Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

RAIS WANGU KIKWETE MKUU WA NCHI AKIYUMBA NCHI YOTE HUYUMBA!


RAIS WANGU KIKWETE MKUU WA NCHI AKIYUMBA NCHI YOTE HUYUMBA!
Rais wangu ukimsikia mtu anasema oh! Nimefanya mengi, oh! Nimefanya makubwa, jua hajafanya lolote la maana la kuonekana au kutiliwa maanani na jamii yake. Matendo makubwa, yanaoonyesha weledi au ujasiri wa hali ya juu hayahitaji kusemewa. Yenyewe hujisema! Hata mambo tu ya kawaida hujisema yenyewe. Uliwahi kumsikia Tausi akisema yeye ni mzuri! Tausi hasemi. Ukimwangalia tu, uzuri wake unakwambia kuwa Tausi ni mzuri.
Viongozi wengi wanalazimika kuwaambia wananchi wao kuwa wamewafanyia mengi au makubwa na kuwaapiza kuwa watakuja kuwakumbuka wakishapita. Ukijikuta katika hali kama hii jua una mapungufu.
Nani aliwahi kumsikia Hayati Edward Moringe Sokoine akiwaapiza Watanzania kuwa atakapokuwa amepita watakapomkumbuka kwa makubwa aliyotenda? Mambo makubwa na ya msingi huthaminiwa kwa wakati uleule yanapofanyika. Hayangoji mtu apite!
Tuwekane sawa na wala tusiongopeane! Hakuna atakayekumbukwa kwa ujenzi wa kilomita nyingi za barabara za lami katika awamu hii ya nne, zaidi ya John Pombe Magufuri! Hili ndilo pekee linaweza likatajwa kuwa ni mafanikio makubwa ya awamu ya hii. Tumefanya nini kuwapiga vita maadui wetu wakuu wale watatu ndilo lingekuwa jambo la kusema mtanikumbuka!
Katika Elimu, kuna ‘Big results now’ huku maandamano ya wanafunzi walionyimwa mikopo na migomo ya walimu vikirindima. Tunampumbaza nani!  Migomo ya madaktari na ‘Ambulance za Bajaj’ vijijini kusiko na barabara kutaimarisha afya ya mwananchi gani? Kama mabilioni ya JK hayakuonyesha njia ya kuondoa umaskini hata wa vijana wetu tu, tuna nini cha kusema tutakuja kukumbukwa? Kujiridhisha kuwa tunafanya makubwa lakini hayaonekani kwa sasa mpaka hapo tutakapopita ni sawa na kujilisha upepo! Tunaoamini hivyo tunajiridhisha wenyewe kuwa tunachokifanya au ni kweli hakionekani, au kinaonekana lakini kinaonekana kama vile upuuzi unavyoonekana.
Rais wangu baada ya kufanikiwa kutoa Elimu bure kwa wote mpaka watu wazima, kutoa huduma za afya bure kwa wananchi wote na pia huduma nyingine za jamii kama maji, nani aliwahi kuwasikia viongozi wa awamu ya kwanza wakijisifia kuwa, ‘Tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele?’
Lakini viongozi wetu wote wa juu wa sasa Nyerere aliwasomesha wote bure mpaka wakamaliza. Aliwatibia wananchi wake wote bure, toka aliyesumbuliwa na kidole mpaka aliyesumbuliwa na moyo! Matibabu na dawa vyote alitoa bure nchi nzima toka Zahanati mpaka Hospitali za rufaa! Leo wanatokea watu sijui toka wapi, wanasema wamethubutu bila kuwaonyesha wananchi wamethubutu nini! Wanasema wameweza kipi walichokiweza? Sasa wanawaambia wanasonga mbele wala hawaonyeshi mbele yao ni ipi! Huwezi kuongoza nchi kwa vibwagizo vya kwenye ngoma!
Mwenyezi Mungu alivyotuumba ni kwamba vijana aliwapa nafasi kubwa yakufanya utoto. Inapokera ni pale mtu ambaye kwa macho anaonekana mzima anapopewa fursa ya kujadili rasimu ya katiba mpya, yeye anamshambulia Joseph Sinde Warioba kama mtu binafsi. Huyu ni mpuuzi wa kisiasa. Anathibitisha kuwa si kila mzazi ana busara, wala si kila Mwenyekiti ana hekima! Wako wazazi, wako wenyeviti makapi!
Wananchi wanaanza kujiuliza, chama chake kimefilisika pia! Anapoachwa bila kukemewa na viongozi wa chama chake, anawapa nafasi watu kudhani kuwa huja viongozi wake ni kama yeye! Kwa chama ambacho kimesheheni watu makini na wenye fikra nzito huyu ni wakufuzwa kama anavyofukuzwa Paka mwizi! Kwanini akichafue chama?
Rais wangu kila nchi ina wendawazimu wake. Hata hapa kwetu tunao wetu. Wakati wewe kwakutumia busara zako unawaita Wapinzani waje Ikulu kwa majadiliano muhimu, hawa wakwetu wamesikika wakipingana na wewe. wanasema milango ya Ikulu imefungwa! Utadhani yeye ni bawaba za milango na madirisha ya Ikulu au ni bawabu wa lango kuu la kuingilia Ikulu. Haikubariki mtu tu apingane na kauli ya Rais wangu. Uhuni wa viongozi wa aina hii ndiyo huifanya Serikali yoyote ionekane ya kihuni popote! Tusikubali uwendawazimu wa wachache uichafue serikali yetu. Baba waondoe hawa mapema wananchi wasije wakakufananisha nao. Muda wa matumizi wa ubongo wao kufikiri ‘ume-eksipaya’, wanapaswa waondolewe!
Rais wangu kama kuna jambo kubwa litakalokujengea heshima kubwa katika nchi hii kwa sasa na kwa vizazi vingi vijavyo, ni kuipatia nchi hii katiba mpya na iliyo bora. Ni bahati mbaya sana kuwa hili lilikataliwa na viongozi wachache ndani ya chama na serikali yako wanaofaidika na katiba iliyopo.
Ni kwa utashi wako peke yako ndani ya chama na ndani ya serikali yako uliamua mchakato wa hili jambo jema uianze. Ni jukumu lako kuhakikisha kuwa unalifikisha katika mwisho mwema! Wapinzani wako wa jambo hili waliomo ndani ya chama chako na ndani ya serikali yako mwenyewe wanafanya kila njia ili uaibike! Jipatie faraja kwa maandiko yaliyoko ukurasa wa 26 katika kitabu cha Mwalimu mkuu wa watu.
Imeandikwa, “Uamuzi wako ni mzito, lakini kiongozi mwelewa anajua kuwa wakati mwingine ni lazima kuchukua uamuzi mzito na mchungu kuwaelimisha watu kuwa wao ni wasimamizi tu wa mazingira ya sasa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Amali ya nchi hii ni kwa ajili ya vizazi vyote.
“Elewa kuwa siku zote wale wanaosimama kidete kutetea haki za wengi hukumbwa na misukosuko mingi. Lakini wewe kwasababu unaitafuta haki ya watu wetu utaipata na wadhalimu wanaotafuta kukuhujumu hawataambulia chochote bali majuto ya kushindwa!
“Utakumbukwa na vizazi vingi vijavyo, naam, pamoja na wote waliolazimika kuundoka ulimwengu huu kwa sababu kwa kufanya unayoyafanya kuliwaudhi wakubwa na hivyo wakawatanguliza mbele ya haki.”
Rais wangu wako wakubwa wengine ambao sasa wameamua kuichafua haiba nzuri ya nchi yetu kimataifa kwa kuyafungia magazeti. Natambua fika kuwa nimedumu katika kuandika hapa, kwa wema wako tu baba! Hivyo kwa ajili ya Rais wangu nawashukuruni wanawema wote.
Siandiki hili kwa lengo la kuyalilia magazeti yaliyofungiwa, la hasha! Naandika hapa, ili nipate kuyazika magazeti yaliyofungiwa! Wakubwa wamesema yameandikwa uchochezi. Nao hao waliosema, ni watu waheshimiwa!
Rais wangu wakubwa wamesema gazeti la mwananchi limeandikwa habari iliyokusudiwa iwe siri. Mishahara halali nayo siri! Nijuavyo mimi siri, ni siri sirini. Ikitoka nje mpaka kiasi cha kulifikia gazeti, hiyo si siri tena. Lakini wakubwa wamesema hata ikifichuka inakuwa bado ni siri. Na hawa ni watu waheshimiwa!
