Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

MAKALA: NANI ANAJALI

Na Charles Misango

Udhalilishaji wa dini nyingine?
NIANZE kwa kuungana na wananchi wote duniani walioweza kutamka, kusikitika na kulaani filamu ya mmarekani mmoja ambayo inaelezwa kukashifu imani ya dini ya Kiislamu.
Naungana nao kwa sababu mimi ni miongoni mwa wanaoamini uhuru wa kuabudu na kuheshimu sio mawazo tu, bali hata imani ya mwingine hata kama kwangu sikubaliani nayo.
Filamu hiyo imeleta madhara makubwa katika baadhi ya nchi nyingi duniani. Kumefanyika maandamano makubwa katika nchi hizo, lakini lililo baya zaidi, kumetokea vifo vya watu wengi wasiohusika, wala hawakuwa na taarifa yoyote juu ya kuwepo kwa filamu hiyo.
Waliokufa wengine hata huyo mtengeneza filamu hiyo hawamjui wala hawajawahi kumwona. Wameponzwa na kitu wasichokijua. Wamekufa! Wamekwenda! Hawatarudi tena!
Hapa nchini tukio hilo halikupita bure.  Viongozi wengi wa Kislamu walitoa matamko ya kulaani filamu hiyo. Tumshukuru Mungu kwamba, kwa busara za viongozi hao, walifanikiwa kufikisha ujumbe wao bila kuhamasisha waumini wao kufanya vurugu na maandamano ambayo kwa namna yoyote yangeleta balaa.
Narudia. Nakubaliana na kuungana kwa dhati na wale wote waliolaani filamu hiyo, ingawa nimesikitishwa sana na vifo vya watu wasio na hatia wala kuhusiana na mtengenezaji kwa namna yoyote ile, kwa sababu maisha yao yamekatishwa bure. Nasikitika pia juu ya uharibifu wa mali uliofanywa na wenzetu ambao wamechukizwa na filamu hiyo. Nina uhakika, walioharibiwa, masikini ya Mungu hawana mchango wowote na uwepo wa filamu ya kumkashifu Mtume Mohammed (SAW).
Ni tukio jingine baya kama lile la kile kitabu cha AYA ZA SHETANI kilichotungwa na Salmine Rushidde miaka ile ya 90. Wenye kumbukumbu njema wanajua kile kilichotokea duniani kwa wake ule.
Bila kujikomba kwa yeyote, kitabu, filamu, chapisho lolote lile ama hata mahubiri yanayodhalilisha, kutukana na kukashifu imani ya dini ama dhehebu jingine, hufanywa na mtu ama watu wasiojali imani za wengine. Hufanywa na watu waliokosa staha, wabinafsi, wachoyo, wenye upeo mdogo wa kufikiri, na mbaya zaidi wasiosumbua akili zao kuona madhara yatakayotokana na matendo yao katika jamii.
Suala la imani ya dini ni zito kwa maana ya uzito! Linalogusa uhai wa mtu. Kucheza na imani ya mtu ni kucheza na roho ya mtu, hivyo, kwa namna yoyote ile linahitaji kuchukuliwa kwa uzito na kila mtu. Kila anayetambua kuwa ni muumini wa dini ama dhehebu fulani, anajua kuwa kile anachokiamini ndicho bora, safi na sahihi kuliko cha mwingine. Kwake, wale wasioamini kama yeye waliopotea.
Kumbe, mtu makini anayejali wengine, sharti awe mwangalifu na mwenye staha anapojaribu kugusa imani ya mtu mwingine.  Watu waliojaliwa kuwa na upeo wa kufikiri, wenye kujali utu na hadhi ya wengine, kamwe huwasikii katika kutangaza imani zao wakigusia kwa namna ya kudhalilisha na kuudhi imani za wengine. Daima watazama kuhubiri, kufundisha na kutangaza kile wanachoamini wao. Wataonesha uzuri wa dini zao, watanogesha tunu ya dini zao, na watatoa matumani ya baadaye yanayopatikana kwa wale waliondani ya dini zao na watakaojiunga nazo baadaye.
Wakati sote tunaungana kulaani filamu hiyo inayoudhalilisha uislamu na Mtume Mohammed (SAW), hapa nchini na hususan katika jiji la Dar es Salaam, kwa miaka kadhaa sasa kumeibuka kundi la watu ambao bila woga, wala kujali na kuheshimu uhuru wa kuabudu na imani ya dini nyingine, wamekuwa wakiendesha mahubiri dhidi ya dini nyingine kwa lugha zilizojaa matusi, kejeli, dhihaka na udhalilishaji wa hali ya juu.
Kundi hili, limefanya hivi mchana kweupe na wanaendelea hadi nyakati za usiku, wakitumia vipaza sauti vyenye nguvu kubwa na hivyo, matusi yao husikika kwa umbali mkubwa. Watu hawa ambao huendesha mambo yao kwa mtindo wa maswali, ni mabingwa wa lugha chafu zilizojaa mafundisho ya uongo wa kutisha! Wanatukana wanavyotaka! Mathalani, wanadiriki hata kuita kuwa watu wa dini hiyo ni wajinga na ndio maana kengere zao hulia…’wajinga njoo, wajinga njoo’ wameitwa makafiri mara nyingi mno!
Swali la kujiuliza, nani kawapa mamlaka ya kutukana na kudhalilisha dini za wengine? Jeuri ya kufanya haya yote bila kujali, inatoka wapi?  Hivi ikiwa wao hawako tayari kuona mtu yeyote anadhalilisha dini, imani na kiongozi wao mkuu, na wako tayari kupambana hata kumwaga damu kutetea imani hiyo, iweje kwao iwe ruksa kusema, kuhubiri na kuendesha mihadhara inayotukana dini za wengine?
Hivi kama sio busara na uvumilivu wa wale wanaotukanwa, ama leo hii nao wakasema yatosha na wakaamua kutetea imani yao kwa njia yoyote dhidi ya wale wanaowatukana, je, itakuwa nchi ya kukalika tena?  Kwa nini basi, wale viongozi makini, wanaojali na kuheshimu uhuru wa dini ya wengine; kwa nini viongozi wa serikali walio na wajibu wa kulinda uhuru wa watanzania wote wakae kimya wakiwaacha watu wachache WASIOJALI kutamba kwa matusi dhidi ya         wengine? Nyote hakuna asiyejali hali hii?

mwisho

No comments:

Post a Comment