Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

MICHEZO




Mzazi wa Kiemba aja juu
Na Bilal Soud
BABA  Mzazi wa Kiungo mahiri wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars  Amri Kiemba aliejitambulisha  kama  Tano Ramdhani almaarufu (Shungo), amesema kua Simba inambania kijana wake kucheza soka la kimataifa.
Akiongea na gazeti hili jana asubuhi posta, shungo amedai kua timu ya simba imekua ikiweka vikwazo vya kutomruhusu kijana wake kucheza  soka la kulipwa nje ya nchi, hii inatokana na ukweli kwamba kijana wake huyo alihitajika na timu ya Moroko iitwayo FAR Rabat.
Akithibitisha hayo Shungo anasema kwamba simba walikataa ofa hiyo na wamekuwa wakitumia mbinu  ya kuweka dau kubwa ili kukwamisha usajili huo, imedaiwa simba wamehitaji kiasi cha sh milioni 250 kwa timu itakayo hitaji huduma ya kiungo huyo.
Akitilia mkazo kauli yake alisema “ Amri Kiemba amekua wa kwanza kuhitajika kabla ya  Shomari Kapombe laikni nashangaa kuona Kapombe akiruhusiwa na kuondoka kwenda Uholanzi kwa majaribio na mwanagu akibaki kaika tetesi tu inauma sana.”
Kiemba ni fauda kwa Tanzania hivyo kucheza kwake soka la kimatifa litampaizoefu wa kutosha na kupausha jina la nchi yetu hivyo Simba watumie malalamiko haya kupitia vizuri maamuzi yao.
Mwisho



Yanga kuanika
vifaa vipya leo



MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga, leo wanatarajia kutambulisha nyota wake wawili wa kimataifa kupitia mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Nyota hao wamekuja kuziba nafasi ya Mzambia Davies Mwape na Mghana Keneth Asamoah waliotemwa hivi karibuni, hivyo Yanga kubaki na nyota watatu wa kimataifa, Mghana Yaw Berko, Mrwanda Haruna Niyonzima na Mganda Hamis Kiiza.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu,
alisema nyota hao wapya ambao hakupenda kuwataja, wataonekana katika mechi
hiyo ya kirafiki ambayo ni kipimo kwa wakali hao wa Jangwani kabla ya Kagame.

Mechi hiyo inafanyika kutokana na ombi la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Seintfiet, akitaka kupima kama vijana wake wameshika mafunzo aliyowapa kwa siku tano kuanzia Alhamisi iliyopita.  
Kuhusu nyota hao wapya, Sendeu alisema ni mapema mno kutaja majina na wanatokea wapi, akiwataka wapenzi na mashabiki wa soka kujitokeza kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kujionea nyota hao na ubora wa kikosi hicho kwa ujumla.

“Siwezi kuwataja  majina wala wanatoka wapi, lakini ukweli ni kwamba kesho (leo)
 ndio tutawaweka wazi nyota wetu wawili wa kimataifa watakaoziba nafasi za Mwape
na Asamoah,” alisema Sendeu.

Sendeu aliongeza kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na amewataka wapenzi na mashabiki kujitokeza kwa wingi jioni ya leo kujionea wenyewe uwezo wa kila mchezaji, wasisubiri kuhadithiwa.
Aidha, mechi hiyo itakuwa wa kwanza kwa kocha huyo mpya Mbelgiji, Saintfiet tangu ajiunge nayo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa mkataba wa miaka miwili akirithi mikoaba ya Mserbia Kostadin Papic.

Saintfiet aliyeikuta timu hiyo ikijiandaa na michuano ya Kombe la Kagame itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa na Chamazi, jijini Dar es Salaam, anakabiliwa na mtihani wa kutetea taji hilo ililolitwaa Julai 10, 2011.

Yanga iliyo kundi C, lenye pia timu za APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini,  itaanza kampeni yake siku ya ufunguzi wa michuano hiyo, Julai 14 dhidi ya Atletico ya Burundi.
Katika hatua nyingine, mratibu wa mechi hiyo, Salum Mkemi, kiingilio cha chini kitakuwa ni sh 3,000 kwa viti vya kijani na bluu; viti vya   rangi ya chungwa sh 5000; VIP B na C ni sh 10,000 na VIP A watalipa sh 15,000.
                                               

Kocha Yanga
afagilia amani 


KOCHA mkuu wa timu ya Yanga, Mbelgij Tom Seintfiet, amefurahishwa
na tunu ya amani iliyopo Tanzania kiasi cha viongozi wakubwa kuwa karibu zaidi na raia wao.
Tom aliyasema hayo juzi alipozungumza gazeti hili katika Uwanja  wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati wa mechi iliyowakutanisha wabunge mashabiki wa Simba na Yanga iliyochezwa uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo ambayo iliisha kwa Simba kushinda kwa penalti 3-2, ilikuwa
ni maalumu kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana nchini chini ya uratibu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Alisema, amefurahia hali ya umoja na amani iliyopo nchini tofauti na nchini nyingine ambapo si rahisi kuona raia wakiwa karibu na viongozi wakubwa kwa kiwango alichojionea Tanzania.
 “Nimefurahi sana kuona umoja na amani ya kiwango hiki katika nchi hii, naamini hata kazi yangu ya kufundisha soka itafanyika vizuri kutokana na mshikamano mkubwa uliopo kuanzia kwa wakubwa wa nchi,” alisema.

Kuhusu kiwango cha wabunge, Tom alisema Tanzania ni nchi iliyo na
vipaji vingi vya soka, kwani kwa mazingira halisi ya wabunge na umri, hakutarajia kama wangecheza kwa kiwango alichokishuhudia.

Alisema kwa kiwango chao, kama wangekuwa na mazoezi ya mara
kwa mara kama ilivyo kwa wachezaji ambao soka ni kazi, wangetisha zaidi huku akisifu uwepo wa mechi za aina hiyo.
                                         

Wabunge Simba
sasa nyodo tupu 

NYODO, Vijembe na Majigambo, jana vilitawala bungeni wakati Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipowaambia wabunge wenye mapenzi na Yanga, wavumilie vichapo kutoka kwa watani zao Simba.
Ngudai alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia kipigo cha mabao 3-2 walichopata wabunge ambao wapenzi wa timu ya soka ya Yanga kutoka  wenzao wa Simba.

“Tulichowafanyia Jumamosi pale uwanja wa Taifa, ni  mwendelezo wa utaratibu wa kawaida wa kutoa dozi kwa mwaka 2012, vumilieni,” alisema.

Kiongozi huyo ambaye ni kati ya mashabiki wa Simba, alisema amepata vikaratasi kutoka kwa Mbunge wa Donge (CCM), Sadifa Juma Khamis, kuwa mechi hiyo iliyochezwa irudiwe.
 “Wametaka mechi ile irudiwe na kwamba wachezaji wa Simba walikuwa wamechoka, hivyo walikuwa wakijiangusha hovyo na kumrubuni refa,” alisema.

Alisema wamemtaka atoe uamuzi (rufaa) juu kipigo walichokipata ambacho kimewafanya wasuesue kufika bungeni kutimiza wajibu wa kuwawakilisha wananchi.

Ndugai aliwapongeza wabunge wote walioshiriki katika mechi hiyo akiwemo Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, kwa kupangua mipira kutoka kwa wabunge wa Yanga.
Aidha, alimpongeza Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makala.

Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Neema Hamid, alipongeza Nahodha wao Makala ‘Boban’ kwa kuonesha uwezo mkubwa katika mechi hiyo akiwachambua wapinzani wao na kutoa pasi murua.
“Kipigo tulichowapa kimewapa funzo, siku nyingine watajua sisi ni
wakali, poleni sana watani zetu,” alisema
                                                      




Usagaji waitesa
 Twiga Stars
.Madina agoma kujiuzulu

Na Ruhazi Ruhazi

KASHFA ya vitendo vya usagaji iliyoibuliwa hivi karibuni katika timu ya soka ya Wanawake, Twiga Stars, inawaumiza vichwa viongozi wake.
Baada ya timu hiyo kukosa tiketi ya fainali za Afrika, waking’olewa na Ethiopia kwa mabao 3-1, kukawa na madai kuwa, baadhi ya nyota wamekuwa wakifanya vitendo hivyo.  
Kutokana na tuhuma hizo kuibuliwa wakati ambao timu imefanya vibaya huku wachezaji wakicheza kiwango cha chini, madai hayo yakapata nguvu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha soka la Wanawake (TWFA), Madina Case, alisema madai hayo si ya kweli, ni uzushi mtupu.
Akiungwa mkono na Meneja wa timu hiyo, Furaha Francis na aliyekuwa Kocha wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa, Madina alikanusha kuwepo kwa vitendo hivyo.
Madina alisema kwa vile jambo hilo ni uzushi, limewaumiza wachezaji, viongozi na kuliumiza soka ya wanawake kwa ujumla mbele ya jamii.
Alisema tuhuma hizo sio tu zinawapaka matope wachezaji na viongozi wake, pia zinahatarisha ustawi wa soka ya wanawake kwani wazazi watagoma  kuwaruhusu watoto wao kucheza soka.   
Alisema, licha ya Twiga Stars kucheza kiwango cha chini, akiwa kiongozi mkuu wa soka la wanawake nchini, bado haoni sababu ya kuachia ngazi.
Madina alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kwa nini asijiuzulu kutokana na timu hiyo kufanya vibaya huku kukiwa hakuna mfumo rasmi wa mashindano.
Mkwasa alisema, awali alinukuliwa vibaya kuhusu suala hilo alipohojiwa na moja ya kituo cha televisheni.
“Ukifuatilia mahojiano yangu…mimi sikusema
 kuna vitendo hivyo. Tatizo nadhani lilianzia pale jambo hilo lilipoendelezwa na magazeti.
“Hata kujiuzulu kwangu, hakuna uhusioano na jambo hilo, niliwajibika katika mazingira ya kawaida tu kutokana na matokeo mabaya,” alisema Mkwasa.
Naye Furaha Francis alisisitiza kuwa, hakuna vitu vya aina hiyo katika timu hiyo na kama kuna mtu ana ushahidi wa hilo, ajitokeze.
“Madai juu ya vitendo vya usagaji, vimetuchafua sana. Tunaomba kama kuna mtu ana ushahidi wa jambo hili, atueleze kuliko kuendelea kutuchafua,” alisema.
                         
Mwisho

Yanga  yapeleka
‘chekechea’ Zenji

Na Dina Ismail

WAKATI kiungo wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima, akitua nchini jana, safari ya vigogo vya soka nchini Simba na Yanga kwenda Zanzibar kwa michuano ya Kombe la Tanzania ‘Urafiki,’ imegubikwa na utata mwingi.
Kundi la kwanza la Simba liliondoka jana asubuhi kabla ya  wengine kufuatia jioni, wenzao Yanga kuamua kupeleka kikosi cha pili.
Ingawa awali Yanga waligoma kushiriki michuano hiyo kwa hoja ya kuhofia majeruhi kuelekea michuano ya Kagame, juzi jioni walithibitisha ushiriki wao.
Simba chini ya Kocha wake Milovan Cirkovic na Yanga chini ya Fred Felix Minziro, zinasaka makali ya Kombe la Kagame litakaloanza Julai 14 hadi 28.
Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema mapema jana mchana kuwa, kikosi kingeondoka
jioni ya jana.
Hata hivyo, Sendeu alidai pia kikosi cha Yanga kingefanya mazoezi jioni ya jana kwenye Uwanja wa Kaunda akiwemo Niyonzima aliyetua akitokea kwao Rwanda.
Kauli hizo mbili tofauti za Sendeu, zilionekana
kuleta utata na alipobanwa juu ya timu ipi ingekwenda Zanzibar na ipi ingebaki Kaunda, akaonekana kubabaika kabla ya kusema apigiwe simu baadaye.
Kuhusu Niyonzima, Sendeu alisema nyota huyo alichelewa kutokana na matatizo binafsi nchini kwao Rwanda.
Yanga, mabingwa watetezi wa michuano ya Kagame wataanza kampeni Julai 14 dhidi ya Atletico ya Burundi katika kundi C, huku Simba wakianza na URA ya Uganda.
Habari kutoka Simba, zinasema baadhi ya wachezaji walikatwa kwenye kikosi hicho bila ya sababu ya msingi, hivyo baada ya viongozi kuingilia kati, timu hiyo iliondoka jioni kwenda Zanzibar.
Simba ilitarajiwa kuanza kampeni ya michuano hiyo jana jioni kwa kucheza na Mafunzo ya huko.
Hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa Simba aliyepatikana kuzungumzia suala hilo hadi tunakwenda mitamboni.
                   
Mwisho



Mchina kuwanoa makocha wa wavu Dar

Na Clezencia Tryphone, Kibaha

MKUFUNZI Chuanlun Liu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Wavu (FIVB), anatarajiwa kuendesha kozi ya mchezo huo kwa makocha wa Tanzania Bara na Visiwani itakayofanyika kuanzia Juni 30 hadi Julai 8 mwaka huu ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM).

Akizungumza na Tanzania Daima mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA), Agustino Agapa alisema, kozi hiyo inatarajiwa kushirikisha walimu 35 kutoka bara na visiwani, ikiwa na lengo la kuwajenga zaidi na kuwapa upeo katika kuujua zaidi mchezo huo.

Aidha, Agapa alisema, kozi hiyo ya kimataifa ambayo imeandaliwa na TAVA wakishirikiana na FIVB, itawashirikisha walimu hao kutoka shule za msingi na sekondari.

“Kozi hii ni muhimu kwetu na nina imani kubwa itawafanya walimu, kuzidi kupata mbinu na kuujua vema mchezo   huu ili uzidi kukua na kutamba katika nchi yetu,” alisema Agapa.
Aliongeza kuwa, hadi sasa washiriki 20 wamethibitisha kushiriki semina hiyo na kuwa, siku ya mwisho kuthibitisha ushiriki huo ni leo.





Baiskeli Taifa sasa Septemba

Na Elizabeth John

CHAMA cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), kimebainisha kuwa mashindano ya taifa yaliyokuwa yafanyike Juni 23 na 24 mwaka huu sasa yanatarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHABATA, Nazir Manji, mabadiliko hayo ni kutokana na ukosefu wa fedha, ambapo juhudi zinaendelea kuwaomba wafadhili wawasaidie.
Manji, alizitaka timu za mikoa ziendelee kufanya mazoezi hadi watakapoarifiwa upya tarehe ya mashindano na sehemu yatakakofanyika.
Kuhusiana na uchaguzi mkuu, alisema wamepeleka maombi Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kuomba maelezo ya taratibu za uchaguzi na watatoa taarifa baada ya kupata ushauri kutoka huko.
                 
Mwisho








Yondani atua Yanga, Okwi awatesa Simba

Na Mwandishi Wetu

WAKATI klabu ya Yanga ikitangaza rasmi kumsajili beki Kelvin Yondan kutoka Msimbazi, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, anaupa wakati mgumu uongozi wa klabu ya Simba kumbakisha kwa msimu ujao.
Kwa upande wa Okwi, klabu yake imekuwa ikijitahidi kumwekea wigo kwa kupitia dau kubwa kutokana na nyota huyo aliyepo kwenye kiwango bora, kumezewa mate na klabu nyingi.
Okwi aliyeifungia Uganda bao la kusawazisha dakika ya 87 katika mechi ya Jumamosi dhidi Angola, ameifanya Simba kumweka sokoni kwa dau tofauti ndani ya wiki moja.
Mei 30, Simba kupitia kwa Ofisa Habari wake, Ezekiel Kamwaga, Ilisema klabu itakayomhitaji Okwi, iwe tayari kutoa kitita cha sh bil 2; kumpatia mshahara mnono, pia isiwe klabu yenye mgogoro.
Mbali ya dau jipya lililotajwa jana na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, alisema watachukua hatua dhidi ya atakayemshawishi nyota huyo kwani ni mali yao.
Rage amesema Okwi na Yondan, wote ni mali ya klabu hiyo, wanaowataka wasubiri Juni 15, pale watakapotangaza wa kuwasajili, hivyo kuruhusu mazungumzo dhidi ya nyota wao.
Kuhusu thamani ya Okwi aliyezaliwa Desemba 25, 1992, Rage alisema, klabu inayomhitaji, iwe tayari kutoa Euro 500,000 sawa na sh mil 950 za Tanzania.
“Thamani ya Okwi ni Euro 500,000, na kila mmoja anajua anachokifanya dimbani, hadi sasa kuna mawakala watatu kutoka Uingereza, Serbia na Austria, wanamuhitaji kwa majaribio, tunajiandaa kuzungumza nao kujua tutafikia wapi,” alisema Rage.
Alisema, wakati mawakala wa Serbia na Uingereza wakionesha nia ya kumhitaji kwa majaribio, wakala kutoka Austria anamhitaji haraka zaidi kwa lengo la kuwahi usajili wa kiangazi hiki.
Rage alisema, pia kuna vijana watatu wa chini ya umri wa miaka 20 wanaotakiwa kwa majaribio nchini Ujerumani, akisema watalitolea ufafanuzi zaidi jambo hilo wakati ukifika.
Aidha, Yondan huenda akaingia katika jela ya soka baada ya kusainiwa na Yanga licha ya kusaini mkataba mpya na timu yake ya Simba.
Hatua hiyo inatokana na Yanga kupitia kwa Ofisa Habari wake, Louis Sendeu, jana kusema kuwa wamemsainisha nyota huyo kwa mwaka mmoja kwa thamani ya sh mil 30.
Nje ya dau hilo, Yondan atakuwa akilipwa mshahara wa shilingi 800,000 kwa mwezi na stahili nyinginezo.
Sendeu alisema wameamua kumsajili Yondan kwa mkataba utakaodumu hadi Machi 20, 2013 kutokana na ukweli kuwa, mkataba wa nyota huyo Simba umekoma tangu Mei.
Aliongeza, wamefuata taratibu zote zinazostahili kwa mujibu wa kanuni na sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ikiwemo kufanya naye mazungumzo kabla ya miezi sita.
Sendeu alisema, hawatayumba katika hilo, na hasa vitisho kutoka kwa viongozi wa Simba dhidi ya wachezaji wao wenye nia ya kujiunga na klabu nyingine.
Wakati Yanga wakisema hilo, Mwenyekiti wa Simba, Rage, jana alisisitiza kuwa Yondan ni mchezaji wao halali kwa mujibu wa kanuni na atakayemsajili, atakuwa anavunja kanuni na sheria za Fifa.
Yondan anazirejesha Yanga na Simba kwenye zama za kugombea wachezaji baada kujisajili na klabu mbili kama ilivyowahi kutokea kwa Victor Costa, Athumani Idd ‘Chuji’, Kenneth Assamoh, Amri Said, Mohammed Mwameja na Keneth Mkapa.



Kuiona Gambia ‘buku’ tatu Taifa

Na Dina Ismail

KIMA cha chini cha kushuhudia mechi ya kimataifa ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia mwaka 2014 kati ya timu ya soka ya Tanzania, Kili Taifa Stars na Gambia, itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ni sh 3,000.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kima hicho ni kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, huku kwa mashabiki wa viti vya VIP watalipa sh 30,000.
Wambura alisema, kiingilio kwa mashabiki watakaokaa viti vya rangi ya chungwa ni sh 5,000; VIP C sh 10,000; VIP B sh 20,000 na kuongeza kuwa, mechi hiyo itaanza saa 10.00 jioni.
Alisema tiketi hizo zitaanza kuuzwa keshokutwa kuanzia saa 2 asubuhi kwenye vituo mbalimbali, ikiwemo Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Soko Kuu la Kariakoo na Uwanja wa Taifa.
Aidha, siku ya mechi pia mauzo yatafanyika katika vituo hivyo na baadaye kuhamia Uwanja wa Taifa.
Kuhusiana na ujio wa Gambia, Wambura alisema kamati ya maridhiano inayoendesha Chama cha Soka Gambia (GFA) hadi leo mchana ilikuwa haijatuma taarifa rasmi kwao, ingawa kuna habari utakuwa msafara wa wachezaji 23 na viongozi tisa.
Kwa mujibu wa Wambura, kupitia vyombo vya habari vya nchi hiyo, Ofisa Habari wa GFA, Bakary Balder, alisema msafara wa timu hiyo utakuwa chini ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo, Malang Jassey.
Viongozi wengine ni Ofisa Utawala wa timu, Modou Sowe; Kocha Luciano Machini, makocha wasaidizi, Peter Bonu Johnson na Lamin Sambou; kocha wa makipa, Alhagie Marong; mtaalamu wa tiba mbadala (physiotherapist), Pa Matarr Ndow; mtunza vifaa, Sanna Bojang na daktari wa timu, Kalifa Manneh.
Wachezaji ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso, Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju, Yankuba Mal Ceesay, Demba Savage, Saihou Gassama, Alieu Darboe, Momodou Ceesay, Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh na Bubacarr Sanyang.
Wengine ni Christopher Allen, Musa Yaffa, Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.
Stars itakutana na Gambia iliyotoka kuvuna sare ya bao 1-1 na Morocco, ikiwa ni wiki moja tangu icheze na Ivory Coast, mjini Abidjan na kufungwa mabao 2-0, yakifungwa na Didier Drogba na Solomon Kalou.

                  Mwisho.





MKUU wa wilaya ya Handeni Muhingo Rweyemamu pamoja na mwanachama wa klabu ya Yanga Abdallah Binkleb jana wamechukua fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe katika uchaguzi wa klabu ya Yanga uliopangwa kufanyika Julai 15.

Katibu wa kamati ya uchaguzi ya Yanga  Francis Kaswahili alisema jana kwamba wanachama hao wanafanya idadi ya wagombea waliochukua fomu za kuwania nafsi mbalimbali za uongozi katika klabu hiyo kufikia  10 .

Alisema zoezi hilo ambalo lilianza jumamosi iliyopita limekuwa la kusuasua tofauti na ilivyotarajiwa hivyo amewaomba wanachama wa klabu hiyo wenye sifa kujitokeza kabla ya kufungwa Juni 6.

Mbali na hao wanachama wengine waliochukua fomu ni pamoja na John Jambele anayewania uenyekiti, huku Ayoub Nyenzi akiwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.

“Waliochukua fomu kuwania ujumbe wa kamati ya Utendaji mbali na Muhingo na Binkleb  ni  Isack Chandi, Jumanne Mwamwenye na Salehe Hassan,”alisema.

Uchaguzi huo unafuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Lloyd Nchunga  baada ya kushinikizwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na baraza la wazee wa klabu hiyo kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio klabu hiyo chini ya uongozi wake.

Pia nafasi ya Makamu mwenyekiti iliyokuwa inashikiliwa na Davis Mosha ambaye alijitoa miezi michache baada ya kuchaguliwa kutokana na kutoelewana na Nchunga, huku mjumbe Theonest Rutashoborwa akitangulia mbele ya haki.
 
Uchaguzi huo pia utajaza nafasi nne za Wajumbe  walioachia ngazi ambao ni pamoja na Mzee Yusuf, Charles Mgondo na Ally Mayay.Mpaka sasa  Yanga imebaki na wajumbe wanne, Mohammed Bhinda, Sarah Ramadhan, Tito Osoro na Salum Rupia.

Baada ya kufanyika kwa uchaguzi kamati ya utendaji itateua wajumbe wengine watatu kwa mujibu wa katiba, hiyo inatokana na wajumbe hao wa kuteuliwa Seif Ahmed, Mbaraka Igangula na Pascal Kihanga kujiuzulu.

mwisho
.



