Polisi Dar wamvamia
Mbowe usiku wa
manane
·
Walibeba
silaha za moto
·
RPC,
RCO wageukana
·
CDM
wamvaa JK, Mwema
Na
Waandishi wetu
KUNDI la Polisi wenye silaha za moto, jana usiku
walivamia nyumbani kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Freeman Mbowe, kwa nia ya kumkamata.
Askari hao wanaikisiwa kufikia saba wakiwa na
silaha nzito katika gari la wazi, waliwasili nyumbani kwa Mbowe majira ya saa
saba na nusu usiku, na kuwaamuru askari wanaolinda nyumbani kwake, kumtoa Mbowe
nje ili waonane naye.
Walinzi wa Mbowe walihoji uhalali wa ukamataji huo
na kuwataka polisi wawaoneshe hati ya kumkamata, lakini hawakuweza kuionesha,
hali iliyozusha wasiwasi kwa walinzi wa
kiongozi huyo.
Hata hivyo, walinzi hao waliwaambia polisi hao
kuwa Mbowe ambaye pia ni kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alikuwa
safarini, jibu lilipokelewa kwa shingo upande na askari hao.
Polisi hao baada ya kuona wameshindwa kukamilisha
kazi hiyo, waliwaachia walinzi hao namba ya simu 0754-085600 ya Mkuu wa Upelelezi
Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Ernest Kimola, wakiwaagiza kuhakikisha
wanamwambia Mbowe awasiliane na kamanda huyo.
RCO,
amsukumia RPC, akana
Hata hivyo, alipohojiwa na Tanzania Daima Jumapili
kwa njia ya simu, mkuu wa upelelezi Kimola aligoma kuzunguzia suala hilo na
kumtaka mwandishi kuwasiliana na mkuu wake wa kazi ambaye ni kamanda wa polisi
mkoa wa Kinondoni, Kamilius Wambura
akidai ndiye mwenye haki ya kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.
“Unajua mimi sio msemaji wa polisi, wasiliana na
kamanda wa mkoa maana ndiye mwenye uwezo wa kutoa maelezo” alisema Kimola na
kukata simu. Lakini, alipopigiwa simu,
Kamanda Wambura aliruka kimanga kwa mshangao akidai kutojua lolote kuhusiana na
polisi kuvamia nyumbani kwa Mbowe.
“Kwa kweli ndiyo napata taarifa hizo kutoka kwako
kama kiongozi huyo alifuatwa na polisi maana silijui suala hilo hata kidogo,”
alisema Wambura, naye kama alivyofanya Kimola akakata simu.
Kauli
ya Chadema
Lakini wakati Kimola akikataa kusema chochote,
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbord Slaa alisema kuwa alizungumza kwa njia ya
simu na Kimola kuhusiana na kitendo cha polisi kuvamia nyumbani kwa kiongozi
huyo wa juu wa kisiasa, na kudai kupewa majibu ya kushangaza.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Manzese, wilaya ya Kinondoni, Dk Slaa alisema Kimola alijitetea
akidai kwanza kukana kufika nyumbani kwa Mbowe usiku wa manane. Pili, alisema
kuwa hawakwenda kumkamata Mbowe, isipokuwa kufanya naye mazungumzo na kisha
wangemwacha.
Slaa alisema kitendo hicho kimewashitua na ni cha kinyama
na kilichokiuka sheria za nchi na haki za binadamu. Aliongeza kwamba, daima
wamekuwa wakilishutumu jeshi la polisi kwa kutumika vibaya kukandamiza
wapinzani, lakini mara zote Chadema kimepuuzwa na sasa jeshi hilo limeamua
kuvamia makazi ya viongozi wa kisiasa kwa madhumuni yasiyoeleweka.
Alisema, haijulikani nini kingetokea ikiwa Mbowe
angekuwa ndani, ikiwa walinzi wangeamua kugoma kumwachia kiongozi wao. “ Tuna
hofu kubwa na usalama wetu, maana pale wangeweza kufanya lolote na hata kumuua
na kisha kutoa matamshi kuwa walikuwa wanajibishana kwa risasi kama ambavyo
imekuwa jadi ya askari polisi kutoa taarifa za uongo na upotoshaji wanapoua
watu” alisema Slaa.
Alisema ikiwa polisi walikuwa na shida ya kweli,
wangemwita kwa njia sahihi na sio kumvamia na kuingilia uhuru wake na wa
familia yake kama wanakamata gaidi ama jambazi hatari.
Dr Slaa alisema Mbowe anayo ofisi inayojulikana,
na kama kweli hakukuwa na jambo baya lililopangwa na polisi hao, wasingeweza
kufanya uhuni kama walioufanya.
“Kama wanaweza kuvamia nyumbani kwa kiongozi
mkubwa kama Mbowe wakiwa na silaha nzito, itakuwaje kwa viongozi wa kawaida na
raia” alisema Slaa.
Kutokana
na tukio hilo la kuogofya, Chadema imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza
watanzania maana ya matukio haya ambayo yamedhamiria kuleta vurugu kubwa
nchini. Kadhalika, wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema
kuueleza umma kile kilichokusudiwa na askari wake kuvamia nyumbani kwa Mbowe
mithiri ya jambazi.
Itakumbukwa
pia kuwa hivi karibuni, askari polisi wa mkoa wa Arusha walivamia nyumbani kwa
Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema wakiwa na silaha nzito na mbwa, na
kumkamata kisha kumtupa lumande kwa siku nzima.
No comments:
Post a Comment