makali ya kupanda kwa gharama za maisha.

Hata hivyo Serikali ilitangaza kurekebisha mishahara ya watumishi wake kwa asilimia 40.2 kwa kuzingatia uwezo wake wa bajeti.

Kutokana na hatua hiyo, fungu la mishahara liliongezwa kwa sh bilioni 938, sawa na ongezeko la asimilia 40.2 ya fedha zilizotengwa kugharamia mishahara mwaka jana.

Katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imetenga sh trilioni 3.7  kwa ajili ya mishahara ya watumishi wake wakati  katika mwaka wa fedha 2011/2012  ilitenga  sh. trilioni 3.2 tu kwa ajili ya malipo ya mishahara, upandishwaji vyeo na kulipa madai ya malimbikizo ya mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala na Taasisi za Serikali.

Katika Bajeti hiyo ya trilioni 15, mapato ya ndani ni trilioni  8,714,671 ambapo mapato ya  kodi (TRA) ni trilioni 8,070,088 mapato  yasiyo ya kodi ni sh bilioni 644,5

Mapato ya  Halmashauri ni sh bilioni  362,2, mikopo na misaada ya kibajeti ni sh bilioni 842,4, mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo ikijumuisha MCA trilioni 2.3, mikopo ya ndani trilioni 1.6, mikopo yenye. masharti ya kibiashara ni trilioni 1.2.

Jumla ya mapato yote ni. Trilioni 15, ambapo trilioni 10 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Ends










 Huyu ni mtoto Rukia Abdallah ambaye amungua vibaya kwa maji ya moto huko kwao wilaya ya Luangwa mkoani Lindi. alipoungua wazazi wake masikini waliweza kumpeleka katika zahanati ya kijiji ambayo ilimpa huduma ya kwanza na kutakiwa apelekwe hospitali ya Ndanda ama Muhimbili jijini Dar es Salaam. Kutokana na umasikini mkubwa wa wazazi wake, mtoto huyu ameendelea kuteseka hadi sasa. Kwa kutambua kwamba kila mmoja wetu ni mgonjwa na sote ni ndugu, tumeamua kuungana na kuomba msaada wa mchango kutoka kwa kila mtu mwenye mapenzi mema ili kusaidia kumleta jijini Dar es salaam kuokoa maisha yake. 
Mkoani Lindi, mchango unakusanywa na Mwenyekiti wa Lindi Press Club Bw. Abdulaziz mwenye namba 0716-483532 na wilayani Luangwa inapokelewa na Bw Victor namba0715-754494 au 0755-754494, na hapa Dar es Salaam inakusanywa nami C. Misango namba 0756-219342 au 0713 235592. Tuna chochote kwa njia ya tigo pesa ama voda pesa tuokoe maisha yake.
Hadi sasa fedha chache zilizopatikana tumekubaliana zitumike kumsafirisha mtoto huyo kwenda hospitali ya Nyangao, kazi iliyofanywa na Bw Victor. Mtoto amelazwa katika hospitali ya Nyangao wodi namba 3 kitanda namba 2.




NSSF yaiumbua Serikali

Na Betty Kangonga

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limedai kuwa serikali imeshindwa kulipa kiasi cha sh. bilioni 14 ilizokopa kujenha Chuo Kikuu cha Dodoma, hivyo kushusha mapato yake.

Akizungumza jana katika kikao cha kamati ya kudumu ya bunge ya maendeleo ya jamii,wakati wakiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi kwa mwaka 2011 na 2012 pamoja na malengo ya mwaka 2012 na 2013, Mkurugenzi wa mipango, uwekezaji na miradi wa shirika hilo, Yacoub Kidula,alisema kuwa  hadi sasa serikali haijalipa hata senti katika mradi huo.

Alisema kuwa mradi huo uligharimu kiasi cha sh bilioni 35 na serikali ilipaswa kulipa fedha hizo kwa awamu katika kipindi cha miaka 10 lakini hadi sasa hakuna fedha iliyolipwa.

Alisema walitakiwa kujenga mabweni elfu 5000 kwa awamu tatu na  kukabidhi mwaka 2009 lakini serikali ilipunguza muda na kuwataka wakabidhi mwaka 2008.

Alisema hatua hiyo ilihitaji kupata kibali kutoka serikalini pamoja na kuingia mkataba ili kuweza kumtaarifu mkandarasi hatua ambayo ilishindwa kutekelezwa kwa wakati na serikali.

“Tumeshalifikisha suala hilo kwa mwanasheria mkuu wa serikali na amepitia nyaraka zote za mradi na amewaandikia wizara ya fedha na uchumi ili haweze kutoa msimamo wake juu ya suala hilo,” alisema.
Kidula
Mwisho





CAG na Kamati

MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, sasa amezipa meno zaidi Kamati za Bunge, ambapo kwa sasa zitakuwa na wajibu wa kufuatilia miradi mahali ilipo ili kufahamu utekelezaji wake.

Wakati CAG, akiwapa mamlaka hayo, Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), Deo Filikunjombe, amesema wamejipanga na mambo waliyoanza bungeni hawatayaacha.

Filikunjombe  pia, serikali ikae macho na iwajibike katika matumizi ya fedha.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, CAG, alisema Kamati zitakuwa na mamlaka ya kufichua ubadhirifu wa mali na fedha za umma kwenye taasisi za Halmashauri.

Alisema Kamati hizo zitafuatiliana miradi mbalimbali mahali ilipo kwa lengo la kufahamu utekelezaji wake.

“Bajeti ya serikali ya 2012/2013 inakaribiwa, mimi ushauri wangu tu kwa hizi Kamati hasa za Kamati za Fedha na Uchumi, ni ukweli kwamba bajeti ya serikali kwa miaka iliyopita kidogo imekuwa haiendi vizuri kwa sababu makusanyo ya pesa yamekuwa hayatoshelezi mahitaji, kwa hiyo tuachane kuangalia kimazoea, tuangalie je serikali inawezaje kuongeza mapato yake vinginevyo, kwani matumizi yake ni makubwa mno” alisema

Akichangia hoja hiyo, Spika wa Bunge Anne Makinda alisema mabadiliko hayo kwa Kamati yanawapa fursa kufuatilia zaidi utekezaji wa miradi kwa ukaribu.

Alisema ni mabadiliko makubwa katika Ukaguzi ambapo zitafanyakazi na taasisi za serikali na Halmashauri.

Aliongeza kwamba kwa utaratibu huo mpya, Kamati hizo zitafuatilia namna ya miradi ilivyotumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekezaji.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo alisema hawataangalia kama hesabu zimeenda sawasawa bali watafuatilia.

Alisema lengo ni kufahamu kama thamani iliyotolewa inaendana na hali halisi ya mradi husika.

Aliongeza kwamba ni jambo zuri hata nchi nginyine za Ulimwengu zinatumia njia hiyo, ambapo nchi kama Uingereza wanatengeza ripoti nzuri ya fedha kupitia mfumo huo.

Katika mkutano huo, ulihudhuriwa na wajumbe wa Kamati hizo pamoja na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Mwisho






Samaki hatarini kutoweka Ziwa Victoria
* Sangara aleta kilio, umasikini kwa wavuvi
* Mkuu wa wilaya Muleba ataka ziwa lifungwe
Charles Misango, Bukoba
SAMAKI katika Ziwa Victoria wako katika hatari ya kutoweka miaka michache ijayo ikiwa juhudi za makusudi za kunusuru viumbe hao hazitachukuliwa.
Uchunguzi wa Tanzania Daima uliofanywa katika visiwa kadhaa na fukwe za ziwa hilo katika wilaya za Bukoba mjini na Muleba, umebaini kuwa zaidi ya asilimia themanini ya aina mbalimbali ya samaki wa asili waliokuwa wakivuliwa kwa wingi kwa karne nyingi wametoweka na wachache waliobaki wanapatikana kwa nadra.
Wavuvi wengi waliohojiwa na Tanzania Daima katika visiwa vya Bumbile na Kerebe pamoja na kijiji cha Rwazi, wilaya ya Muleba mkoani Kagera walisema samaki aina ya Sato (tilapia), Gogogo na wadogo wanaojulikana kama fulu ndio wanaopatikana kwa kiwango kidogo.
Mujili Hamza ambaye ni kiongozi wa wavuvi katika Kijiji cha Mahiga, Kisiwani Bumbile alisema kuwa hali ya upatikanaji wa samaki katika ziwa hilo ni mbaya kwa vile hata sangara waliopatikana kwa wingi na wakiwa wakubwa mwanzoni mwa miaka ya 80 wamepungua na hivyo wavuvi wengi wameanza kuingiwa na wasiwasi wa kutoweka samaki katika ziwa hilo kubwa.
Mvuvi  Filemon Nyagawa (30) wa Rwazi alisema kuwa upungufu wa samaki umesababisha wavuvi wengi kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
“Miaka ya nyuma tulipata samaki wengi, na wanunuzi walikuwa wanakuja kununua hadi tunafikisha sh 40,000 hadi 100,000 kwa siku kama samaki wamekubali. Lakini sasa baada ya kuja hawa wavuvi wakubwa, samaki wamekuwa adimu na hali ya mapato ni mbaya kwani unaweza kurudi toka ziwani na samaki wawili ambao ukiwauza unaambulia sh 6,000 tu” alisema Nyagawa.
Katibu wa BMU katika kisiwa cha Kerebe, Kileo Lukabura’s alionesha hofu ya kutoweka kwa samaki, akidai kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wavuvi wenye zana kubwa na za kisasa.
Alisema miaka mitano ya nyuma, kisiwa hicho kilikuwa na wavuvi wanaomiliki boti za injini na mitumbwi ya kawaida kati ya 30 hadi 40 kwa siku lakini sasa wanafika 100 hadi 200 kila siku jambo linaonyesha samaki anavyowindwa.
Aliongeza kuwa miaka hiyo wavuvi wakubwa waliweza kuvua wastani wa tani mbili hadi tau kwa wiki, lakini kwa sasa huwachukua hadi mwezi mmoja kupata kiasi hicho cha samaki.
Alisema nyakati hizo wavuvi wadogo waliweza kupata kati ya samaki 100 na 200 kwa siku lakini hivi sasa hali imekuwa mbaya ambapo kwa sasa wanaambulia kati ya samaki watano hadi kumi, na wakati mwingine hawapati kitu.
“Hivi sasa mitumbwi mingi inafika mwaloni ikiwa na samaki 10 tofauti na zamani, mtumbwi mmoja uliweza kuvua samaki wengi mno lakini hivi sasa ni ndoto” alisema.
Uchunguzi wa Tanzania Daima, umebaini kuwa kupungua kwa samaki katika ziwa hilo, kumechangiwa  na sababu nyingi zikiwemo uvuvi haramu wa kutumia kemikali, nyavu zilizopigwa marufuku, chumvi na kubwa zaidi kupandwa kwa samaki aina ya sangara miaka kadhaa iliyopita.
Diwani wa Kata ya Bumbile Sweetbert Mtembei (62), alikiri kuwa ujio wa sangara katika ziwa hilo, ingawa awali ulionekana kuleta neema kubwa kwa wavuvi, sasa umegeuka kuwa balaa baada ya samaki hao kuwashambulia na kuwamaliza samaki wa asili.
“Hali kwa kweli ni mbaya kuliko watu wanavyodhani. Ukiacha wale wachache kama sato, ngenge na fulu, samaki wengine wote wametoweka kabisa kwa sababu wanaliwa kwa wingi na sangara” alisema diwani huyo.
Alikiri kuwa ingawa kuingia kwa sangara kulileta neema na utajiri kwa baadhi ya watu katika miaka ya mwanzo, sasa samaki hao wamekuwa balaa kubwa kwa kuwa wameteketeza waliokuwepo tangu awali.
“Sangara walipoingia wakati huo wakiitwa mbuta, kutokana na ukubwa wao ambapo mmoja aliweza kufikia kilo 150 hadi 200, waliwashambulia kwa kasi samaki wa asili kama chakula chao”
 “Wakati huo, hata uvuvi wa sangara haukuwa wa kisasa kama ilivyo sasa. Tulikuwa tukiwakamata kwa wingi hasa wanapoibuka na kuelea juu ya maji kwa sababu ya joto” alisema diwani huyo.
Katika kijiji cha Rwazi, Kata ya Kagoma wilaya ya Muleba, wavuvi wamekiri kuwa pamoja na kutoweka kwa samaki wa asili kwa zaidi ya miaka kumi sasa, hata wale aina ya sangara wamepungua kwa kisi kikubwa kutokana na sababu nyingi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Rwazi, Faustine Lubingo alisema kuwa moja ya sababu za kupungua kwa samaki katika ziwa hilo, ni vitendo vya baadhi ya wavuvi wakubwa kutengeneza nyavu za bandia zinazojulikana kama “Double six” ambazo ni hatari kwa vile zinazoa samaki wengi bila kujali ukubwa wake.
“Hizo nyavu ni sawa na zile tunazonunua wavuvi wadogo, lakini baadhi ya wavuvi wakubwa wanaunga vipande vya nyavu hadi kufikia sita na kuzizamisha katika kina kirefu cha maji, kiasi kwamba samaki atakayepita katika eneo hilo atanaswa tu” alisema Lubingo.
Mwenyekiti huyo alisema uongozi wa juu wa serikali unalifahamu jambo hilo, lakini baadhi ya wahusika wanashindwa kuchukua hatua kali dhidi ya wavuvi wakubwa kwa madai kuwa ndio walipa kodi wakubwa, na hivyo kuwaacha waendelee na uharibifu huo.
Hata hivyo, Kaimu Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Muleba, Ignatus Rwiza alikanusha madai ya kuwalinda wavuvi wakubwa, na kwamba wamekuwa wakifanya ukaguzi wa nyavu wa mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuangalia namna wanavyoendesha shughuli zao.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Utawala wa Mkoa wa Kagera (RAS) Juma Mokiri ambaye ni mshauri wa afisa huyo alikiri hatari ya kutoweka kwa samaki katika ziwa hilo.
Mokiri alidai kuwa hali hiyo imesababishwa na mambo mengi ikiwemo uvuvi haramu unaofanywa na makundi karibu yote ya wafugaji, uendeshaji shughuli za kijamii kama ufugaji, kilimo na nyinginezo.
Kwa mujibu wa afisa huyo, kiwango cha samaki wanaovuliwa kwa mwaka kimeshuka kutoka tani 41,000 hadi kufikia 27,000
Aliongeza kuwa baadhi ya wafugaji wamejiingiza katika uvuvi haramu ambao wanatumia sumu na nyavu zisizokubalika zinazovua hata samaki wadogo na wakati mwingine katika mzalia ya samaki.
Katika kukabiliana na uvuvi haramu, afisa huyo alidai kuwa kumekuwa na doria mbalimbali zilizosababisha kukamatwa kwa wavuvi haramu 324, yakiwemo mkokoro 317, timba 469, makila 6,089, nyavu za dagaa 146, katuli 6, ambavyo vyote vilikuwa na thamani ya Tshs. 611,395,000/=.
Lakini Mwenyekiti wa kikundi kinachosimamia Rasilimali Uvuvi Mwaloni katika Kata ya Bumbiile (BMU) Ramadhan Abubakar alikosoa operesheni za kukamata wavuvi haramu akisema zinaendeshwa kwa upendeleo, ambapo ni  wavuvi wadogo tu ndio wanaokumbana na mkono wa sheria wanapobainika kujihusisha na uvuvi haramu na uchafuzi wa mazingira kwa kutozwa faini na onyo kali, lakini wale wakubwa hawaguswi.
Akizungumzia  hatari hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Angelina Mabula alikiri kuwepo kwa tishio hilo na akaenda mbali zaidi akitaka shughuli zote za uvuvi katika ziwa Victoria zifungwe kwa muda.
Aliongeza kuwa kwa hali ilivyo kwa sasa, hakuna namna yoyote ya kufanya kunusuru samaki waliobaki zaidi ya kusitisha shughuli za uvuvi kwa muda fulani.
“Ni vema uvuvi ufungwe kwa muda na kuwepo uvuvi wa misimu, yaani ‘seasonal fishing’, ili kusaidia kuwepo na muda wa kuzaliana kwa samaki wengi.