Dawa zamchelewesa Sajuki kurudi

Na Nasra Abdallah

BAADA ya kufanikiwa kufanyiwa upasuaji wa uvimbe uliokuwa ukimsumbua mwigizaji na muongozaji wa filamu nchini, Juma Kilowoko ’Sajuki’, imeelezwa kwamba dawa anazozitumia kwa sasa ndizo zinazomchelewesha kurejea nchini.
Rafiki wa karibu wa msanii huyo, Dennis Sweya ’Dino’, alisema dawa ambazo Sajuki anazitumia kwa sasa zina nguvu sana kiasi cha kwamba anatakiwa kuwa chini ya uangalizi maalumu wa wauguzi.
Dino alisema kwamba kadiri siku zinavyopita ndivyo Sajuki anavyoendelea vizuri na akawaomba Watanzania kuendelea kumuombea ili arudi nyumbani salama.
“Tunashukuru ndugu yetu Sajuki ameshafanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri sana kwa kweli hivi sasa hawezi kurudi kwa kuwa anatumia dawa ambazo ni lazima asimamiwe na wauguzi lakini hali yake inaimarika kila kukicha,” alisema Dino.
Alisema kuwa juzi mchana aliweza kuongea na Sajuki mwenyewe kwa simu na sauti yake ilikuwa yenye kuleta faraja ikiwa imeimarika sana kulinganisha na wakati alipoondoka.
Sajuki alikuwa katika hali ngumu ya kuumwa kutokana na uvimbe kwenye ini ambao ulimsababisha kupungua uzito na kutokana na kutokuwa na fedha za kugharamia matibabu nchini India ilibidi aombe msaada kutoka kwa wasamaria wema ambao walifanikisha.

Mwisho


Twanga kuzindua ‘amshaamsha’ Club Bilicanas

Na Khadija Kalili

BENDI ya Twanga Pepeta International  ‘Kisima cha Burudani’ imetangaza kuanzisha kampeni ya kujitangaza itakayokwenda kwa jina la ‘Amsha amsha ya Twanga’ itakayozinduliwa ukumbi wa Club Bilicanas jijini Dar es Salaam kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Asha Baraka, alisema, onesho hilo litaanza majira ya saa 3:00 usiku ambapo kiingilio kitakuwa ni sh 8,000 kwa kila mtu.
Asha alisema, wameamua kuanzisha kampeni hiyo, ambapo watakuwa wakipiga kwa mtindo wa ‘Non Stop’ hadi kunakucha.
Pia mkurugenzi huyo, alimtangaza msemaji mpya wa bendi, ambaye ni Muddy Pizaro, huku Hamisi Kayumbu ‘Amigolas’ akikamata mikoba ya meneja.
Aliongeza kuwa, bendi yake bado iko imara kama chuma na wanajivunia kuwa, wao ni sawa na shamba au mti wenye matunda, hivyo ni jambo la kawaida kwao kupopolewa.
“Sisi tulianzisha Twanga Academia, leo matunda yake yanaonekana tuna wanamuziki wengi, hivyo hatuwezi kutetereka katika muziki, kwa sababu jadi yetu hapa ni bandika bandua labda waninunue na mimi mwenyewe,” alisema.
Hivi sasa Twanga inatamba na wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la ‘Shamba la Twanga’ uliotungwa na Rapa Greyson Semsekwa na kutiwa nakshi na waimbaji wa bendi hiyo kwa ujumla.







Twiga Stars walia fitna Ethiopia
Na Clezencia Tryphone

BAADA ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ethiopia, timu ya taifa ya soka ya wanawake Tanzania ‘Twiga Stars’ imerejea jijini Dar es Salaam jana huku ikilia fitna ndiyo imewafanya wapoteze mchezo huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kurejea, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa, alisema kufungwa kwao kumetokana na fitna iliyosababisha mchezo kuwa mgumu.
Mkwasa alisema wachezaji wake walionekana kuondoka mchezoni baada ya kufanyiwa fitna nyingi ambazo hakutaka kuziweka wazi.
Alisema licha ya kufungwa lakini wanajivunia bao la ugenini na kwamba sasa kazi ni moja kujipanga ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi wa zaidi ya mabao 2 ili waweze kusonga mbele.
Aliwataka wachezaji wake, kujituma na kuongeza bidii katika mazoezi, ili kuepuka kufungwa kwenye uwanja wa nyumbani, Juni 16.
Mshindi katika mechi hiyo atafuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWC), zitakazochezwa Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

Mwisho





Makalla ajitoa Simba

Na Clezencia Tryphone

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla amejitoa katika Kamati ya Fedha ya klabu ya Simba na kuanzia sasa atakuwa akizisaidia timu zote hapa nchini.
Makalla alibainisha hayo juzi, katika sherehe za klabu hiyo kujipongeza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zilizofanyika ukumbi wa Dar Live Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Makalla, alisema, sababu ya kujitoa ni kutokana na wadhifu mkubwa alionao kwa sasa.
“Mimi nilikuwa ni mmoja wa viongozi waliokuwa katika Kamati ya Simba na kuchangia mafanikio haya ambayo Simba imeyapata, lakini kwa sasa kwa kuwa ni waziri, jukumu langu ni kusaidia timu zote nchini bila ya kujali Simba wala timu yoyote,” alisema Makalla.
Aliuasa uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, kutoridhika na mafanikio hayo na kuwaomba kuzidi kupigana kufa na kupona ili kuendeleza hali ya mafanikio ndani ya klabu hiyo na kujipanga ili kufanya vizuri zaidi.
Alisema ana imani kubwa klabu ya Simba ina uwezo mkubwa wa kujenga uwanja mzuri wa kisasa kutokana na ukongwe ambao inayo.
Katika sherehe hizo, Makalla akimkabidhi nahodha wa Simba, Juma Kaseja, tuzo na medali maalumu kwa ajili ya aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, marehemu Patrick Mafisango aliyefariki hivi karibuni kwa ajali ya gari, ambapo nahodha huyo alishindwa kujizuia na kuangua kilio na kuwafanya baadhi ya wachezaji wenzake, mashabiki na wapenzi kuanza kumwaga machozi.
Kabla ya kutolewa kwa tuzo hiyo, ulipigwa muziki wa ‘Kazi yake Mola Haina Makosa’ wa Msanii Madee kumkumbuka Mafisango na mara baada ya wimbo huo kumalizika, shughuli zote ukumbini hapo zilisimama kwa dakika moja na watu wote walisimama na kumwombea mchezaji huyo.
Naye Meneja wa Global Publishers Limited, Abdallah Mrisho, alikabidhi sh milioni 3 kwa Kaseja, kama zawadi yao kwa wachezaji na benchi la ufundi ikiwa ni pongezi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika msimu uliopita wa 2011/12 hadi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Sherehe hizo zilipambwa na wanamuziki na bendi mbalimbali hapa nchini, ikiwemo Msondo, Mshauzi Classic, Young D.



Sekretarieti Yanga yapewa rungu
Na Clezencia Tryphone

KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imebainisha kuwa, uteuzi uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya Yanga Mei 21 kujaza nafasi zilizo wazi ni batili hivyo kuagiza klabu hiyo iongozwe na sekretarieti.
Kamati hiyo iliyokutana juzi chini ya Mwenyekiti wale Alex Mgongolwa, imebatisha uamuzi huo kwa vile
Kamati hiyo iliyofanya uteuzi huo haikuwa na akidi iliyojitosheleza.
Mgongolwa alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, ili kamati hiyo ya utendaji ya Yanga yenye wajumbe 13, inatakiwa kuwa wajumbe asilimia 50 ya wote, hivyo ili wafanye uamuzi halali, hawatakiwi kupungua saba.
Alisema, kutokana na wajumbe kadhaa wa klabu ya Yanga kujiuzulu na kubaki wanne, ambao ni Sarah Ramadhan, Mohamed Bhinda, Tito Osoro na Salim Rupia, kwa sasa hawawezi kufanya shughuli zozote za klabu hiyo, hadi nafasi zilizo wazi zitakapojazwa.
Aliongeza kuwa, kutokana na wajumbe kutotimia, kazi zote za klabu hiyo kama inavyoelekeza Katiba ya Yanga, shughuli za kila siku zitaendelea kufanywa na Sekretarieti ya Yanga chini ya Katibu Mkuu, Selestine Mwesigwa.
Aidha, Mgongolwa alisema, baada ya kupata taarifa rasmi kutoka Yanga, wamebaini kuwa, Kamati ya Utendaji ya Yanga imekosa akidi baada ya wajumbe wake wengi kujiuzulu, hivyo kutokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 32(1) ya Katiba ya klabu hiyo.
Alisema, wametoa mwongozo kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, ambayo ndiyo msimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuwa, ili Kamati ya Utendaji ya Yanga iwe na nguvu za kikatiba kufanya shughuli zake ikiwemo uamuzi wa masuala mbalimbali ndani ya klabu hiyo ni lazima iwe na akidi.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya Yanga, nafasi zilizo wazi katika Kamati ya Utendaji zinatakiwa kujazwa katika Mkutano Mkuu wa kawaida ujao.

Mwisho.

Kim alia na washambuliaji Kili Taifa Stars
Na Clezencia Tryphone
KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Soka Tanzania, ‘Kilimanjaro Taifa Stars’ Mdenish Kim Poulsen, amesema licha ya kuwa ni mara yake ya kwanza kukinoa kikosi hicho ugonjwa unaokisumbua ni umaliziaji.
Akizungumza mara baada ya pambano la kirafiki kati ya Stars na Malawi ‘The Flames’ juzi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lililomalizika kwa sare ya bila kufungana, Poulsen alisema, umaliziaji ndio tatizo linalowakabili vijana wake.
Poulsen alisema, endapo tatizo hilo litakwisha, ana imani kikosi chake kitafanya vema licha ya kuwa ni mara ya kwanza kukabidhiwa mzigo mkubwa kama huo na kuwa, kwa sasa analifanyia kazi tatizo hilo kubwa juzi.
“Nimetazama na nilikuwa makini sana, lakini tatizo ni umaliziaji, ukiangalia utafutaji kwa maana ya kiungo walijitahidi kufanya kazi yao kwa umakini zaidi, tatizo ilikuwa katika kumalizia na hasa hapo wapinzani wetu ndipo walipokuwa wakichukulia mpira,” alisema Poulsen.
Aidha Poulsen aliwapongeza vijana wake kwa jinsi ambavyo walijituma na kusema kuwa mapungufu ni sehemu ya mchezo na ndo sababu ya kuwa na mchezo wa kujipima nguvu kabla ya kuvaa na Ivory Coast kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayofanyika ugenini Juni 2 mwaka huu.
Naye Kocha wa The Flames, Kinnah Phiri, amelipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kuona umuhimu na kuwaomba kuja hapa nchini kucheza mchezo huo wa kirafiki na kuwa ni kipimo kizuri kwa timu yake.
Aliongeza kwa kuwapongeza wachezaji wa Stars, kwa uwezo wao na kusema kuwa, hata kama kuna upungufu ni kidogo, kwa kuwa ni moja ya makosa katika soka kwani hata timu yake ina upungufu iliyouonesha.
Katika hatua nyingine, pambano hilo kati ya Stars na The Flames, limeingiza sh 40,980,000, kutokana na mashabiki 10,767 waliokata tiketi kushuhudia

Mwisho






TFF yambeba Nchunga
.Yagoma kutambua mapinduzi Jangwani
.Mwakalebela ashangazwa na ukimya wake

Na Dina Ismail

SIKU moja baada ya wanachama zaidi ya 700 wa klabu ya Yanga kutangaza kuupindua
uongozi wa klabu hiyo chini ya Lloyd Nchunga kwa hoja ya kushindwa kazi, Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), limesema halitambui uamuzi huo.

Juzi wanachama walikutana kwenye Uwanja wa Kaunda, kujadili mustakabali wa klabu  yao na kuamua kuung’oa uongozi wa Nchunga huku wakipanga kwenda kwa Msajili wa  Vyama na Klabu za Michezo wilaya ya Ilala, kumwomba awaitishie uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa hoja zilizoibuliwa kwenye mkutano huo na baraza la wazee wa klabu hiyo  chini ya katibu wake Ibrahim Akilimali na vijana wakiongozwa na Bakili Makele, wamefikia  hatua hiyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa uongozi wa Nchunga.
Mbali ya wanachama hao kupanga kuwasilisha majina na sahihi za waliohudhuria mkutano  huo wa juzi kwa Msajili, pia waliteua kamati ya usajili wa wachezaji kwa msimu ujao.

Akizungumzia maamuzi hayo ya wanachama, Katibu Mkuu wa TFF, Angetille Osiah, amezitaka pande husika kukutana haraka kupata ufumbuzi wa kile kinachobishaniwa kwa lengo la kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Kagame.
Yanga ambao ni mabingwa wa kombe hilo, wamezama kwenye malumbano huku michuano  hiyo ikitarajiwa kutimua vumbi mwezi ujao.

Angetile alisema shirikisho hilo linasimamia katiba kwa wanachama wake wote, hivyo taratibu zozote zinazofanywa na wanachama wake bila kufuata katiba hawazitambui; hivyo  wataendelea kuutambua uongozi wa Nchunga. Alisema maadam uongozi wa Nchunga umepanga mkutano mkuu Julai 15, wanachama walipaswa kuwa na subira, badala ya kuitisha mwingine nje ya matakwa ya katiba hiyo.

“Busara zinatakiwa katika mgogoro huo kupata nafasi ya kuiandaa timu yao kuelekea michuano  ya Kombe la Kagame, kuna mambo mengi yanapaswa kufanywa katika kipindi hiki ikiwemo  suala la usajili,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wameielezea hatua ya shirikisho hilo kama ni kukawia kuchukua hatua dhidi ya mvutano wa muda mrefu ndani ya klabu hiyo ukihusisha wanachama na uongozi kutokana na hoja kadha wa kadha, kubwa ni ukata wa fedha uliokithiri.

Katibu mkuu wa zamani wa TFF, Frederick Mwakalebela, alisema TFF kupitia kurugenzi yake  ya utawala na wanachama, ilipaswa kuchukua hatua muda mrefu dhidi ya sintofahamu  inayoendelea katika klabu hiyo tangu walipopokwa ushindi wa Coastal Union.
Alisema miaka ya nyuma, walikuwa wakisimamia machafuko ya aina hiyo kwa baadhi  ya maeneo, hali ambayo ilisaidia kupunguza migogoro iliyokuwa kama utamaduini  kwa baadhi ya klabu.
                                               


DC Mvomero  bosi mpya RT

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), wamempa kura za kishindo  Antony Mtaka  kuwa Rais wa Shirikisho hilo akimbwaga Kanali mstaafu, Juma Ikangaa.

Katika nafasi hiyo, Mtaka ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mvomelo, Morogoro, alishinda kwa kura 50  dhidi ya 29 za Ikangaa, Katibu Mkuu wa zamani wa shirikisho hilo wakati huo ikijulikama kama TAAA. Mtaka alipata kura hizo katika kura za marudio baada ya raundi ya kwanza kukosekana
mshindi wa moja kwa moja miongoni mwa wagombea wanne waliokuwa wamejitosa  katika nafasi hiyo kwa Ikangaa kupata kura 25 na Mtaka kura 36.

Waliochemkia raundi ya kwanza ni Francis John aliyeambulia kura 15 na Henry Nyiti aliyepata kura 7,
hivyo raundi ya pili kushudia ushindani mkali kati ya Ikangaa na Mtaka.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo majira ya saa 3:30 usiku, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huo, Henry Tandau, alisema  kurudiwa kwa nafasi ya Rais na Katibu Mkuu, ilitokana na wagombea kushindwa kufikia asilimia iliyohitajika kwa mujibu wa kanuni.

Ushindani mwingine ulikuwa kwenye nafasi ya Katibu Mkuu iliyokuwa ikishindaniwa na watu wanne, akiwemo Suleiman Nyambui aliyekuwa akitetea, John Bayo, Zainab Mbiro na John Manyama, lakini Nyambui alishinda kwa kura 41 dhidi ya 38 za Bayo, katika raundi ya pili.

Wagombea wawili katika nafasi tofauti, Makamu wa Kwanza wa Rais (Utawala) ilikwenda kwa William Kallaghe, aliyekuwa mgombea pekee kwa kura 78.

Katika nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais (Ufundi), iliyokuwa ikiwaniwa na wagombea wawili, Dk. Hamad Ndee alishinda kwa kura 55, akimbwaga Herman Ndisa aliyepata kura 42. Nafasi nyingine iliyokuwa na ushindani ni Katibu Mkuu Msaidizi , iliyokuwa ikiwaniwa na watu wanne, lakini Ombeni Zavalla akishinda kwa kura 40, Julius Murunya (32), Lucas Nkungu na Leonard Mandara, kila mmoja akipata tatu. Nafasi ya Mweka Hazina ilikuwa na mgombea mmoja, Is- Haq Seleman, aliyepata ushindi wa kimbunga wa kura 78  kati ya 79.

Mbali ya nafasi ya Rais na Katibu Mkuu, kivumbi kingine kilikuwa kwenye nafasi 10 za ujumbe wa shirikisho hilo, zilizokuwa zikiwaniwa na wanachama zaidi ya 30. Hata hivyo, mhariri wa michezo wa gazeti la Tanzania Daima, Tullo Chambo, alifunga pazia la nafasi zilizokuwa zikiwania baada ya kupata kura 37, akiungana na Mwinga Mwanjala ( 53), Lwiza John (50), Peter Mwita ( 50)
na Zakaria Gwandu ( 47). Wajumbe wengine ni Meta Petro Bare ( 46), Zakaria Barie (45), Rehama Killo ( 42), Robert Kalyahe ( 41) na  Christian Matembo (38).
                          



Jezi ya Mafisango
kutovaliwa Simba
.Maelfu waaga mwili wake Dar
.Rage ashindwa kumaliza risala

Na Clezencia Tryphone

JEZI namba 30 iliyokua ikivaliwa na nyota wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango katika kikosi cha Simba, haitavaliwa tena na mchezaji wa timu hiyo kama sehemu ya kumuenzi nyota huyo aliyefariki usiku wa kuamkia
juzi kwa ajali ya gari, eneo la Veta-Keko, jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo mgumu ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, wakati akitoa risala
fupi katika tukio la kuuaga mwili wa mchezaji huyo lililofanyika jana kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe
 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya watu.
Zoezi hilo la kuaga mwili wa marehemu lililoanza majira ya saa 5 asubuhi, lilitarwajiwa kufungwa saa 9 alasiri kwa lengo la kutoa nafasi kwa watu wa kada mbalimbali kuuaga mwili wa nyota huyo kabla ya mwili wake kusafirishwa
leo kwenda kwao DR Congo. 
Hatua ya Simba, ni kama ilivyokuwa Manchester City ambao waliamua kuienzi jezi namba 23 ya Marc Vivien Foe, aliyekuwa amefariki dunia akiwa na timu ya taifa ya Cameroon katika michuano ya Kombe la Mabara, mwaka 2003 kwa kutovaliwa tena.
Akizungumza kwa simanzi kubwa, Rage alisema ni pigo kubwa kwa Simba, kwani Mafisango alikuwa ni nguzo muhimu sio tu kwa umahiri wake dimbani, bali akiwa mshauri kwa wachezaji wengine ndani na nje ya dimba,
hivyo ni pengo kubwa mno.
Rage alisema, kifo hicho kilichoacha pengo kubwa katika kikosi cha sasa, kimewakumbusha wanachama na
wapenzi wa klabu hiyo tukio la mwaka 1978, Simba ilipompoteza mchezaji wake Hussein Tindwa, aliyekuwa
ameteza maisha kwenye Uwanja wa Uhuru.
Kwa mantiki hiyo, jezi namba 30 iliyokuwa ikivaliwa na Mafisango, haitatumika tena kwa lengo la kuendelea kuenzi mchango wa mchezaji huyo aliyewakuwa akiichezea Simba kwa moyo wake wote na kuwataka wenzake kuiga yote mazuri yote ya nyota huyo.
“Ni pengo kubwa kwa sababu, mbali ya umuhimu wake kiuchezaji, alikuwa msaada mkubwa kutokana na umahiri wake wa kujua lugha nyingi kikiwemo Kiswahili, Kingereza na Kifaransa, hivyo kuwa mchezaji muhimu ndani na nje ya nchi tutamkubuka sana,” alisema.
Kutokana na kulemewa na simanzi, Rage alishindwa kumalizia risala katika zoezi la kuaga mwili ya nyota huyo,
hivyo kupokewa na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliyeimalizia, kubwa zaidi ikiwa ni simanzi na
pigo kubwa katika kikosi cha timu hiyo. 
Kabla ya kutua Simba, Mafisango aliwame kukipiga katika timu za Azam FC ya Tanzania, APR ya Rwanda na TP Mazembe ya DR Congo, akiwa na sifa zote wa kuitwa mchezaji wa kimataifa. 
Zoezi hilo la utoaji huo wa heshima za mwisho, uliambatana na ibada iliyoongozwa na Mchungaji Tito Kihame,
Dk. Fenella Mukangara na viongozi wengine wa kada mbalimbali, wote wakiwa na simanzi kubwa ya kumpoteza mchezaji huyo mahiri.
Akizungumza na ufupi, Mukangara aliwataka wachezaji wa Tanzania kuifa mfano wa Mafisango katika kujituma, akisema hiyo ndio siri kubwa ya mafanikio ya jambo lolote katika maisha ya mwanadamu.
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa Simba na Tanzania kwa ujumla, tunamshukuru kwa kuvuka mipaka
na kuja kucheza kwetu. Wachezaji wa Simba wasikate tamaa, kitu muhimu kwao kuendeleza yote mazuri ya
marehemu, ” alisema.
Nyota kadhaa wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars walijitokeza kubeba jeneza la nyota huyo wakati wa kupelekwa viwanja vya Sigara, wakiongozwa na Juma Kaseja, Jonh Bocco, Mwinyi Kazimoto, Shabani Nditi, Amiry Maftah, Nurdin Bakari, Agrey Moris  na Juma Nyoso.
Aidha, Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema katika msafara wa kwenda DR Congo, Haruna Moshi Boban ndiye atakuwa mwakilishi wa wachezaji katika mazishi hayo huku uongozi ukiwakilishwa na Joseph
Itang’are ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji.
Kamwaga alisema, msafara wa kwenda DR Congo utakuwa alfajiri ya leo huku mtoto wa marehemu, Chris Paul mwenye umri wa miaka mitano, ametanguliwa na Haruna Niyonzima, nyota wa kimataifa wa Rwanda anayekipiga katika klabu ya Yanga.
                                                                        Mwisho.

Wazee, Vijana Yanga SC
wabariki masharti ya Manji
.Waitisha mkutano mzito kesho

Na Dina Ismail

BARAZA la Wazee wa klabu ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake Dk. Jabir Katundu na kundi la Vijana, wameunga mkono masharti yaliyotolewa na mfadhili wao wa zamani, Yusufu Manji kukubali kurejea, kama masharti yake matano, yatatimizwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, alisema
mbali ya wao kuunga mkono masharti ya Manji, pia wanausihi uongozi wa Lloyd Nchunga,
kujiweka kando kabla ya kesho Jumapili.
Akilimali alisema, ni heri Nchunga akatumia busara ya kawaida kujiweka kando mwenyewe
badala ya kusubiri kuondolewa kwa nguvu ya wanachama katika mkutano wa kesho kutokana
na kushindwa kuongoza klabu hiyo.
“Leo (jana) tunatoa agizo la mwisho kwa Nchunga na wenzake kuachia ngazi mara moja kwa sababu wameshindwa kuongoza, wachezaji wanalia njaa, makocha wapo hoi kifedha, hili
halivumiliki, Yanga inadhalilika,” alisema Akilimali akiungwa mkono na wazee wenzake.
Alisema, wanamtaka Nchunga na wenzake wajiondoe wenyewe kabla ya mkutano wa
kesho Jumapili ambao utafanyika makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga
na Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Akilimali alisema tayari baadhi ya wanachama kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Zanzibar, wameshaanza kuwasili kwa ajili ya mkutano huo wa kuikomboa klabu hiyo katika hali ngumu kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa Vijana, Bakili Makele alisema jana,  wanaunga mkono masharti yaliyotolewa na Manji kwani yatasaidia kuleta uwazi wa mambo yahusuyo matumizi ya fedha kwa kipindi cha kuanzia 2006 hadi 2012.
“Tunaunga mkono masharti ya Manji kabla ya kurejea kwenye ufadhili, katika hali ya kawaida,
 mtu huwezi kutoa fedha bila kujua zinatumikaje… tumekuwa tukilipigia kelele jambo hili kila
siku, tukitaka mikutano ya kikatiba, lakini viongozi wetu wamekuwa wagumu,” alisema Bakili.
Bakili aliyeungana na wazee kutoa tamko hilo, alisema mkutano wa wanachama wa kesho, utafanyika kama ulivyopangwa huku akitoa wito kwa wanachama wa klabu hiyo kujitokeza
kwa wingi kufanya maamuzi ya kuiokoa Yanga.
Alisema kutokana na ukata ambao unaikabili klabu hiyo hadi kuwa na madeni yanayokadiriwa kufikia mil 106, kuna hatari mali za klabu hiyo kupigwa mnada kama si jingo la makao makuu, kitu ambacho wasingependa kitokee.
Makele alisema, leo wanachama wa klabu hiyo kutoka matawi mbalimbali wanatarajiwa kukutana katika tawi la Buguruni kujadili ajenda mbalimbali ambazo watawasilisha katika mkutano huo wa kesho.
Kauli ya Akilimali na Bakili, imekuja siku moja tangu Manji atoe masharti ya kurejesha ufadhili
wake katika klabu hiyo, baada ya vijana kumsihi afanye hivyo kuokoa jahazi; wachezaji na
makocha wakilia ukata mkali.
Masharti hayo ni kufanywa uhakiki wa mahesabu ya akaunti ndani ya siku 90, tena ukaguzi huo ufanywe na kampuni binafsi kwa hesabu za kuanzia mwaka 2006 hadi 2012.
Aidha, kuanzia sasa akaunti za Yanga zichapishwe kwenye magazeti, siku 15 baada ya
kumalizika robo ya mwaka,  pia kuwepo na upigaji wa kura ya maoni ndani ya siku 60,
kuamua kama wanachama wanautaka mfumo wa kampuni au la.
Sharti jingine, ni kuwepo marekebisho ya katiba ndani ya siku 90,  juu ya muundo wake
wa uongozi kwa kukubali mojawapo ya mfumo huu chini ya Katiba ya Yanga.
                                                                      mwisho
Banyana yatua
kuivaa Twiga

Na Ruhazi Ruhazi

TIMU ya soka ya taifa ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ilitarajiwa kuwasili nchini jana jioni kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Twiga Stars itakayopigwa kesho  kwenye Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari za Shirikisho la soka Tanznaia (TFF), Boniface Wambura, msafara wa wageni hao, utakuwa na watu 26, wakiwemo wachezaji 18, wakifikia kwenye hoteli ya Sapphire Court Hotel, tayari kwa mechi hiyo.
Twiga Stars inataka kuitumia mechi hiyo kama kipimo kabla ya kucheza mechi ya kwanza ya mchujo katika kuwania tiketi ya fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia itakayochezwa Mei 27, jijini Addis Ababa.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu zaidi kwani Banyana Banyana nayo inasaka makali ya kuwanyoa Zambia katika kampeni hizo, wakianzia ugenini mjini Lusaka kabla ya kurudiana
nchini Afrika Kusini.
Wambura alisema, makocha wa timu zote mbili, Boniface Mkwasa wa Twiga Stars na mwenzake Joseph Mkhonza wa Banyana Banyana, leo mchana wazungumzia maandalizi yao kuelekea mechi hiyo.
Twiga Stars na Banyana, zipo kwenye raundi ya mwisho ya kuwania tiketi kwani kama zitafanikiwa kuvuka hatua ijayo, zitakuwa zimejitwalia  tiketi ya fainali hizo zitakazofanyika Novemba mwaka huu, nchini Guinea ya Ikweta.
                                                                            mwisho



TANZIA


Patrick Mafisango, ambaye ni mchezaji mahiri wa Simba, amefariki dunia leo asubuhi kwa ajali ya gari katika eneo la Tazara. Juzi alikuwa mmoja wa wachezaji waliokosa penalti pambano huko Sudan, lakini pia alikua ameitwa tena timu ya Taifa ya Rwanda baada ya kuonesha kiwango cha juu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyomalizika. 
RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA, NA MWANGA WA MILELE AANGAZIWE, APUMZIKE KWA AMANI- AMANI


Mafisango afariki Dunia

Na Clezencia Tryphone

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Rwanda, anayekipiga katika klabu ya Simba, Patrick Mutesa Mafisango, amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari alfajiri
ya jana, jijini Dar es Salaam.
Mafisango, kati ya nyota mahiri walioitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Rwanda, ‘Amavubi’ chini ya Kocha Mserbia, Sredejovic Milutin ‘Micho,’
amefariki kwa ajali aliyopata eneo la Veta- Chang’ombe, wilayani Temeke.
Kwa mujibu wa Olilemba Mafisango ambaye ni mdogo wa marehemu, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 9, baada ya gari waliyokuwa wamepanda, kupinduka
katika harakati za kumkwepa mwendesha pikipiki.
“Katika harakati za kumkwepa mwendesha pikipiki kwa lengo la kuokoa maisha yake, ndipo gari ikapinduka nay eye kuumia vibaya,” alisema Olilemba na kusema wakati gari hiyo ikipata ajali, ilikuwa na watu watano ndani yake.
Alisema, kati yao  wavulana walikuwa watatu na wasichana wawili,  wakati huo wakirejea nyumbani kutokea Maisha Klabu iliyopo Masaki, jijini Dar es Salaam.
“Ni kweli mwandishi, Kaka yangu amefariki dunia, wengine tuko poa, ila mmoja wetu amaepata majeraha kidogo kichwani, amepelekwa Muhimbili (Hospitali ya Taifa), kwa uchunguzi,” alisema.
Akizungumza kwa simanzi kubwa kwa njia ya simu jana asubuhi, Olilemba alisema, hadi muda huo kifo cha nduguye kwake kilikuwa kama alikuwa akiota ndoto, lakini ndio ukweli kwamba, Patrick amefariki dunia.  
Baada ya hapo mwandishi wa habari hizi, alikwenda hadi Hospitali ya Muhimbili
na kukuta umati wa watu-kila mmoja akiwa kwenye majonzi makubwa, wakishindwa kuamini kifo hicho cha ghafla.
Kati ya watu waliokuwa wamefikia Hospitalini hapo wakati huo mwili wa marehemu ukisubiri kufanyiwa uchunguzi zaidi, ni wachezaji wenzake wa Simba, viongozi kadhaa na wanamuziki wa Bendi ya Akudo ambao walijikuta wakiangua kilio.
Baadhi ya nyota waliofika Hospitalini kwa muda huo, ni Uhuru Suleiman, Emmanuel Okwi, Haruna Moshi Boban, Derick Walulya (Simba) na Haruna Niyonzima, nyota wa kimataifa wa Rwanda anayechezea Yanga na wanamuziki, Chiristian Bella, Clary Boteku na Canal Top.
Akizungumzia msiba huo, Makamu Mwenyekiti wa Godfrey Kabulu alisema mwili wa nyota huyo utaagwa leo katika  viwanja vya TTC Chang’ombe, kuanzia saa 2:00 asubuhi kabla ya kusafirishwa kesho kwenda kwao Rwanda kwa mazishi.
Kaburu alisema, kifo cha Mafisango ni pigo kubwa kwa kikosi cha Simba na nchi yake ya Rwanda iliyokuwa ikimtegemea kwani amefikwa na umauti akiwa
ameitwa kwenye kikosi cha Amavubi.
“Kifo cha Mafisango ni pengo kubwa kwetu (Simba) kutokana na umuhimu wake, lakini hatuna mengi zaidi kwani hatuna la kufanya mbele ya kazi ya Mwenyezi Mungu, Mafisango amemaliza safari yake Duniani,” alisema.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepokea kwa masikitiko
kifo cha nyota huyo kilichoacha pengo na simanzi kubwa kwa familia ya soka kutokana na moyo wake wa kujituma uwanjani.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Boniface Wambura, kifo cha Mafisango sio pigo tu kwa timu yake ya Simba na nchi ya Rwanda, bali
kwa soka ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.  
Wambura alisema Mafisango amefikwa na umauti kipindi ambacho nchi yake
ikihitaji mchango wake, akiwa kati ya nyota walioitwa kwenye kikosi cha Amavubi kwa mechi za mchujo wa kuania tiketi ya Kombe la Dunia kwa Kanda ya Afrika.
“TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA), tunawataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao,” alisema Wambura.

Mwisho


Manji atoa msharti
kurudi Yanga SC

Na Salum Mkandemba

ALIYEKUWA mfadhili wa Yanga Yusufu Manji, ameibuka kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa migogoro ndani ya klabu hiyo na kudai kuwa yupo tayari kurudi kuifadhili kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa masharti.
Manji ameyasema hayo jana kupitia barua yake aliyosambaza katika vyombo vya habari na kusema kuwa yuko tayari kufikiria kushiriki kikamilifu, kurudi Yanga kwa mwaka mmoja kwa masharti makubwa kadhaa.
Sharti la kwanza ambalo amelitoa kwa uongozi wa Yanga ni ikubalike kufanywa uhakiki wa mahesabu ya akaunti za Yanga ndani ya siku 90 na wakaguzi wa hesabu wa kujitegemea kukagua hesabu za kipindi cha 2006 hadi 2012 kwa ajili ya fedha zilizopokelewa na klabu.
Pili kuanzia sasa na kuendelea akaunti za Yanga zichapishwe katika magazeti siku 15 baada ya kumalizika kwa robo ya mwaka.
Katika sababu ya tatu, Manji ametaka kuwapo na upigaji wa kura ya maoni ndani ya siku  60 na kuamua kama wanachama wa Yanga wanataka kuendesha kampuni ya Yanga au la.
Sharti la nne, Yanga ifanye mabadiliko ya katiba ndani ya siku 90 juu ya muundo wake wa uongozi kwa kukubali mojawapo ya mfumo huu chini ya Katiba ya Yanga.
Katika barua hiyo Manji pia ameutaka uongozi kuidhinisha mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa klabu kuchagua Makamu Mwenyekiti wake na wafanyanye kampeni kwa pamoja kupitia tiketi moja, na tiketi yoyote ile itakayo fanikiwa kushinda itaunda Kamati ya Utendaji na Kamati zote chini ya Kamati ya Utendaji kama wanatakavyoona inafaa kwa muda wao wa miaka 4, ikiwa ni pamoja na kuondoa au kuongeza Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kulingana na uamuzi wao.
Manji ambaye ni kipenzi cha Wanayanga, pia ameupa masharti uongozi uliopo chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga, wagombea wa Kamati ya Utendaji wafanye kampeni na baadaye wajumbe 12 wachaguliwe kwa muda wa mwaka wa nne.
Baada ya Kamati ya Utendaji ya kuchaguliwa, basi ichague Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kwa muda wa mwaka mmoja kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji na kila mwaka wao kupiga kura ya ama kumbakiza au kumbadilisha Mwenyekiti na au Makamu Mwenyekiti kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji.
Sharti la mwisho ni Mkutano wa Wanachama uitwe ndani ya siku 30, ili kujadili masuala yaliyopo hapo juu na kama kutakuwa na makubaliano ya masharti yaliyowekwa hapo juu, basi  na yeye rasmi atarudi kushiriki kikamilifu Yanga kwa muda wa mwaka mmoja.
Uamuzi wa Manji kutaka kurejea Yanga kwa masharti, unakuja kufuatia wito hivi karibuni wa kundi la wanachama vijana wa klabu hiyo likiongozwa na Bakili Makele, kumtaka kurejesha ufadhili wake kuinusuru klabu hiyo na hali mbaya kifedha chini ya uongozi wa Nchunga.

Mwisho



Nchunga ahofia
maisha yake Yanga

Na Salum Mkandemba

MWENYEKITI wa Yanga Lloyd Nchunga, amesema kwa sasa anahofia usalama wa
uhai wake ndani ya klabu hiyo kutokana na mvutano uliopo kati ya uongozi wake
na Baraza la Wazee, wakimtaka aachie ngazi.

Kabla ya baraza hilo chini ya Mwenyekiti wake, Dk. Jabir Katundu, kutoa tamko hilo,
liliomba kukabidhiwa timu kuelekea mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Simba ya
Aprili 6, kwa hoja ya kuiepusha na aibu ya kufungwa baada ya kuvuliwa ubingwa.
Akizungumza siku tatu kabla ya mechi dhidi ya Simba ambayo iliisha kwa Yanga
kufungwa mabao 5-0, Katibu wa Baraza hilo, Ibrahim Akilimali, alisema waliitaka
timu kutokana na uongozi wa Nchunga kushindwa kuiendesha.
Wazee walifikia hatua hiyo baada ya uongozi wa Nchunga kushindwa kuwalipa
wachezaji mishahara kwa miezi miwili, hivyo kushindwa kucheza kwa ari, wakifungwa
na Toto Africa na Kagera Sugar.
Kitendo cha Yanga kupoteza pointi hizo sita na zile kutoka kwa Coastal Union ya Tanga kwa kosa la kumchezesha Nadir Haroub ‘Cannavaro,’ kukaifanya Yanga ibaki nyuma ya Simba na Azam kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Licha ya wazee kuitaka timu, uongozi wa Nchunga uligoma ukiwataka kwanza kuainisha vyanzo vya fedha za kuendesha timu hiyo, kitendo ambacho kiliwakera wazee hao na kuamua kujiweka kando kuelekea mechi dhidi ya Simba.
Kitendo cha Yanga kufungwa, ndicho kikawapa nguvu zaidi wazee, wakimtaka
Nchunga aachie ngazi, hoja ambayo iliungwa mkono na kundi la wanachama vijana
wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wao, Bakili Makele.
Akiizungumzia hali hiyo jana katika mahojiano na Radio One kupitia kipindi cha Kumepambazuka, Nchunga alisema kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na vinara wa harakati za kutaka uongozi wake uong’oke, ni kitisho cha usalama wake, ingawa hajachukua hatua za kisheria.
“Kauli tata juu yangu zinazotolewa tangu kuanza kwa harakati za kutaka niondoke madarakani, ni hatari kwa usalama wangu, ingawa sijachukua hatua zozote za kisheria,” alisema.
Nchunga alisema kama atapatwa na lolote baya la kudhuriwa au vinginevyo, serikali itakuwa inatambua nani wa kuulizwa, kwani amekuwa akitishiwa maisha, ikiwamo kupitia vyombo vya habari.
Kupitia kipindi hicho, Nchunga aliendelea kushikilia msimamo wake akisema pamoja na yote hayo yanayofanywa dhidi yake binafsi na uongozi wake, lakini yupo Yanga kisheria, hivyo hata kuondoka, yapaswa iwe kisheria.
“Kama inatokea leo, napatwa na tukio lolote baya la kudhuliwa au vinginevyo, ni wazi kuwa serikali inamtambua anayepaswa kuwa kiini cha hilo. Natishiwa maisha, tena kupitia vyombo vya habari,” alisema Nchunga na kusisitiza:
“Nipo Yanga kisheria, kuondoka kwangu pia kufuate sheria, si matakwa ya kundi fulani,” alisema Nchunga aliyeingia madarakani Julai 18, 2010, akirithi kiti kutoka kwa Imani Madega, aliyekuwa amemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba.
Nchunga alisema ukimya wake wa kujibu mashambulizi kwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika, ndio unauponza uongozi wake, kwani serikali inamtambua mtuhumiwa namba moja kama ikitokea akapata madhara.
Kuhusu kiini cha mvutano, Nchunga alisema mfumo wa muda mrefu wa uendeshaji wa klabu hiyo ndio chimbuko la  migogoro ya kila mara huku wazee nao wakiwa sehemu ya tatizo hilo kutokana na kutaka kuwa na sauti.
Alisema, ndiyo maana amekuwa mvumilivu kiasi cha kuamua kuitisha mkutano na wazee Mei 20 kabla ya Mkutano Mkuu wa Julai 15 na kusema, anashangazwa kusikia siku hiyo itakuwa ya kuung’oa uongozi wake.
Zaidi ya hilo, Nchunga alionesha kushangazwa kwake na wazee hao kwamba yeye hakuwa chaguo lao, akisema hiyo ni kutokana na kupinga matakwa yao, lakini akisema ni kweli kama si ridhaa yao, asingeshinda.
Kuhusu madai ya wachezaji, Nchunga alisema ni majungu, kwani wachezaji ambao wanadai ni wawili tu, Jerry Tegete na Nurdin Bakar; tena kwa sababu maalumu. Kuhusu kipigo cha mabao 5-0, amesema si pekee wa kubebeshwa mzigo.
                                                      
Mwisho

No comments:

Post a Comment