Mbunge wa Ubungo John Mnyika amenusurika kupigwa na bomu
lililorushwa kutoka kwenye gari ya polisi viwanja vya Sahara jijini Dar es
Salaam, badala yake bomu hilo lilimlenga mtu aliyekuwa karibu na Mnyika
anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa sehemu ya paja. Baada ya kutokea tukio
hilo Polisi waliwahi kutaka kkumchukua majeruhi huyo na kumweka kwenye gari
lao, lakini Mnyika aliwaelekeza wafuasi wa Chadema kumchukua majeruhi huyo
kwani polisi wangemchukua wangeficha ushahidi wa jambo hilo. Wafuasi wa Chadema
walimchukua na akafanyiwa taratibu za kupelekwa hospitali, hali yake inaendelea
vizuri na Chadema wamesema watalilipeleka suala hilo kisheria.
Akielezea jinsi suala hilo lilvyotokea akiwa katika Mkutano
mwingine Ubungo, Mnyika alisema Polisi walifika katika viwanja vya Sahara
wakiwa na magari matatu wakiwa na lengo la kuja kutawanya wafuasi wa Chadema
wasifanye Mkutano huo kwa kigezo kuwa kulikuwa na ziara ya makamu wa Rais
katika Wilaya ya Kinondoni, maeneo ya Kinondoni na Kawe, wala sio Ubungo ambapo
yeye alikuwa anafanya Mkutano. “Nikiwa nimejiandaa kupanda jukwaani ndio polisi
walikuja kusema tuache tusifanye Mkutano, nilisogea karibu na gari kumlalamikia
afisa wa polisi kwani kitendo cha kuahirisha mkutano kwa barua waliyoileta saa
sita mchana siku ya mkutano wakati sisi tuliwapa taarifa siku nne zilizopita
ilikuwa sio haki, nilimwambia Afisa huyo wa Polisi, nilikuwa najadiliana kwa
simu na viongozi wakuu wa jeshi la
Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi
Mwema kuwa huku ni kutumika vibaya kwa jeshi la polisi, nilipokuwa bado
najibizana naye bila fujo zozote bomu lilirushwa kutoka ndani ya gari ya polisi
na kupita karibu na mimi likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu yangu na kumjeruhi”
Katika purukushani zilizotokea baada ya bomu kupigwa, Mnyika
alipoteza nyaraka mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi kuwaonyesha
wafuasi wa Chama hicho hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge wake
walivyopitisha kodi ya huduma za simu, na kodi ya laini za simu, kufuatia hali
hiyo, Mnyika aliishia kuwatajia wafuasi wa Chama hicho namba za Mwenyekiti wa
kamati ya Bajeti, Mbunge wa Bariadi Andrew Chenge ili aweze kujibu maswali ya
wananchi kuhusu kodi hiyo kandamizi kwa watanzania masikini. Alisema kuwa
Mbunge yeyote wa Chama cha Mapinduzi au Kiongozi yeyote anayepinga kodi ya
huduma za simu na kodi za laini za simu ni mnafiki kwa kuwa walipitisha wote
kwa kura za ndio, tena baada ya kumshauri waziri wa fedha Wiliam Mgimwa, na
Spika akakiuka utaratibu wa kanuni akasema wote waliokuwa na majedwali ya
mabadiliko kuhusu sheria hiyo walipaswa kupeleka kwenye kamati badala ya
kujadiliwa bungeni kwa uwazi, “sasa mimi sio mwenyekiti wa kamati, na kikanuni
sipaswi kusema hayo yaliyojiri kwenye kamati, muulizeni Chenge”
Aidha, Mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa ungehutubiwa
na Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk Wilbrod Slaa, haukuweza kuhutubiwa na Dk Slaa
kwa kile alichosema kuwa watu wake wa usalama walimwambia mapema kuwa katika
huo mkutano hali sio salama. “nilipata taarifa toka vyanzo vyangu kuwa polisi
walikuwa na mpango wa kuleta fujo, hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda
nisingeenda kuhutubia, pengine bomu lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwa
kiongozi huyo au mwingine” alisema Dk Slaa alipoongea na gazeti hili kwa njia
ya simu baada ya kutoonekana Mkutanoni.
Jeshi la Polisi, kanda maalumu Dar es Salaam, jana
liliahirisha mkutano wa Chadema kabla viongozi hao kupanda jukwaani, uliokuwa
unapaswa kufanyika katika viwanja vya sahara Jijini Dar es Salaam, ingawa
walishindwa kuzuia kabisa mikutano isifanyike baada ya Chadema kuwa wameomba
vibali viwili maeneo tofauti, baada ya kuzuiliwa Mabibo, kibali cha Ubungo
kilikuwa halali, hivyo Mbunge wa Ubungo aliyekuwa amefika Sahara mabibo kwa
ajili ya kuhutubia aliandamana kwa miguu na wafuasi wa Chama hicho hadi Ubungo,
huku kukiwa na makachero wengi wa polisi waliofuatilia maandamano hayo
Akizungumza na wananchi katika mkutano mwingine uliofanyika
Ubungo baada ya ule wa Mabibo kukataliwa na polisi, Mbunge wa Ubungo John
Mnyika alisema, Polisi walifanya kitendo cha kikatili, kusubiri watu wamalize
maandalizi, wakusanyike uwanjani ndipo wanaleta barua ya kupiga marufuku
mkutano kwa kisingizio kuwa katika Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na ziara ya
makamu wa Rais katika Jimbo la Kawe na Kindondoni. “Sisi tupo Ubungo, makamu wa
Rais yupo Kawe na Kinondoni, sasa suala la kuzuia mikutano isifanyike lilikuwa
na maana gani? Kama Jeshi la Polisi walisema hawana askari wa kutosha kulinda
mkutano wetu mbona katika kuutawanya wamekuja na magari matatu? Alihoji Mnyika.
Chadema walikuwa wamepeleka taarifa kwa jeshi la Polisi
tangu tarehe 17 Julai kwamba wangefanya mkutano katika viwanja hivyo tarehe 21
Julai 2013, lakini jeshi la polisi halikuwajibu hadi walipokuwa wanaenda
mkutanoni ndio walipelekewa barua ya jeshi la Polisi yenye kumb.
Na.DSM/KINONDONI/SO/7/2/CHADEMA/309, inayosema
“kumbuka barua ya tarehe 17 Julai, yenye kumb. CHADEMA/MKT/UBUN/015/2013
uliyomwandikia kamishna wa polisi kanda maalumu Dar es Salaam, Kamishna wa
polisi kanda maalumu ya Dar es salaam amezuia kufanyika kwa mkutano huo tarehe
12 Julai 2013 katika viwanja vya Sahara, Mabibo kwa sababu siku mliyoomba
kufanya Mkutano wenu wa hadhara, Wilaya ya Kinondoni ina mapokezi ya ugeni wa
ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Mnyika alitumia muda mwingi kulilaumu jeshi la polisi kwanza
kwa kuahirisha mkutano muda mfupi kabla
ya viongozi kupanda jukwaani, lakini alilaani
kitendo cha kurushiwa bomu mahali ambapo hakukuwepo fujo zozote,
isipokuwa kulikuwa na utendaji mbovu wa polisi.
No comments:
Post a Comment