Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

UJAMBAZI WA MALIASILI Uvunaji haramu na holela



Na Bakari M Mohamed

TANZANIA imejaaliwa maliasili ya kutosha! Hapana shaka yoyote kwamba kama maliasili ya nchi ingalitumika vema na kimkakati, Tanzania isingalikuwa maskini kama ilivyo.
Hata hivyo, matumizi ya maliasili ya taifa yameshindwa kuifanya Tanzania kupanga mipango ya uvunaji endelevu, utekelezaji wa mipango na program makini za uvunaji unaozingatia ustawi wa sekta ya uchumi na kuongeza mchango wa maliasili kwenye pato la taifa. Kwa ujumla, maliasili ya Tanzania yamekuwa yakichangia sehemu ndogo sana kwenye pato la taifa kuliko uvunaji wake.
Tanzania ina madini mengi ya aina kadha wa kadha. Ni nchi pekee duniani yenye madini ya Tanzanite yenye soko lisilokuwa na ushindani. Hata hivyo, kutokana na “uzezeta” wa mipango, madini hayo hayajainufaisha nchi kwa jinsi nchi nyingine duniani zinavyonufaika na aina ya maliasili za kipekee kama vile nchi zinazozalisha mafuta (dhahabu nyeusi) zinavyonufaika! Achilia mbali Tanzanite; Tanzania kuna dhahabu (ya kutosha) na kijiolojia inasemekana ni nchi ya tatu kwa wingi wa dhahabu isiyochimbwa katika Afrika!
Dhahabu ya Tanzania inachimbwa na makampuni ya kigeni ambayo yanafaidika sana kwa faida kubwa mno huku yakilipa mrahaba kiduchu kana kwamba madini ni mali yao na Tanzania imefanywa shamba la bibi.
Dhahabu, mawe ya thamani (kama vile yakuti, marijani, lulu, na zumaridi), chumvi (ya pwani na Uvinza), makaa ya mawe (ya Kiwira), chuma (cha Mchuchuma), risasi (ya Kaliua, Mpanda), na aina nyingine ya madini yasiyotajika; yote haya yangaliweza kuifanya Tanzania itawale uchumi na wananchi wangaliweza kuondokana na umasikini wa kipato kwa uchumi wa kubangaiza na utegemezi wa kilimo cha kujikimu cha jembe la mkono!
Hii ni aibu kwa serikali kushindwa kusimamia maliasili zake na kuacha watu wachache wenye uchu, uroho na umero wa wavune maliasili za taifa kwa njia za haramu na holela. Kama nchi, basi Tanzania imekosa wenyewe (au wenyewe wamejisahau) na kuwaachia wachache kwenye mfumo wa menejimenti wa shughuli zinazotawala maliasili kufanya maamuzi yasiyozingatia maslahi ya umma.
Tazama maliasili ya gesi asilia inayochimbwa na kuvunwa Songosongo! Wanaovuna ndio wanaofaidika na faida ya uvunaji, siyo?! Hata wananchi wanaoishi eneo linalochimbwa na au kuvunwa maliasili ya gesi asilia hawafaidiki kiasi wanachofaidika wavunaji.
Huu ni unnyang’anyi wa hali ya juu; ati mwenye maliasili yake anapata chini ya asilimia 5 ya pato la uvunaji ilhali mwekezaji (mfanyabiashara) anachukua asilimia 95! Kama si aibu hii ni nini kwa serikali inayosimamia uvunaji huu?! Hapana shaka yoyote kwamba huu ni ujambazi wa maliasili na wale wote (pomoja na serikali inayosimamia mchakato wake) ni majambazi wanaokwapua kwa nguvu maliasili ya wananchi wa Tanzania.
Takwimu za Benki ya Dunia (2011) zinazopatikana kwenye “The Changing Wealth of Nations: Measuring Sustainable Development in the New Millennium” zinaonyesha kwamba mchango wa maliasili kwenye pato ghafi la taifa (GDP) kwa Tanzania kwa mwaka husika ni kama ilivyo kwenye mabano (kutaja kwa uchache wake): makaa ya mawe (0.00%, 1990; 0.04%, 2008; na 0.03%, 2010); misitu (7.85%, 1990; 2.07%, 2010); madini (0.00%, 1994; 4.24%, 2010); gesi asilia (0.00%, 1988; 0.89%, 2008; 0.47%, 2010); na mchango jumla wa maliasili kwa mwaka 2010 ni asilimia 6.78.
Ushahidi huu unaonyesha jinsi tusivyokuwa madhubuti na thabiti katika menejimenti ya maliasili zetu! Wafanyabiashara wanavuna kwa gharama ndogo ilhali wanapata faida kubwa na kuchangia kiasi chini ya asilimia 10 kwenye pato la taifa!
Kwa sehemu kubwa matokeo ya maliasili za Tanzania kushindwa kuchangia sehemu kubwa kwenye pato ghafi (au sanifu) la taifa, pamoja na mambo mengine, yametokana na serikali kushindwa kusimamia menejimenti ya uvunaji wa maliasili.
Kwa jinsi hii, serikali imeiacha sekta ya uvunaji wa maliasili kwenye mikono ya wezi, wabadhirifu, majambazi (au majangili) na mafisadi waliyemo ndani ya mfumo wa kifisadi wa menejimenti ya shughuli za maliasili (na utalii).
Maliasili za Tanzania, kwa jinsi zinavyovunwa holela na kwa njia za haramu, ndio kusema zimefanywa “hazina mwenyewe” kwa “wajanja” kuvuna watakavyo kwa jinsi wanavyoweza kunufaika na mfumo wa ujambazi wa kiserikali kwenye maliasili.
