Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

Nani anajali: mtuhumiwa wa mauaji akipandishwa cheo?



Na Charles Misango
SIJAWAHI kushitushwa na kuumia mno nisiamini kabisa kama nilichokisoma na kukisikia ni mawazo na maamuzi yaliyotolewa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kikitumika jina la Rais Jakaya Kikwete.
Hata sasa sielewi kilichotokea, na  sijajua hasa ujumbe kamili ambao serikali ya CCM inakusudia kuufikisha kwa mamilioni ya Watanzania walioiweka madarakani. Najua msomaji hujanielewa. Ni hivi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani juzi, Rais Jakaya Kikwete amewatunuku vyeo maafisa kadhaa wa juu wa jeshi la polisi nchini. Mmoja wa maafisa hao, ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, ambaye hadi sasa hajakana kusimamia kuteswa na kisha kuuawa kikatili kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituol cha Luninga cha Channel Ten, Daud Mwangozi.
 Kamuhanda amepandishwa cheo, kutoka nafasi ya Kamishna Msaidizi Mweandamizi wa polisi, (SACP) kwenda  kuwa Naibu Kamishina wa polisi (DCP). Kabla ya kuhamishiwa Iringa, Kamuhanda alikuwa Kamanda wa polisi Mkoa wa Ruvuma baada ya tukio la askari polisi kuwaua kwa risasi waandamanaji madereva wa bodaboda.
Mauaji ya Mwangosi yalikuwa ya kikatili mno, na yaliyofanywa na polisi wakiangaliwa kwa kila hatua na Kamanda Kamuhanda, tangu alipoanza kuteswa na kushambuliwa kama mbwa mwizi na kundi la polisi. Kosa la Mwangosi halijulikani, na hata kama angekuwa ametenda kosa, polisi hana mamlaka ya kutesa mtu na hata kumuua!
Mauaji ya mwandishi huyu, yalibainisha bila shaka uzembe mkubwa wa Kamuhanda, na kwamba tume zote mbili zilizoundwa kufuatilia suala hilo; ile ya haki za binadamu na utawala bora pamoja nay a MCT, zilimbebesha lawama kamanda huyu.
Uundwaji wa tume hizo, ulikuja baada ya maandamano makubwa ya waandishi wa habari yaliyoratibiwa na Jukwaa la Wahariri kulaani mauaji ya Mwangosi. Sote tunakumbuka namna Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanue Nchimbi, alivyojitokeza pasipo kualikwa kupokea maandamano ya waandishi, kabla ya kupingwa na kutakiwa kuondoka.
Mimi nikiwa ‘mwongozaji’ wa maandamano hayo, kwa busara za viongozi wa jukwaa, nililazimika kumwomba Nchimbi aondoke, lakini akiacha ameniomba kumpelekea maoni na maazimio yatakayofikiwa na waandishi katika maandamano hayo.
Katika nchi yoyote inayojali sheria na kuheshimu uhai wa watu, suala la kujizulu na kuwajibishwa kwa Kamuhanda halikuwa na mjadala. Pili, kwa mtu yeyote anayejiheshimu, anayejali watu, anayejua kuwa cheo ni dhamana, hata kama asingewajiobishwa, tukio hili na sauti kutoka kwa watu, zingemlazimisha kuomba kuachia ngazi ili kulinda heshima yake nay a taasisi yake hata kama hakuhusika moja kwa moja na mauaji ama kuwepo sehemu ya tukio.
Hayo yote mawili, hayakufanyika kwa Kamuhanda wala kwa serikali. Badala yake, amepewa tuzo ya kuongezewa cheo, na kwa maana nyingine mshahara posho na marupurupu yanayoambatana na ukubwa huo! Inaumiza sana!
Dalili za kutojali kwa watawala wetu kuhusu mauaji haya zilianza kujitokeza mara tu baada ya kuawa kwa Mwangosi. Watanzania watakumbuka kuwa, taarifa ya jeshi la polisi mara tu baada ya mauaji haya, ziliobainisha kuwa mwandishi huyu aliuawa na kitu chenye ncha kali, kilichorushwa kutoka nyuma ambako kulikuwa na kundi la wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kwa lugha nyingine, serikali ilitaka kutuambia kuwa waliomuua Mwangosi walikuwa wafuasi wa Chadema!
Masikini watawala wetu, hawakujua kuwa Mwenyezi Mungu kamwe hachezewi na damu ya mtu mnyonge haimwagiki bure. Mpiga picha mashuhuri Joseph Senga na mwandishi Abdallha Khamis wa gazeti hili, wakachukua picha za tukio zima bila kubainika na Kamuhanda na wakubwa wenzake wakaumbuliwa!
Kana kwamba hiyo, haitoshi, serikali pamoja na vilio, malalamiko, maoni, wosia na kila aina ya neno jema kutoka kwa wananchi wakiitaka kuchukua hatua dhidi ya Kamuhanda na pia kukomesha vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji ya waandishi wa habari na raia, ikasimama bila kujali kamwe na kutoa pongezi na sifa lukuki kwa Kamanda huyu!
Katika Bunge hili hili linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, akisahau kabisa wala kujali kwamba ni yeye aliyedamka asubuhi kuwahi na kutaka kuungana na waandishi wa habari katika maandamano ya kupinga mauaji ya Mwangosi, alisimama na kumsifia Kamuhanda eti kama mmoja wa makamanda watenda kazi wazuri.
Nchimbi  hakujali kipigo kikali alichopewa Daud Mwangosi toka kwa maafisa wa polisi mbele ya Kamuhanda kabla ya kuuawa kikatili! Waziri Nchimbi hakujali kutamka haya akitambua kuwa mjane wa Mwangosi bado ana uchungu mkubwa wa kuuawa kwa mumewew! Nchimbi hajali wala hakuguswa na huzuni na simanzi za watoto wa Mwangosi waliolazimishwa kuwa yatima kutokana na utendaji wa kipuuzi wa polisi wale chini ya usimamizi wa Kamuhanda!
Waziri mwingine, William Lukuvi, wa serikali hii hii ya CCM, kama shabiki wa soka naye akaruka kimanga na kudakia hoja hiyo. Akasukuma kwa madaha, tabasamu na bashasha kubwa pongezi nzito kwa Kamuhanda!  Watanzania wakashuhudia mawaziri Wakiungwa mkono kwa makofi ya mezani na baadhi ya wabunge wa chama hicho (sio wote maana najua wengine walibaki wameduwaa wakiwashangaa mawaziri hao na wenzake)
Imeniuma na sio mimi tu, bali wengi kuona kwamba serikali na katika hali ya sasa ambayo imekuwa ikishindwa kujibu hoja nyingi zinazohusiana na vitendo vya kikatili kwa waandishi, wanaharakati, wanasiasa na raia wanyonge, inatonesha kidonda kwa kumpa ulaji Kamuhanda.
Kwamba serikali imeshindwa kabisa kujali sauti na mawazo ya watanzania kuhusiana na mauaji haya ya Mwangosi! Inatuambia kwamba mawazo yooote yalikuwa ya kipuuzi na kelele za mlango ambazo hazimnyimi mwenye nyumba usingizi?
Tuwe wakweli, naomba niwaulize kwa upole na upendo mwingi enyi waheshimiwa na wateule wa Mungu kupendekeza kupandishwa cheo kwa Kamuhanda; tuseme ingekuwa Mwangosi ni mtoto wenu, mdogo wenu, mkwe wenu, ama mpwa wenu, mngempa ulaji huu?
Tuache hilo, tuchukue mfano mwingine. Enyi mlioshiriki kumpongeza Kamuhanda ambaye alikuwa hatua chache na alipokuwa akila kipondo  Mwangosi, na mkajua kuwa alifuatwa akaambiwa anayepigwa ni mwandishi wa habari, lakini hakujali, badala yake akafunga dirisha la gari na kuendelea kuangalia ‘sinema’ hiyo katili; hivi marehemu angekuwa ni Kada wa CCM, angepandishwa cheo na kuingia katika ‘hansad’ za bunge kwa kupongezwa?
Kwa kumpa cheo Kamuhanda, serikali itakuwa na ubavu gani sasa wa kusema hadharani kuwa iko madarakani kwa ajili ya maendeleo ya watu? Itakuwa na nguvu gani ya kudai kuwa inajali, kulinda na kutetea uhai na maisha ya watu? 

No comments:

Post a Comment