|
SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, kukutana
na viongozi wa vyama vyenye wabunge kuzungumzia upungufu katika muswada wa
marekebisho ya sheria ya sheria mabadiliko ya katiba, viongozi wa vyama
hivyo wametoa mapendekezo mazito.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa
mapendekezo hayo mengi ni yale yaliyokataliwa na wabunge wa Chama Cha mapinduzi
(CCM) wakati wakipitisha muswada huo bungeni.
Mapendekezo hayo ya wapinzani yanaonekana yatazua
mtafaruku mkubwa bungeni iwapo serikali itaamua kuyapeleka, hasa baada ya
Rais Kikwete kuwataka wapinzani kuandaa mapendekezo ya kina ya upungufu wa
sheria hiyo na wayawasilishe haraka iwezekanavyo serikalini ili iunde
kamati maalumu ya kujadili upungufu.
Tanzania Daima Jumatano limebaini kuwa viongozi
hao wa vyama vya upinzani waliokutana Oktoba, 17, 2013 walijadili na
kutoa mapendekezo kadhaa mbayo wameyawasilisha serikalini kama
walivyoagizwa na Rais Kikwete.
Mapendekezo
Wapinzani hao wanapendekeza kifungu 22 (2A) cha
sheria kama ilivyo sasa kifutwe kabisa, na kwamba wajumbe waliotajwa katika
kifungu cha 22 (1) (c) watateuliwa na taasisi watakazowakilisha, na
kwamba idadi ya wajumbe hao iongezeke kutoka 166 kwa mujibu wa sheria ya
sasa hadi 438.
Wamependekeza kuwa makundi yote yanayostahili
kuwakilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba yatafafanuliwa na idadi ya
wawakilishi wao kuwekwa wazi katika jedwali la pili la sheria.
Pendekezo jingine linataka kuzingatia usawa wa
kijinsia, kifungu kidogo (2b) kifutwe na kuandikwa upya “uteuzi wa
wajumbe wa Bunge Maalumu chini ya kifungu kidogo (1) ( c ) utazingazia kanuni
za sifa na zuoefu wa watu walioteuliwa, na idadi ya wajumbe wanawake
haitapungua theluthi moja ya wajumbe walioteuliwa kutoka katika makundi
hayo.”
Kwa kuzingatia dhana ya usawa wa wabia sawa wa
Muungano bila kujali ukubwa wa kila nchi, idadi ya watu wake na kuzingatia
haja ya kujenga muafaka na maridhiano ya kisiasa kuhusu muungano wetu,
viongozi wa vyama, wamependekeza kama ilivyokuwa katika uteuzi wa wajumbe
wa Tume ya Katiba ya Mabadiliko ya Katiba, kutakuwa na uwakilishi
sawa katika Bunge Maalumu kati ya washiriki wa Muungano.
Vile vile wamependekeza kuwa kifungu 22(1)
kirekebishwe kwa kuongeza aya ya (d) isomeke “wajumbe wa Bunge Tume
ambao hawatakuwa na haki ya kupiga kura katika Bunge Maalumu yaani watakuwa
wajumbe kwa nafasi zao ‘ex officio’ kwenye Bunge Maalumu.”
Hivyo kifungu (c) cha zamani za 37 (1) kirejeshwe
ili kuwezesha uwepo wa tume hadi baada ya matokeo ya kura ya maoni
kutangazwa, na idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu itakuwa 908, kwa
mchanganuo wa 357 Bunge la Jamhuri, 81 Baraza la Wawakilishi, na 438
watakaoteuliwa na makundi tajwa katika kifungu 22(1) (c) na wajumbe 32 ‘ex
officio’ wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia wamependekeza kwamba kifungu 26 (4) na (5)
vifutwe badala yake kifungu (3) kirekebishwe ili kuweka wazi kwamba wajumbe
wa Bunge Maalumu wataendelea na majadiliano hadi kifungu husika
kitakapoungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu
kutoka Tanganyika na idadi hiyo hiyo kutoka Zanzibar.
Mapendekezo hayo pia yamesema kwa jinsi sheria
ilivyopitishwa kuzungumzia nafasi ya kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu sifa zake ni lazima mgombea awe na Shahada ya Chuo Kikuu
kilichotambulika na uzoefu na ujuzi uliothibitika wa kuongoza mihadhara na
mabaraza, kifungu hicho kitakuwa cha kibaguzi miongoni mwa wajumbe wa Bunge
Maalumu ambao wengine hawajahitimu vyuo vikuu hivyo kukosa sifa ya
kuteuliwa au kuchaguliwa.
Hata hivyo kwa kuwa kifungu hicho hakikutoa
tafsiri ya neno mihadhara au mabaraza na mthibitishaji mwenyewe kutotajwa,
wamependekeza kuwa mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu awe na sifa ya kugombea
na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, na
viongozi hao wachaguliwe badala ya kugombea.
Wapinzani wataka ushirikiano
Wakati Tanzania Daima Jumatano ikidokezwa
kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo serikalini, viongozi wakuu wa vyama vya
CCM, CHADEMA, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UPDP, wametaka mchakato wa kupata
katiba mpya ulenge maslahi mapana ya nchi na wananchi kuliko kufikiria
maslahi ya vyama au makundi fulani katika jamii.
Viongozi hao walikutana na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, ambapo Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia
nchini (TCD), James Mbatia alisema kutokana na umuhimu wa upatikanaji wa
katiba mpya, vyama vimedhamiria kuhakikisha kuwa mchakato wa katiba
unafanyika kulenga maslahi mapana ya nchi.
“Sote kwa pamoja tunatambua tofauti mbalimbali
ambazo ziko baina ya vyama vyetu kiitikadi na kimtizamo, lakini tunachukua
jukumu kwa nia safi kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata katiba
wanayoitaka,” alisema.
Vyama hivyo pia kwa tamko la pamoja vimesema
vilikubali wito wa Rais Jakaya Kikwete alioutoa kupitia hotuba yake kwa
Watanzania Septemba 4 na walipokutana naye Oktoba 5, mwaka huu, vimepongeza
juhudi za rais kuhakikisha mchakato wa katiba unakwenda mbele ukihusisha
wadau wote na wale walioachwa wasikilizwe kwa lengo la kuwaleta pamoja.
Mbatia alisema vyama vyao vinampongeza Rais
Kikwete kwa nasaha zake kwa njia ya mazungumzo wakisema ni sahihi na ahadi
ya kutoa ushirikiano mkubwa katika kila hatua ya mchakato wa katiba akiwa
na lengo la kuona katiba inakuwa ya wote.
Kwa mujibu wa tamko hilo la TCD mkutano
huo wa Ikulu na vyama sita vyenye wabunge na rais vilikubaliana
kushirikisha vyama vingine 15 visivyo na wabunge kuandaa mapendekezo ya
kina ya upungufu wa muswada ambao sasa umekuwa sheria na kupendekeza
marekebisho maalumu na kuyawasilisha haraka iwezekanavyo.
Vile vile walipendekeza kuwa baada ya kuwasilisha
mapendekezo hayo serikalini ili serikali iunde kamati maalumu ya kukutana
na vyama hivyo kujadili kwa kina juu ya upungufu katika sheria husika na
kukubaliana juu ya maeneo muhimu yanayohitaji marekebisho kwa lengo la
kuufanya mchakato wa katiba kuwa shirikishi.
Mbatia alisema kulingana na makubaliano
waliyofanya na rais, baada ya pande zote kukutana serikali itaandaa hati ya
dharura ili sheria husika irejeshwe bungeni haraka katika mkutano wa Bunge
unaoanza wiki ijayo.
Alisema kuwa katika mjadala wa kitaifa, taasisi
mbalimbali katika umma, makundi ya kijamii na wadau wote muhimu wahusishwe
ili kutengeneza maridhiano ya kitaifa.
Mbatia alitoa wito kwa niaba ya vyama vyote vya
siasa kuwaomba Watanzania wote hususani wabunge waunge mkono juhudi hizo za
vyama na Rais Kikwete kuhakikisha mchakato wa katiba mpya unakuwa
shirikishi utakaolinda maslahi mapana ya taifa.
Tamko hilo lililosomwa na Mbatia lilikuwa
limesainiwa na Philip Mangula (CCM), Freeman Mbowe ambaye aliwakilishwa na
Dk. Slaa (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia
(NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema aliyewakilishwa na Nancy Karia (TLP),
John Cheyo aliyewakilishwa na Isaac Cheyo (UDP) na Fahmi Dovutwa wa
UPDP kwa niaba ya vyama visivyo na wabunge.
Mangula agoma kuisema CCM
Baada ya tamko hilo, wakati wa maswali, waandishi
walitaka kujua kauli ya CCM kwani wamekuwa wakisisitiza kuwa mchakato huo
ulikuwa huru na ulipitia hatua zote, kama wapo tayari kufanya mabadiliko
kama alivyopendekeza rais na vyama vyenye wabunge.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula
aligoma kuzungumza kwa undani na kusema: “Mimi sio mbunge siwezi kuwasemea
wabunge.”
Kauli hiyo ilisababisha Mbatia kuanza upya
kuwataka waandishi na Watanzania waache tofauti zao, waache kauli zote
zilizowahi kutolewa na kutoa fursa mpya ya kuanza mchakato kwa njia ya
amani kwa maslahi mapana ya taifa.
juu 
|
No comments:
Post a Comment