|
MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Rosweeter Kasikila (60), amejikuta kwenye kashfa nzito ya kufunga
ndoa na kijana, kinda wa miaka 26, Michael Christian.
Ndoa hiyo ambayo ilifungwa katika Kanisa la
Tanzania Assembles of God (TAG), linaloongozwa na Mchungaji Getrude
Rwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, imebaki kuwa
gumzo na kuwaacha hoi baadhi ya mawaziri, wabunge wanaoifahamu pamoja na
majirani wanaoishi na mbunge huyo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya wanandoa hao na
majirani wanaowazunguka, vililiambia gazeti hili kuwa ndoa hiyo ilifungwa
Septemba Mosi mwaka 2011, na imebaki kuwa siri kabla ya wawili hao
kukorogana.
Kabla ya wawili hao kuamua kufunga ndoa, mbunge
huyo kutoka mkoani Rukwa, mwenye makazi yake Bagamoyo mkoani Pwani, alikuwa
akimtumia Michael kwenye shughuli mbalimbali na muda wote alikuwa akiishi
nyumbani kwa mbunge huyo.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo ambaye ana familia ya
watoto wawili ambao kiumri wanalingana na Michael, alianza uhusiano wa
kimapenzi na kijana huyo kwa siri kubwa na baadaye alifanikiwa kumshawishi
wafunge ndoa huku akimuahidi kumpa huduma mbalimbali anazotaka.
Kwa mujibu wa habari hizo, wawili hao waliamua
kufunga ndoa katika Kanisa la TAG baada ya mbunge huyo kufanikiwa
kumshawishi Mchungaji Rwakatare kwamba ndoa hiyo itakuwa siri, hasa
kutokana na tofauti ya kiumri kati yao.
Hata hivyo ndoa hiyo kwa sasa imekumbwa na mgogoro
mkubwa, huku mbunge huyo akidaiwa kuzuia kila kitu cha mumewe huyo, hasa
vyeti vyake vya shule kama njia ya kumbana warudiane.
Siku ya harusi
Kwa mujibu wa mashuhuda wa harusi hiyo ya aina
yake, mbunge na kijana huyo walikwenda kanisani wakiwa wawili bila
mashahidi kama ilivyo kawaida, na ndoa hiyo ilifungwa katika ofisi ya
kanisa na sio ndani ya kanisa.
Mashahidi wa ndoa hiyo waliitwa hapo hapo kanisani
na walisimamia na kushuhudia utiaji saini wa cheti cha ndoa na kisha
wanandoa hao kutawanyika kwenda kwenye fungate (Honey Moon).
Hakukuwa na sherehe baada ya kufungwa ndoa.
Inadaiwa kuwa hakukuwa na ndugu yeyote wa maharusi
hao aliyeshuhudia tukio hilo la kihistoria la wawili hao kuunganishwa na
kuwa mwili mmoja.
Kauli ya Bwana harusi
Tanzania Daima Jumatano, lilifanikiwa kumpata
Michael, ambaye katika mazungumzo yake alikiri kufunga ndoa na mbunge huyo
Septemba Mosi mwaka 2011, lakini kwa sasa wametengana kutokana na sababu
ambazo hakutaka kuziweka wazi.
“Mimi nadhani hili ni jambo binafsi, sio vizuri
kulizungumza hadharani ila kweli nilifunga naye ndoa maana inaonekana
mnajua mambo mengi kunihusu, na ni kweli kwa sasa tumeachana,” alisema kwa
kifupi.
Alisema walikutana na mbunge huyo Bagamoyo wakati
alipokuwa akifanya mafunzo kwa vitendo katika hospitali ya wilaya hiyo kama
muuguzi mkunga wakati mbunge huyo akiwa muuguzi mkuu wa wilaya katika
hospitali hiyo.
Alipoulizwa sababu za kukubali kufunga ndoa na
mama wa umri wa miaka 60 wakati ana miaka 26 na sababu za ndoa hiyo
kuvunjika, Michael alisema ana historia ndefu katika maisha yake kwani
alizaliwa yatima na amekua na kulelewa kwa ufadhili wa kituo cha
Safina Street Network.
“Katika mazingira niliyokulia, unaweza kujua
kwanini nilikubali kuingia kwenye ndoa hiyo. Sina ndugu hata wa kunishauri.
Hata hivyo, hayo tuyaache. Lakini ukweli ndio huo, lakini kwa sasa
tumeachana, kila mtu ana maisha yake,” alisema Michael kwa masikitiko.
Michael ambaye kwa sasa anasoma katika Chuo Kikuu
cha Muhimbili, pia alikiri kuwa mbunge huyo anashikilia vyeti vyote vya
shule ambavyo anavihitaji sana kwa ajili ya kusaka ajira baada ya kumaliza
masomo yake Muhimbili.
Alitaja sababu ya kuvunja ndoa hiyo kuwa ni
manyanyaso kwa vile ni mdogo na masikini kwani hakuwa na sauti na alibanwa
kwa kila kitu kiasi cha kukosa kabisa amani katika maisha yake.
“Kimsingi ndoa yangu na mama imevunjika na
ilivunjikia mikononi mwa Rwakatare wakati akijaribu kutusuluhisha,
alinitaka nirudi kwa mama, hapana, siko tayari na hapa nataka vyeti vyangu
tu basi,” alisema Michael.
Mbunge ang’aka
Kwa upande wake, mbunge huyo alipoulizwa, kwanza
alikuwa mbogo na kukataa katakata kuzungumza kwa madai kuwa hawezi
kuzungumzia jambo hilo zito kwenye simu.
Mbunge huyo alikiri kuwapo kwa ndoa hiyo, lakini
alipinga kwamba haijavunjika na kumhoji mwandishi wa habari hizi kama
anajua taratibu za kuvunja ndoa.
“Michael kakuambia hiyo ndoa imevunjika? Wewe si
unajua taratibu za ndoa kuvunjika? Kwanza nimeshasema sitaki kuzungumzia
suala hili kwenye simu ukitaka tuonane kesho kwani kuna haraka gani? Jambo
la haraka ni la mjamzito kutaka kujifungua, lakini kama ni suala hilo
hakuna sababu ya uharaka,” alisema mbunge huyo.
Hata hivyo baada ya kubanwa, mbunge huyo alimtaka
mwandishi wa habari hizo kukutana naye katika ofisi ndogo za Bunge jijini
Dar es Salaam kwa ajili ya kupata ufafanuzi, lakini cha ajabu mwandishi
alipofika katika ofisi hizo hizo, mama huyo alizima simu yake na
hakupatikana tena.
Mchungaji Rwakatare
Alipotakiwa kuzungumzia ndoa hiyo, Mchungaji
Rwakatare kwanza aling’aka kwamba hajawahi kufungisha ndoa ya aina hiyo.
Lakini alipobanwa alikiri kuikumbuka ndoa hiyo na
kwamba ilifungishwa na mchungaji wa kanisa lake, aliyemtaja kwa jina
la Mchungaji Mtetumo.
Alimtetea mchungaji wake kwamba alichokifanya ni
kutimiza wajibu wake wa kichungaji wa kufungisha ndoa, hasa kama wanandoa
wametimiza vigezo.
“Wajibu wa kanisa ni kufungisha ndoa, kama
wanandoa wamekidhi vigezo vya kanisa. Sio kazi ya kanisa kuwachagulia
wachumba kwa maana hakukuwa na sababu ya kuhoji umri wao, wala jambo lolote
zaidi ya kufungisha ndoa hiyo,” alisema Mchungaji Rwakatare.
juu 
|
No comments:
Post a Comment