Malawi kubariki ushoga

LILONGWE, Malawi
RAIS wa Malawi Joyce Banda amesema kuwa, nchi hiyo itabadili sheria inayopinga mapenzi ya jinsia moja, hivyo kuruhusu ndoa ya jinsi moja.

Banda alitoa kauli hiyo wakati akilihutubia taifa kwa mara ya kwanza jana tangu atawazwe kuwa rais wa nchi hiyo.

Mageuzi hayo yataifanya Malawi kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kubariki watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja tangu mwaka 1994.

Viongozi kadhaa wa nchi za Magharibi hivi karibuni walisema kuwa wataziondolea misaada nchi ambazo hazitambui haki za mashoga na wasagaji.

Kauli ya Rais Banda ambaye ameingia madarakani mwezi uliopita imekuja baada ya wanaume wawili wa Malawi kuhukumiwa kifungo cha miaka 14 jela mwaka 2010 baada ya kusema kuwa walikuwa wakifunga ndoa.

Baada ya kimbunga cha shutuma kutoka kwa mataifa makubwa, Mutharika aliwasamehe wanaume hao kwa sababu ya mazingira ya kibinadamu lakini alikaririwa akisema kuwa;  “wanaume hao walikiri kuwa wamefanya uhalifu dhidi ya tamaduni zetu, dhidi ya dini zetu na sheria zetu ".


Rais Banda alichukua madaraka mwezi uliopita baada ya mtangulizi wake, Bingu wa Mutharika kufariki dunia kwa shambulio la moyo.

Tangu atawazwe kuwa Rais wa nchi hiyo, Rais Banda amefanya mabadiliko ya sera kadhaa za mtangulizi wake, ikiwa ni pamoja na kushusha thamani ya sarafu ya nchi hiyo ikiwa ni moja kati ya matakwa muhimu ya Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Hata hivyo katika nchi nyingi za Kiafrika mapenzi ya jinsia moja hayaruhusiwi na ni kosa kisheria kujihusisha nayo.

Nchini Uganda, Mbunge mmoja aliwasilisha Muswada ambao unataka watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wapewe adhabu ya kifo.

Hata hivyo baada ya mataifa makubwa kuingilia kati na kukosoa kauli hiyo na hata kutishia kusitisha misaada yake, baadae Mbunge huyo alibadili muswada wake na kutaka wafungwe kifungo cha maisha jela

No comments:

Post a Comment