KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), kimewataka wabunge na wadau wengine watakaoshiriki katika bunge la
katiba kufuta ibara ya 69 ya rasimu inayompa rais mamlaka ya kuidhinisha
utekelezwaji wa adhabu ya kifo.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen
Kijo-Bisimba alisema hayo alipokuwa akitoa tamko kwa vyombo vya habari katika
maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani.
Dk. Bisimba alisema, wabunge hao
wanapaswa kuwezesha katiba ijayo kutoa ulinzi wa uhakika kwa haki ya kuishi
kama nchi za Msumbiji, Rwanda, Burundi, Angola na Namibia zilivyofanya.
“Hii ni kutokana na ukweli kuwa adhabu
hii imeshindwa kukomesha au kuondoa kabisa makosa yanayohukumiwa kwa adhabu
hiyo,” alisema.
Mkurugenzi huyo pia alishauri kujifunza
kutoka kwa nchi nyingine duniani ambazo hazitekelezi adhabu ya kifo, jinsi gani
zimekuwa zikishughulikia watu wenye makosa makubwa kama ya kuua.
Alipendekeza wale watakaokutwa na hatia
kutokana na makosa ambayo walipaswa hukumu ya kifo, wafungwe katika gereza
maalum, na uanzishwe mfuko wa kuhudumia watoto wa familia za wale wote
walioathirika kwa ndugu zao kuuwawa na hao wafungwa.
“Fedha hizo zigharamie matunzo na elimu
ya waathirika wa vitendo vya wauaji,” alisisitiza.
Vile vile alishauri kuwa, sheria ya
kiwango cha chini cha adhabu irekebishwe ili jaji asilazimishwe kutoa adhabu ya
kifo kwa kila mtu atakayepatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifo.
Awali alisema kwa miaka 19 sasa adhabu ya
kifo haijatekelezwa hapa nchini ijapokuwa watu wengi wameendelea kuhukumiwa
adhabu hii kwa makosa ya mauaji ya kukusudia.
Pia alisema tangu Tanzania ipate uhuru
1961 hadi sasa watu 238 wamenyongwa na idadi ya watu waliohukumiwa kunyongwa
imeongezeka kutoka watu 46 mwaka 1961 kufikia 2562 mwaka 2007.
Alisema, kituo hicho kinapinga utekelezwaji
na uwepo wa adhabu hiyo kwenye sheria za nchi, kwani pamoja na kuwa inakiuka
haki ya kuishi, lakini ikumbukwe kuwa hakuna nchi au mtu mwenye haki ya
kuchukua au kukatisha maisha ya binadamu.
No comments:
Post a Comment