Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

Natafakari vua Gamba vaa Gwanda



Na Absalom Kibanda
MOJA ya sifa za kihistoria za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kila mara kinapojaribu kujijengea uhalali wa kukabiliana na vyama vya upinzani na makundi mengine ya kijamii yanayotishia uhai wa chama hicho ni ile ya kujiua yenyewe.
Huu ndiyo ujumbe wangu wa kwanza ninaoutoa kwa CCM kupitia katika safu hii baada ya kupumzika na kukaa kando kwa muda wa wiki kadhaa nikitafakari mustakabali wa taifa hili linaloongozwa na viongozi wasiojali, wakomoaji, walipa kisasi na mabingwa wa kutengenezeana fitina.
Miaka saba na ushee ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete ndani ya CCM na hata serikalini imethibitisha jambo moja bayana kabisa kwamba, CCM kama chama kinayumba kwa kiwango ambacho huenda hakijapata kufikiwa wakati mwingine wowote.
Kwa namna mambo yanavyokwenda, angefufuka leo mmoja wa waasisi wenye maono ya chama hicho, Mwalimu Julius Nyerere angefuta maneno aliyopata kuyasema miaka ya mwanzoni mwa 1990.
Katika mazingira ya sasa ya kifo kitarajiwa cha CCM, iwapo Mwalimu angepanda jukwaani leo au kesho kumnadi mgombea ajaye wa urais kwa tiketi ya chama hicho, asingekuwa na jeuri ya kuyatamka tena’ yale aliyosema wakati akimnadi, Benjamin Mkapa mwaka 1995 pale alipokaririwa akisema; ‘japo vyama vya upinzani ni dhaifu lakini vipo….tusivipuuze!”
Kauli pekee ambayo angeisema kwa msisitizo kwa maana ya kusisitiza utimilifu wa unabii wake wa kisiasa ni ile aliyoitabiria CCM udhaifu na pengine kifo pale aliposema; “Bila CCM Madhubuti nchi itayumba.”
Hivi ni nani halioni hili, ambalo tumelisema kwa zaidi ya miaka mitano sasa kwamba, taifa linakabiliwa na ombwe la uongozi linaloitafuna CCM, serikali yake na taifa kwa kiwango ambacho wale wanaojifanya hamnazo au kutojali ni wale walio katika kilele cha madaraka.
Taarifa zinazowakariri washauri wa karibu wa viongozi wetu wakuu zimekuwa zikituthibitishia kila siku kwamba, wakubwa hao hawataki kabisa kukisikiliza au kukifanya kuwa jambo la maana hiki kinachoitwa ombwe la uongozi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, dhana ya ombwe kwa jicho la wakubwa hao ni hadithi ya kufikirika ya watu wenye wivu wa madaraka na hasira ya watu waliokosa fursa za kukaa ikulu.
Kwa wakuu hawa, kukumbushwa mapungufu yao ni kutukanwa na kama hiyo haitoshi aina yoyote ya kuwakosoa ni wanaiona kuwa ni hujuma dhidi yao.
Hasira za wakuu hawa kwa watu wanaowakosoa au kuwaonyesha udhaifu wao hujibiwa kwa kila namna ya shari ambazo zina sura moja tu ya matumizi mabaya ya madaraka. Hapa ndipo tulipofikishana sasa na kimsingi safari yetu huko tuendako.
Ni jambo la bahati mbaya sana vita miongoni mwa watu wanaopingana imepenya hadi ndani ya kuta na kwenye viambaza wanavyoishi watawala wenyewe.
Hulka ya kisasi, kuwindana, kutafunana kama mchwa imepenya ndani ya serikali na kwa kiwango kikubwa imejipambanua na kuwa taswira halisi ya kikazi ndani ya CCM.
Leo hii Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama anaona fahari kubwa kumrarua kwa hoja za kibabe na za kimamlaka, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Kwa staili na mwelekeo huo huo, Rais Kikwete na Waziri Mkuu wake Mizengo Pinda nao wanaingia katika mkumbo wa kushangilia anguko la mawaziri wao waliokumbwa na tuhuma ama za ufisadi au za kupwaya kimamlaka.
Katika hadhira ya watu, Rais ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri anatamka kwa kujiamini kabisa kwamba, alikuwa ana kila sababu ya kuunga mkono mtafaruku ulioibuka serikalini kati ya mawaziri wake na wabunge.
Kamati Kuu ya CCM inakaa na kuja na tamko la kizushi la eti kuipongeza kamati ya uongozi ya wabunge wa chama hicho kwa hatua yao ya kuwataka mawaziri wanane wawajibishwe kutokana na wizara zao na baadhi yao kukumbwa na tuhuma ama za ufisadi au matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kwa staili hiyo hiyo, Waziri Mkuu aliyeponea tundu la sindano kung’olewa bungeni naye anapata nguvu ya kutamba kwamba kile kilichotokea kwa Rais kufanya mabadiliko ya mawaziri ni mwanzo wa safari ya uwajibikaji mpya serikalini. Huu ni mzaha wa hatari sana.
Ni mzaha kwa sababu Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Vikao vya Kazi vya Mawaziri, ndiye kiranja wa mawaziri waliovurunda na kimsingi alipaswa awe alishaujua mwenendo mbaya wa kikazi serikalini hata kabla Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali hajatoa ripoti yake.
Anapokuwa mtu wa kwanza kuwanyoshea vidole watu walio chini yake kwa kuharibu kazi kwa mtindo ule ule anaoutumia mkuu wake, maelezo ya matendo haya hayawezi kupewa jina jingine zaidi ya kuonekana kuwa ni aina mpya ya mzaha wa kisiasa.
Mzaha huu tunaouona serikalini leo, ukifanywa na wakubwa kwa namna ya kuwaumiza wengine kwa staili ya miye niliyekupa ndiye ninayekunyang’anya ndiyo hiyo hiyo inayoutafuna uongozi wa CCM leo.
Huko CCM ndiko ziliko zile hadithi na ngano za alinacha ambazo zilianzishwa mwaka 2008 na maharamia wachache wa siasa za kufitiniana ndani ya chama hicho ambazo hitimisho lake ni kuzaliwa kwa dhana ya kujivua gamba.
Kwa namna ile ile lilivyozaliwa kundi haramu ndani ya CCM la makamanda wa ufisadi waliojipatia umaarufu mkubwa katika mgongo wa mapambano yaliyoanzishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ndivyo ilivyopenya nadharia hiyo mpya iliyobuniwa na kuratibiwa na Kikwete mwenyewe.
Wakati hadidu kadha wa kadha rejea zikionyesha namna ofisi kuu kimamlaka serikalini ilivyoshiriki nyuma ya pazia wakati wote wa sakata la Richmond katika kipindi cha kati ya mwaka 2007 na 2008 ndivyo hivyo hivyo ilivyokuwa wakati dhana ya kujivua gamba ilipoasisiwa.
Makamanda wote waliojitoa mhanga kuongoza na kuratibu mafanikio ya dhana zote mbili zilizozaa vita batili ya ufisadi ndani ya CCM ikilenga kuhujumu mafanikio ya Chadema wakaongezewa nguvu na wale walioratibu ile ya pili ya kujivua gamba ikiwa na malengo yale yale.
Katika mazingira yanayoonyesha namna viongozi wakuu wa CCM na serikali yake walivyochoka kufikiri, harakati zote hizo mbili zimeendelea kuwatafuna wao wenyewe, chama na serikali yao kwa namna ambayo haijapata kutokea kabla.
Pigo ambalo chama hicho lilikumbana nalo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambao ulishuhudia Chadema ikipata umaarufu mkubwa sambamba na CCM kubatiza rasmi sifa ya kuwa chama cha kifisadi, lilipaswa kuwa fundisho la kutosha.
Waswahili wanasema sikio la kufa halisikii dawa. Makamanda wa ufisadi ambao walishindwa kukinusuru chama chao kuchafuka kwa sababu ya wao wenyewe kunusurika kifo cha kisiasa, hawakukoma wala kukomeshwa.
Kwa namna ile ile ya kudanganywa na kina cha maji ya bwawa la kuogolea, CCM, jemedari wake mkuu Kikwete na makamanda wake wa ufisadi wakashindwa kubaini kwamba jitihada za kuwapachika watu wachache sifa ya ufisadi zilikuwa zimegonga mwamba na badala yake ubatizo huo ukawa ni wa chama kizima. Hawakukata tamaa na kwa sababu ya ulafi wa madaraka hawajachoka.
Kwa sababu hizo hizo za kutokata kwao tamaa majemedari wa CCM wakamwingiza kiongozi wao mkuu katika mkenge wa pili mbaya zaidi uliopachikwa jina la kujivua gamba dhana ambayo msingi na malengo yake ni yale yale.
Walengwa katika mradi huu wa pili uliotangazwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Rais Kikwete mwenyewe siku ya sherehe ya kuzaliwa kwa chama hicho tawala wakawa ni wale wale waliolengwa wakati wa zama zile za sakata la Richmond.
Alipoanguka mmoja wa walengwa wakuu wa ajenda hii ya kujivua gamba, mashambulizi dhidi ya wengine wawili waliokuwa wamebakia ndani ya uongozi wa chama hicho yakaendelea kwa nguvu, ari na kwa kasi kubwa.
Miaka miwili na ushee tangu Kikwete azindue harakati hizo za kujivua gamba ambazo hata msamiati wenyewe ulitangazwa hadharani na yeye mwenyewe, majibu yako dhahiri kwamba wanaelekea kukwama nap engine kujijengea njia ya kung’oka kabisa madarakani.
Dhana iliyopigiwa chapuo kwa nguvu kubwa na akina Nape Nnauye, John Chiligati na Mukama ikilenga makada wawili waliobaki sasa imegauka na kuanza kuitafuna CCM yenyewe kwa namna ambayo makali yanaweza yakawa na athari kubwa kwa chama hicho na serikali yake.
Uamuzi wa Chadema kuja na kauli mbiu ya ‘vua Gamba vaa Gwanda’ imekitishwa chama chote tawala sifa ya kuwa gamba badala ya dhana hiyo kuwalenga watuhumiwa watatu tu?
Kwa namna ile ile vita ya ufisadi ilivyokitafuna CCM kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ndivyo ilivyo sasa kwa dhana ya gamba na pengine ndivyo itakavyokuwa wakati huu tunapoelekea mwaka 2015.
Vijana, wanawake na watu wazima kwa makumi, mamia na maelfu wanaaminishwa na kuamini kwamba, CCM ndiyo gamba halisi na njia pekee ya kuondokana nalo ni kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema.
Ile laana ya wana CCM kutafunana wenyewe kwa wenyewe wakijipambanua kwa makundi ambayo yamefikia hatua ya kudhibiti uwezo wa kimaamuzi wa Rais inakiandalia chama hicho msiba mkubwa huko tuendako. Tusubiri tuone.
Mwisho   

No comments:

Post a Comment