Mnyika
amshukia JK
Na Efracia
Massawe
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amemjia juu Rais
Jakaya Kikwete akimtaka atoe maelezo ya utekelezaji wa ahadi zake wakati wa
kampeni za mwaka 2010 kuhusiana na mambo mbalimbali, likiwemo suala la ajira
milioni moja kwa Watanzania.
Mnyika pia amemtaka Rais Kikwete awaambie wakazi wa Ubungo
kuhusiana na viwanda kadhaa vilivyo ndani ya jimbo lake, ambavyo vingekuwa
chachu ya maendeleo ya wananchi, lakini vimefungwa.
Mbunge huyo alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika
ziara yake ya kuzindua ofisi, pamoja na kuweka mawe ya misingi katika kata ya
Mabibo ambapo alieleza kushangazwa kwake na kutotekelezwa kwa ahadi hewa
zilizotolewa na kiongozi huyo wakati wa uchaguzi mkuu uliyopita.
Mnyika alivitaja baadhi ya viwanda hivyo
vilivyobinafsishwa kuwa ni Ubungo
Garments, Spinning Mill, Polysack Lmt, Tanzania Sewing Thread, Coastal Diaries,
pamoja na kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI).
“Tunamshinikiza Kikwete kama kiongozi wa nchi pamoja na
Baraza la Mawaziri kurejesha viwanda vilivyobinafsishwa kiholela katika jimbo
la Ubungo ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira linalowakabili
Watanzania,” alisema Mnyika.
Katika hilo, alimtaka mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni
Rais kutoa kauli ya matokeo ya maafikiano ya pamoja waliyoafikiana na mawaziri
juu ya ajira hizo ili kuondoa utata uliopo baina ya wananchi na viongozi wao wa
kada husika.
Alitanabaisha kuwa ili kukabiliana na tatizo la ajira katika
jimbo hilo, manispaa ya Kinondoni imetenga fedha zaidi ya sh milioni 200 kwa
ajili ya mikopo kwa vikundi vya kinamama pamoja na vijana.
Alitumia fursa hiyo kuitaka manispaa hiyo kutoa kipaumbile
katika suala la ajira hasa kwa kuwafikia walengwa badala ya kuishia mikononi
mwa wachache.
“Nawataka na ninyi wananchi mliojiunga katika vikundi
mbalimbali vya kukopeshwa kufuatilia kwa makini fedha hizo ngazi husika, ila
mkikwama tafadhali rudini kwangu kwa ripoti maalumu ili nifuatilie suala hilo
ambalo ni muhimu kwetu,” alisema mbunge huyo.
Rais Kikwete ndiye mgombea aliyeongoza kwa kutoa ahadi
nyingi wakati wa kampeni za uchaguzi kuliko wagombea wengine wa nafasi ya urais
kutoka vyama hasa vya Chadema na CUF.
Mwisho
No comments:
Post a Comment