Taarifa iliyotolewa na CCM na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 18 Julai 2013 ya kuitaka Serikali inayoongozwa na CCM kuangalia njia nyingine mbadala ya kukusanya kodi na kuachana na hatua yake ya kukusanya kodi ya umiliki wa kadi ya sh. 1000 kila mwezi imethibitisha maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba ‘chama lege lege huzaa serikali legelege’.
Aidha, taarifa hiyo ni mkakati
legelege wa kujinasua katika malalamiko, kukusanywa kwa saini, kuandaliwa kwa
miswada ya sheria, migomo ya kuzima simu kwa muda maalum na maandamano
dhidi ya Serikali ya CCM kutokana na chama hicho kushindwa kuwa sera
sahihi na mikakati makini.
Taarifa hiyo haiwezi kurudisha nyuma
hatua ya wananchi kukikataa chama hicho na kuunga mkono mabadiliko ya kweli
kupitia CHADEMA kuwa kuzingatia kuwa CCM imeshindwa kuhakikisha kwamba Ilani
zake za uchaguzi ya mwaka 2005 na 2010 zinatekelezwa. Ikumbukwe kwamba kupitia
ilani hizo CCM iliahidi maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake maisha ya
wananchi yamezidi kuwa magumu kutokana na ongezeko la bei na gharama za maisha.
Ili taarifa hiyo isiwe maneno matupu,
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM ajitokeze na kuagiza
utozaji wa kodi hiyo usitishwe kuanzia sasa. Izingatiwe kwamba Muswada
huo ambao Rais aliusaini mwanzoni mwa mwezi Julai ulianzisha pia ushuru
mwingine na tozo zingine mbalimbali zenye kuongezea mzigo wa gharama za maisha
wananchi hususan wa kipato cha chini badala ya kuweka mkazo katika kupanua wigo
wa vyanzo mbadala nchini.
Kadhalika, kwa kuwa chanzo cha hali
hiyo ni maamuzi yaliyofanywa katika Mkutano wa kumi na moja wa Bunge
uliopitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013; ufumbuzi lazima uhusishe
marekebisho ya sheria kufuta makosa yaliyofanywa na Serikali ya CCM na kupigiwa
kura ya ndio na Bunge lililohodhiwa na CCM.
Hivyo, Rais Kikwete awasilishe katika
mkutano wa Bunge kwa hati ya dharura muswada wa sheria wa kufuta vifungu
vilivyoingizwa kwa marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 na
kuondoa ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu (sim card) kwa wamiliki wa simu za
kiganjani/mkononi.
Taarifa hiyo isipoambatana na hatua za
Rais Kikwete kuagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kuacha kutoza ushuru huo na Rais
kuwasilisha muswada bungeni kupitia Waziri wa Fedha itakuwa ‘kiini macho’ kama
ilivyokuwa taarifa nyingine kama hiyo iliyotolewa na msemaji huyu huyu wa CCM
mwaka 2011.
Taarifa ya Nape Nnauye inapaswa
kupuuzwa kwa kuwa alitoa taarifa nyingine kwamba CCM kupitia kikao cha kamati
kuu yake Agosti 2011 ‘imeagiza’ Serikali ‘kutafuta njia ya kushusha bei
ya mafuta ya taa’ iliyopanda baada ya kuongeza kodi ya mafuta ya taa.
Badala ya agizo hilo kutekelezwa
mafuta ya taa yaliendelea kupanda bei na kinyume na agizo hilo katika mkutano
wa 11 wa Bunge mwaka 2013 Serikali hiyo hiyo ya CCM ikawasilisha bungeni
muswada wa sheria ya fedha na majedwali ya marekebisho ya kuongeza kodi ya
mafuta ya taa kinyume cha agizo hilo.
Taarifa hiyo haiwezi kuinasua CCM
dhidi ya kuendelea kukataliwa kwa kuwa imehusika katika maaandalizi ya bajeti
ya Serikali na muswada wa sheria ya fedha kabla na wakati wa mkutano wa Bunge
uliofanya maamuzi ya kuwaongezea gharama za maisha wananchi. Chama hicho
kimeshiriki moja kwa moja kupitia vikao vyake vya kikatiba ikiwemo kamati kuu,
sekretariati na kamati ya wabunge wa chama hicho.
Taarifa hiyo imethibitisha madhara ya
Serikali ya CCM na wabunge wanaotokana na chama hicho wanavyoshindwa kusimamia
maslahi ya umma kwa kuwa iwapo dhamira hiyo ingekuwepo katika hatua za awali
wasingewasilisha bungeni mapendekezo hayo. Hata baada ya kuyawasilisha
wangeyaondoa katika hatua zote kufuatia kodi hiyo kupingwa na kambi rasmi ya
upinzani inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
CCM itambue kwamba wananchi
wanakumbuka kuwa kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya kwanza ndani ya
ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha wa aliposoma bajeti
ya Serikali ya CCM. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya Waziri huyo ambaye
pia ni mbunge wa CCM lakini wakati wa kusoma akaruka sehemu hiyo na kutangaza
kwamba imefutwa.
CCM ieleze katika hatua hiyo, wazo
hilo lilitoka kwa nani mpaka likaingia katika kitabu cha hotuba ya Waziri na
nini maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti ni Rais (ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM) kwenye kikao kilichofanyika siku moja kabla ya yeye kusoma
hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).
Kifungu hiki kilirejeshwa kwa mara nyingine
tena kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha kupitia jedwali la Marekebisho
lililowasilishwa na Waziri wa Fedha mwenyewe kwa niaba ya Serikali ya CCM
na Bunge lenye kuhodhiwa na CCM likakipitisha. CCM iwapo ilikuwa na msimamo wa
kuona kwamba kodi hiyo ni mzigo kwa wananchi kwanini haikuwasiliana na wabunge
wake ambao ndio wengi katika Bunge kuhakisha kwamba wanaikataa.
Iwapo CCM haijitokeza kutoa majibu na
Rais hataagiza kwamba kodi hiyo isitishwe na muswada kuwasilishwa bungeni
kuifuta, natoa mwito kwa wananchi kujitokeza katika mkutano wa hadhara
nitakaoshiriki tarehe 21 Julai 2013 katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo
kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11 Jioni.
Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la
kutoa mrejesho kuhusu yaliyojiri bungeni katika mkutano uliopita na kupokea
masuala ya kuyawasilisha katika mkutano ujao. Aidha, uchambuzi utafanyika
kuhusu rasimu ya katiba sanjari na juu ya mchakato wa katiba mpya.
Hivyo, kupitia mkutano huo saini
zitaendelea kukusanywa kwa ajili ya kutaka kodi hiyo ya kumiliki kadi za simu
isitishwe na muswada kupelekwa bungeni kuifuta kodi hiyo yenye kuongeza gharama
za maisha kwa wananchi na kuathiri haki ya kupata na kutoa taarifa pamoja na
uhuru wa mawasiliano.
Taarifa hiyo imedhihirisha namna
ambavyo tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu wa Serikali ya CCM, uzembe wa
Bunge (ambalo limehodhiwa na CCM) na ulegelege wa CCM.
Hivyo, umma uipuuze na kuendelea
kuchukua hatua za kuiunga mkono CHADEMA katika dhamira na dhima yake ya kuleta
uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa
maendeleo endelevu ya Tanzania.
Imetolewa tarehe 18 Julai 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment