Afisa ‘feki’
usalama wa taifa adakwa
JESHI la polisi linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za
utapeli na wizi huku mmoja akikutwa na kitambulisho cha usalama wa taifa.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema kuwa watu hao
walikamatwa kutokana na juhudi zilizofanywa na jeshi la polisi.
Kamanda Wambura alisema kuwa watu hao walikamatwa juzi
usiku katika maeneo ya Kawe ambapo walikutwa na kadi mbalimbali za benki
zinazosadikiwa kuporwa katika matukio mbalimbali.
Alisema kuwa mbali na kadi za benki walikutwa na laini za
M- Pesa, Tigo –Pesa na Airtel Money ambazo zinadaiwa kutumika katika kutapeli
watu.
Alidai kuwa watu hao hutongoza kina dada na kuahidiana nao kukutana
ambapo huwawekea dawa katika vinywaji na kisha huwalewesha na kuwapora kila
kitu.
Alisema kuwa baada ya kuwalewesha wadada hao huwalazimisha
kutaja namba za siri za kadi zao za benki na hutumia nafasi hiyo kwenda kukomba
fedha yote.
Kamanda Wambura alisema kuwa mbali na kuwalewesha wamekuwa
wakiwatumia kwa shughuli nyingine na hata kuwabaka.
“Hili ni kundi kubwa na tunahofu kuwataja majina hadharani
kwa kuwa tutashindwa kuendelea na upelelezi lakini hawa ndiyo wanatusaidia
kulibaini kundi hilo na inaonekana wamefanya vitendo vingi vya kitapeli na
wizi,” alidai
Alisema kuwa wameghushi kitambulisho cha usalama wa taifa
ili kupata urahisi wa kuwatongoza wanawake hao.
“Hiki kitambulisho ni cha kughushi maana inaonyesha
wamekuwa wakikitumia kuwalaghai wakina dada na wamekuwa wakirubunika na kujikuta
mikononi mwa vijana hao ambao huwafanyia mambo ya udhalilishaji,” alidai
Mwisho
No comments:
Post a Comment