Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

Pinda abanwa, kuvunja uongozi Misungwi

Na Sitta Tumma, Magu.

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, juzi alibanwa kwa maswali magumu na kutoa majibu ya sababu zinazoifanya Serikali yake kushindwa kuboresha hudum muhimu za kijamii, ikiwemo sekta ya afya, maji na barabara, jambo ambalo linadidimiza ukuaji wa maendeleo ya Watanzania.

Pinda amekumbana na hali hiyo juzi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya sabasaba mjini Magu, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo.

Baadhi ya wananchi walimweleza waziwazi Pinda juu ya kukithiri kwa ubovu wa huduma za kibinadamu, na hasa tatizo kubwa la ukosefu wa dawa hospitalini, licha ya kulipia fedha, hivyo wanaona kama serikali imewatelekeza wananchi wake.
  
"Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa nini serikali mmeshindwa kuiwekea lami barabara hii ya kwenda hospitali ya wilaya ya Magu?. Huduma zenyewe za afya ni mbovu, tunakosa hata dawa ya panaldo kwa nini lakini?

"Nina hasira sana mheshimiwa usinione hivi. Sasa tunaomba utuambie leo hapa" alisema mkazi mmoja wa wilaya hiyo ya Magu, kisha kushangiliwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika mkutanoni hapo.

Hali hiyo ilimkumba pia Waziri Mkuu Pinda, alipokuwa wilayani Ukerewe Jumatano wiki iliyopita baada ya wananchi kumtaka awaeleze sababu ya serikali kugawa umeme kwa upendeleo katika baadhi ya maeneo wilayani humo.

Akijibu maswali ya wananchi wilayani Magu, Pinda alisema Serikali haiwezi kuhangaika na uwekaji barabara lami huku wananchi wengi wakikosa huduma ya maji safi ya kunywa.

"Punguza jazba mama unisikilize na mimi. Mikakati ya serikali imeelekezwa kutatua kwanza adha kubwa ya maji hapa Magu. Ni afadhali fedha za kuweka lami kipande cha barabara ya kwenda hospitali ya wilaya tukazitumia kununulia dawa".

Kuhusu uhaba wa dawa za binadamu hospitalini, Pinda alisema tatizo hilo ni la kitaifa, na kwamba serikali imeweka mipango mikakati yake katika suala zima la kutatua adha hiyo ya maji, kwani ni asilimia 17 tu ya wakazi wa wilaya ya Magu ndiyo wanapata huduma ya maji safi na salama ya kunywa.
  
"Wewe mama sikiliza, hospitali utakwenda tu hata kama barabara ni mbovu. Lakini acha kwanza tuboreshe huduma hii ya maji, au mnasemaje wana Magu?", alisema Pinda huku baadhi ya wananchi wakisikika wakisema: "Kauli hiyo ni funika kikombe mwanaharamu apite".

Kuvunja uongozi Misungwi

Katika hatua nyingine, Pinda, alilazimika kutangaza kuivunja Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ndani ya siku chache zijazo, kutokana na kile kinachodaiwa kukithiri kwa vitendo vya kifisadi  vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo.

Mbali na nia hiyo pia aliiagiza Taaisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), mkoani Mwanza ihakikishe inaanza mara moja kuandaa mashtaka, na kuwapeleka mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi katika halmashauri hiyo yenye madiwani 36 wote kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kubanwa kwa maswali mazito kutoka kwa wananchi kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika mjini Misungwi. Wananchi wa wilaya hiyo wakionekana kuwa na hasira walimtaka Pinda awaeleze hatima ya halmashauri hiyo na tuhuma nzito za ufisadi zinazomkabili mwenyekiti wa halmashauri hiyo pamoja na baadhi ya vigogo wanaotuhumiwa kutafuna mabilioni ya fedha za miradi ya maendeleo.

Wananchi hao ambao walidiriki kumzoea mwenyekiti wa halmashauri hiyo alipoitwa kuwasalimia, walimtaka Waziri Mkuu kuchukua hatua za haraka kunusuru mali za umma zinazodaiwa kutafunwa na watumishi hao

Tuhuma hizo, ziliwahi kumfanya Waziri Mkuu Pinda kuagiza aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Exavieri Tilweselekwa, ashushwe cheo na ashitakiwe mahakamani kwa tuhuma hizo nzito.

Akizungumzia tuhuma hizo, Pinda aliyeonekana kukasirishwa na tuhuma hizo, alisema halmashauri hiyo imeelemewa na mchwa mkali unaotafuna fedha za maendeleo, kwani mwaka 2009/2010 ilipata hati yenye mashaka, na mwaka wa fedha 2010/2011 halmashauri hiyo chini ya mwenyekiti wake, Polcarp ilipata hati chafu, jambo linalothibitisha kuwepo kwa ulaji mkubwa wa fedha unaofanywa na baadhi ya vigogo wa halmashauri hiyo.

Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, pamoja na ripoti ya Tume ya ukaguzi maalumu zimeonesha wazi kuwepo kwa upotevu mkubwa wa fedha za maendeleo wilayani humo, na kwamba madai ya mwenyekiti huyo wa halmashauri kuwa Mbunge wa Misungwi na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga kuingilia ukaguzi huo, hayana ukweli wowote, kwani vyombo hivyo ni vikubwa na vina heshima yake kubwa ndani na nje ya nchi.

"Ripoti ya CAG na ile ya tume maalumu zinatueleza ukweli wa tatizo hapa Misungwi lipo wapi. Mwenyekiti wenu huyu amekuwa akifanyabiashara na halmashauri yake kupitia kampuni yake ya ujenzi. Kimaadili, kiuongozi na kisiasa ni jambo lisilokubalika hata kidogo.

"Kiongozi mzuri na makini huwezi kufanya hivyo, maana lazima italeta mgongano tu wa kimaslahi. Ni dhahiri hapa Misungwi hakuna kinachofanyika katika kusimamia maendeleo ya wananchi. Nataka TAKUKURU ifanye kazi yake tena kwa haraka sana. Na wahusika wote wa ufisadi huu wapelekwe mahakamani".

"Swali la kujiuliza hapa. Kwa nini mwenyekiti ufanyebiashara na halmashauri?. Kama una kampuni yako kwa nini usingetafuta mtu ukamuweka akawa ndiye mwenye kampuni badala ya wewe mwenyewe?.  Je ukijipatia tenda ya ujenzi utajisimamiaje, na nani atakuwajibisha?", alihoji kwa jazba Waziri Mkuu Pinda, wakati akijibu swali la Victor Thomas aliyesema mwenyekiti huyo hahitajiki tena kuiongoza halmashauri hiyo.

Alisema, kulingana na uwepo wa tuhuma hizo dhidi ya mwenyekiti huyo, yeye (Pinda), alimshauri zaidi ya mara mbili juzi kwenye kikao cha ndani na madiwani wote wa halmashauri hiyo ajiuzulu nafasi hiyo, lakini alikataa ushauri wa Waziri Mkuu ambaye ndiye mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa nchini (TAMISEMI).

”Juzi (majuzi), Polcarp alinifuata kuja kuongea na mimi. Lakini nilimshauri ajiuzulu nafasi yake akakataa. Aliniambia Misungwi hakuna tatizo (wananchi wakazomea). Akaniambia kwamba anayesababisha yeye achukiwe na wananchi ni mbunge (Kitwanga)” alisema Pinda mbele ya wananchi.

"Mwnyekiti huyu amekataa ushauri wangu wa kumtaka ajiuzulu. Mimi ndiye Boss wake na ndiye mwenye kauli ya mwisho. Ngoja nirejee Dar es Salaam na ndani ya muda mchache kisheria nitaivunja halmashauri hii ya Misungwi.

"Maamuzi haya ni mazito maana hapa Misungwi hamtakuwa na madiwani hadi mwaka 2015, na hatua kali za kisheria lazima zichukuliwe kwa wahusika wote", alisema Waziri Mkuu, huku wananchi wengi wakishangilia na kumtaka aivunje halmashauri hiyo papo hapo, kwa madai wamechoshwa na ufisadi.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment