Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

MAKALA ZA SIASA





Nacheka kwa uchungu
Tanzania na uongozi wa damu
Na Charles Misango
NIMELAZIMIKA kuyakumbuka maneno mazito aliyotoa Spika wa Bunge la Tanzania Anne Makinda wakati wa msiba wa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa aliyefariki mwanzoni mwa mwezi huu nchini Afrika Kusini.
Mbele ya umati wa waombolezaji, Makinda alisema ingekuwa ni amri yake angekufa mtu (kwa namna nyingine waziri) mwingine lakini sio Mgimwa!
Sitaki kurejea namna alivyoshambuliwa kwa maneno, na mijadala ilivyotamalaki katika vyombo vya habari kuhusiana na kauli hiyo.
Kilichonisukuma kukmumbuka maneno ya mama Makinda ni kile kinachoendelea katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Juzi nililazimika kushuka katika mji huo mdogo nikitoka Musoma kikazi ili niwe kama Yule Thomaso tunayemsoma katika Biblia ambaye alipoambiwa Yesu Kristo amefufuka alikataa hadi amwone kwa macho yake na kugusa makovu ya misumari aliyoshindiliwa msalabani.
Mji mzima wa Bunda unatikisika kwa sasa kutokana na kampeni za uchaguzi mdogo wa diwani wa kata ya Nyasura, baada ya kiti hicho kubaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wake Zamberi Ngobayi (Chadema).
Katika kampeni hizi ambazo vyama viwili, Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni dhahiri kitamsimamisha Alex Mwikwabe ambaye inadaiwa alipatikana baada ya wagombea wawili wa awali kujitoa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichomsimamisha Magambo Webiro zinaendeshwa katika hali inayodhihirisha ubabe, vitisho, hila na ubabaishaji wa hali ya juu.
Nimeshuhudia kampeni za kuchafuana majina, hadhi na heshima ya wagombea zikifanywa na watu wazima kabisa, tena viongozi waliostahili kuionesha jamii kuwa wanawathamini watanzania na wanaheshima matakwa ya watu ya nani awe kiongozi wao.
Nimeshituka zaidi hata baada ya kuona upande mmoja ukijaribu kuwadanganya wapiga kura kwa hoja za kipuuzi za kwamba mgombea wa Chadema ni mganga wa kienyeji na hivyo hafai kuchaguliwa. Tena wanaosema hivyo ni viongozi wengine wa CCM ngazi ya wilaya. Ni hoja ya ajabu kwa sababu hakuna popote katika katiba ambapo mtu anayetibu watu kwa kutumia dawa za kienyeji haruhusiwi kuchaguliwa na kuwa kiongozi. Na kwa kutambua hilo, hao hao wanaosema hivyo, wanasahau kuwa mmoja wa wabunge wake wa bunge la Muungano ni mganga wa kienyeji ambaye katika uchaguzi uliopita alimbwaga daktari mwenye PhD!
Je viongozi wa CCM wa wilaya ya Bunda kwa hoja hiyo ya uganga iliyokanushwa na mhusika mwenyewe, wanataka kusema kuwa wapiga kura Korogwe vijijini walifanya kosa kumchagua mganga wa kienyeji pia Prof Maji Marefu (CCM)kuwa Mbunge wao?

Na katika namna ya kushangaza, baadhi ya viongozi wa CCM sasa wanadaiwa kumwandaa mwana mama mmoja atakayetembea kata nzima kueleza namna mgombea wa Chadema alivyotapeli kwa kutumia uganga wake. Mama huyo anadaiwa kuwa atatangaza jinsi mgombea wa Chadema alivyomtapeli mamilioni ya fedha ili amtibu!
Fikiri tu kwamba suala la uganga limechukua nafasi kubwa katika kampeni huku upande wa pili yaani Chadema, badala ya kupuuza propaganda hizo, nao wamejikita kujibu hoja na kusahau kutangaza sera.
Mbali na hoja ya uganga, wapinzani wa mgombea huyu wameingiza ubaguzi wa kikabila na kimaeneo. Wanajaribu kuwaaminisha wapiga kura kuwa ni hatari kumchagua mgombea huyo kwa sababu sio mzawa wa Nyasura bali mhamiaji aliyefukuzwa kutoka Kata nyingine ya Kunzugu katika kitongoji cha Bokole.
Kana kwamba hoja hizo kwa viongozi wa chama tawala hazina madhala kwa taifa, sasa wanatuhumiwa kuibua jambo baya zaidi ambalo limeanza kuwatisha na kuwapa kiwewe baadhi ya wananchi sio wa Kata ya Nyasura tu bali wilaya nzima ya Bunda.
Hili ni kuwepo kwa tuhuma kwamba zipo njama za kutaka kumkamata mgombea wa upinzani na kumbambika kashfa ya kuiba nyaraka sa siri za serikali.
