Na Mwandishi Wetu
WAKATI taasisi ya Kijerumani ikitoa ripoti iliyoainisha
‘madudu’ mengi yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania, Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kimeanika matukio yote mabaya yaliyofanywa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kikitumia kikundi cha vijana wake wa Green Guard.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa Chadema, John Mnyika, amekitaja kikundi cha Green Guard kuwa cha
hatari kutokana na kuhusika na matukio mengi ya kigaidi.
Mnyika amesema matukio hayo yana baraka zote za CCM na
serikali kutokana na ukweli kwamba kikundi hicho hakiguswi wala kuchukuliwa
hatua na vyombo vya dola, pamoja na kuhusishwa kwa ushahidi mwingi na matukio
mengi.
“Hawa wameshiriki matendo mabaya ya utekaji, upigaji,
kujeruhi na yapo ya vifo. Lakini kwa sababu kinafanya haya kwa baraka za CCM na
serikali yake, hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya yeyote.
“Tumetoa taarifa nyingi tu na zenye ushahidi wa waziwazi wa
kuhusika kwa kikundi hicho, ambacho sasa kinasimamiwa na Mwigulu Nchemba,
lakini polisi hao hao wanaotusakama leo kwa vile tumeamua kusema ukweli,
hawajachukua hatua zozote dhidi ya yeyote yule,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa Chadema imesema sana kuhusu ukatili huo, lakini katika hali
ya kusikitisha viongozi wa siasa wanaojitokeza kulaani hatua ya chama hicho
kuamua kutoa mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake, wamegeuka mabubu kuikemea
CCM na serikali yake.
Malalamiko hayo ya Chadema yanafanana pia na yale
yaliyotolewa juzi katika ripoti ya Shirika la Konrad Adenauer Stiftung la
Ujerumani linalojihusisha na utafiti wa masuala ya siasa nchini.
Shirika hilo
katika ripoti yake ambayo inadaiwa kusambazwa ndani na nje ya nchi, imeshutumu
vikali matukio hayo, huku ikisukuma lawama kwa vyombo vya dola kwa kushindwa
kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaodaiwa kuhusika na ukatili huo.
Pia shirika hilo
limetahadharisha kuwepo kwa uwezekano mkubwa zaidi wa vitendo vya kikatili kwa
viongozi wa vyama vya upinzani, wanaharakati na wakosoaji wa serikali kadiri
chaguzi zinavyokaribia.
Ripoti hiyo iliyoandikwa na Danja Bergman na Stefan Reith,
iliyotolewa tangu mwezi uliopita, inazungumzia matukio mbalimbali yaliyolikumba
taifa kwa siku za karibuni, yakiwemo ya mabomu yaliyolipuliwa katika mkutano wa
Chadema na Kanisa Katoliki la Olasiti jijini Arusha.
Hata hivyo, wachunguzi hao wana maoni kuwa ongezeko la
matumizi ya mabavu kutoka kwa vyombo vya dola dhidi ya maandamano halali na
ukosoaji, ni dalili tu ya mambo makubwa zaidi yanayoweza kutokea katika kipindi
cha miaka miwili ijayo, ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu
unatarajiwa kufanyika.
Ripoti hiyo pia inasema katika hali hiyo, kwa kadiri ya hali
ilivyo kila aina ya vitisho, udanganyifu na matumizi ya mabavu vitakuwa vikibadilishwa
badilishwa na kutokea katika sura tofauti ikiwemo vurugu ili kupotosha umma,
huku watuhumiwa wakishindwa kutambuliwa, na wale wanaotambuliwa watafichwa au
kutochukuliwa hatua zozote za kisheria na mamlaka husika.
Ripoti hiyo imeenda mbali zaidi na kusema kuwa hata pale
vyombo vya dola vinapohusishwa na mauaji, kwa ushahidi wa wazi, watuhumiwa
wamekuwa wakilindwa na kuendelea kutesa mitaani bila kuchukuliwa hatua zozote
za kisheria, badala yake wahanga wa matukio hayo wamekuwa wakishitakiwa kwa
kesi mbalimbali za kubambikiza, zikiwemo uchochezi, ugaidi na kuhamasisha chuki
kati ya wananchi na serikali yao.
Chadema imeorodhesha matukio yanayodaiwa kutendwa na vijana
wa CCM kama ifuatavyo:
Juni 16 na Julai 14 katika uchaguzi wa kata nne za Arusha
vurugu nyingi ziliripotiwa zikiwahusu wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi kuteka,
kujeruhi na kupewa mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kusimamia shughuli za ulinzi
katika chama hicho kikongwe nchini.
Vijana Chadema watekwa
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Bunda, Joshua Mirumbe, aliyekaimu
nafasi hiyo pia Wilaya ya Serengeti alituhumiwa kuwateka vijana kadhaa wafuasi
wa Chadema akitumia magari STK 8430, T
286 BFB, T 245 BFE, yanayomilikiwa na CCM pamoja na gari T 352 AHD, T 573 BEW
akisaidiwa na askari magereza na kuwapeleka kwenye jengo moja la chama tawala.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mkuu wa wilaya huyo alitaka kuwatumia polisi, lakini Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo alimkatalia, hali iliyomlazimu kwenda kuwachukua askari magereza kwa ajili ya kutekeleza operesheni hiyo iliyodumu usiku kucha kabla ya kuwapeleka vijana hao polisi baada ya kubanwa na Chadema.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mkuu wa wilaya huyo alitaka kuwatumia polisi, lakini Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo alimkatalia, hali iliyomlazimu kwenda kuwachukua askari magereza kwa ajili ya kutekeleza operesheni hiyo iliyodumu usiku kucha kabla ya kuwapeleka vijana hao polisi baada ya kubanwa na Chadema.
Katika Kata ya Iyela, gari la CCM lenye namba T 704 BEU,
likiwa na watu wawili wanaotambulika kwa majina ya Moris na Nosy, waliwateka
vijana wa Chadema ambapo mmoja wao Meshack Bernad alichomwa kisu.
Pikipiki yapigwa moto
Pikipiki ya Chadema ilichomwa moto na vijana wa CCM (Green
Guard) na Katibu wa Chadema wilaya ndugu, Lucas Daniel amepigwa na kuumizwa,
huku mwenyekiti wa jimbo hilo,
Kibam Ally Mohamedi akijeruhiwa na katibu Mwenezi Severine Matanila kukatwa
vidole.
Risasi za moto
Watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), waliwafyatulia risasi za moto viongozi na makada wa Chadema katika
uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi Sengerema wakati wafuasi wa CCM na Chadema
walipokutana kufuatilia hali ya mambo katika vituo vya kupigia kura Kata ya
Nyampulukano.
Katika tukio hilo,
milio ya risasi zaidi ya nne ilisikika kutokea upande wa pili wa CCM, ambapo
magari matatu yalilizunguka gari moja la Chadema Kanda ya Magharibi likiwa na
kiongozi wa Kikosi cha Movement for Change (M4C), Kanda ya Ziwa Magharibi,
Alfonce Mawazo, Hussina Amri na makada kadhaa.
Green Guard waitwa Janjaweed Zanzibar
Kundi hilo lililoasisiwa
mwaka 2005 limewahi kuvitingisha visiwa vya Zanzibar wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005.
Wakati wa kampeni za uchaguzi huo vijana wa kundi hilo
walipelekwa visiwani humo kwa lengo la
kudhibiti nguvu za Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuwapiga na kuwatesa viongozi
na wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo.
Kutokana na vitendo vyake vya vurugu na ghasia za kupiga na
kutesa watu, kundi hilo lilipachikwa jina la
Janjaweed, likilinganishwa na wanamgambo wa Kiarabu waliotekeleza mauaji ya
zaidi ya watu 300,000 huko Darfur, nchini Sudan.
Wabunge wa Chadema wakiona cha moto
Juni 17, mwaka huu, vijana wa Green Guard walimshambulia na
kumuumiza vibaya mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, wakati wa
uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli.
Machi, 2012, wabunge wawili wa Chadema mkoani Mwanza,
Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatory Machemuli wa Ukerewe walivamiwa na
kushambuliwa vikali kwa mapanga na nondo na vijana wa Green Guard wa CCM
wakiongozwa na mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Ahmed Mkilindi.
Shambulio hilo
lilitokea wakati wabunge hao wakiratibu kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa
Kata ya Kirumba, mkoani humo, ambapo Chadema kilishinda.
Wamteka kada
Septemba 28, 2011, Green Guard walimshambulia kada wa
Chadema Odero Odero wakati mwenyekiti huyo akielekea kwenye kampeni za uchaguzi
wa udiwani huko Engototo ambao ulitarajiwa kufanyika Oktoba 2, 2011.
Kada huyo alitekwa na mwenzake aitwae Maganga ambaye
alifanikiwa kutoroka na kwenda kutoa taarifa polisi ambao walianza msako wa
kumtafuta Odero na kumkuta akiwa ametelekezwa katika pori moja huko Engototo akiwa hoi kwa kipigo
huku watekaji wakiwa wameondoka na nyaraka zote alizokuwa nazo.
Wamvunja mbavu mwanachama
Mei 22, 2009, vijana wa Green Guard walimshushia kipigo na
kumvunja mbavu mwanachama wa Chadema katika Jimbo la Busanda, mkoani Geita.
Polisi hawakuchukua hatua zozote dhidi ya kundi hilo la kihalifu.
