MTANGAZAJI wa kituo cha runinga cha ITV, Ufoo Saro
amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mbili
tumboni na kifuani na mzazi mwenzake, Antel Mushi ambaye ni mhandisi wa
mawasiliano kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN) kinachofanya kazi
nchini Sudan.
Katika tukio hilo la kutisha lililotokea jana saa
12:30 asubuhi, Mushi pia alimuua mama mzazi wa Ufoo kwa kumpiga risasi
kifuani na kisha kujiua mwenyewe kwa kujipiga risasi eneo la kidevu,
iliyomfumua kichwani.
Mauaji hayo yalitokea eneo la Kibamba, Njia panda
ya Shule, nyumbani kwa mama mzazi wa mtangazaji huyo, Anastazia Salo (58)
ambako wawili hao; Ufoo na mpenzi wake walikuwa wamefika muda mfupi kabla
tukio.
Mushi na Ufoo wamezaa mtoto mmoja, Alvinen Mushi
(10), na wakati wanatoka nyumbani kuelekea kwa mama mzazi wa mtangazaji
huyo, walimuacha mtoto wao akiwa amelala na dada yake wa kazi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kinondoni, Camillius Wambura, tukio hilo linahusishwa na ugomvi wa
kifamilia ambao hadi sasa haujafahamika chanzo chake.
Shuhuda wa tukio hilo, Habelis Innocent ambaye ni
ndugu wa karibu wa Ufoo, aliliambia gazeti hili kuwa mtangazaji huyo
alijeruhiwa vibaya eneo la tumboni na mkononi.
Habelis alisema kuwa mapema alfajiri jana, Ufoo na
Mushi waliondoka nyumbani kwao eneo la Magari Saba kuelekea Kibamba kwa
mama wa Ufoo, kwamba wakiwa njiani mtangazaji huyo alimpigia mama yake simu
na kumwambia aondoke nyumbani haraka.
Alisema kuwa Ufoo alimtaka mama yake kuondoka
nyumbani kwa kuwa mchumba wake ana hasira, na hivyo anaweza kufanya fujo,
lakini baada ya mama huyo kupata taarifa hizo hakuweza kuondoka haraka hadi
walipofika.
Habelis alifafanua kuwa walipofika nyumbani hapo
waligonga mlango na kisha mama yao kuwafungulia. Kwamba muda huo alikuwa
anajiandaa kwenda kanisani, lakini hakuweza tena kuendelea na alichokua
anakifanya, badala yake aliketi kuwasikiliza kilichowaleta.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wakati mama, Ufoo na
Mushi wakiwa sebuleni yeye alikuwa chumbani huku akisikia mazungumzo
yaliyodhihirisha kulikuwa na mgongano ambao ulitakiwa kutafutiwa ufumbuzi.
Alisema kuwa wakati mazungumzo hayo yakiendelea,
ghafla akasikia mlio wa risasi na sauti ya mama akiomba msaada kutoka
kwake, akimtaka atoke haraka aliko ili kama kufa wafe wote.
Habelis alisema kuwa alipotoka alikuta tayari mama
yake ameuawa na baadaye Mushi alimpiga risasi ya tumboni na mkononi Ufoo.
“Baada ya kushuhudia tukio hilo, nilianza kujihami
na kukimbilia kwenye chumba kingine huku nikiwaambia wenzangu niliokuwa
nimelala nao wasitoke nje.
“Wakati natafuta namna ya kujihami kwa kupanda
darini, Mushi alipiga risasi nne mfululizo ili mlango ufunguke zinipate,
lakini alishindwa na hivyo alihamia chumba alichokuwa mdogo wa Ufoo na
kupiga risasi mbili mfululizo ili zimpate yoyote aliyekuwemo,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati akipiga risasi hizo, vijana
waliokuwa katika chumba hicho walifanya jitihada za kubomoa dari na kisha
kupata upenyo wa kujificha darini na hatimaye Mushi akawakosa.
Aliwataja wenzake hao waliokoswakoswa na risasi
katika tukio hilo kuwa ni Godluck Saro na Jonasi Saro na kuongeza kuwa
baadaye Mushi alikimbilia jikoni na kukuta jiko la gesi, aliwasha na
kuchoma nguo ili nyumba ilipuke waliomo ndani wateketee.
Shuhuda huyo alisema kuwa baada ya kuchoma nguo,
Mushi alirudi sebuleni na kisha kujimalizia mwenyewe kwa kujipiga risasi na
kupoteza maisha papo hapo.
Ufoo alikimbizwa Hospitali ya Tumbi, Kibaha ambako
alipatiwa huduma ya kwanza na kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, uchunguzi wa awali uliofanyika
katika gari alilotumia Mushi walikuta begi likiwa na kompyuta ndogo
(laptop), kamba za kujinyongea, panga, pingu, kisu na risasi.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini
Muhimbili, Kova alisema kwa mujibu wa madaktari, hali ya mgonjwa ilikuwa
inaendelea vizuri na alikuwa akitarajiwa kufanyiwa upasuaji nyakati za
mchana.
Kova alisema japo mhusika alijiua baada ya kumuua
mkwewe na kumjeruhi kwa risasi Ufoo, bado kitendo hicho hakiliondolei jeshi
hilo kuchunguza tukio hilo.
Alisema kuwa wanatarajia Ufoo atakuwa miongoni mwa
watu watakaolisaidia jeshi hilo kupata taarifa zaidi za tukio hilo.
Naye, ofisa upelelezi wa makosa ya jinai, Ahmed
Msangi alisema hadi sasa hakuna taarifa kamili, bali jeshi limejigawa
sehemu tatu, kila kundi likikusanya taarifa.
Alisema baada ya makundi hayo ambayo yalikuwa
katika maeneo ya nyumbani lilikotokea tukio, Tumbi hospitali na Muhimbili,
kukusanya taarifa watazitoa kwa waandishi wa habari.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP,
Reginald Mengi alisema kipindi hicho madaktari walikuwa wakiendelea na
uchunguzi kwa ajili ya kukamilisha upasuaji.
Alisema kuwa hali yake Ufoo sio mbaya bali ilikuwa
inaendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.
|
No comments:
Post a Comment