Inadaiwa kuwa hizo zinazoitwa nyaraka za siri za serikali, zile zinazohusiana na sakata la ardhi katika wilaya ya Bunda.
Kwamba mgombea huyo anatembea na nyaraka za mikataba feki iliyotumika kutaifisha ardhi ya mlima Balili inayosemekana ni mali halali ya shule ya msingi Balili na pia ya Kanisa la Wasabatho.
Inasemekana tuhuma hizo zinawagusa baadhi ya watendaji wa wilaya na mkoa, akiwemo mkuu wa mkoa mmoja hapa nchini.
Nyaraka hizo zinazoitwa za siri, pia zinadaiwa kuwa ni zile zinazofichua kile kinachoitwa tuhuma za waziri mmoja mwandamizi wa serikali ya CCM anayedaiwa kuchukua kwa mabavu sehemu ya ardhi ya shule moja ya sekondari.
Kampeni hizo za uchaguzi wa udiwani kata ya nyasura na zigine 28  nchini utakaofanyika Februari 9,2014, zinaashiria jambo moja tu. Umwagaji wa damu!
Hali sio shwari, viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wameungana na lugha inayotamba sasa ni kwamba..’heri kufa kuliko kuonewa, kuliko kudhulumiwa’
Wapenzi na wanachama wa CCM, nao wanatamba na kauli,….’kwa gharama yoyote lazima tukomboe kata yetu”.
Kauli hizi sio njema hata kidogo hasa zinapopaliliwa kwa nguvu na wanasiasa wakomavu ambao chama chao kinaongoza nchi. Ni kauli ambazo zinaonesha kuwa uwezekano wa kupata viongozi wazuri, wakweli, waadilifu na wachapakazi kama alivyokuwa waziri Mgimwa ambaye Spika Makinda hakutaka afe ni ndoto.
Inatia uchungu zaidi ikiwa leo watanzania wanazidi kushuhudia haki na demokrasia ikikandamizwa kwa gharama za walipa kodi, ili tu watu wanaowataka wachaguliwe kuwa viongozi wa watu hata kama hawana sifa na hawapendwi.
Spika Makinda hata kama kauli yake, haikuwa njema masikioni mwa watu, ajue kuwa chama chake kitasaidia kupatikana kwa viongozi kama marehemu Mgimwa kikiacha mizengwe, hila, ujanja wa kishamba kuendesha kampeni zisizo na mashiko.
Spika Makinda ajue kuwa ni jukumu la CCM kushika na kusimama kama ‘baba wa demokrasia’ na hivyo, kuacha ghiriba za aina yoyote ile katika chaguzi ziwe ndogo ama kubwa.
Kampeni za kudhalilisha, kukomesha na kutesa wasiokuwa wapenzi na wanachama wa CCM na kulazimisha kumweka mtu wa ovyo madarakani kamwe haziwezi kuleta watendaji bora wa serikali. Haziwezi kulipatia taifa madiwani, wabunge na mawaziri bora.
Kampeni zinazosukumwa na ubabe, uonevu, wizi wa kura na hata kumwaga damu za wananchi, haziwezi kamwe kuleta manufaa katika nchi zaidi ya machafuko na umwagaji damu. Kauli ya wana wa Bunda kwamba liwalo na liwe ni ishara ya kwamba watu wamechoka kunyanyaswa. Ni kauli za waliokosa matumaini dhidi ya serikali yao, na hawaitaki.
Spika Makinda atatamani wafe mawaziri wengi ikiwa leo hii katika kampeni za uchaguzi wa marudio ya udiwani, polisi wanatumika kupiga na kufungulia watu kesi za kubambika ili tu CCM ishinde.
Makinda ajue kuwa kama kweli ana uchungu na taifa hili, basi awaambie viongozi wenzake kuwa wanalo jukumu la kuheshimu matakwa ya watu. Wanalo jukumu la kujua na kutekeleza kile watanzania wanachokitaka na sio kuwalazimisha kwa mbinu chafu hata za kumwaga damu.
Bado watanzania wanakumbuka jinsi viongozi wa upinzani walivyofunguliwa mashitaka ya ovyo, kupigwa, kudhalilishwa na kuteswa kisa tu walisimama kuwania uongozi katika chaguzi mbalimbali. Ni viongozi hao hao wa CCM ambao Spika Makinda ni mmojawao, ambao wametumia nguvu na maarifa mengi kuwaaminisha watanzania kuwa wapinzani ni watu wa ovyo, hatari na wanaotakiwa kuogopwa kama ukoma.
Kibaya zaidi, Spika Makinda mwwenyewe mara nyingi tu ameruhusu na kushiriki kukandamiza haki za wapinzani hata katika masuala ya msingi ya nchi. Kiti chake kimeshiriki mara nyingi kunyamazisha sauti za watanzania kupitia wabunge wao.
Wabunge wangapi wa upinzani wamekandamizwa walipokuja na hoja zenye maslahi ya nchi? Wabunge wangapi wa upinzani wameitwa wazushi na waongo walipoibua tuhuma dhidi ya mawaziri? Kama Kiti cha Spika kingeruhusu hoja kujadiliwa na hatua madhubuti kuchukuliwa, leo hii uovu na uvundo katika sekta ya elimu ingefikia hatua hii?
Ni mawaziri wangapi walilindwa na kiti cha Spika pale walipotoa majibu ya uongo, ubabaishaji na yenye hasara kwa taifa? Kwa nini kiti cha spika kiliwakingia kifua alafu leo kiti hicho hicho kinalia? Dhihaka?
Inatia uchungu basi tunaposikiaNi ajabu kwamba leo eti analiachuklia wapinzani na kuwanachama makini na anayeheshimu demokrasia hawezi kufurahia ushindi uliopatikana kwa kukandamiza na kuonea watu.



KUMBUKUMBU YA NYERERE (1999 - 2013)
Usomi, Uhuru na Ukweli
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922 – 1999) anakumbukwa kwenye historia ya Tanzania kwa kuwa msomi wa kwanza kupata shahada ya uzamili kwenye taaluma ya ualimu wa historia ya uchumi. Kwa jinsi ya pekee, Mwalimu Nyerere alionesha matumizi mazuri ya akili ya usomi tangu alipokuwa akisoma chuo kikuu cha Afrika ya Mashariki (Makerere) na baadaye Edinburg. Kwa jinsi hiyo, Mwalimu Nyerere anaweza kuingia kwenye historia ya wasomi waliyesoma katika Tanganyika ya wakati wake na baadaye Tanzania chini ya muungano!
Hatuwezi kumkumbuka Mwalimu Nyerere kama wafanyavyo kasuku kwa kurudia yaleyale kila siku kwenye kipindi cha ‘Wosia wa Baba.” Na hatuwezi kujiweka kwenye mizani ya usomi, kama ni wasomi kweli kwenye vyuo vikuu na kada zote za shahada za uzamivu, uzamili na shahada za taaluma kama hatutasimama kwenye uhuru (wa kutoa maoni) na kusimamia ukweli ambao ndio chimbuko la uhuru!
Zamani nilipokuwa mtoto wa miaka mitano hadi naanza darasa la kwanza (mwaka 1978) nilikuwa na fikra kwamba, usomi ni kujua kwamba ukweli ni kweli na lazima usimamiwe! Kadri siku zilivyokuwa zikinitupa mkono, hadi nilipoingia chuo kikuu kama mwanafunzi nilitamani nisome ili niwe ‘mkweli’ na msadikishaji wa ukweli. Baada ya kusoma na kuanza kazi kwenye kada ya taaluma, nilikuwa na tamaa kubwa ya kumsoma Mwalimu Nyerere na wanafalsafa wengine wa dunia wenye mitazamo tofauti na wanaosimama kwenye uhuru na ukweli. Na kwa kuanzia nilianza na walimu waliyenifundisha na kwa sasa sehemu yao ndio ninaofanya nao kazi ya kusoma ukweli kwa njia ya utafiti, hoja za kisayansi na mantiki.
Mwalimu Nyerere alitaka wasomi wawe huru; hata hivyo, sehemu kubwa ya wasomi wa siku hizi kwenye vyuo vingi ni watumwa wa akili (mental slaves). Kama alivyowahi kuimba mwanamuziki nguli wa reggae duniani, Robert Nester Marley (Bob Marley); sijui ni lini wasomi hawa uchwara watajikomboa kutoka kwenye utumwa wa akili? Sijui! Uhuru wa wasomi, si kukariri maandiko kama wendawazimu, bali wanatakiwa wawe wakweli kwa maandiko yao kwa kuzingatia utafiti na hoja za kisayansi zenye mantiki iliyo kuu na inayozingatia mizani ya haki, uhuru, usawa na insafu ya hoja kwa mujibu wa ukweli unaopatikana kwa misingi ya kutafuta ukweli uliyofichwa na au kujificha (hidden truth).
Katika kusimama kwenye nukta hii; Mwalimu Nyerere aliwahi kutumia fursa ya kuhutubia kwenye Chuo Kikuu cha Liberia mwaka 1968 kwa kuzungumzia: jinsi usomi unavyotakiwa kuwatumikia wananchi; jinsi vyuo vikuu vinavyotakiwa kufanyakazi; jinsi wanafunzi wanavyotakiwa kujifunza ukweli; na jinsi walimu wanavyotakiwa kusimama kwenye ukweli. Nukta hizi zilitolewa na Mwalimu Nyerere (1968) aliposisitiza juu yake na kuonesha kwa jinsi gani usomi unavyoweza kutumika katika kupambana na ufisadi.
Mwalimu Nyerere alianza kwa kusema, ‘Nimekuwa nikitoa maombi kwenye vyuo vikuu vya Afrika, na kwa wanafunzi waliomo katika vyuo vikuu vya Afrika, pamoja na wale wengine wote wanaopata elimu ya juu, wawe wazalendo wenye kujitoa kwa nchi zao, na kufanya kazi zao zote ziwe na shabaha ya kuhudumia nchi zao.’ Leo tunashuhudia sehemu kubwa ya wanafunzi wa vyuo vikuu wakikosa uzalendo na wengi wao wakijielimisha kwa utashi wa kibinafsi na si kwa maendeleo ya watu. Huu ni uzezeta wa usomi mamboleo uliyowashika wanafunzi wengi na baadhi ya walimu wa vyuo vikuu wanaoyeogopa kusimama kwenye uhuru na ukweli!
  Mwalimu Nyerere alisisitiza kwenye hotuba hiyo kwamba, ‘Kazi ya vyuo vikuu ni kuchimba na kutafuta ukweli.’ Bahati mbaya sana, siku hizi wasomi wengi wa vyuo vikuu wameacha kuchimba na kutafuta ukweli badala yake wanafanyakazi kwa kutumia ‘majungu’ na taarifa za kupikwa zisizo na ushahidi wa kisayansi na mantiki. Kibaya zaidi kwa baadhi ya wasomi waliyepewa dhamana ya kuatamiza fikra za usomi kwa kizazi kipya wamekuwa waoga wa kukosolewa na wanapokosolewa hujificha nyuma ya matumizi ya sheria na kanuni kandamizi katika kuficha akili zao tepetepe zilizoshikwa na ufisadi wa kimfumo huku wakitumia nafasi zao kuminya uhuru na kuzuia ukweli usijulikane.
Mwalimu Nyerere aliamini kwamba, ‘Nchi huhudumiwa na ukweli;’ na kwa msisitizo alisema, ‘Naamini kwamba nchi inataka vyuo vikuu, na wanafunzi na walimu wake, wasimame katika kweli kama wanavyoiona, bila kujali yale yatakayowatokea wao binafsi.’ Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa anasisitiza juu ya dhima ya vyuo vikuu katika kusimamia ukweli; wanafunzi na walimu kusimama ngangari katika kutafuta ukweli wanaouona kwa jicho la uchunguzi na mantiki ya hoja bila ya kuogopa! Kwa kuwa marazote mtu anaposimamia ukweli anaodhani ni kweli kuna kila sababu ya kufikwa na madhara kwa wale wasiyetaka ukweli ujulikane!
Kwa kutaka vyuo vikuu viwe vitivo vya kukosoa utendaji wa viongozi wa wananchi, Mwalimu Nyerere alisema, ‘Hakuna binadamu asiyekosa, viongozi na wananchi wanaoongozwa pia; inawezekana kwamba sisi tumekosea ama kwa sababu ya kutokujua ama kwa sababu ya inda ya watu. Ni sehemu ya kazi ya wale wasiobeba wajibu wa kuendesha mambo siku hata siku kutusaidia na kuwasaidia wananchi kwa ukomo wa uwezo wao. Na kufanya hivyo, wakati mwingine hulazimu kusema maneno yasiyowapendeza watu, mradi mnayaamini kuwa ni kweli.’ Sehemu ya hotuba hii inapatikana kwenye kitabu cha Uhuru na Maendeleo (Nyerere, 1973 ukurasa wa 14 hadi wa 15).
Kwa wale wote, pamoja na vyuo vikuu vinavyojinasibisha na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kutenga siku maalumu na au kuanzisha vigoda na hata kuweka wiki ya kumbukumbu; ni wajibu kujifunza mambo makubwa matatu kwenye hotuba hii. Mosi, umuhimu wa kuchimba na kutafuta ukweli kuhusu mazingira yanayotuzunguka na hususan kuangalia utendaji wa viongozi waliyepewa dhamana ya kuongoza umma. Pili, wasomi wanatakiwa kuwa na ujasiri wa kuwakemea viongozi wanaokwenda kinyume na maslahi ya umma ili kuwaelimisha juu ya wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa haki, uhuru na usawa. Tatu na mwisho, kujitoa mhanga (kama ikibidi) ili kutetea haki za wananchi na kufanya hivyo kwa uhuru, haki, ukweli na uwazi katika kufikia malengo ya ‘elimu lazima itumike kwa manufaa ya wote’ au ‘tujifunze kwa maendeleo ya watu.’
Nukta zilizoainishwa hapa zinaafikiana sawasawa kama alivyoandika aliyewahi kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ibrahim Mohamed Kaduma kwenye kitabu chake cha ‘Maadili ya Taifa na Hatma ya Tanzania: Enzi kwa Mwalimu Nyerere.’ Kaduma (2004) ameandika, ‘Mawazo haya (ya Mwalimu Nyerere) ni muhimu sana kwa Watanzania hasa katika kipindi hiki cha mmomonyoko mkubwa wa Maadili ya Taifa letu.’ Kaduma (2004, ukurasa wa 66) amesisitiza, ‘Inafaa wasomi wetu wamtafakari Mwalimu Nyerere kwa makini zaidi ili kuyaendea mausia (wosia) yake mema kwa ajili ya vizazi vijavyo.’
Siku hizi wasomi wetu wengi wanamtumia Mwalimu Nyerere kwa mtindo wa kutafuta sifa za kijinga na maslahi ya kujipendekeza kwa kulitaja jina la kiongozi huyu huku matendo yao yamejaa ufisadi, wizi na ubadhilifu wa mali ya umma! Wengi wamekuwa mstari wa mbele katika kutumia mali ya umma kwa matumizi binafsi kuliko kuwatumikia wananchi. Kwa mfano, baadhi ya viongozi wa vyuo vyetu vya umma badala ya kutafuta ukweli na kusimama kwenye uhuru na ukweli wanajipendekeza kwa viongozi wa siasa mafisadi ili wanufaike na ushirikiano kwa ahadi za kupata nafasi za kiutendaji serikalini ambazo ndizo zinazotumika kuendeleza ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo.
Mwalimu Nyerere (1962 na 1968) alifundisha kwamba, ‘Kujielimisha siyo maana yake kwenda shule; isipokuwa, kujielimisha ni kutafuta ukweli na kutumia ukweli kwa ajili ya maendeleo ya watu wote. Hata hivyo, vyuo vyetu vikuu siku hizi vina baadhi ya wasomi hususan waliyepewa madaraka ya kuongoza vyuo hivyo wenye ugonjwa wa upumbavu. Mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na anashauri dawa isiyo ya kweli (Nyerere, 1962: 8). Inasikitisha kuona baadhi ya wasomi na walimu wa vyuo vikuu wanayedhaniwa wamesoma na kuelimika wakishindwa kuyapatia matatizo ya wananchi majibu. Baadhi ya vyuo vikuu, wanafunzi wengi wa vyuo vikuu na baadhi ya walimu wa vyuo vikuu vya Tanzania wamekuwa sehemu ya mfumo wa ufisadi, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere, ‘nchi inanuka rushwa.’
Natambua kwamba, wengi hawapendi kuambiwa ukweli; na au wanapofanya mambo yao ya kibaradhuli, kifedhuli na au kifisadi! Wasomi wa sampuli ya wale wanaoogopa ukweli ni sawasawa na nyani anayechutama kuficha ngoko yake huku hatoweza kutembea hadi ngoko itakapoonekana! Usomi ni ukweli na ukweli ni uhuru; msomi wa kweli haogopi kukosolewa. Tujisahihishe, tuache upumbavu!
             
Mwandishi wa makala ni:

Bakari M Mohamed
Simu ya kiganjani: +255 713 593347
Barua pepe: maligwa1968@yahoo.com 

                       




RAIS WANGU KIKWETE UONGOZI WETU KAMA KISHADA TUTOKAKO TUENDAKO HAKUJULIKANI!
Rais wangu moja kati ya sifa nyingi za mtu dhaifu ni uoga. Anaogopa hata kivuli chake. Serikali ya Awamu ya nne ikisikia kuna mgomo au hasa maandamano, inatetemeeeka, utadhani ni utete dhaifu unaosukumwa na mkondo mkali wa maji ya mto yaendayo kasi! Yohani, ‘John Pombe Magufuli’ ni uzao halisi wa udongo wa nchi hii. Amefukua vya kufukua!
Katumbua jibu na sasa usaha unamwagika. Mwenye jipu yaani serikali, inanuka usaha mwili mzima! Kwakuwa Wahenga wenye busara walisema dawa ya jipu ni kulitumbua na kwakuwa Waziri wetu wa Ujenzi amelitumbua, basi wote wenye mapenzi mema wanapaswa kumpongeza kwa kazi njema aliyoifanya.
Rais wangu palipo na ukweli tutasema. Lazima tuusimamie ukweli hata kama kwa kuusema ukweli huo mjinga atasema tunamchukia mtu na mpumbavu atasema tumenunuliwa na mtu! Kuacha kusema ukweli kwa kuogopa kuonekana unamchukia mtu au kuogopa kusemwa umenunuliwa ni upungufu alionao mwanadamu dhaifu. Jasiri hatikiswi na hilo!
Magufuli sifahamiani naye, lakini ni mtu mwema gani asiyeujua utendaji kazi wake ulivyo mahiri? Tangu waende akina Sokoine na Mrema nani mwingine wakutolea mfano?
Huyu siyo malaika. Aliposhirikiana na genge la walanguzi tukulangua nyumba zetu, wenyewe wakiziita za serikali tulimlaani wote! Na kwa hilo hajasamehewa! Na hatasamehewa mpaka pale atakapowarudishia wananchi nyumba zao! Lakini kwakuwa hatuko hapa kuangalia sura za watu, tuko hapa kujadili utendaji kazi mahiri kwa maslahi ya nchi yetu na wananchi wake, anayefanya jambo jema kama alilolifanya Magufuli, kusimamia sheria za nchi, hatuna budi tumpongeze wote.
Kiongozi wa haki mwenye ufahamu timamu akiambiwa ukweli hata kama utamuumiza, atamheshimu aliyemwambia huo ukweli, akijua kuwa huyo ndiye aliye na mapenzi ya kweli naye. Na ikimpendeza atamtumia!
Rais wangu wapinzani wanapokwambia waondoe mawaziri wanaokupotosha hawamchukii mtu wala hawawachukii hao mawaziri! Wanakutakia mema Rais wangu! Hawataki uonekane wa ajabu mbele ya watu wako! Tunaoishi na wananchi huku mitaani, vijijini na mashambani tunaambiwa mengi. Ningekuwa na faragha na wewe mengine ningekuwa nakunong’oneza, ili ukinieleza niwaeleze wapate kukuelewa kwa maana wako wanaokupenda! Kwa kuwa sina faragha na wewe nakuwekea maneno ya wananchi wako hapa ili ukiyasoma ujue ni picha gani wanaokuzunguka wanakutengenezea mbele ya wananchi!
Mwanamwema kutoka Iringa aliniandikia ujumbe ambao na mimi nauweka hapa vilevile alivyoandika! Aliandika, “Mwalimu nimesikitishwa sana na hotuba ya rais iliyoangaliwa hata na watoto wadogo. Hivi kwa nini anamshambulia mwananchi wake kwa maneno makali kama yale? Halafu kwa nini kila kitu anasema ‘nimeambiwa’? Falsafa yake ya mbayuwayu imemshinda? Sasa tena tunaambiwa kumbe hata mswada wenyewe hajausoma. Kazi tunayo. Nchi za kiafrika haziendelei na moja ya sababu ni kuongozwa na watu wenye kuambiwa.”
Rais wangu usipokuwa na pupa utaona kuwa watu wako wanakujali lakini unawakatisha tamaa! Dunia na Ulimwengu vinatambua hivyo! World Happiness Report 2013 iliyoandaliwa na kundi la wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa imedai kuwa Watanzania ni miongoni mwa watu wasio na furaha na waliokata tamaa hapa Duniani!
Ndugu Rais yaliyojiri katika sakata la wenye malori na serikali limezidi kuwakatisha tamaa Watanzania. Iliandikwa, ‘Pinda amuonya Magufuli’, wengine wakaandika, ‘Serikali yamzima Magufuli’. Wananchi wakabaki kuulizana, hivi Pinda na Magufuli wako serikali mbili tofauti? Ni serikali gani hii yenye viongozi wenye kauli tofautitofauti? Hawakutani kwenye Baraza la mawaziri kuweka msimamo wa serikali?
Waliosema serikali inapasuka mwanzoni sikuwaelewa. Utoto siyo uchache wa miaka ya kuzaliwa peke yake! Wala kufanya upuuzi siyo lazima umtukane mtu. Kwakuwa hawa ni waheshimiwa huwezi kuweka neno watoto au wapuuzi. Isipokuwa viongozi wa serikali moja kuonekana mbele ya wananchi kama wanatunishiana misuli, ni vyote viwili, utoto na upuuzi!
Rais wangu Magufuli anasema anazilinda barabara zetu zisife haraka! Mpaka hapa kuna ubaya gani? Je, mamlaka hayo anayo? Kaonyesha sheria iliyotungwa na Bunge kihalali kabisa! Kumbe mamlaka anayo kufuatana na sheria! Sasa ndugu Rais huyu anayemzima Magufuli au kumuonya yeye alisomea wapi?
Kwa mdomo wake Waziri Mkuu wetu anasema, “Hatua zilizochukuliwa na Dk Magufuli kufuta vifungu vilivyokuwa vikiruhusu asilimia tano zilifuata sheria. Tatizo lililojitokeza ni kutoshirikisha pande zinazohusika ili kushauriana na kupata uamzi wa pamoja”. Jamani sheria ikishatungwa mnashauriana nini tena?
Akaongeza, “Sasa suala la asilimia tano, lilitokana na ombi la wadau wa usafirishaji kwa aliyekuwa waziri wa Ujenzi miaka ya nyuma na haikuwa sheria kamili. Limeondolewa baada ya kuonekana linatumiwa vibaya.” Kudai kwa nguvu wakati huna sheria nikufanya fujo!
Bado anakiri kuwa limeondolewa baada ya kuonekana linatumiwa vibaya! Yaani wenye malori walitumia vibaya ombi lao. Magufuli kuona hivyo amelifuta. Kwa maelezo haya ya Waziri mkuu Magufuli amekosea wapi? Kama ombi hilo ovu liliridhiwa na Waziri wa Ujenzi wa miaka ya nyuma kwa maslahi ya nchi au kwa maslahi ya wenye malori na waziri mwenyewe haijulikani. Kinachojulikana ni kwamba waziri huyo hivi sasa serikali imemfikisha mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa ofisini siku hizohizo za nyuma.