Washambulia wananchi
Oktoba 25, 2012, vijana wa Green Guard waliwashambulia na
kuwaumiza vibaya wananchi wa Daraja Mbili, mkoani Arusha, baada ya kuonyesha
ishara ya vidole viwili inayotumiwa na Chadema.
Wavamia hoteli
Septemba 24, 2011, vijana wa Green Guard waliokuwa
wakipatiwa mafunzo haramu ya kijeshi na kigaidi katika makambi maalumu mkoani
Singida, walivamia hoteli waliyofikia viongozi wakuu wa Chadema wilayani Igunga
wakiwa na gari aina ya Toyota Landcruiser VX mbili mali ya CCM wakitaka kuchoma moto
magari mawili ya matangazo (PA).
Jaribio hilo
lilishindwa baada ya kudhibitiwa na walinzi wa Chadema na kufanikiwa kuwakamata
na kisha kuwapeleka polisi, lakini katika mazingira ya kushangaza, vijana hao
waliachiwa huru bila kufikishwa mahakamani.
Washambulia mwandishi
Septemba 25, 2011, vijana wa Green Guard walimshambulia kwa
ngumi na mateke mwandishi wa gazeti la Dira ya Mtanzania, Mussa Mkama aliyekwenda katika hoteli waliyofikia
viongozi wa CCM ili kuzungumza na mbunge wa viti maalumu, Ester Bulaya (CCM).
Walimshambuliwa kwa maelekezo ya Mwigulu Nchemba, kutokana
na mwandishi huyo kuandika habari ya kushikwa ugoni kwa kiongozi huyo wa CCM
ambaye katika kampeni za uchaguzi mdogo wilayani Igunga alikuwa meneja wa
kampeni za chama chake.
Mwandishi Tanzania Daima anusurika kuchinjwa
Oktoba 4, 2011, mwandishi wa gazeti hili George Maziku
aliyekuwa wilayani Igunga kuripoti uchaguzi mdogo wa ubunge, alinusurika
kuchinjwa na vijana wa Green Guard wa CCM akifuatilia vurugu zilizofanywa na
vijana hao wakitaka kuwadhuru wafuasi wa Chadema huku wakiwa wamebeba silaha za
jadi, yakiwemo mapanga, visu, nondo, marungu, na majembe.
Maziku alijikuta akiwa amezingirwa na vijana hao ambao
hawakutaka kuandikwa maovu yao,
wakiwa tayari kumtoa uhai.
Aliokolewa na kiongozi mmoja wa CCM aliyekuwa katika hoteli
ya viongozi wa CCM, na kumtoa kwa nguvu kwenye mikono ya Green Guard waliokuwa
tayari kumcharanga mapanga na visu.
Tindikali
Septemba 11, 2011, mmoja wa vijana wa Green Guard alikamatwa
na kiasi kikubwa cha tindikali na polisi. Ndiyo siku aliyomwagiwa tindikali
Mussa Tesha.
Kada wa Chadema auawa
Oktoba, 2011, Green Guard walimteka, wakampiga na kumtesa,
na kisha kumuua kada wa Chadema Mbwana Masudi mkazi wa Dar es Salaam ambaye alipelekwa na chama
chake wilayani Igunga kuwa wakala katika uchaguzi mdogo wa ubunge.
Mashambulizi kituo cha polisi
Kiteto (2007) waliwashambulia wafuasi wa Chadema ndani ya
kituo cha polisi.
Wakata mapanga
Tarime (2008) wanatuhumiwa kuwakata mapanga wanachama wa
Chadema, na wakafanya tena hivyo Busanda na Biharamulo (2009)
Kambi za mafunzo
Kambi ya vijana iliyofanyika Kijiji cha Ughaugha, mwaka
2005, kabla ya Uchaguzi Mkuu, vijana zaidi ya 200 walikaa wiki sita, chini ya
Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Singida Mjini.
Kata ya Unyambwa, katika Shule ya Msingi Ipungi, Kijiji cha
Kisasida, chini ya Katibu wa UVCCM wa
Singida Mjini, Musa Sunja, kijana kutoka Kata ya Mwankoko na walikaa wiki mbili
wakipata mafunzo yaliyoitwa ya ukakamavu.
Kambi iliyoundwa mkoani Mbeya baada ya Mwigulu kufika mkoani
humo, iliyokuwa na vijana 376, katika Shule ya Sekondari ya Ivumwe, Kata ya
Mwakibete, na walifanya vitendo vya utekaji, kauli iliyothibitishwa na Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya.
Kambi nyingine kubwa ni ile ya Ulemo, iliyofanyika kwa ajili
ya kuhusika na fujo katika uchaguzi mdogo wa Igunga na mmoja wa washiriki
amekiri chini ya kiapo mafunzo waliyokuwa wanafanya.
mwisho
No comments:
Post a Comment