Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

NACHEKA KWA UCHUNGU; TANZANIA NA UONGOZI WA DAMU



Nacheka kwa uchungu Jan 14
Tanzania na uongozi wa damu
NIMELAZIMIKA kuyakumbuka maneno mazito aliyotoa Spika wa Bunge la Tanzania Anne Makinda wakati wa msiba wa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa aliyefariki mwanzoni mwa mwezi huu nchini Afrika Kusini.
Mbele ya umati wa waombolezaji, Makinda alisema ingekuwa ni amri yake angekufa mtu (kwa namna nyingine waziri) mwingine lakini sio Mgimwa!
Sitaki kurejea namna alivyoshambuliwa kwa maneno, na mijadala ilivyotamalaki katika vyombo vya habari kuhusiana na kauli hiyo.
Kilichonisukuma kukmumbuka maneno ya mama Makinda ni kile kinachoendelea katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Juzi nililazimika kushuka katika mji huo mdogo nikitoka Musoma kikazi ili niwe kama Yule Thomaso tunayemsoma katika Biblia ambaye alipoambiwa Yesu Kristo amefufuka alikataa hadi amwone kwa macho yake na kugusa makovu ya misumari aliyoshindiliwa msalabani.
Mji mzima wa Bunda unatikisika kwa sasa kutokana na kampeni za uchaguzi mdogo wa diwani wa kata ya Nyasura, baada ya kiti hicho kubaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wake Zamberi Ngobayi (Chadema).
Katika kampeni hizi ambazo vyama viwili, Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni dhahiri kitamsimamisha Alex Mwikwabe ambaye inadaiwa alipatikana baada ya wagombea wawili wa awali kujitoa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichomsimamisha Magambo Webiro zinaendeshwa katika hali inayodhihirisha ubabe, vitisho, hila na ubabaishaji wa hali ya juu.
Nimeshuhudia kampeni za kuchafuana majina, hadhi na heshima ya wagombea zikifanywa na watu wazima kabisa, tena viongozi waliostahili kuionesha jamii kuwa wanawathamini watanzania na wanaheshima matakwa ya watu ya nani awe kiongozi wao.
Nimeshituka zaidi hata baada ya kuona upande mmoja ukijaribu kuwadanganya wapiga kura kwa hoja za kipuuzi za kwamba mgombea wa Chadema ni mganga wa kienyeji na hivyo hafai kuchaguliwa. Tena wanaosema hivyo ni viongozi wengine wa CCM ngazi ya wilaya. Ni hoja ya ajabu kwa sababu hakuna popote katika katiba ambapo mtu anayetibu watu kwa kutumia dawa za kienyeji haruhusiwi kuchaguliwa na kuwa kiongozi. Na kwa kutambua hilo, hao hao wanaosema hivyo, wanasahau kuwa mmoja wa wabunge wake wa bunge la Muungano ni mganga wa kienyeji ambaye katika uchaguzi uliopita alimbwaga daktari mwenye PhD!
Je viongozi wa CCM wa wilaya ya Bunda kwa hoja hiyo ya uganga iliyokanushwa na mhusika mwenyewe, wanataka kusema kuwa wapiga kura Korogwe vijijini walifanya kosa kumchagua mganga wa kienyeji pia Prof Maji Marefu (CCM)kuwa Mbunge wao?

Na katika namna ya kushangaza, baadhi ya viongozi wa CCM sasa wanadaiwa kumwandaa mwana mama mmoja atakayetembea kata nzima kueleza namna mgombea wa Chadema alivyotapeli kwa kutumia uganga wake. Mama huyo anadaiwa kuwa atatangaza jinsi mgombea wa Chadema alivyomtapeli mamilioni ya fedha ili amtibu!
Fikiri tu kwamba suala la uganga limechukua nafasi kubwa katika kampeni huku upande wa pili yaani Chadema, badala ya kupuuza propaganda hizo, nao wamejikita kujibu hoja na kusahau kutangaza sera.
Mbali na hoja ya uganga, wapinzani wa mgombea huyu wameingiza ubaguzi wa kikabila na kimaeneo. Wanajaribu kuwaaminisha wapiga kura kuwa ni hatari kumchagua mgombea huyo kwa sababu sio mzawa wa Nyasura bali mhamiaji aliyefukuzwa kutoka Kata nyingine ya Kunzugu katika kitongoji cha Bokole.
Kana kwamba hoja hizo kwa viongozi wa chama tawala hazina madhala kwa taifa, sasa wanatuhumiwa kuibua jambo baya zaidi ambalo limeanza kuwatisha na kuwapa kiwewe baadhi ya wananchi sio wa Kata ya Nyasura tu bali wilaya nzima ya Bunda.
Hili ni kuwepo kwa tuhuma kwamba zipo njama za kutaka kumkamata mgombea wa upinzani na kumbambika kashfa ya kuiba nyaraka sa siri za serikali.
Inadaiwa kuwa hizo zinazoitwa nyaraka za siri za serikali, zile zinazohusiana na sakata la ardhi katika wilaya ya Bunda.
Kwamba mgombea huyo anatembea na nyaraka za mikataba feki iliyotumika kutaifisha ardhi ya mlima Balili inayosemekana ni mali halali ya shule ya msingi Balili na pia ya Kanisa la Wasabatho.
Inasemekana tuhuma hizo zinawagusa baadhi ya watendaji wa wilaya na mkoa, akiwemo mkuu wa mkoa mmoja hapa nchini.
Nyaraka hizo zinazoitwa za siri, pia zinadaiwa kuwa ni zile zinazofichua kile kinachoitwa tuhuma za waziri mmoja mwandamizi wa serikali ya CCM anayedaiwa kuchukua kwa mabavu sehemu ya ardhi ya shule moja ya sekondari.
Kampeni hizo za uchaguzi wa udiwani kata ya nyasura na zigine 28  nchini utakaofanyika Februari 9,2014, zinaashiria jambo moja tu. Umwagaji wa damu!
Hali sio shwari, viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wameungana na lugha inayotamba sasa ni kwamba..’heri kufa kuliko kuonewa, kuliko kudhulumiwa’
Wapenzi na wanachama wa CCM, nao wanatamba na kauli,….’kwa gharama yoyote lazima tukomboe kata yetu”.
Kauli hizi sio njema hata kidogo hasa zinapopaliliwa kwa nguvu na wanasiasa wakomavu ambao chama chao kinaongoza nchi. Ni kauli ambazo zinaonesha kuwa uwezekano wa kupata viongozi wazuri, wakweli, waadilifu na wachapakazi kama alivyokuwa waziri Mgimwa ambaye Spika Makinda hakutaka afe ni ndoto.
Inatia uchungu zaidi ikiwa leo watanzania wanazidi kushuhudia haki na demokrasia ikikandamizwa kwa gharama za walipa kodi, ili tu watu wanaowataka wachaguliwe kuwa viongozi wa watu hata kama hawana sifa na hawapendwi.
Spika Makinda hata kama kauli yake, haikuwa njema masikioni mwa watu, ajue kuwa chama chake kitasaidia kupatikana kwa viongozi kama marehemu Mgimwa kikiacha mizengwe, hila, ujanja wa kishamba kuendesha kampeni zisizo na mashiko.
Spika Makinda ajue kuwa ni jukumu la CCM kushika na kusimama kama ‘baba wa demokrasia’ na hivyo, kuacha ghiriba za aina yoyote ile katika chaguzi ziwe ndogo ama kubwa.
Kampeni za kudhalilisha, kukomesha na kutesa wasiokuwa wapenzi na wanachama wa CCM na kulazimisha kumweka mtu wa ovyo madarakani kamwe haziwezi kuleta watendaji bora wa serikali. Haziwezi kulipatia taifa madiwani, wabunge na mawaziri bora.
Kampeni zinazosukumwa na ubabe, uonevu, wizi wa kura na hata kumwaga damu za wananchi, haziwezi kamwe kuleta manufaa katika nchi zaidi ya machafuko na umwagaji damu. Kauli ya wana wa Bunda kwamba liwalo na liwe ni ishara ya kwamba watu wamechoka kunyanyaswa. Ni kauli za waliokosa matumaini dhidi ya serikali yao, na hawaitaki.
Spika Makinda atatamani wafe mawaziri wengi ikiwa leo hii katika kampeni za uchaguzi wa marudio ya udiwani, polisi wanatumika kupiga na kufungulia watu kesi za kubambika ili tu CCM ishinde.
Makinda ajue kuwa kama kweli ana uchungu na taifa hili, basi awaambie viongozi wenzake kuwa wanalo jukumu la kuheshimu matakwa ya watu. Wanalo jukumu la kujua na kutekeleza kile watanzania wanachokitaka na sio kuwalazimisha kwa mbinu chafu hata za kumwaga damu.
Bado watanzania wanakumbuka jinsi viongozi wa upinzani walivyofunguliwa mashitaka ya ovyo, kupigwa, kudhalilishwa na kuteswa kisa tu walisimama kuwania uongozi katika chaguzi mbalimbali. Ni viongozi hao hao wa CCM ambao Spika Makinda ni mmojawao, ambao wametumia nguvu na maarifa mengi kuwaaminisha watanzania kuwa wapinzani ni watu wa ovyo, hatari na wanaotakiwa kuogopwa kama ukoma.
Kibaya zaidi, Spika Makinda mwwenyewe mara nyingi tu ameruhusu na kushiriki kukandamiza haki za wapinzani hata katika masuala ya msingi ya nchi. Kiti chake kimeshiriki mara nyingi kunyamazisha sauti za watanzania kupitia wabunge wao.
Wabunge wangapi wa upinzani wamekandamizwa walipokuja na hoja zenye maslahi ya nchi? Wabunge wangapi wa upinzani wameitwa wazushi na waongo walipoibua tuhuma dhidi ya mawaziri? Kama Kiti cha Spika kingeruhusu hoja kujadiliwa na hatua madhubuti kuchukuliwa, leo hii uovu na uvundo katika sekta ya elimu ingefikia hatua hii?
Ni mawaziri wangapi walilindwa na kiti cha Spika pale walipotoa majibu ya uongo, ubabaishaji na yenye hasara kwa taifa? Kwa nini kiti cha spika kiliwakingia kifua alafu leo kiti hicho hicho kinalia? Dhihaka?
Inatia uchungu basi tunaposikiaNi ajabu kwamba leo eti analiachuklia wapinzani na kuwanachama makini na anayeheshimu demokrasia hawezi kufurahia ushindi uliopatikana kwa kukandamiza na kuonea watu.

No comments:

Post a Comment