·
Wamalizana na Chadema bungeni
Na
Edson Kamukara, Dodoma
SIKU
moja baada ya vyama vya CUF na Chadema kuvurugana bungeni na kusababisha Bunge
kuahirishwa mara mbili, hatimaye muafaka umefikiwa kwa viongozi wake kuombana radhi
hadharani.
Vyama hivyo viliingia
kwenye mtafaruku mkubwa juzi baada ya wabunge wa CUF kuomba mwongozo wakita
msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Ezekiah Wenje aondoe maneno ya kikidhalilisha chama chao kwenye
hotuba yake.
Maneno yaliyoleta
mtafaruku yalikuwa ukurasa wa nane ambapo katika hotuba hiyo, Wenje alikuwa
akielezea itikadi za vyama rafiki vya nje vinavyoshirikiana kuviwezesha na
vyama vya CCM, CUF na Chadema.
Wenje alisema kwa upande
wa CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa Kiliberali ambazo miongoni mwa
misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji
na ushoga”.
Kutokana na vurugu hizo
baada ya Wenje kukataa kuomba radhi akisema haoni kosa lake na hivyo kukubali
kuondoa maneno, Naibu Spika, Job Ndugai aliliahirisha Bunge mara mbili na
kuiagiza Kamati ya Haki, Kinga, Madaraka na Maadili ilijadili suala hilo na
kushauri.
Hatimaye jana baada ya
kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Ndugai alimpa nafasi Makamu
Mwenyekiti wa kamati hiyo, John Chiligati ili aeleze kile kilichojadiliwa na
kuafikiwa.
Chiligati alisema kuwa
walikutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kama walalamikiwa na upnde
wa CUF kama walamikaji alikuwepo mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim.
Alisema
kuwa katika utetezi wake, Mbowe alisema kuwa wako tayari kuondoa maneno hayo
lakini hawawezi kuomba radhi kwa vile kilichosema ni sahihi.
Katika
hoja yake ya pili Mbowe alisema kuwa CUF walimtukana Wenje na kumdhalilisha,
kuchana hotuba na vurugu zao ziliahirisha Bunge, hivyo akataka mambo hayo
yazingatiwe katika mjadala.
“Mbarouk
yeye alikiri kuwa CUF ni wanachama wa Liberal International lakini
hawakubaliani na sera zote za umoja huo. Na isitoshe Tanzania kama nchi
ilishatoa msimamo wakati Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun alipotoa
masharti misaada kwa mataifa yanayoendele kwa kutaka wakubali ushoga”.
“Hivyo
kama nchi tumekataa, hivyo Masoud alihoji kwanini Chadema waliweka maneno hayo
kwenye hotuba ili kuwadhalilisha. Anataka waombwe radhi na kuondoa maneno hayo,”
alisema.
Chiligati
aliongeza kuwa ili kujenga mshikamano ndani ya Bunge waliafikiana kuwa Mbowe
kwa niaba ya Chadema awaombe radhi CUF, Bunge zima na Naibu Spika na maneno
hayo yaondolewe kwenye hotuba.
“Pia
CUF kupitia mnadhimu wao, wawaombe Chadema radhi kutokana na baadhi ya wabunge
wao kutukana, kuchana hotuba yao na vile vile waliombe radhi Bunge na Naibu
Spika kwa usumbufu hadi kuahirisha Bunge,” alisema.
Muafaka
wapatikana
Baada
ya Chiligati kumaliza, Ndugai alimwita Mnadhimu wa CUF, Rashid Ali Abdallah
ambaye alianza kwa kuwaomba radhi naibu Spika na Waziri Bernard Membe kutokana
na vurugu hizo kukwamisha mjadala wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Alisema
kuwa Chadema kwa makusudi, kuto kujua au kwa bahati mbaya waliweka maneno ya
kuidhalilisha CUF, kwamba wao wameweka maslahi ya taifa mbele kukubali kufikia
muafaka.
“Kwa
kitendo kile wabunge wa CUF walichemka na kutoa maneno ya kashfa, hivyo naomba
samahani kwa yote yaliyotokea,” alisema Abdallah na kushangiliwa na wabunge.
Naye
Mbowe alisema kuwa katika dhamira ya usuluhisho na kurejesha amani ndani ya
Bunge, hana sababu ya kuhoji mambo yote aliyowasilisha Chiligati.
Mbowe
pia alimpongeza mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa
wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) akisema alialikwa na kamati hiyo kama
mshauri na kutoa msaada mkubwa wa kimawazo kutokana na uzoefu wake.
“Katika
kikao kile nilitanguliza kusema kuwa ile kauli ya Wenje haikuwa yake pekee bali
ni ya kambi nzima kama ilivyo kwa serikali, kauli ya waziri si yake bali ya
serikali, hivyo tusikwepe kuwajibika wote,” alisema.
Alisema
kuwa CUF walikwazika na maneno hayo potelea mbali yalikuwa na ukweli au hapana,
hivyo ni lazima wapate muafaka ili kuonesha umoja wao kwani taifa ni zaidi ya
vyama.
“Kuna
mambo mazito ya kujadili na kusuguana ya msingi zaidi ya hili, nipende kuwaomba
radhi CUF na Bunge zima. Pia kwako Naibu Spika, tumeahirisha Bunge mara mbili
bila sababu ya msingi. Pole kwa usumbufu mlioupata wote, tumetafakari na kuona
tulikojikwaa,” alisema Mbowe na kushangiliwa na Bunge.
Ndugai
katika kuhitimisha jambo hilo, aliwasihi wabunge kujiepusha na kauli ambazo
zinaweza kuudhi wengine na vile vile aliwataka CUF na Chadema kuzingatia
makubaliano.
Mwisho
No comments:
Post a Comment