SHIRIKISHO la Vyama
vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limeshangazwa
na kitendo kilichofanywa na madaktari wanaofanya kazi chini ya usimamizi wa madaktari bingwa
(interns), na kusema kuwa hatua waliochukua inaweza kuleta vurugu ndani ya
nchi.
Madaktari wanaofanya kazi chini ya
usimamizi wa madaktari bingwa (interns), ambao walisimamishwa wakati wa mgomo
wa madaktari juzi walijitokeza na kuomba radhi kwa wananchi na serikali kwa
kushiriki migomo na kusababisha madhara makubwa kwa baadhi ya wananchi.
Madaktari hao ambao walikusanya
saini zaidi ya 200 kutoka kwa wenzao, walienda mbali zaidi na kuapa kwamba
hawako tayari kushiriki tena kwa namna yoyote katika migomo inayoweka rehani
maisha ya wananchi.
Akizungumza na Tanzania Daima
Jumatano, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya, alisema kuwa, hatua
iliyochukuliwa na madaktari hao ni cha kushangaza kwa kuwa bado madai
waliyokuwa wakihitaji yameshindwa kutekelezwa jambo linaloweza kuchangia kuwepo
kwa vurugu.
Mgaya, alisema kuwa Tucta alielewi
ni kitu gani kimewasibu madaktari hao hadi kufikia hatua ya kuomba radhi.
Alisema kuwa inawezekana madaktari
hao sio wanachama wa vyama vya wafanyakazi hivyo wameshindwa kujua sheria za
kuitisha kwa mgomo.
“Sasa inatupa mashaka juu ya mgomo
wao…maana hawajapata walichogomea wanaanza kuomba radhi hapa ni lazima ‘system’
imefanyakazi yake na inawezekana kulikuwa na mamluki wengi katika mgomo ule,”
alisema.
Katibu Mkuu huyo, alisema kuwa
Tucta imejipanga kukutana na viongozi wa madaktari hao ili kuweza kuwaelewesha
maana ya mgomo na kuacha kutoa matamko yasiyo kuwa na tija.
Alisema madaktari hao wakiingia
katika vyama vya Wanyakazi wataweza kujua sheria za kuitisha mgomo na
kuhakikisha wanasimamia na kupata kile walichokuwa wanakihitaji kuliko
wanavyofanya sasa.
“Hawa waliotoa tamko hilo inaelekea hawapo
katika chama cha wafanyakazi, hivyo wakiingia katika vyama wataacha kutoa
matamko ya aina hiyo maana wanaonekana hawaelewi na wanajifunza,” alisema
Hata hivyo Mgaya alisema kuwa inaonyesha
madaktari hao kama wametishwa na kulazimika kutoa tamko hilo.
“Hapa kuna jambo limefanyika kwa kuwa hata Dk
Steven Ulimboka hatumsikii tena, lazima kuna kitu kinafanyika lakini hatua
waliyoifanya watapata hasara zaidi kwani hawawezi kukutana tena na serikali
…kwa kifupi wamekalia kuti kavu,” alisema
Mwisho
No comments:
Post a Comment