RAIS Jakaya Kikwete amepongezwa kwa hatua ya
kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani Ikulu na kuwa kitendo hicho ni pigo
kwa baadhi ya mawaziri ambao wameifanya ikulu kuwa hatimiliki yao.
Akizungumza na Tanzania Daima jana Mwenyekiti wa
kamati ya viongozi wa dini wa taaluma, maadili na haki za binadamu kwa jamii,
Mchungaji William Mwamalanga, alisema kuwa kiongozi huyo ana nia njema lakini
watendaji wake wamekuwa wakimpotosha.
Mwamalanga alisema kuwa hatua hiyo ya kuwa na
majadiliano ya pamoja yameonyesha ujinga uliokuwa ukifanywa na baadhi ya
watendaji ambao wamekuwa wakitoa kauli za kudhalilisha dhidi ya viongozi wa
vyama vya upinzani juu ya kukutana na Rais Kikwete.
“Huwezi kuwa na hatimiliki ya Ikulu hili ni lazima
Waziri William Lukuvi, Mathias Chikawe na Steven Wasira wakatambua…maana hatua
ya Rais Kikwete kukutana na viongozi hao kimewadhalilisha wao,” alisema.
Kiongozi huyo alisema kuwa watendaji hao ndiyo
waliokuwa wakipotosha suala hilo na kumlazimisha Rais Kikwete asaini haraka.
Alisema kuwa ni muhimu sasa Rais Kikwete
akasimamia utekelezaji wa makubaliano hayo ili malengo yaliyowekwa yakaweza
kufikiwa.
Mwamalanga alisema kuwa iwapo Rais Kikwete
atayaacha makubaliano hayo na kuwaachia watendaji hao kuna uwezekano wa kutokea
kwa mtafaruku mkubwa ndani ya nchi katika suala hilo.
Alisema kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa baadhi
ya vipengele kurejeshwa Bungeni pamoja na muswada huo kusainiwa lakini hilo
halitafanya mchakato huo kushindwa kuendelea.
Mwisho
No comments:
Post a Comment