Waziri mkuu anasema kosa la Magufuli ni kuilinda hiyo sheria bila kuwashirikisha wanaoivunja. Jamani, unapomkamata mwizi unamshirikishaje? Unashauriana naye nini ili mpate uamuzi wa pamoja kama siyo kutaka kumwomba rushwa?
Mzee Peter Kisumo anasema, “Chama kimebaki cha walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi!”
Rais wangu bado Waziri mkuu bila sababu ya msingi anaunda tume sijui kamati ambayo hata hivyo haina uwezo wa kuifuta wala kuirekebisha sheria hiyo! Huku ni kufuja kodi ya wananchi? Ndugu Rais ni hivi majuzi tu wananchi kwa huzuni kubwa wameshuhudia mwandishi wa habari Ufoo Saro, baada ya kujeruhiwa vibaya kwa risasi kadhaa wanawema walimkimbiza hadi Hospitali ya Serikali ya Tumbi lakini akakosa huduma ya matibabu kwasababu Hospitali hiyo haikuwa na mashine ya Xray.  Kwanini fedha zitakazotumika na tume hii na tume nyingine za aina hii zisingetumika kununulia mashine ya Xray kwa Hospitali hii? Umuhimu wa Hospitali ya tumbi uko wazi. Inapokea majeruhi kila siku watokanao na ajali za mara kwa mara zitokeazo katika barabara hii katili ya Morogoro! Mungu huyu! Maisha ya wananchi hayana maana mbele ya wenye malori!
Serikali inayojiendesha bila kutegemea ufadhili wa wafanyabiashara hasa wakati wa kampeni, wenye malori wangepata wapi kiburi cha kugoma? Sheria kama haifai hurudishwa Bungeni ikafutwe au ikarekebishwe huku kazi zikiendelea! Wakati wa Uwaziri mkuu wa Sokoine au wakati wa Mrema, mwenye lori gani angethubutu kuinua pua yake juu? Serikali kuruhusu kikundi fulani cha watu, wawe wenye malori au wenye asili fulani, waendelee kuvunja sheria halali huku wananchi wengine wakiona ni mfano halisi wa uongozi mbovu! Bila kufahamu serikali inawasukuma na wengine wavunje sheria zinazowakera. Chanzo cha maandamano na migomo isiyokwisha ni uongozi mbovu!
Ndugu wananchi kitabu cha mwalimu mkuu wa watu kinaelekeza wazi kuwa jiandaeni kupokea fedha zitakazochangwa na hawa jamaa. Mkiletewa wakati wa kampeni zichueni, lakini kura msiwape! Kuita wenye malori ili muafikiane wakati sheria iko wazi ni kielelezo cha uongozi ulioshindwa kuongoza! Yanini Kuwa na kiongozi wa namna hiyo? Tumeliona hili kwenye tozo ya simu. Baada ya kusikia kelele za wananchi ikaamriwa mawaziri na wamiliki wa kampuni za simu au wadau wakae pamoja wafikie muafaka. Kiko wapi! Uongozi ulioshindwa!
Rais wangu uongozi wa nchi unapokuwa laini kiasi hiki, wananchi wanapoletewa habari za kutisha kuwa magaidi wameshamiri nchini mwetu matumaini yao wayaelekeze wapi? Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, linawashikilia vijana 11 kwa tuhuma za kukutwa mafichoni katika msitu wa mlima Makolionga wilayani Nanyumbu wakifanya mazoezi ya kijeshi. CD walizokutwa nazo ni za kundi la kigaidi la Al Shabaab. Zinaonyesha watu wakichinjwa, mauaji ya kiongozi wa Al Qaeda Osama Bin Laden, Zindukeni Zanzibar, kuaandaa majeshi, mauaji ya Idd Amin na Mogadishu Sniper.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara Zellote Stephen anasema watuhumiwa walikamatwa, baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema. Wananchi wanauliza bila wasamaria wema magaidi hao si wangemaliza mafunzo yao halafu wakaenda kwenye utekelezaji bila polisi kuwa na habari? Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilikuwa wapi?
Katikati ya habari hizo zinakuja habari nyingine zinazoarifu kuwa, Ramadhani Twaha mkazi wa mtaa wa Kirumba jijini Mwanza amefikishwa katika mahakama ya Mkoa wa Mara. Anatuhumiwa kukutwa akisambaza CD zenye machapisho ya kigaidi katika msikiti wa Ibadhi ulioko mjini Bunda ambazo zina mafunzo ya kijeshi na zinazochochea vurugu. Matukio haya mawili yanaashiria jinsi mtandao wa kigaidi ulivyosambaa nchini. Zinaingizwa vipi na kusambazwa vipi nchini? Nani wanaingiza CD hizi? Usalama wetu ni wa mashaka matupu!
