Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

NI ZAMA ZA UFASHISTI


Ni zama za ufashisti mambo leo

Na Absalom Kibanda

BAADA ya kuwa nje ya ofisi kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa kwa likizo maalumu ya kikazi niliyoichukua baada ya kufanya kazi mfululizo kwa miaka takriban miwili pasipo kupata mapumziko ya kutosha, nimerejea tena kazini.
Kwa makusudi niliamua kutumia sehemu ya likizo yangu kusafiri kwa mafunzo ya muda mfupi hadi katika mji mdogo wa Grahamstown nchini Afrika Kusini ambako nilihudhuria mafunzo ya uandishi wa habari wa takwimu au kwa kimombo, ‘data journalism’.

Siku moja baada ya kumaliza mafunzo hayo ambayo yalihusisha pia wanahabari wengine kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, nilipata fursa ya kuhudhuria mkutano wa kila mwaka ujulikanao kama ‘Highway Africa’ unaoandaliwa na Shule ya Uandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Rhodes kilichoko katika mji huo huo wa Grahamstown.

Highway Africa ni mkutano mkubwa unaowakutanisha waandishi wa habari, wadau wa habari na wanataaluma wengine ambao fani zao zinaingiliana na uandishi wa habari kutoka katika nchi takriban zote za Afrika na nje ya bara hili. Zaidi ya watu 600 walihudhuria mkutano huo wa siku mbili.

Ulikuwa ni mkutano muhimu na nyeti ambao ulinipa fursa ya kubadilishana mawazo na wanahabari wenzangu wa mataifa mbalimbali ya Afrika kuhusu afya ya taaluma ya habari katika taifa langu na mengine Afrika na namna uhuru wa upashanaji habari na utoaji maoni unavyokabiliwa na changamoto lukuki nyakati hizi.

Mijadala rasmi na ile isiyokuwa rasmi ambayo nilishiriki ilinifumbua macho na kuanza kuliangalia taifa langu na mengine kadha wa kadha ya Afrika na yale ya nje ya bara hili kwa jicho ambalo lilinipa majibu ambayo pengine nisingeyabaini iwapo ningekosa fursa ya kukutana na magwiji wa habari wa Afrika na ulimwenguni wanavyoitazama afya ya tasnia ya habari katika bara hili na pengine katika nchi moja moja.

Mbali ya kushangilia ushindi aliopata Mtanzania mwenzetu, Ndesanjo Macha kwa kuwa mwanahabari wa Afrika mwenye blogu bora, kikubwa ambacho niliondoka nacho katika mkutano huo ni kubaini kwangu kuwa Tanzania na baadhi ya mataifa yaliyo katika bara hili yanapita katika kipindi kigumu cha mabadiliko ya kimfumo na kiutawala.

Kipindi hiki kinachokuja miaka 50 baada ya uhuru wa mataifa mengi ya Afrika, kinabeba taswira ya kuanza kuzorota na kukwama kwa kile ambacho kilianza kuonekana kuwa ni kuongezeka kwa wigo wa uhuru wa kutoa maoni na kupashana habari.

Hali hii ilionekana kuwagusa wanazuoni wengi ambao tayari wameshaanza kufanya tafiti ili kubaini ni kitu gani hasa kimekuwa kikitokea ndani ya tawala za kidemokrasia ambazo katika mwelekeo wa kushangaza na kushtusha ghafla zinaonekana kuanza kubeba chembechembe hatari zinazoashiria kuminywa kwa uhuru wa habari.

Nje ya vyumba vya mikutano huko Grahamstown nilihojiwa na wadau wa habari waliokuwa na shauku kubwa ya kufahamu kile walichokiona kupitia mitandao ya intaneti kuhusu kuuawa kwa mwandishi wa habari Daudi Mwangosi wakati akiwa katika mikono ya polisi.

Kilichoonekana kuwashtua wadadisi hao ni picha iliyopigwa na Mpigapicha Mkuu wa gazeti hili, Joseph Senga ambayo ilikuwa ikionyesha namna Mwangosi alivyokuwa amezongwa katikati ya kundi la askari polisi sekunde chache kabla ya kufikwa na mauti yaliyocharanga kabisa mwili wake kwa kiwango cha kusababisha picha za mauti yake kuwa za kuogofya sana.

Picha ya Senga iliyosambazwa katika mitandao mbalimbali ya inteneti na katika ukurasa wa mbele wa gazeti la Mwananchi la siku ya pili ya tukio kabla ya kurudiwa tena katika gazeti hili siku iliyofuata iliibua tafakari ya namna yake dhidi ya serikali za baadhi ya watawala waliochaguliwa kidemokrasia zinavyoonekana kuchukua maamuzi ya kikatili kama si ya kimabavu dhidi ya uhuru wa habari, wa kujieleza na ule wa kutoa maoni.

Taswira ya picha zile za Mwangosi ilikumbusha wadadisi hao matukio kama yale yaliyotokea huko huko Afrika Kusini siku chache tu zilizopita ambako askari polisi waliwaua kwa kuwafyatulia risasi wafanyakazi zaidi ya 40 wa migodi katika eneo la Marikani waliokuwa wakiandamana kudai nyongeza ya mishahara yao.

Hawakuishia hapo, mijadala ilikwenda mbali zaidi na kuzungumzia matukio kama yale ya kufungiwa kwa gazeti la MwanaHALISI ambalo kwa jicho la wasomaji wa taarifa zake wanaotoka nje ya Tanzania wanaliona kuwa lililokuwa likiibua hoja nzito dhidi ya serikali na viongozi wake.
Wadadisi hao walipojua kwamba mimi ndiye mhariri ninayekabiliwa na kesi ya uchochezi kwa sababu ya makala iliyoandikwa katika gazeti hili na kwamba ndiye ninayeshikilia wadhifa wa uenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, walitarajia mengi kutoka kwangu kuhusu afya ya uhuru wa habari wa kujieleza na kutoa maoni.

Kwa kuwa kesi yetu ingali bado iko mahakamani, itoshe tu kutambua kwamba, nilitumia vyema fursa ya kuhudhuria mkutano huo na kukutana na magwiji wa habari duniani kwa kuweka kumbukumbu sawia kuhusu hali tete ya utendaji kazi wa vyombo vya habari hapa nchini zama hizi za serikali ya awamu ya nne.

Wako walioahidi kuandika vitabu katika siku zijazo kuhusu kile nilichowaeleza nikitumia taarifa zilizopata kuripotiwa magazetini na zile ninazozijua kwa undani kuhusu nini hasa kilikuwa kikitokea ndani ya vyumba vya habari na namna wanahabari wa Tanzania tunavyofanya kazi katika mazingira yaliyojaa mizonge mingi, tabu na misukosuko ambayo aghalab imefikia hatua ya kutufanya tusiijue kesho yetu.

Bado naamini nilifanikiwa kufikisha ipasavyo ujumbe wangu kuhusu matukio kama yale ya kufungiwa kwa gazeti la MwanaHALISI na lile la kumwagiwa tindikali kwa Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, Saed Kubenea, miaka kadhaa iliyopita kama mfano wa matukio ambayo yanaeleza nini kipo nyuma ya pazia ya kile kinachoitwa uhuru wa habari, kutoa maoni na wa kujieleza hapa nchini na hususan zama hizi za Serikali ya Awamu ya Nne.

Mmoja wa waandishi wakongwe alieleza kuguswa na namna vitendo hivi vya baadhi ya watendaji wa taasisi za dola vinavyoiweka Tanzania karibu kabisa na tanuri la kuzalisha watuhumiwa wa kwanza wa kesi ya kukandamiza haki za binadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu iliyoko The Hague, Uholanzi.

Mwandishi mwingine alitaka wanahabari wa Afrika tufanye utafiti wa kina kuhusu kile alichokiita udikteta wa kidemokrasia ambao alisema unaonekana kuanza kuibuka katika Afrika na ukitoa mwelekeo wa kuminya uhuru wa habari na ule wa kutoa maoni kwa njia za panya.

Mwandishi huyo aliitaja Rwanda ya Paul Kagame na Ethiopia ya zama za Meles Zenawi kuwa mfano wa mataifa ya Afrika ambayo yalikuwa yamefikia hatua ya kuminya uhuru wa habari na ule wa kutoa maoni kwa kuwashitaki waandishi na wahariri kwa makosa mbalimbali kutokana na kile kilichoandikwa au kuripotiwa katika vyombo wanavyofanyia kazi.
Ni nyakati hizo hizo tukiwa Grahamstown likaibuka tukio la mchora vibonzo wa India aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kudhalilisha mamlaka za dola kutokana na katuni aliyoichora dhidi ya Bunge la nchi hiyo kwa namna ambayo iliikera serikali.

Ingawa sote tulikubaliana kwamba uhuru wa habari na ule wa kutoa maoni ulikuwa unayo mipaka ambayo inatupasa wahariri, waandishi wa habari na wadau wa habari kuitambua, bado sote tuliondoka Grahamstown tukiwa na taswira moja kubwa kwamba, Afrika na dunia kwa ujumla zinapita katika zama za aina mpya si ya udikteta bali ya ufashisti uliojificha nyuma ya pazia lenye majina mengi mazuri.

Hitimisho hilo la Grahamstown nililoondoka nalo nje ya vyumba vya mikutano ya Highway Africa ndilo ambalo limezaa kichwa cha habari cha makala hii leo ambacho wanazuoni wana kila sababu za kuanza kukifanyia utafiti kwani dalili za wazi zinaonyesha na mazingira ya sasa yanathibitisha kwamba tumeanza kushuhudia aina mpya ya ufashisti wa kistaarabu.

Aina hii ya ufashisti imebeba sura nyingi. Kwa upande mmoja inabeba sura ya kuheshimu utawala wa sheria na kwa upande mwingine unaweka ukomo kwa watawala waliochaguliwa kupitia sanduku la kura kuchokozwa, kukosolewa au hata kuguswa.

Kama ilivyokuwa kwa ubeberu uliokuja baada ya ubepari kuamua kutoka nje ya mipaka ya mataifa husika na kwa namna ile ile ukoloni ‘mambo - leo’ ulivyojijenga katika mataifa huru yaliyoushinda ukoloni halisi ndivyo ilivyo sasa kwa Afrika inayoshangazwa na namna ufashisti wa kina Musolini, Hitler na wengine unavyorudi kwa mlango wa nyuma. Hakika hizi ni zama za ufashisti mambo leo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment