Nani anajali, taifa likienda gizani?
“Pole Bwana
Misango kwa kufungiwa kwa kikaratasi chenu cha udaku (yaani gazeti hili)
kinachomilikiwa na chama cha wachaga
(Chadema).
“Itabidi
sasa kwa hiyo miezi mitatu, mjifunze adabu na kuiheshimu serikali, maana ninyi ni wa …(tusi) sana, ,mnastahili
kukomeshwa na ningekuwa mimi ndio JK (Rais Jakaya Kikwete) nisingewafungulia
hadi namaliza urais wangu’.
Haya ni
maneno ya msomaji wangu mmoja aliyenipigia simu mwanzoni mwa wiki hii, mara tu
baada ya tangazo la serikali la kuyafungia magazeti mawili maarufu ya Mwananchi
na Mtanzania.
Nilicheka
kwa uchungu, kwa sababu masikini mtanzania huyu amesukumwa na ushabiki wa
kisiasa kiasi cha kushindwa kujua kuwa gazeti la Tanzania Daima ni mali ya
nani. Anaamini kwa sababu linaandika habari nyingi za Chadema, basi ni mali ya
chama hicho!
Kwamba
pamoja na kuwa bingwa wa kuzodoa wengine na kutoa maneno ya hario, amekosa kabisa kujua kuwa Mtanzania
na Tanzania Daima ni magazeti mawili tofauti kabisa na yenye sera na wamiliki
wawili tofauti pia!
Ujumbe wa
msomaji huyu, unatokana na hatua ya serikali ya
kufungia magazeti mawili ya Mwananchi na Mtanzania kwa tuhuma za
uchochezi na kuhatarisha amani.
Najua
yamesemwa mengi kutoka kwa watu wengi, wakilaani na kulalamikia hatua hii ya
serikali. Kwa wengine, wanaweza kudai kuwa kwa sababu watu wamepiga kelele
kiasi cha kutosha, hakuna haja ya
kuendeleza malumbano. Sio kweli.
Tuanze na
tamko la kufungia gazeti la Mwananchi. Kwa hili, watawala wetu wametuambia kuwa
wamelifungia kwa siku hizo 14 kwa sababu liliandika habari za uchochezi na
uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha
amani na mshikamano ulipo nchini.
Watawala
wametamka kuwa gazeti hili, lilichapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na
uvunjifu wa amani, kwa kuchapisha habari ya SIRI ‘
juu ya MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013”. Kisha likachapa habari nyingine iliyosema “WAISLAM WASALI CHINI YA
ULINZI MKALI” , na kukolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira, iliyotoa
tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka
Mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya kiislam jambo ambalo halikuwa
la ukweli na ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini
wa dini ya iislam maana mbwa ni najisi hapaswi kuingia katika maeneo
ya ibada.
Kwa gazeti
la MTANZANIA lililofungiwa kwa siku tisini(90), linadaiwa kuandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA DAMU”, na
tena lilichapisha makala isemayo
“MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”. Likaibuka tena na Kichwa cha habari kisemacho “SERIKALI
YANUKA DAMU” taarifa hiyo ilikolezwa na
picha zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza
rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika .Katika habari hiyo gazeti hilo
limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga
waliomizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa
na kujeruhiwa vibaya.
Mbaya zaidi
gazeti hilo liishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye
sura ya kigaidi. Hayo, serikali imesema ni uchochezi wenye lengo la kuwafanya wananchi wavichukie
vyombo vya ulinzi na usalama wavione kuwa haviwasaidii.
Taarifa ya
serikali, ikawataka wamiliki,wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini,kuzingatia
weledi,miiko, madili yataaluma uandishi wa habari na kuweka mbele maslahi ya
taifa letu kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu.
Kufungiwa
kwa magazeti haya ni ishara mbaya ya giza nene linalolinyemelea taifa. Ni
kuzima mshumaa wa matumaini, na uhuru wa watanzania kwa namna nyingi. Kwa watu
wanaojali uhai wa taifa, kufungia magazeti ni kuua uhai wa taifa. Ikumbukwe
kuwa wakati haya yakifungiwa, serikali yetu sikivu, iliapa kutolifungulia gazeti la Mwanahalisi kwa kosa lile lile la
kuandika habari za uchochezi.
Kosa la
mwanahalisi, ni kuanika kweupe mlolongo mzima wa mawasiliano ya kutekwa na
kuumizwa vibaya kwa kiongozi wa
madaktari nchini, Dk Stephen Ulimboka na watu anaodai kuhusika na tukio hilo
baya. Kwa serikali badala ya kufuatilia ikaamua kulinyamazisha!
Najua wapo
watanzania na hasa watawala wababaishaji, wanaotumia nafasi zao kujineemesha,
bila kujali maslahi ya mwananchi, wameshangilia! Hawajali kinachoweza kutokea,
ama nini kitakachoingia vichwani kwa watu wengi kutokana na hatua hii. Hawajali
ya kesho. Nani anajali?
Hawajali
kwamba hata ukifungia gazeti, kuna teknolojia nyingine nyingi za kupashana
habari. Kuna mitandano mingi ya mawasiliano inayoweza kutumika kutuma ujumbe
kwa kasi mno. Inasikitisha kwamba
waliofungia magazeti haya
hawajali kuwa, tofauti na gazeti linalochapa nakala chache tu na kusambazwa kwa
shida kubwa sehemu chache tu za nchi, mitandano ya jamii na mawasiliano mengine
ni ya hatari zaidi kwa sababu, mtu
yeyote anaweza kusambaza habari za uongo, uzushi, uchochezi na kusababisha
vurugu kubwa ndani ya kipindi kifupi na kwa eneo kubwa!
Ni hatari
kwa taifa lililonyimwa mawasiliano, kwa sababu anaweza kuibuka ‘kichaa’ mmoja
akatumbukiza ujumbe mchafu na kuchochea vurugu za kidini ama kikabila na
ukaendea kama moto wa nyasi kavu msituni!
Ni giza nene
kwa taifa, linalotaka nchi itawaliwe bila watu walioombwa kwa unyenyekevu
katika kampeni kuwachagua watu fulani watawale, na ghafla wanakuwa mbogo
kuhojiwa pale yanapokuja mashaka na mambo yasiyopenmdeza.
Andiko la
mtu mmoja katika moja ya mitandao ya kijamii, inaonesha sura na haiba ya aina
hii ya watawala. Andiko hilo linasema; (nanukuu) “ Haiwezekani gazeti liandike
"Mapinduzi hayaepukiki" halafu liachwe bila hatua. Huo utakuwa ulevi
wa uhuru wa maoni ambayo haitofautiani sana na
ya madaraka. Rwanda waliuana kwa uchochezi wa magazeti na redio!
ya madaraka. Rwanda waliuana kwa uchochezi wa magazeti na redio!
Nakubali
kwamba mauaji ya Rwanda yalichangia umwagaji damu. Nakubali kuwa hakuna uhuru
usio na mipaka, na demokrasi bila utaratibu ni fujo.
Kama watu
tunaojali taifa letu, na tunaosukumwa vema na moyo wa ukweli, tusiopenda
kujipendekeza kwa yeyote, tudurusu kidogo tu hoja za serikali zilizosababisha
kivangaito katika tasnia ya habari na taifa. Tunafanya hivi kwa sababu
tunaijali nchi yetu na kamwe hatutaki
taifa liende kwa mtindo wa kufafaruka!
Hivi ni
watanzania wangapi wana imani na utendaji kazi wa baadhi ya askari wa jeshi la
polisi? Tuhuma ngapi zimesukumwa kwa jeshi hili na ni hatua ngapi zimechukuliwa
dhidi ya wanaotuhumiwa ili liwe safi na kudumisha imani inayopiganiwa usiku na
mchana?
Raia wangapi
wameteswa na kufia mikononi mwa polisi? Mwandishi Daud Mwangosi alipigwa vibaya
na kuuawa kikatili mikononi mwa nani? Nani alimwaga damu ya Mwangosi? Nani
alimwaga damu ya wafanyabiashara wa Morogoro waliosingizwa ujambazi? Nani alimpiga risasi
Mwandishi Shaaban Matutu wa Tanzania Daima?
Plisi
wamemkamata nani mateso ya Mhariri Kibanda, kuuawa kwa Padri huko
Zanzibar? Hivi walioumizwa wakihoji
utendaji huu, ama mtu kuihoji serikali yako kuhusiana na usalama wako, ni
uchochezi? Kumbe, watoe pongezi kwa dola inayoshindwa kuwakamata watu walioua,
kumwagia watu tindikali na kuhatarisha usalama wa raia?
Hivi
anayehoji uhakika wa maisha yake, na anayepuuza kufuatilia matukio haya mabaya
kwa kuwaondoa watendaji wote wanaolichafua jeshi la polisi na vyombo vingine
vya dola, nani anastahili kuitwa mchochezi?
nani anastahili kutimuliwa kati ya wale wanaondika, na mtendaji goigoi
anayeshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo kufanya serikali ichukiwe na
wananchi? Hivi serikali haikuwa na
washauri wazuri katika hili? Hawakujali matokeo ya hatua hii?
Serikali
inapotaka waandishi kuwa wazalendo, wafanye hivyo mara ngapi? Tumeandika na
kuanika madudu na uozo kiasi gani? Nani kachukuliwa hatua, nani kakamatwa?
Badala ya shukrani, tumetendewa mangapi, tumetishwa mara ngapi? Maisha ya
waandishi yamekuwa ya wasiwasi kwa sababu tu tunahatarisha maslahi ya wachache
kwa kiwango kikubwa. Nani amejali?
No comments:
Post a Comment