Mbuga na mapori ya taifa yamefanywa mitaji kwa ugawaji wa vitalu, uwindaji holela na ujangili. Ukichukua ugawaji wa vitalu; wengi waliyegawiwa vitalu aidha wamepewa kwa njia za rushwa au kwa matumizi yasiyozingatia leseni na vibali vya umiliki na uwindaji.
Taarifa zinazopatikana kutoka kwa watu mbalimbali wanaozunguka vitalu na au wanaofanyakazi kwenye vitalu hivyo wanabainisha hali halisi ilivyo kwenye shughuli za vitalu zinazofanywa na wamiliki wakishirikiana na majangili.
Uwindaji wa wanyama kwa minajili ya kuuza “nyama-pori” kwenye maeneo mbalimblai ya nchi na hata kuuza nje ya nchi. Wanyama-pori wamekuwa wakiuawa holela huku faida ya uwindaji huo ikichukuliwa na wafanyabiashara wanaomiliki vitalu.
Ujangili dhidi ya wanyama kama tembo kwa kukata meno; vifaru kwa kukata pembe; chui na twiga kwa kuchuna ngozi; mamba, viboko na wanyama wengine kwa ngozi, zinazofanywa biashara kwenye soko la kitaifa na la kimataifa kwa njia za haramu. Mfano wa ushahidi huu ni huu: tarehe 21 Julai, 2009 watuhumiwa wanaosafirisha nyara za serikali walifikishwa Mahakama ya Kisutu. Miongoni mwa watuhumiwa hao walikuwamo maofisa wa wizara (ya maliasili na utalii), mamlaka ya bandari na mamlaka ya mapato (forodha).
Hii ilitokana na ushahidi wa tarehe 2 Machi, 2009 ambapo maofisa wa forodha na bandari ya Kaohziung, Taiwan kusini walipokamata meno ya tembo yenye uzito wa tani 5.217 kwenye makontena mawili yenye namba PONU 0713898 na Maeu 7915043 yaliyosafirishwa tarehe 14 Aprili, 2006 kwa meli ya Munstar kupitia bandari ya Tanga!
Huu ni mfano mmoja; lakini, ukamataji wa nyara za serikali zinazosafirishwa umekuwa ukitokea na kuripotiwa mara kwa mara huku ujangili ukichukua kasi ya kutisha! Maliasili ya wanyama imekuwa ikivunwa na watu wenye uchu na tamaa ya kupata faida ya kuuza maliasili hizo nje ya nchi hata kwa kuvunja sheria, kanuni na taratibu kwa kushirikiana na watendaji wa serikali wanaohusika na menejimenti na udhibiti wa uvunaji wa maliasili.
Viongozi wa kisiasa na watendaji wa serikali, kama vile kwenye ofisi za wiziara zinazohusika na maliasili, wamekuwa wakitumika kwa njia moja au nyingine katika kutoa idhini (kwa njia za kifisadi) ya uvunaji wa maliasili kwenye vitalu, mbuga na mapori ya Tanzania kwa kuwahusisha maofisa wa maliasili.
Mfumo wa ujangili unaotumika kwenye kuvuna kwa njia za haramu maliasili umefungwa kwenye mfumo tata wa ndani na nje ya taasisi na au idara zinazohisika na uvunaji huo.
Ukiachilia mbali sera ya maliasili inayoelekeza uvunaji unaozingatia ukuaji wa sekta ya maliasili, kumekuwapo na ukwepaji wa uwajibikaji wa moja kwa moja. Watendaji waandamizi na wa kada za chini kwenye mfumo wa menejimenti ya maliasili wamekuwa wakishiriki kwa njia za moja kwa moja au kwa nyuma ya pazia katika kufanikisha ujangili na hatimaye ujambazi wa nyara za taifa.
Nyara za taifa zimekuwa zikisafirishwa kwa njia za magendo zikiwahusisha watu wenye nafasi kwenye siasa na serikali. Kwa jinsi hii, ujangili unaendelezwa na watu wenye nafasi za kimamlaka kuanzia wizarani na kwenye taasisi nyingine zinazohusiana na udhibiti wa utoroshaji wa maliasili.
Kama ilivyo kwenye ujangili na uvunaji wa wanyama-pori; ndivyo ilivyo, kwenye uvunaji wa misitu. Magogo ya miti adimu na inayodhaniwa kutoweka yamekuwa yakivunwa na kuuzwa na wafanyabiashara wenye mahusiano ya kifisadi na watendaji wa mamlaka zilizokabidhiwa menejimenti ya misitu na maliasili ya miti.
Pamoja na kuwapo kwa sheria, kanuni na taratibu kadha wa kadha zilizoainisha juu ya uvunaji na aina ya misitu inayotakiwa kuvunwa huku zikiweka zuwio kwa aina nyingine za miti, wafanyabiashara haramu wamekuwa mstari wa mbele katika kuvuna magogo na miti ya mikoko na hata kutishia uharibifu wa mazingira ya maeneo nyeti ya uzalishaji wa misitu ya asili na inayoashiria kupotea au kutoweka.
Kama ilivyo kwa uvunaji naodhaniwa halali na unaoratibiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu; uvunaji wa maliasili unaozingatia sehria za uvunaji hususani kwenye madini na gesi asilia hauna tija kwa nchi na wananchi sawiya. Hivi ndivyo ilivyo kwa jinsi ileile ya uvunaji haramu. Kwani kama nchi hainufaiki na uvunaji wa kisheria, ndio kusema kwamba, “maliasili za Tanzania zimefanywa shamba la bibi.”
Wale waliyepewa ruhusa na leseni ya uvunaji na kuwekeza mitaji ya uvunaji wanachukua zaidi ya asilimia 90 na kuacha asilimia 4 kwa Tanzania! Huu ni uvunaji holela na kama ilivyo kwa uvunaji haramu, uvunaji holela ni haramu vilevile! Nani anufaike na maliasli ya Tanzania kama si wananchi wa Tanzania?

Tunasifika kuwa na maliasili ya utalii kama vile: mbuga zenye wanyama wa kila aina; bahari na fukwe zenye mchanga na mandhari nzuri katika Afrika Mashariki; mali-kale (antiquities); magofu ya kale (Bagamoyo, Kilwa na Mji Mkongwe); mapori yaliyohifadhiwa (kama Selous); mito na vijito; na milima (pamoja na Kilimanjaro).
Maliasili yote hii haitumiki vile nchi inavyoweza kunufaika na mapato yenye ujazo unaokidhi thamani yake. Ni nini Tanzania inaweza kujivunia kama si maliasili iliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu? Kama tuna maliasili ya kutosha kwa kila maliasili, tungetarajia tupate mchango wake kwa kuzingatia uzalishaji wake kwenye pato la taifa kwa jinsi ya hali halisi tofauti na sasa!
Lazima tutafute ni kina nani wanaofanya shughuli za ujambazi wa maliasili ya Tanzania! Na kwa jinsi hii tuna masuala kadhaa ya kuuliza. Serikali, hata sasa, imechukua hatua zipi kushughulikia uvunaji holela wa mazao ya maliasili ya taifa?
Kwa nini watendaji, kwa njia haramu na za kifisadi, wamekuwa wakijihusisha na mitandao ya majambazi wa maliasili na ujangili dhidi ya wanyama-pori? Na kwa nini wakati mwingine wanasiasa waandamizi, watendaji wa juu serikalini na kwenye taasisi za uhifadhi wa maliasili wamekuwa wakishiriki kwenye ujambazi na ujangili wa waziwazi huku wakiachwa wafanywe hivyo?
Tunaweza kutafuta majibu ya masuala haya na mengineyo kwa muda mrefu; na japokuwa majibu yangalipo na ni rahisi, nani awezaye kumfunga paka kengele? Tukichukua kama mifano tu; awamu ya tatu ya Benjamin William Mkapa wizara ya maliasili na utalii iliwahi kushikwa na Zakhia Meghji na yaliyofanyika kwenye wizara hii yanafahamika!
Hata tukirudi nyuma yake, yaani enzi za Mzee Rukhsa (Ali Hassan Mwinyi), nadhani mtakumbuka “Kashfa ya Liliondo” iliyokuwa ikichunguzwa na kuandikwa na mwandishi mchunguzi (Marehemu Stan Katabalo aliyekuwa akiandikia gazeti la Mfanyakazi). Inaonyesha kwamba maliasili na utalii ni sekta yenye utajiri uliofichika, siyo?!
Kubwa kuliko ni enzi ya Ezekiel Maige (aliyeondolewa kutokana na ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo). Mfumo wa menejimenti ya maliasili na utalii katika miaka mitatu na ushei iliyopita imechukua sura ya ujambazi mkubwa na ujangili wa waziwazi hata kusababisha vurugu kwenye ugawaji wa vitalu na uvunaji wa wanyama hai na uwindaji wa wanyama kwa (1) kulenga shabaha, (2) biashara ya nyama-pori, na (3) biashara ya nyara.
Wafanyabiashara wamekuwa wakinufaika na mfumo uliyojengwa ndani kwa ndani na mahusiano yasiyozingatia uhuru, haki na uwazi unaohitajika kwenye ugawaji wa vitalu na utowaji wa leseni (vibali) vya biashara na uvunaji wa maliasili na shughuli za utalii.
Kama maliasili ya Tanzania imekosa uangalizi makini, wa kimkakati na madhubuti; kama ilivyo sasa, kuna uwezekano mkubwa kwa mitandao ya ujangili wa wanyama-pori kuendelea na kuliingiza taifa kwenye upotevu wa rasilimali zinazotokana na wanyama. Vilevile, menejimeni dhaifu ya ukusanyaji wa maduhuli na mirabaha itaendelea kuifanya sekta ya uvunaji wa maliasili (na utalii) kufanywa “biashara kichaa” ambayo faida yake itakuwa ni kuwatajarisha wafanyabiashara na wawekezaji wachache wanaotumia njia haramu na uvunaji holela bila ya kuzingatia maendeleo endelevu ya watu na maliasili husika.
Kama tujuavyo, maliasili (kama vile madini, gesi asilia, misitu na hata wanyama-pori) yanapovunwa holela hayaongezeki! Hali hii isipodhibitiwa kimkakati inaweza kuifanya Tanzania kupoteza urithi wa maliasili kwa vizazi vijavyo!
Maliasili za Tanzania, kwa jinsi ushahidi wa moja kwa moja unavyoonyesha imekabidhiwa kwenye mikono ya watu wasiowajibika kwa utunzaji wake kwa faida ya vizazi vya sasa na vya baadaye. Kwa jumla, Tanzania ni budi kuchukua hatua za makusudi za muda mfupi na za muda mrefu katika kuhakikisha kwamba maliasili yanalindwa na uvunaji wake unazingatia matumizi endelevu ya rasilimali katika kuleta maendeleo ya watu na nchi sawia.
Kwa kuwa mchango wa maliasili kwenye pato la taifa ni mdogo; serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba menejimenti ya maliasili inawezesha upatikanaji wa tija na ufanisi kwa kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya maliasili na faida inayotokana na uvunaji wake.
Ni wajibu usioyoepukika kwa wizara zote zinazohusika na maliasili (madini, gesi asilia, ardhi, maji, wanyama-pori, mali-kale na utalii) kufanyakazi kwa uwajibikaji wa moja kwa moja kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za umiliki, menejimenti na udhibiti wa maliasili za taifa kwa faida ya wananchi wa Tanzania. Kwa jinsi hiyo, ni lazima hatua za makusudi na za kimkakati zichukuliwe katika kuivunja na au kuibomoa mitandao ya “ujangili,” “ujambazi” na “wizi” wa maliasili za taifa.
Ndiyo kusema kwamba waliopewa dhamana ya usimamizi na menejimenti ya maliasili za Tanzania lazima wachukue dhamana hiyo wakijua kwamba wataulizwa kwa utendaji au uwajibikaji wao kwa faida ya matumizi endelevu ya maliasili za Tanzania.
Inawezekana kila mmoja kwa nafasi yake, ashiriki katika kulinda matumizi ya kimkakati na endelevu ya maliasili kwa minajili ya watu na kwa faida ya wananchi wa Tanzania. Kwa nini tuendelee kuwa maskini kama Mwenyezi Mungu ametujaalia maliasili ambayo nchi nyingine hawana?
Ni haki na wajibu wa wananchi kuhakikisha kwamba maliasili ya Tanzania inatumika kwa manufaa ya sasa na wakati ujao. Kwa jinsi hiyo; wezi, majangili na majambazi ya maliasili za taifa wasipewe nafasi kuhujumu uchumi wetu.
 
Mwandishi wa makala  hii anapatikana kwa simu namba +255 713 593347 au Barua pepe: maligwa1968@yahoo.com

No comments:

Post a Comment