Gazeti hilohilo Mwananchi liliandikwa kuwa Waislamu walisali chini ya ulinzi mkali. Ni nani hakuwaona askari wetu ambao ndio watoa ulinzi, wakilinda amani katika maeneo ya misikiti yetu? Na hivi si ndivyo wanavyotoa ulinzi makanisani na sehemu zingine zenye mkusanyiko mkubwa wa watu? Cha kushtua mishipa ya fahamu hapa ni kipi? Wakubwa wamesema kwakuandikwa hivyo gazeti limeandikwa uchochezi! Lakini wakubwa hawa ni watu waheshimiwa!
Ndugu Rais, timamu wote wanaelewa kuwa popote duniani, mbwa mnyama ni alama ya ulinzi. Picha yake pia ni alama ya ulinzi kimaandishi. Gazeti la Mwananchi liliwekwa picha ya mbwa katika ukurasa wake. Wakubwa hawa wakachukua picha ya mbwa aliyeko vichwani mwao wakaipeleka katika misikiti yao iliyoko pia vichwani mwao. Lengo lao kulifanya gazeti la Mwananchi lionekane limepeleka mbwa msikitini! Wanatafuta kuungwa mkono na baadhi ya watu wanaotumia dini zetu kufanya vurugu nchini! Kwa hili hata maamuma wamewashtukia!
Rais wangu Gazeti la Mtanzania lenyewe liliweka picha za wahanga wa kile ambacho wengine wanaita ugaidi uliojitokeza nchini mwetu katika awamu hii ya nne! Ilikuwapo picha ya Sheikh Soraga na Padre Mwang’amba. Wote wawili miili yao ilikuwa inatisha kutokana na unyama waliofanyiwa, kumwagiwa tindikali. Pia ilikuwapo picha ya majeruhi Steven Ulimboka aliyetekwa, kufanyiwa unyama mkubwa na kisha kutupwa kama maiti katika msitu wa Pande. Ilikuwapo pia picha ya majeruhi Absalom Kibanda akiwa amelala nusu mtu nusu mfu! Huyu aling’olewa meno, akakatwa kidole na kujeruhiwa vibaya kichwani na kitu chenye ncha kali kisha wakamtoboa jicho!
Picha zilionyesha wahanga wakivuja damu nyingi. Kuonyesha damu ikimwagika yaonekana ndiko kulikowakasirisha zaidi waheshimiwa hawa. Kwao damu ya kwenye gazeti imeuma zaidi kuliko damu halisi iliyomwagika wakati wakifanyiwa unyama huo! Lakini yawezekana vipi meno yang’olewe, kidole kikatwe na kujeruhiwa vibaya kichwani eti damu isimwagike? Eti utoboe jicho la mtu damu isimwagike? Hawa ni waheshimiwa wa ajabu kabisa!
Gazeti lilionyesha damu nyingi ikimwagika! Likatahadhalisha kwa kuandikwa kuwa serikali inanuka damu kama kichwa cha habari. Wakasema gazeti limeandikwa uchochezi! Lakini hawa ni watu waheshimiwa!
Kufungiwa kwa magazeti haya kumetonesha kidonda kisichopona kinachowauma Watanzania kwa muda wa mwaka sasa! Kufungiwa kwa gazeti pendwa Mwanahalisi. Yaliyolipata gazeti la Mwanahalisi mpaka kufungiwa yanatia shaka utu wa watu waliolifungia! Serikali ilijichongea yenyewe kwa wananchi kwa kulifungia gazeti la Mwanahalisi. Imeathirika zaidi na walengwa wamekwezwa zaidi kwa hili! Kuachiwa huru kwa mtuhumiwa wa Suleima Kova, Joshua Mhindi na mahakama kumewaumbua wote waliohusika katika hilo! Madhali sasa hamna kesi tena mahakamani kuhusiana na jambo hili ni mategemeo ya wengi kuwa swala zima litaongelewa kwa kirefu zaidi sasa katika kikao kijacho cha Bunge.
Rais wangu wakubwa hawa wanawaambia wananchi kuwa magazeti haya yamefanya uchochezi. Kama haya niliyoyasimulia ni uchochezi kweli, basi hilo lilikuwa ni kosa kubwa ambalo magazeti haya yamelipa aghali! Nayaandika haya kwa wema wako tu ili nipate kuhutubia matanga ya magazeti haya, kwa maana wewe ni mtu mheshimiwa. Na wakubwa hawa nao ni watu waheshimiwa.
Yalikuwa ni magazeti huru, yaliyotawaliwa na ukweli na uwazi huku yakijali haki na hivyo kupendwa mno kusomwa na wasomaji wengi. Wakubwa wanasema yamefanya uchochezi. Ndugu Rais kuwa mchochezi kwataka moyo mgumu! Mchochezi anapendwa na nani? Lakini wakubwa wamesema yameandikwa uchochezi! Na hawa ni watu waheshimiwa!
Waheshimiwa wameyafungia magazeti haya kwa ufinyu tu wa fikra wakidhani wanawaumiza watu wachache tu wanaoyamiliki. Kwa kutokuwa na ufahamu na athari zinazoambatana na uamuzi huo, hawakujali wanawaumiza wangapi wasiohusika kabisa na kilichoandikwa katika magazeti hayo! Kwa kuyafungia magazeti hayo wamewafungia wananchi wengi haki yao ya kupata habari kutoka kwenye vyombo vya habari walivyovipenda. Wamewafungia ajira wafanyakazi wa magazeti hayo ambao maisha yao yalitegemea ujira uliotokana na mauzo ya magazeti hayo.
Kuna wauzaji wa mitaani na wauzaji wa jumla hawa wameadhibiwa kwa kufungiwa kwa magazeti hayo! Kama hawa wangetaka habari hizo zisichapishwe wangeweza vipi kuzuia zisichapishwe? Wenye viwanda waliokuwa wanayachapa magazeti hayo ambao nao wameajiri wananchi wengine pia wamefungiwa kupata kipato kutokana na magazeti hayo kufungiwa. Wachora katuni, wafanya usafi ofisini na watoa matangazo, hawa walichangia vipi katika kuchapisha habari zile? Waheshimiwa hawa kwa ufinyu wa kufikiri na kutafsiri halihalisi, wameuhamasisha umma na kuwalazimisha wote walioguswa na kufungiwa kwa magazeti haya waichukie serikali yao! Serikali ni Rais nitaendelea kurudia hivyo!
Kwa utendaji wa watendaji hawa serikali itapendwa vipi? Chuki ya wananchi kwa serikali ni chuki ya wananchi kwa Rais! Hawa ndiyo waheshimiwa wetu wanaomchafua Rais wetu mbele ya wananchi. Kuendelea kuwachekea ni kuyanyong’onyesha maisha ya Rais wetu akisha kuondoka madarakani. Nani atawajua hao wengine?
Rais wangu mara zote tumeona ajali na uvujifu wa sheria barabarani ambapo dereva au mmiliki wa chombo husika ndiye hufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Hatujawahi kuona gari au pikipiki au chombo chochote kikihukumiwa kufungwa au kufungiwa! Gazeti huendeshwa na watu. Gazeti huandikwa, gazeti halijiandiki. Iweje wasituhumiwe walioandika habari hizo badala yake liadhibiwe gazeti?
Hivi sasa wanawema Absalom Kibanda, Samson Mwigamba na Makunga wako mahakamani wakituhumiwa kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi. Hata kama ni kwa kuonewa ni watu ndio wafikishwe mahakamani!
Rais wangu kama hutawadhibiti mapema hawa waheshimiwa walioivua soni inayomtoa mwanadamu katika kundi la wanyama wengine, ukawaacha waendelee kuisokota amani ya nchi hii, mwishowe amani hii itakatika! Nchi itaingia katika vurugu za maangamizi na wewe utaingia katika kumbukumbu chafu za nchi hii! Vizazi na vizazi vingi vijavyo vitapata fursa ya kukusoma katika historia ya nchi yetu! Nao watafyonya na kutikisa vichwa vyao huku wengine wakitema mate kwa kuushuhudia uongozi bomu wa viongozi, BOMU!

PASCHALLY MAYEGA
TEL 0788 37 27 87

No comments:

Post a Comment