Napenda kuufahamisha umma
kwamba mimi ndiye NILIYERUHUSU Gazeti la Mwananchi kuendelea na utoaji wa
taarifa/habari kwenye tovuti yake, pia Gazeti la Rai kutoka kila siku.
Ninalazimika kutoa ufafanuzi
kwa njia ya maandishi kutokana na kupigiwa simu nyingi na waandishi wa habari
kuhusiana na tamko jipya la Mkurugenzi wa Habari – Maelezo, Ndg Assah Mwambene
kuhoji uhalali wa Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila
siku, badala ya mara moja kwa wiki (Alhamisi).
Tarehe 4/10/2013 nilifanya
mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) na New
Habari Corporation (2006) Ltd kwa upande mmoja na msajili wa magazeti kwa
upande mwingine.
Katika kikao hicho cha pamoja
na viongozi wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania maombi matatu yaliwasilishwa;
1. Ombi la kumuomba waziri
apitie upya adhabu iliyotolewa kwa mageazeti hayo. Katika hili Majibu yangu
niliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni waziri mwenye dhamana na
masuala ya habari pekee.
2. Ombi la Gazeti la Mwananchi
kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamis.
2.1 New Habari walieleza kuwa
siku zilizopita waliwahi kuomba kwa maandishi (barua) kwamba gazeti la Rai
litoke kila siku. Maelezo ya Naibu Msajili wa Magazeti katika kikao hicho
yalikuwa kwamba, kulikuwa na tatizo la kiufundi katika kurejea maombi hayo na
akakiri kuwa hakuna kinachozuia gazeti la Rai kutoka kila siku. Kutokana na
maelezo hayo mimi niliridhia gazeti hilo sasa liruhusiwe kutoka kila siku.
2.2 Kuhusu gazeti la Mwananchi
kuwa online, Naibu Msajili alisema hakuna sheria yeyote inayoweza kuzuia gazeti
hilo kuwa online
ila aliwataka lisionekane
gazeti zima kama lilivyo pia wabadili nembo (Master Head) kwamba waweke nembo
ya MCL na siyo ya gazeti husika ambalo limefungiwa. Pia baada ya maelezo hayo
niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa kuzingatia angalizo lililotolewa na
Naibu Msajili wa Magazeti.
3. Hoja ya tatu ilikuwa ni ile
ya Serikali kupitia Idara ya Habari - Maelezo kuwa na uhusiano mzuri na vyombo
vya habari, ili kuepuka misuguano isiyo ya lazima.
3.1 Pendekezo hili nililipokea
na niliwasilisha kwa Mhe Waziri wa Habari kwa hatua zaidi, likiwamo suala la
kupitia upya adhabu na ushauri wa kujenga uhisiano na vyombo vya habari.
3.2 Masuala ya Gazeti la
Mwananchi kuwa online na Rai kutoka kila siku, NILILITOLEA UAMUZI siku hiyo
hiyo, na uamuzi ni kwamba niliwaruhusu baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na
ukiukwaji wa sheria yoyote uliofanywa na waombaji.
Nimeamua kuweka sawa jambo hili
kutokana na taarifa ya Mkurugenzi wa Maelezo ambayo ninaamini kwamba kutolewa
na kusambazwa kwake ni kukosekana kwa mawasiliano kati yake kwa uipande mmoja
na Mhe. Waziri, Naibu waziri na Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.
Hivyo aliyeruhusu Gazeti la
Mwananchi kuwa online na Rai ni mimi na ndiyo maana kuanzia tarehe 5/10/2013
Gazeti la Rai lilianza kuchapwa kila siku na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi
likaanza kuwa mtandaoni kwa kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti.
Imetolewa na:
Amos G. Makalla
Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
No comments:
Post a Comment