SIKU moja baada ya
Rais Jakaya Kikwete kuridhia hoja za wapinzani na kutaka muswada wa sheria ya
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba urejeshwe bungeni, Chama cha
Mapinduzi(CCM) kimetaharuki huku viongozi wake wakiwa na kauli tofauti kuhusu
uamuzi huo.
Wakati Mbunge wa
Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) akimpongeza Rais kwa hatua hiyo,na
kumtahadharisha awe makini na wabunge wa chama hicho akidai wamekuwa wakitumia
uwingi wao vibaya bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na
Uratibu), Stephen Wassira amegoma
kuzungumzia hatua hiyo akimsukumia mpira Waziri mwenzake.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti jana, viongozi hao walikuwa na mawazo ya kusigana ambapo baadhi
walimuunga mkono Rais Kikwete na wengine wakionyesha kutokubaliana na uamuzi
huo.
Kwa mtazamo wake,
Filikunjombe alisema Kikwete ameonyesha ukomavu, na ndio Demokrasia ya
kuwasikiliza wachache pia, kwenye Katiba hakuna mshindi, muswada uliopitishwa
sio wa CCM, Katiba sio ya CCM inapaswa kuwa ya wananchi wote hata wachache
wasikilizwe, katika hili hakuna mshindi, ushindani unakuwepo kati ya nani na
nani wakati katiba ni ya watanzania wote.
“Katiba mpya haikuwa
ajenda ya CCM, Rais aliichukua labda kutoka Chama kiingine akaona inafaa, CCM
wamepokea suala la mabadiliko ya Katiba bila kukubali maumivu yake ndio maana
tunafikia hatua hii, ni sawa na mtu unataka kufika mbinguni halafu hutaki kufa,
tukubali mabadiliko na maumivu yake”. Alisema Filikunjombe.
Aliongeza kwamba “mimi
ninamtia moyo Rais Kikwete asimamie vizuri suala la Katiba, ila ajue wabunge
wengi wa Chama cha Mapinduzi tunamharibia, awe makini na sisi wabunge wa CCM,
kwani mara nyingi tunatumia wingi wetu vibaya, na imekuwa aibu sasa mara ya
pili Rais anarejesha muswada kufanyiwa marekebisho, ingefaa wabunge wa CCM
tujitafakari sisi tunamtumikia nani? Kwenye hili Kikwete ameonyesha amedhamiria
kwa dhati kuusimamia mchakato tumuunge mkono .”
Aidha akizungumzia
kauli za Mawaziri waliotoa kauli za kejeli, kusema hakuna muda wa mazungumzo na
wapinzani, au wapinzani wanaenda Ikulu kutafuta Juice, Filikunjombe alisema
“Hao wana akili
mgando tu, yafaa waombe radhi watanzania, na hii ni kwa sababu hapa kwetu
utamaduni wa kujiuzulu haupo, lakini vinginevyo hizo sio kauli za kusemwa na
Mawaziri.”.
Kwa upande wake
Wassira alipotafutwa aliomba aulizwe Chikawe katika maana kwamba yeye hakuwa na
la kusema {On that sina Comment, mtafute Chikawe}
Hata hivyo Naibu
Spika wa Bunge alionyesha kushangaa katika maana kuwa hajui wapinzani
wanabishania nini na walienda kumuona Rais kwa suala lipi?
Alisema “Ni ishu gani
hasa ambayo inahitaji udharura wa aina hiyo, unaposema watalirejesha bunge
lijalo je Kanuni zinaruhusu? Mimi sioni mantiki yoyote, labda wanaozungumza
hoja ya uteuzi wa wajumbe 166,kama Rais hataki hilo ni suala jingine ila sisi
tuliona Rais ndio chombo kinachofaa kuchuja wajumbe hao, bila mamlaka ya
kuchuja tunaweza kujikuta kuwa na wajumbe au wakatoka kanda moja wote, au dini
moja wote au wa jinsia moja, hivyo mamlaka ya kuchuja inahitajika”.
Kuhusu muswada
kurejeshwa bungeni Ndugai alisema , hana uhakika kama utarejeshwa ila
anachofurahi yeye ni kusikia kuwa muswada umesainiwa
Mwenyekiti wa Umoja
wa Vijana wa Chama cha Mpinduzi, na Mbunge wa Donge, Sadifa Khamisi alisema “Bunge
ni chombo huru, tutaangalia kama kuna masuala ya kubadili, na yanaposhindikana
tutapiga kura na wingi wa kura ndio utakaoamua, alipoulizwa pengine wingi huo
unaweza kutumika vibaya alisema “Wewe kama una mawazo yako unayotaka kaandike
sisi tunamuunga Rais mkono ingawa bungeni huko nako masuala ni tofauti”.
Kauli ya Chama cha
Mapinduzi kupitia msemaji wake, Nape Nnauye Kikwete kwa kusaini kama
tulivyosikia inaonyesha anafuata sheria, lakini pia tunampongeza kwa kukutana
na Wapinzani ameonyesha ukomavu, yale yatakayorejeshwa bungeni wabunge wataamua
kama wakiona yana hoja wasikilize wakiona hayana hoja watajua wao, bunge ni
muhimili huru”. Aidha kuhusu kejeli za Mawaziri walizotoa kwamba hakutakuwa na
nafasi ya wapinzani kuzungumza na Rais, Nape alisema hajui na hajawahi kusikia,
lakini pia kabla ya mwandishi kuhoji hilo ahoji kwanini wapinzani wameenda
Ikulu wakati wanajua muswada umesainiwa na walisema Rais akisaini hawatakubali
kuonana naye.
Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Alexanda Makulilo kwa upande wake alisema “Rais
ametumia busara kuwasikiliza wapinzani, aliona wana hoja ndio maana
akawasikiliza na kuomba marekebisho yafanyike, wabunge sasa wakafanye
majadiliano vizuri, waone umuhimu wa hoja, waweke maslahi ya vyama pembeni,
waangalie maslahi mapana ya katiba kwa manufaa ya nchi, maana wasipokuwa makini
utakuta wanajadili ili wale waliotawala wabaki na wale ambao hawajatawala
wanatengeneza mbinu za kutaka kuingia hayo si maslahi mapana ya Katiba”.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment