JWTZ yakiri kuuawa kwa wanajeshi
*JK awalilia askari wake
Edna Bondo na Shabani Matutu
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
limekiri kuuawa kwa wanajeshi wake saba na wengine 14 kujeruhiwa akiwamo askari
polisi katika shambulio la ghafla lililofanyika Darfur juzi.
Taarifa rasmi
ya JWTZ iliyotolewa na msemaji wake Kanali Kapambile Mgawe imesema kuwa
shambulizi hilo lilitokea
juzi saa tatu asubuhi baada ya kikundu cha
waasi wa Darfur kuvamia ghafla na kukishambulia kikosi cha askari 36 na ofisa
mmoja umbali wa kilomita 20 kutoka Makao Makuu ya kikosi hicho.
Kanali Mgawe
alisema kuwa wanajeshi hao walikuwa wakiwasindikiza waangalizi wa amani kutoka
Khor Abeche kuelekea eneo la Nyara huko Darfur, ambao pia ulikuwa na
maofisa na askari kutoka mataifa mengine ambao walijeruhiwa.
Aliongeza
kwamba wanajeshi walipatwa na mkasa huo wakitekeleza jukumu la kulinda amani la
Umoja wa Mataifa (UN), nchini Sudan
katika eneo la Darfur
Alisema miili
ya marehemu na majeruhi imechukuliwa kutoka katika eneo la tukio na kupelekwa
katika hospitali Kuu ya Nyara ambalo ni eneo la operesheni kwa hifadhi na
huduma ya matibabu kwa majeruhi.
alisema JWTZ
inawasiliana na familia za marehemu kuhusu taratibu za mazishi sambamba na Umoja
wa Mataifakuhusu taratibu zote muhimu zinazohusiana na matibabu ya
waliojeruhiwa.
Mgawe alisema
tayari ujumbe maalumu umeteuliwa kwenda
Khartoum na Darfur kuzungumza na mamlaka kuhusiana na tukio hilo.
“Tunahitaji
jeshi letu kuongeza uwezo wa kujilinda na mashambulizi inapobidi pindi kikundi
chetu kinapokabiliwa na mashambulizi ya aina hiyo,” alisema Kanali Mgawe
Akifafanua
kuhusu hilo alisema kuwa kwa sasa wanatumia aina ya ulinzi unaojulikana kama
‘Chapter 6’ usiowahitaji kutumia nguvu sana na badala yake wamepanga
kushauriana na UN kutumia ‘Chapter 7’ itakayo toa nafasi kwa wanajeshi
kujilinda kiusalama zaidi.
JK awalilia
Rais Jakaya
Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ameshtushwa na tukio la
kushambuliwa na kuuawa kwa askari hao, na kujeruhiwa kwa wengine 14 kulikofanywa
na kundi la waasi wa Sudan.
Katika salamu
zake na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania na kwa familia za wafiwa wote.
Aidha, Rais
Kikwete anaungana na Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na
familia za wafiwa kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia
anaungana na Watanzania wote kuwaombea wale walioumia katika tukio hilo waweze
kupona haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa
Mataifa.
Katika salamu
zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunynge na
familia za wafiwa, Rais Kikwete alisema:
“Sina maneno ya
kutosha ya kuelezea mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo
vya vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya
utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika
eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa
kushambuliwa na waassi.
”Napenda kwa
niaba ya Watanzania wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana
wetu hao tokea walipokwenda Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea
Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya
kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo
imeiletea nchi yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi
yao.”
Rais Kikwete
alisema: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za
dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa. Kupitia kwao, natuma salamu za
rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapigaji wote wa Jeshi
letu kwa kupotelewa na wenzao. “
“Aidha, kupitia
kwako, nawatuma salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na
ndugu zao katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza.
Wajue kuwa uchungu wao ni uchungu wangu pia na wa Watanzania wote na kuwa kwa
pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika
kipindi hiki kigumu. Vile vile kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze
peponi roho za marehemu. Amina.’
Kwa walioumia,
Rais Kikwete ametoa salamu za pole na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone
haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa
Mataifa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment