Hellen Kijio- Bisimba:
Tanzania iwe na Rais Mwanamke
Ni mmoja kati ya wanawake wasomi wakubwa hapa nchini, mwenye kiwango cha elimu ya udaktari katika sheria. Ni mwana harakati maarufu na mashuhuri ambaye msimamo na kauli zake katika kupigania haki zimewatisha na kuwatikisa viongozi walafi, wabadhilifu na wazembe.
Ni mtu anayestahili
kupewa hadhi zote za usomi, kwa maana kwamba sio tu katioka sheria, bali
amebobea pia katika mambo ya elimu hususan katika shule za sekondari na vyuo. Akazama
zaidi katika ujuzi na weledi katika masuala ya haki za watoto, na mambo ya
ardhi
Ujasiri wake katika
kupigania mambo ya msingi, haki, maendeleo ya wananchi hususan makundi
yanayoonewa, wakiwemo wanawake na watoto, uliusukuma Umoja wa Mataifa kumpa tuzo
ya mwanamke jasiri mapema mwaka jana.
Huyu ni Hellen
Kijo-Bisimba, ambaye ni mmoja ya matunda ya shule ya sekondari ya wasichana ya
Weruweru iliyoko mkoani Kilimanjaro, iliyotimiza miaka 50 tangu kuanzishwa
kwake.
Kabla ya kuingia katika ulimwengu wa kazi na wajibu
nyingine za kuwa mke na mama wa familia, Hellen Kiji-Bisimba aliyezaliwa Oktoba
10, 1954 amepata kufanya kazi sehemu mbalimbali, kuandika vitabu na machapisho
kadhaa yanayohusu elimu, haki za watoto na ardhi.
Hakuna shaka kwamba mafanikio makubwa aliyonayo,
yanatokana na msingi mzuri na imara wa elimu ya sekondari aliyoipata katika
shule ya sekondari ya wasichana Weruweru alikosoma hadi kidato cha nne kisha
kufaulu na kuingia kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Korogwe alikohitimu mwaka 1974.
Alipata stashahada ya elimu kutoka chuo cha ualimu, mwaka
1977, kabla ya kubadilisha taaluma na kuchukua masomo ya sheria toka chuo kikuu
cha Dar es salaam na kupata shahada yake mwaka 1985.
Akisukumwa na kiu ya masomo, alihitimu shahada ya uzamili
katika sheria kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam mwaka 1994 na akatimiza ndoto
yake baada ya kupata shahada ya uzamivu (Doctor of Philosophy in Law) PhD kutoka chuo kikuu cha Warwick, (UK) mwaka 2012
Katika mahojiano maalum na
Tanzania Daima, Bisimba haachi kusema kile anachoamini kuwa msingi wa
mafanikio, maendeleo yake binafsi, ya wanafunzi wenzake waliosoma shuleni
Weruweru; lakini zaidi akikosoa kile anachoamini kimechangia sana kuangusha
fani nzima ya elimu hapa nchini.
Tanzania Daima: Wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga Weruweru nyakati zenu walijisikiaje, kulinganisha na
wale waliokwenda shule nyingine?
Hellen: Wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga Weruweru wakati huo ikiwa Assumpta College walijisikia vizuri sana. Kwenda
shule hiyo ilimaanisha kuwa ulifanya vizuri sana hasa kwenye masomo ya
Kiingereza na Hesabu. Mimi nilijiunga mwaka mmoja kabla haijawa Weruweru (1969)
Tanzania
Daima: Hali ya ushindani ilikuwaje? Uliwahi kuchaguliwa
kushika wadhifa wowote shuleni.
Hellen: Hali ya ushindani shuleni
ilikua zaidi kati ya wale waliokuwa wanasoma Sayansi na wale wa Arts. Waliokuwa
wanasoma Arts walijaribu kuwaonyesha wa Sayansi kuwa hata nao wana uwezo kwa
vile wa sayansi walionyesha wao ndio wasomi zaidi.
Sikuwahi kushika wadhifa
wowowte maana nilikua mtoto mpekupeku sana, hivyo isingekua rahisi kupewa hata
‘umonita’ tu.
Tanzania
Daima: Hali ya ufundishaji na mazingira ya shule yalikuwa ya
aina gani; je, yaliwapa hamasa ya kusoma ama mlifanya hivyo kwa sababu ya woga
wa wazazi/walimu?
Hellen: Hali
ya ufundishaji ilikua ni nzuri sana.Tulikua na Waalimu kwa kila somo na vitabu
vya kiada na ziada. Tulikua na maktaba nzuri sana. Kila siku jioni tulikua na
muda wakujisomea (PREP.) Mazingira ya shule yalikua safi sana na shule ilikua
chini ya Mlima Kilimanjaro kwa hiyo majira ya usiku ukiangalia unaona mlima
unang’aa inapendeza sana.
Usafi wa shule ulikua si
wa kawaida kwani Sehemu za vyooni tuliweza kutumia kujisomea usiku kwa vile taa
za vyoo zilikua hazizimwi. Mandhari ya shule ilikua na miti na ukoka mzuri sana
na maua siku ya kutembelewa tunakaa na wageni wetu kwenye ukoka chini ya miti.
Mabweni yalikua si mambwalo kwa maana ya hanga kubwa lililo wazi. Yalikua
katika mfumo wa vyumba vidogo tukiviita ‘cubicles’ ambapo wasichana watatu huishi
kwenye chumba kimoja kwa viongozi na wadada wa form four (kidato cha nne) wao
walikua wanaishi wawili tu.
Tulikua tunahamasishwa sana kusoma tukiambiwa kuwa elimu
tu ndio itatukomboa watoto wa kike. Hatukulazimishwa lakini mazingira yalifanya
tu uwe na hamu ya kusoma.
Tanzania Daima: Unadhani
kipi kilichangia kuporomoka kwa umaarufu wa shule hiyo?
Hellen: Kuporomoka
kwa shule hiyo kumechangiwa na mambo mengi, moja mabadiliko ya kuifanya shule
kuwa ya ’high school’ tu na si kuanzia kidato cha kwanza. Pia serikali kutojali shule zake kama
ilivyokuwa hapo mwanzo
Tanzania Daima: wanafunzi ambao kwa sasa
mnalitumikia taifa kwa nyanja mbalimbali, unaweza kusema mmelisaidia taifa
kuinuka kimaendeleo kwa kiwango gani?
Hellen:
Sisi
wanafunzi wa Weruweru tulioko katika utumishi sehemu mbali mbali tumetoa
mchango mkubwa sana kwa taifa kuinuka kimaendeleo kwani wengi wetu tumekuwa
viongozi popote tulipo. Na uongozi wa
wengi wetu umekuwa mzuri kwamba huwezi kusikia masuala ya ubadhirifu.
Tumewajengea uwezo wengi
ambao wamefanya mengi katika kuendeleza familia zao na sehemu walipo ambapo
ndio mchango katika maendeleo ya nchi
kwa ujumla. Kuwa tu na watoto ambao nao wameelimika na wanafanya kazi kujenga
taifa pia ni mchango mkubwa.
Tanzania Daima: Unajisikiaje
unapowaona wanafunzi wenzako wakiongoza kwa ufanisi katika nafasi walizonazo?
Hellen: Ninasikia
fahari sana kuona wenzetu wengi wakiwa katika nafasi za uongozi na wakiongoza
kwa ufanisi sana na penda sana kuwatambulisha kama wasichana wa Weruweru.
Tanzania Daima: Unadhani
elimu yetu imepanda ama imeporomoka? Kama imeporomoka unadhani ni kwa sababu
gani?
Hellen: Elimu yetu imeporomoka. Kwanza kwa kukosa utashi wa
kisiasa wa kuikuza na kuiendeleza. Kuwakosea waalimu ambao ndio nguzo katika elimu.
Mawaziri kufanya watakavyo katika mitaala kwa kuondoa masomo muhimu,
kuchanganya masomo na kadhalika. Pia kuwepo na shule binafsi zinazojiamulia
masomo kwa kadri ziwezavyo na wakubwa kuwa na nafasi kupeleka watoto wao kusoma
nje.
Tanzania Daima: Wanafunzi
wengi wa elimu ya juu sasa wamezama zaidi kusoma masomo yale wanayodai
'yanalipa zaidi', je hii inasababishwa na nini?
Hellen: Hii
inasababishwa na kazi zote kutothaminiwa
sawa lakini pia kuwepo na mianya ya kazi
fulani fulani kuonekana ndio zenye bei kwa maana ya njia za kupata fedha kwa
urahisi wakati nyingine zikiangaliwa kama kazi kavu. Kazi zote hazipewi hadhi
sawa kimaslahi na hata kiheshima.
Tanzania Daima: Nini
mtazamo wako kama mwanamke msomi, kuhusiana na mwenendo mzima wa utawala na
uendeshaji wa siasa ya vyama vingi nchini?
Hellen: Inasikitisha kuwa mfumo wa siasa za vyama vingi
ulikubalika kisheria lakini kiutashi ulikua haujakubalika kwa wale waliokua
madarakani na kwa sababu hii mfumo huu umekua ukinyimwa nafasi ya kukua na
kufikia dhima yake. Unaonekana kama ni uadui na haupati kabisa nafasi ya kutosha
kufanya yale yanayotarajiwa katika mfumo wa siasa ya vyama vingi. Badala ya
demokrasia kukua inasinyaa.
Tanzania Daima: Je, kwa
imani na mtazamo wako, unaamini na ungependa rais ajae awe mwanamke? Kama ndio,
unawafikiria akina nani walio katika vyama ama nje wanafaa kuongoza?
Hellen: Ingefurahisha sana kama tungepata rais mwanamke katika
uchaguzi ujao. Si rahisi kufikiria watu kwani inategemea sana na mtu mwenyewe
kama ana njozi hizo au la, ila tukiangalia kwa uwezo wapo wengi wanaoweza kuwa
marais. Mfano Ana Tibaijuka, Mama Getrude Mongela , Dr. Asha rose Migiro.
Tanzania Daima: Kukithiri
kwa matukio ya biashara ya dawa za kulevya, utoroshaji wa nyara za taifa,
unadhani kunachangiwa na ukosefu wa elimu, maadili ama tamaa na kunatoa ishara
gani kwa vijana wetu?
Hellen: Hili ni tatizo la tamaa na ubinafsi kuwa mtu anachojali
ni yeye kupata mali bila kuangalia athari kwa wengine na kwa taifa kwa ujumla.
Ishara iliopo ni kuuawa kwa kizazi
kijacho kwani vijana wengi nao wangependa kupata mali kwa haraka haraka na
wakati hu huo kujiingiza katika kutumia madawa yanayopotea uwezo kiakili na hata kimwili hatima yake ni kuwa
na taifa la mateja. Mungu apitishie mbali.
mwisho
No comments:
Post a Comment