Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

NACHEKA KWA UCHUNGU;TAIFA LIKIONGOZWA KWA SIASA CHAFU





Nacheka kwa uchungu: jan 8,2014
Taifa likiongozwa kwa siasa chafu
SIKUTAKA kamwe kujadili kinachoendelea ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini, ali maarufu kama Chadema.
Sikutaka kwa sababu, taifa langu linayo mambo mengi makubwa ya kujadili na kuyatendea kazi. Mambo ya msingi yanayoweza kuwakomboa wanyonge na umasikini wao wa kukosa elimu bora, afya bora, maisha bora na usalama wa uhakika!
Nimelazimika kuyajadili katika mada ya leo kwa sababu yanayotokea ndani ya Chadema yanaelekea kwa kasi kubwa kuchukua sura ya kitaifa. Sio siri kwamba sasa yanashabikiwa kwa waziwazi ama kwa kificho na umma wa watanzania, baadhi yao wakiwa wanasiasa wakongwe, wakubwa kabisa na wengine wakiwa watendaji waandamizi ndani ya serikali ya CCM.
Mtu waweza kucheka kwa uchungu unapofikiria siasa za Tanzania zilivyo kwa sasa. Ni kama igizo la mwendawazimu! Linaloumiza zaidi, ni kwamba ‘upuuzi’ huu wa siasa ninazothubutu kuziita za kishamba zinaligharimu taifa na kuleta hasara kubwa ambayo kwa bahati mbaya, hakuna anayeiona.
Zinagharimu muda wa watu kufanya kazi za kuzalisha mali. Zinagharimu fedha halisi za watanzania kwa kuwa, wanaoziendesha wanatumia fedha kwa kuliwasiliana, kulipana posho na hata ‘kuhongana’ ili tu mambo wanayotaka yaweze kwenda.
Tukio la kuvuliwa madaraka wa Zitto Kabwe na tishio la kunyang’anywa uanachama sio la kwanza katika siasa za Tanzania. Ukiachilia mbali wale waliofikwa na jambo linaloelekea kumtokea Zitto ndani ya upinzani, wapo waliopatwa na hayo enzi za TANU na CCM chini ya utawala wa siasa ya chama kimoja.
Wengine walilazimishwa kujiondoa wenyewe huku wakificha sababu halisi za kujivua kwao madaraka. Wakabaki wanaishi kama wanachama wa kawaida kwa miaka mingi. Wapo waliorudishiwa nafasi za uongozi baada ya kupita miaka kadhaa.
Tunakumbuka jinsi wanasiasa na viongozi wengine walivyotimuliwa uongozi na uanachama baada ya kugoma kujiuzulu wenyewe. Wapo baadhi kwa hofu ya usalama wa maisha yao, walilazimika kuondoka nchini, na wengine waliendelea kuishi kwa kufanya shughuli nyingine za maendeleo na maisha yao yakasonga mbele kwa mafanikio makubwa kuliko walivyokuwa katika ulingo wa siasa.
Yaliyopendeka haya, watanzania hawakusikia malumbano yaliyojaa matusi, kashifa, dharau, udhalilishaji na aibu kubwa kama tunayoshuhudia sasa.
Sitaki kusimama upande wowote, lakini swali ambalo watanzania wanatakiwa kujiuliza bila unafiki ndani yake, ni kwamba iweje leo wanaotuhumiwa kusaliti chama chao, ndio wanaibuka na kututangazia ‘uozo’ wa viongozi wenzao ndani ya chama?
Kiongozi anayejaribu kuwashawishi watanzania waamini kuwa wenzake pia ni waovu kiasi cha kuzua hata utata wa kumiliki nyumba za umma, kana kwamba watendaji wakuu wa shirika hilo nao ni wapuuzi kiasi cha kuingia katika mkataba tata, anatushawishi tumuaminije?
Watu makini wanaposikia kwa mfano, watuhumiwa wa kinachoitwa usaliti sasa wakirusha kete wakidai eti  kiongozi fulani naye alipewa fedha mwaka 2005 wakati wa uchaguzi mkuu, wanajiuliza huyu anayetoa tuhuma hizi leo alikuwa wapi kuyasema miaka yote hiyo?
Ikiwa kwa mfano pana ukweli wa tuhuma za viongozi wenzake anaowataja kupokea fedha kutoka kwa kiongozi wa CCM, sababu zipi zilimfanya afumbe mdomo miaka yote hiyo, hadi leo anazitoa baada ya kutishiwa kufukuzwa? Mtu gani mwenye akili timamu atamwamini tena mwanasiasa wa aina hii. Mtu gani mwenye busara ataendelea kusadiki yale anayosema sasa na yale atakayotamka?
Lakini kinachotisha zaidi, sasa zinapotolewa tuhuma zinazolenga kubainisha kuwa hata kifo cha Chacha Wangwe kilikuwa na ‘mkono’ wa mtu!

Ni siasa zinazotia uchungu mkubwa kuona kwamba, kiongozi anayetaka watu wamwamini anatangaza waziwazi na kurejea leo mwaka 2014
matukio ya 2005! Alikuwa wapi siku zote? Kipi kilimzuia asiseme? Na kwa nini aseme leo baada ya kutimuliwa?  Ina maana kama asingechukuliwa hatua angenyamaza? Na kwa nini alikuwa bingwa wa kurusha makombora kwa viongozi wa CCM huku akijua (kama ni kweli) kwamba na wenzake wanapokea fedha kutoka huko huko CCM?
Nacheka kwa uchungu kuona mtu msomi, anayetaka demokrasia ya kweli anaibuka na upuuzi huu leo hii, na katika nyakati ambazo watanzania wamepigika kimaisha. Ni watu wasiofikiri sawa sawa watakaomuamini tena. Ataamini tu na watu waliochoka kimaisha, wanaokubali kuwa kapu la kubeba kila aina ya umbea, na walio tayari kusema, kutenda na kushabikia lolote na chochote kwa sababu wanajua wanapewa pesa. Watu wa ovyo ovyo tu!
Inatia hasira kuona kuwa wakati tunawajibika kujadili mambo mazito ya mustakhabari wa taifa letu, anasimama kiongozi anayetaka kuwalisha watanzania ajenda za mambo binafsi ya mtu na familia yake.
Ni upuuzi mkubwa kwa watu waliokomaa kisiasa kujadili uzinzi bungeni ama kwenye majukwaa, bila ushahidi makini na huku ukitambua kuwa jambo hilo sio tu litamdhalilisha anayetuhumiwa, bali familia yake, ndugu na jamaa zake.
Zitto anataka kuwaambia watanzania kuwa wanahitaji kujua nani mzinzi na nani mtakatifu? Yaani watanzania kweli wanafikishwa mahali pa kulishwa utumbo wa inzi kiasi hiki?
Tuseme ukweli bila unafiki. Hivi nani anastahili kulalamika katika hilo linaloitwa sakata la uzinzi wa Mbowe? Ni Mwigulu Nchemba aliyesema bungeni na Zitto anatutangazia sasa, au mume wa mbunge huyo na mke wa Mbowe? Kwa nini wamenyamaza? Mtu makini, atanyamaza. Hawezi kujibu ujinga. Ndivyo walivyofanya mke wa Mbowe na Mume wa Joyce!
Lakini pia mtu unajiuliza, hawa wanaowatuhumu wenzao kwa uzinzi, wao wana usafi kiasi gani basi? Ni malaika wao?
Katika haya yanayoendelea, inahuzunisha zaidi watanzania wanapobaini kuwa nyuma ya mgogoro huu, kuna mkono wa baadhi ya wanasiasa waliofilisika wa upande wa pili.
Tulishuhudia namna baadhi ya wanasiasa na viongozi wa CCM wakitoa shutuma, matusi na lawama kwa uongozi wa juu wa Chadema kwa kumwondoa Zitto katika madaraka. Swali la kujiuliza, kiliwauma nini? Walikuwa na maslahi gani na nafasi za kiongozi huyo ndani ya Chadema? 
Hivi akitokea mtu akasema, waliumia kwa sababu walijua mtu aliyempandikiza amebainika na ndio maana wanaumia atakuwa amekosea? Nisaidieni hivi Yule waziri wa serikali aliyetamba kuwa Chadema kitakufa kabla ya 2015, alikuwa anajivunia nini?
Ndio alitamka waziwazi na tukasikia akitamba kuwa atahakikisha chama hicho pinzani kinakufa! Waziri mzima, ambaye angetegemewa asimame na kuwaeleza watanzania kuwa nia yake ya chama chake ni kuhakikisha adui ujinga, njaa, maradhi na ufujaji wa mali ya umma vinakufa kabla ya 2015, anakurupuka na kusema Chadema inakufa, kana kwamba ndio kansa ya maendeleo yetu anastahili kuendelea kuwa madarakani kweli kama tuko makini na uhai wa taifa letu?
Je, ni kweli kwamba taifa hili limefikishwa mahali pa watu wanakufa hospitalini kwa kukosa dawa, watoto wanafeli ovyo kwa kukosa elimu bora, walimu wanapiga mihuri ardhini (wanatembea peku) na madaktari wanagoma kwa sababu kuna chama kinaitwa Chadema?
Leo hii mangapi yanatokea hapa nchini, tena mabaya yanayoumiza na kuua utu na heshima yetu kitaifa na kimataifa?  Leo hakuna usalama wa uhakika hapa nchini. Mtu unalala kwa hofu, unatembea kwa hofu, unakunywa kwa hofu,na katika hali isiyoweza kusemeka sasa wakristo wanakwenda makanisani kwa hofu kubwa!
Hawana uhakika wa kurejea nyumbani kwa usalama.  Wanasali huku wanalindwa utafikiri ni wafungwa. Wamepigwa mabomu kanisa, wakiimba, wamepigwa risasi wakienda kusali, wakamwagiwa tindikali bila hatia yoyote.
Leo watu wanakwiba fedha za umma mchana na usiku. Wanahabari tunawafichua, lakini hatuoni hawa wanaoshambulia wenzao wakichukua hatua hata za kukemea tu. Hawaoni uchafu unaofanywa ndani ya nchi. Hawaoni wanyama wanavyoangamizwa. Wao ni kushambuliana tuu!
Badala ya watu kujadili haya, na kujua nani katufikisha hapa achukuliwe hatua, watu wanaibuka na visa vya ovyo na tuhuma za kitoto kabisa za fulani anazini na mke wa fulani. Si mwacheni aliyechukuliwa mke ama mume alalamike?
Watu wazima, wasomi kabisa na watu wanaoonekana kuwa na busara, wanashinda kutwa nzima wakihangaika namna ya kuwazushia wengine tuhuma za kipuuzi na kujiapiza namna watakavyoizika chadema.
Nacheka kwa uchungu kila ninapowaza aina ya viongozi na wanasiasa sasa hawana muda wa kutafuta mbinu za kuinua uchumi wa taifa letu, njia za kuwafanya watanzania waondokane na umasikini,kuokoa rasilimali za nchi zinazoporwa usiku na mchana, badala yake kama mazuzu wanahangaika na vyama vya upinzani na kuendesha siasa za kuchafuana!

No comments:

Post a Comment