WAMILIKI wa Malori nchini wamesema kuwa Serikali imepata
hasara ya sh bilioni 20 hadi 30 kufuatia kusitishwa kwa huduma kwa madai ya
kulinda barabara zisiharibike.
Mbali na hasara hiyo wamiliki hao wamemuomba Rais Jakaya
Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhakikisha wanamchukulia hatua za
kinidhamu Waziri wa Ujenzi John Magufuli kutokana na kupotosha suala hilo na
kutoa maneno yasiyo na busara kwa Watanzania
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam, kwa niaba ya wenzake mwakilishi wa wamiliki wa malori, Azim Dewji,
alisema kuwa Serikali imepoteza mapato hayo kutokana na uwongo wa kiongozi
mmoja.
Dewji alisema kuwa hasara waliyoipata wamiliki hao ni kubwa
na sasa wapo katika kufanya mahesabu ili kubaini hasara hiyo ikiwa ni pamoja na
kumchukulia hatua za kisheria Dk Magufuli na kumfungulia mashtaka.
“Serikali tu imepoteza zaidi ya bilioni 20 na mama lishe
nayo wameshindwa kufanya kazi zao huko bandarini ni ajabu kuwa na kiongozi
anayetesa Watanzania kutokana na uwongo wake,” alisema
Mkurugenzi huyo wa makampuni ya malori ya Simba, alisema
kuwa wamiliki wa mamlori wamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wan chi na
wametoa ajira kubwa kwa Watanzania.
Alisema kuwa kwa kipindi cha siku mmoja malori zaidi ya
1000 yamekuwa yakifanya safari nchini na kuingiza fedha nyingi kwa Serikali.
Alisema kuwa ni muhimu Dk Magufuli akatoa maneno yenye
hekima na busara na sio kutumia mabavu na kutoa maneno ya kejeli dhidi ya
Watanzania.
Mmiliki huyo alisema kuwa kiongozi huyo amewadhalilisha kwa
kueleza kuwa wamekuwa wakitoa rushwa kwa wafanyakazi wa mizani jambo ambalo
halina ukweli wowote.
“Hivi kama sio uwongo na upotoshaji unaofanywa na kiongozi
huyo ni nini…hivi kweli ni mfanyabiashara gani aliyetayari kutoa rushwa ya
fedha kwa vituo vya mizani zaidi ya 14 vilivyopo katika Dar es Salaam hadi
Tunduma na anayeshindwa kuangalia faida,” alihoji
Mmiliki huyo alisema kuwa ni vyema kiongozi huyo akatumia
vyombo vya dola kufanya uchunguzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu barabara
kuliko kutoa kauli za ubabe na za kupotosha.
Alisema kuwa fedha ya faini ya kuzidisha mzigo haizidi sh
elfu 50,000 hivyo hakuna mfanyabiashara anayeshindwa kutoa kiwango hicho.
Dewji alisema kuwa kutokana na kupotosha umma juu ya tozo
hiyo ni vyema Rais Kikwete akamuondoa waziri huyo katika baraza lake na
kumrudisha kufanyakazi za chama.
“Dk Magufuli anafaa sana kufanyakazi za propaganda katika
chama chake naamini nafasi hiyo ataimudu vyema na ndiyo inayomfaa kuliko kuwa
waziri kwa kuwa amemdanganya Waziri Mkuu Pinda juu ya suala hili,” alisema
Alisema kuwa kiongozi ni mtu anayepaswa kusaidia watu na
sio kutoa kauli za kukomesha Watanzania.
Alisema kuwa Dk Magufuli amekuwa na chuki na wamiliki wa
malori baada ya kubaini kuwa walikutana na Kamati ya Miundombinu kipindi cha
Bunge na kueleza changamoto zinazowakabili.
Waziri Mkuu Pinda juzi aliagiza wamiliki wa malori
kuyaruhusu magari yao yasafirishe mizigo kwa utaratibu wa zamani.
Siku kumi zilizopita Dk Magufuli , alitangaza kuanza
kutumika kwa kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 2001.
Sheria hiyo inayataka malori yote yanayozidisha uzito
uliopo ndani ya asilimia tano kupunguza mzigo, kupanga mzigo upya au kulipia
uzito uliozidi mara nne ya tozo ya kawaida.
Mwisho
No comments:
Post a Comment