HATIMA ya mawaziri watano kuendelea na nyadhifa zao
iko shakani baada ya wabunge kuwatuhumu kushindwa kuwajibika ipasavyo na
kusababisha migogoro ya wafugaji na wakulima.
Kufuatia kadhia hiyo iliyojitokeza wakati wa
kutekelezwa kwa Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza Ujangili, Bunge
limeamua kuunda kamati teule kuchunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo
imesababisha vifo, ukiukaji wa haki za binadamu na upotevu wa mali.
Wabunge wengi waliochangia hoja hiyo waliwataja wazi
mawazi kadhaa akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakitaka wawajibishwe kwa
kuondolewa kwenye nyadhifa zao kutokana na kushindwa kuchukua hatua wakati
operesheni hizo zikipoteza maisha ya watu na mifugo.
Mbali na Pinda, wamo pia Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo
ya Ndani), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo
na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Dalili mbaya kwa viongozi hao zilianza kuonekana jana
asubuhi baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutangaza kuwa amekubali hoja za
wabunge wawili waliotaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili kujadili jambo la
dharura.
Alisema Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alitaka
Bunge lijadili kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi,
huku Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alitaka Bunge lijadili vitendo
vinavyofanywa na watendaji katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Lugola alidai watendaji wamekuwa wakiwaua kwa risasi
ng’ombe waliowakamata kwenye operesheni hiyo pamoja na kuwatesa wamiliki
wasiotoa fedha zinazohitajika.
Kutokana na hoja hizo, Makinda alitoa fursa kwa Waziri
wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, David Mathayo kuelezea Operesheni Tokomeza Ujangili na migogoro kati ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Kagasheki ndiye aliyekuwa wa kwanza kueleza operesheni
hiyo inaendelea. Alisema inalenga kutokomeza ujangili ulioshamiri hapa nchini
kiasi cha kutishia sekta ya utalii na tembo.
Hata hivyo, Kagasheki alisema kutokana na malalamiko
ya watu mbalimbali juu ya mwenendo wa operesheni hiyo, serikali imeamua
kuisitisha ili kufanya tathmini.
Waziri huyo pia alisema mifugo yote iliyokamatwa ndani
ya hifadhi kabla na baada ya operesheni hiyo iachiliwe bila gharama yoyote na
watu wenye ushahidi wa ng’ombe wao waliouawa kwa risasi wawasilishe vielelezo
ili achukue hatua zaidi.
Mara baada ya Kagasheki kutoa taarifa hiyo, Waziri
Mathayo alitoa taarifa kuhusu migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Aliwaomba
radhi waliopata hasara ya kujeruhiwa, kupoteza mifugo au vifo katika operesheni
hiyo.
Wabunge wacharuka
Mara baada ya mawaziri hao kumaliza kutoa taarifa zao,
Spika Makinda alitoa fursa kwa wabunge kuchangia. Mbunge wa Kilolo, Peter
Msolla (CCM), alitoa hoja ya Bunge liunde kamati teule kuchunguza migogoro ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Alifuata Lugola, ambaye alisema anashangazwa na
mawaziri Nchimbi, Nahodha, Kagasheki na Mathayo kuendelea kuongoza wizara
wakati damu za wananchi waliofariki katika operesheni zinazohusisha wizara
wanazoziongoza zinawakabili.
Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani (CCM),
aliifananisha serikali na ugonjwa wa miguu na midomo kwenye mifugo, maarufu
kama Sotoka, ambao miaka ya nyuma ulikuwa ukiua ng’ombe wengi.
“Hii serikali ya ajabu sana, yaani ukiwa na mifugo
mingi ni kero kwao. Badala ya kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi,
wanaiua. Mimi naifananisha na Sotoka,” alisema.
Mbunge wa Maswa, Magharibi, John Shibuda (CHADEMA),
aliwataka wabunge wa CCM waache unafiki na wamuondoe Waziri Mkuu, Pinda kwa
kuwa hachukui hatua kila anapopelekewa matatizo.
“Wewe Waziri Mkuu, taarifa za kiintelijensia
hazikufikii? Je, husomi magazeti kujua kinachotokea kwenye maeneo mbalimbali na
mbona huchukui hatua? Nyinyi watu wa CCM msileane,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (CHADEMA),
alimtaka Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi mawaziri wake waliosababisha
operesheni za kinyama zilizosababisha vifo vya binadamu, mifugo na unyanyasaji.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM),
alisema serikali inatia aibu kwa kukamata meno ya tembo, lakini inashindwa
kuwakamata majangili waliohusika.
Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), aliwataka
mawaziri waache porojo za kisiasa wanapoambiwa matatizo ya wananchi na wabunge.
“Wabunge humu ndani tunaeleza matatizo ya wananchi,
eti waziri anasema si mambo ya msingi…acheni porojo, fanyeni kazi, maana tuna
ushahidi wa kile tunachokisema,” alisema.
Kamati teule
Akihitimisha mjadala huo, Makinda aliafiki wazo la
kuundwa kwa kamati teule.
Hata hivyo kamati teule hizo kila zinapoundwa na
ripoti yake kusomwa zimekuwa zikisababisha kuondoka madarakani kwa watendaji
mbalimbali.
Februari 8, 2008, Waziri Mkuu, Edward Lowassa,
alilazimika kujiuzulu baada ya kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza
zabuni iliyoipa ushindi wa kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond
kumgusa.
Mwaka juzi, Bunge liliunda kamati teule
kuchunguza matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, ambayo ilidaiwa kuchangisha
sh milioni 50 kwa idara na taasisi zilizo chini ya wizara, ili kufanikisha
upitishwaji wa bajeti, na ripoti yake ilimng’oa Katibu wake, David Jairo
No comments:
Post a Comment