Mafunzo  katika msitu wa Makalionga yalifanywa kwa muda gani? Je, kundi hilo la watu 11 lilikuwa ni kundi la ngapi? Ni katika msitu wa Makalionga tu ndiyo mafunzo hayo yanakofanyika? Je, waliyokuwa wanapewa mafunzo waliambiwa malengo ya mafunzo hayo? Walimu wao wako wangapi na wako wapi? Wanafadhiliwa na nani? Je, huu siyo mwanzo wa vita vya msituni?
Ndugu Rais raia kutoa taarifa kama hiyo kwa jeshi la polisi ni muhimu na ni ishara ya uzalendo kwa nchi yake, lakini huko kuwe ni kusaidia tu! Hilo ni jukumu la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kugundua vyenyewe hatari zinazolinyemelea Taifa letu! Liwalo na liwe, wenye malori tu hivi! Magaidi mtawaweza vipi?
Rais wangu tunaacha ya kwetu tunadandia ya wengine. Viongozi wako kimbelembele kusaka sifa za bei poa. Nchi yetu ilipopata nafasi adhimu ya kulihutubia Baraza la Umoja wa Mataifa baadhi ya wananchi walisikika wakiusikitikia muda ambao kwa maoni yao uliotumika vibaya kuisema ICC badala ya kuyapa nafasi matatizo lukuki yanayoisibu nchi yetu! Nchi yetu ina ugomvi gani na ICC?
Rais wangu ni uzalendo kwa bara la Afrika na Waafrika wenzetu ndiyo vinatusumbua? Hapana! Ni mihemko ya moyo kwa kujihisi tuko kwenye foleni ya kwenda huko kutokana na tunayoyatenda nchini mwetu? Hili linawezekana! Kwanza ziliisha sikika habari kuwa kuna baadhi ya matukio ya kinyama yaliyotokea nchi mwetu ambayo taarifa zake zinatumwa huko! Kujitoa ICC hakuwezi kuzuia tusihukumiwe na mahakama nyingine. Kinachoweza kuzuia tusihukumiwe ni kutotenda unyama dhidi ya raia wetu, kama tunaona tunatenda.
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bwana Koffie Annan amesema ‘itakuwa ni alama ya aibu’ kwa bara la Afrika iwapo litajiondoa katika mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC. Amesema ikiwa viongozi wa Afrika wataipinga na kuipiga vita ICC na kujiondoa, itakuwa ni fedheha kubwa kwa kila mmoja wao na nchi zao. Tumwombee kwa Mungu Rais wangu asije akawa mmoja wao kati ya marais wanaotaka kuziletea nchi zao fedheha hii kubwa! Mwenye fikra ya kulipeleka wazo hili Bungeni huyo ni mufilisi, hafai kuwa kiongozi wetu! Tuna akili gani kubwa ya kutaka kuunga mkono kujitoa ICC kuliko akili ya viongozi waliotutangulia, waliosaini mkataba wa Roma wa kujiunga na ICC?
Bwana Annan amewashutumu viongozi wa Afrika kwa kulinda maslahi yao binafsi na si kwa Waafrika wote huku akisisitiza kuwa njama za nchi za Afrika kutaka kujiondoa ICC ni ishara dhahiri kuwa kuna desturi ya kutoheshimu sheria.
Watuhumiwa wanaokabiliwa na mashtaka katika mahakama hiyo wamefikishwa kama watu binafsi na si kama Bara la Afrika, hivyo dhana kuwa ICC ina dhamira ya kuwaandama viongozi wa Kiafrika siyo sahihi!
Mtu mzima tena bila aibu anasema kati ya walioshitakiwa 30 waafrika ni 27. Hawa ndiyo wale ambao akishtakiwa mhalifu, kama dini yao ni moja anasema wa dini yetu tunaonewa! Kiongozi kuishiwa fikra ni hatari sana. Muhimu hapa ni kujua je, walioshtakiwa ni wahalifu? Muhimu siyo rangi ya ngozi yao.
Mwanamwema Jaji mpya wa Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu (ICC) Dk Steven Bwana amesema viongozi wa nchi za Afrika wanaotaka kujiondoa kwenye mahakama hiyo, wana lengo la kuficha uovu uliopo katika nchi zao kwani baadhi yao wanajifanya miungu watu!
Amesema, “Afrika kuna viongozi wazuri, lakini tusifiche ukweli wapo waovu, wengine nusu miungu wanaopenda kila kitu kiwe chao, hili halikubaliki. Nchi za kiafrika kujitoa ni aibu, sababu zilizotufanya tujiunge zipo, tunataka kujiondoa kwasababu tunadhani ICC inatufuatilia tunapofanya makosa, ICC inatimiza wajibu, haiwadhalilishi viongozi wa Afrika, watafika kote.”


PASCHALLY MAYEGA
TEL 0788 37 27 87

1 comment: