HATIMAYE Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na
Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Dk. Kitila Mkumbo waliovuliwa uongozi ndani ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamevunja ukimya.
Katika mkutano wao na wahariri na waandishi wa vyombo
mbalimbali vya habari, Zitto ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, ameapa
kuwa hayuko tayari kuondoka ndani ya chama hicho na atakuwa mtu mwisho
kuondoka.
Wakati Zitto akiapa kwamba hayuko tayari kuondoka
CHADEMA, Dk. Mkumbo ambaye amekuwa mshauri mkuu wa chama hicho maarufu nchini,
amesema kuwa kile kinachoitwa uhaini ndani ya CHADEMA ni wasiwasi wa siasa za
ushindani kwa watu wasiotaka mabadiliko.
“Wengi walifikiri nikija hapa leo nitajibu mapigo na
kutoa uamuzi mgumu. Mimi sitoki CHADEMA, wanaotaka nitoke, wanitoe wao, na hiki
kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia dhidi ya
wahafidhina, ni mapambano ya wanaopenda siasa safi dhidi ya wale wanaotukuza
siasa za maji taka,” alisema Zitto.
Akieleza sababu za kutokujitoa CHADEMA, Zitto alisema
zaidi ya nusu ya maisha yake yamekuwa CHADEMA, kwani alijiunga tangu alipokuwa
na miaka 16 hadi sasa ana miaka 37, na amekabiliana na vitisho mbalimbali dhidi
ya wasiotaka mageuzi.
“Nataka niwaeleze wanachama wa CHADEMA kwamba mimi
sitokuwa sababu ya CHADEMA kuvunjika, kimenilea na kunifikisha hapa na
ningependa na mwanangu siku moja awe mwanachama wa CHADEMA, na huu unaoitwa
usaliti kwangu dhidi ya CHADEMA ni sawa na mimi kujikata mguu wangu, sitoweza
kufanya hivyo,” alisema Zitto.
Mbunge huyo ambaye amepata umaarufu mkubwa tangu
alipoingia bungeni, alieleza kuumizwa na shutuma nyingi ambazo zimekuwa
zikielekezwa kwake kwa muda mrefu.
Alisema amekuwa akiItwa msaliti, mnafiki, mla rushwa
akihongwa kwa ajili ya kukisaliti chama.
“Naomba wanachama wanielewe, nimejiunga na chama hiki
nikiwa na miaka 16, ninaposingiziwa, naumia sana, nimefanya kazi ya kuchomeka
milingoti ya bendera za chama kwa viongozi wanaofika katika kijiji chetu,
ninapozushiwa naumia, nimefanya kazi zangu za kibunge kwa weledi mkubwa kwa nia
ya kukitumikia na kukipandisha chama changu, ninaambiwa ninakihujumu, inaniuma
sana,” alisema.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema akiwa mwanasiasa kijana na
binadamu, anaamini ana makosa kwa kuwa hakuna binadamu aliye mkamilifu, na
kwamba upungufu wake unapaswa kupimwa na mema aliyoyafanya.
Ataja tuhuma zake
Akizungumzia tuhuma zilizomfanya apokwe nyadhifa zake
zote na kubaki kuwa mwanachama, Zitto alisema kuna upotoshaji mkubwa wa taarifa
kwani tuhuma alizoambiwa ndani ya Kamati Kuu ni tofauti na zilizotolewa kwa
waandishi wa habari.
Alisema tuhuma zote zimekuwa katika taswira mbili
zinazomuonyesha kuwa ni mbinafsi na mtu anayetumiwa kukisaliti chama kwa
kupokea rushwa kwa ajili ya kufanya hujuma.
Alisema anadaiwa kutoshiriki katika kampeni za mgombea
urais mwaka 2010 tuhuma ambazo alidai zimekuwa zikijirudia kila wakati.
Akitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, Zitto alisema kuwa
yeye ndiye kiongozi na mgombea ubunge pekee mwaka 2010 aliyezunguka majimbo 16
kumfanyia kampeni mgombea wa urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa na Mkoa wa
Kigoma uliongoza kwa kutoa kura nyingi za urais kuliko mingine kwa kupata
asilimia 46.
Kwa mujibu wa Zitto, tuhuma nyingine iliyoelekezwa
kwake ni madai kuwa alishiriki kuwashawishi baadhi ya wagombea katika baadhi ya
majimbo wajitoe katika uchaguzi ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila
kupingwa.
Akijibu hilo, Zitto alisema hakuna ushahidi wowote
unaoonyesha hali hiyo, na kwamba aliomba uchunguzi ufanyike kubaini ukweli.
Mbunge huyo alisema pamoja na tuhuma zote, kuna tuhuma
kubwa ya kudaiwa kukidhalilisha chama chake kwa kutoa tamko kwamba hesabu za
chama hicho, hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) na kwamba chama chake kilimtaka awafahamishe mapema ili wajiandae.
“Kwamba ‘kutowatonya’ kwangu ndio nimekidhalilisha
chama na kukiweka kundi moja na CCM, na kwamba nastahili kuadhibiwa kwani
katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu
niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama
ifuatavyo. Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC
kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia
zilezile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha.
“Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho
kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua
kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa
utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama
vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa
hili ni la nani,” alisema Zitto.
Akizungumzia usaliti, alisema kuwa tangu alipoacha
kuchukua posho mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama
chake wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za
umma, alianza kuitwa msaliti.
Alisema suala la kukataa posho za vikao limo ndani ya
Ilani ya CHADEMA na kwa upande wake kama waziri kivuli wa fedha alikuwa na
wajibu wa kutekeleza jambo hilo kwa vitendo na sio kama alivyotuhumiwa na
Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, kwamba anachukua fedha nyingi sehemu
tofauti.
Kuhusu ripoti ya siri iliyosambazwa katika mitandao ya
kijamii, kwamba amehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama chake, alisema kuwa
viongozi wenzake walikana kuuandaa na kuusambaza.
Alisema hoja iliyopo ni kuwa waraka huo umesambazwa na
watu wa usalama kwa kushirikiana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kwa vile chama kimekana kuhusika, tayari
anakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaohusika iwe ndani au
nje ya chama hicho.
Waraka wa mabadiliko ya uongozi
Akizungumzia waraka wa siri unaoeleza mkakati wa
mabadiliko ya uongozi CHADEMA ulionaswa na kusambazwa kwenye mitandao ya
kijamii, Zitto alisema hajawahi kuuona wala kuusoma na kwa mara ya kwanza
aliusikia kwenye kikao cha Kamati Kuu.
Alipobanwa kueleza kama anakubaliana na mapendekezo ya
waraka huo wa kumtaka agombee uenyekiti wa CHADEMA taifa wakati ukifika, Zitto
alisema kwa bahati mbaya alichelewa kuuona na kama angeupata mapema,
angeyafanyia kazi mapendekezo yake.
“Changamoto hizi tunazopitia zimewahi kupitiwa na
wanasiasa mahiri duniani kama vile akina Mahadhir Mohammed aliyefukuzwa na
baadaye akawa waziri mkuu, Mahindra Gandhi alifukuzwa akiwa waziri mkuu wa nchi
aliondolewa na kwenye uongozi wa chama chake, Zuma, na watu walijua alikwisha
kabisa, lakini matokeo sasa ndiye Rais wa Afrika Kusini, haya ni lazima kupitia
katika kuhakikisha tunajenga demokrasia imara, siasa safi na uongozi bora
katika nchi yetu,” alisema Zitto.
Kuhusu siku 14 alizopewa na Kamati Kuu kwa ajili ya
kutoa utetezi, Zitto alisema hadi sasa hajapata barua ya mashitaka yake na kwa
hali hiyo hajui anatoa utetezi gani.
Dk. Mkumbo amsafisha Zitto na waraka
Kwa upande wake Dk. Mkumbo ambaye alikuwa wa kwanza
kuzungumza, alisema alikiri kuuandaa waraka huo kwa kushirikiana na Mwenyekiti
wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Alisema waraka huo uliandaliwa kwa siri bila
kumshirikisha Zitto, na kwamba hajui lolote kwani walipanga kumpelekea endapo
chama kingetangaza tarehe ya uchaguzi.
“Ule waraka ulikuwa wa siri, unaelezea mikakati ya
kuweka mgombea tuliyeamini kwamba ana sifa za kushika nafasi hiyo, baada ya
kukamilisha tungeenda kwake kumwomba agombee, na tungemwonyesha waraka huo
ambao unaainisha udhaifu na uwezo wake wa kuwa kiongozi, na hili ni jambo la
kawaida na sio la uhaini maana tungetumia boksi la kura kumpata kiongozi,”
alisema Dk. Mkumbo.
Katika waraka huo, Zitto alipewa jina la MM, M1
(Mkumbo), M2 ambaye hajulikani hadi sasa na M3 Samson Mwigamba.
Dk. Mkumbo Aliongeza kuwa hata kukiri kwake kwamba
anaujua waraka huo kulikuwa na lengo la kuamini mawazo yake katika kupata
viongozi ndani ya CHADEMA, aliyoeleza kuwa baadhi ya wajumbe waliutafsiri kuwa
ni uhaini.
“Mimi ni miongoni mwa watu ninaoamini kuwa kuna haja
ya kubadilisha uongozi wa juu wa chama, na kwa kuwa tulitambua uchaguzi huu
ungefanyika kabla ya mwaka huu kuisha, tuliandaa sifa za mtu tuliyemuona
anaweza kupokea kijiti na hili hata kwa hao wanaotafsiri ni uhaini limefanyika,
sema kwa upande wao waliamua kuweka mkakati wao katika mitandao ya kijamii,”
alisema Dk. Mkumbo.
Alisema kuwa hawezi kufanya uhaini wala kukihujumu
chama kwani amepewa nafasi nyingi kubwa na kamwe hakuzitumia kukihujumu.
Akitolea mfano, Dk. Mkumbo alisema kuwa yeye ndiye
aliyeandaa Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA katika uchaguzi uliopita, amemaliza
mgogoro wa kupata viti maalumu ndani ya chama nafasi ambazo angeweza kuzitumia
kukihujumu chama.
“Chama kiliniamini na kunipa nafasi nyingi nyeti, na
kama ningekuwa mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo,
nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010
nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa Baregu, na nilishiriki
kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata wabunge wa viti maalumu
katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti mno ambazo kamwe huwezi
kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’,” alisema.
Alisema kuwa hata sababu ya kutaka kujiuzulu haikuwa
kuogopa aibu ya kufukuzwa, bali ni baada ya kubaini wenzake katika Kamati Kuu
hawakuwa na imani naye.
No comments:
Post a Comment