MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Mkoa wa Arusha ambaye amesimamishwa uongozi kwa tuhuma za usaliti,
Samson Mwigamba, amesema kuwa hakupigana na Mwenyekiti wa Taifa wa chama
hicho, Freeman Mbowe, kama ilivyodaiwa na baadhi ya magazeti.
Mwigamba alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari jijini hapa kuelezea kile kilichojiri mwishoni mwa wiki
hadi akapigwa na baadhi ya wajumbe wa kikao, wakimtuhumu kwamba aliandika
taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums akizungumzia
masuala ya uongozi ndani ya chama.
Mwigamba alisema kuwa hata wakati akivutana na
walinzi wa chama Mbowe hakuwa ndani ya chumba cha mkutano, hivyo akadai kuwa
anashangazwa na wale waliosambaza taarifa hizo kwamba alipigana na kiongozi
huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni.
Aliwataja wale aliodai walimpiga kuwa ni Katibu wa
Bavicha Wilaya ya Arusha, Noel OLovaroya, walinzi wa chama pamoja na Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwamba alijaribu bila mafanikio kumpiga na
kitofali ambapo alikikwepa kwa kujiangusha chini na kujigonga kisogoni.
“Wakati vurugu zikianza Mbowe hakuwa ukumbini,
nilimuona akija Lema na Olevaroya, ambapo Lema alishikwa kabla hajanifikia
huku Olevaroya akiruka juu ya meza na kuja kunipiga ngumi, mimi kwa kujitetea
ilibidi nimpige ngumi kabla hatujaamuliwa,” alisema.
Mwigamba alimtuhumu Lema kuwa amekuwa akimtishia
kumuua kwa kipindi kirefu, ambapo siku ya tukio alirudia kauli hiyo kabla
hajaenda kuchukua kitofali na kujaribu kumpiga nacho ambapo alikikwepa.
Alisema kuwa tayari alishatoa taarifa polisi na
kupewa kumbukumbu: AR/RB/1759/2013 aliyoifungua Februari 12, mwaka huu, baada
ya kuwa anapokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa Lema kupitia simu yake ya
kiganjani.
Kuhusu kusimamishwa uongozi, Mwigamba alisema kuwa
ametii licha ya kuwa kikao kilichomsimamisha hakina mamlaka kisheria, huku
akiweka wazi kuwa hayuko tayari kukihama chama hicho, kwani bado anaamini
ndicho chenye uwezo wa kuleta mabadiliko nchini.
Hata hivyo, tuhuma za Mwigamba zilikanushwa na
Katibu wa CHADEMA wa mkoa, Amani Golugwa, akisema ni uongo dhidi ya Lema,
kwani kwenye taarifa yake aliyowasilisha juzi kwenye kikao cha uongozi wa
kanda alimsifu mbunge huyo kwamba ameongoza harakati mbalimbali za ujenzi wa
chama kwa mafanikio makubwa, zikiwamo kampeni za ushindi wa kata nne
zilizofanya uchaguzi mdogo hivi karibuni.
“Kwa kipindi chote ambacho amekuwa hayuko kazini
Lema amekuwa akimsaidia hata kukamilisha ujenzi wa nyumba yake maeneo ya
Sokon 1, hata anavyokwenda kwenye kesi zake Dar es Salaam ni Lema amekuwa
akimsaidia gharama.
“Hicho alichokizungumza kwenye mkutano wake juu ya
malalamiko ndiyo anatudhihirishia kuwa amekuwa nyoka na mnafiki ndani ya
kundi letu,” alifafanua katibu huyo huku akisema hakuna malalamiko yoyote juu
ya suala hilo ndani ya chama.
Golugwa aliongeza kuwa baada ya kupitia kompyuta ya
Mwigamba wamebaini mambo mengi machafu na ya hatari kwa mustakabali wa chama
ambayo yanawagusa watu wengi.
Hata hivyo hakutaka kuingia kwa undani wala
kuyafafanua akisema yatakisaidia chama katika uchunguzi wake zaidi, na kwamba
tayari kikao cha Baraza la mkoa kimeshakaa na kimemwandikia Mwigamba barua ya
ajieleze ni kwa nini asivuliwe uongozi ikiwa ni sehemu ya mchakato wa
kulifikisha suala hilo mbele ya kikao cha Kamati Kuu ya Taifa.
|
NDOA YANGU, Ningejua!
MWIGAMBA: SIKUPIGANA NA MBOWE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment