Social Icons

NDOA YANGU, Ningejua!

NDOA YANGU, Ningejua!

SERIKALI "YANYONGA' WANAHABARI


 

WAKATI wadau mbalimbali wa habari nchini wakipigania sheria ya uhuru na haki ya kupata habari na ile ya kudhibiti utendaji wa vyombo vya habari, serikali imewasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
Sheria hiyo ya mwaka 1976 inalalamikiwa na wadau kwa kutoa mamlaka makubwa kwa waziri mwenye dhamana ya habari kufungia magazeti mbalimbali akijiridhisha yameandika uchochezi, chuki au taarifa zinazosababisha mtafaruku kwa jamii.
Marekebisho hayo yanaonekana ‘kuvitia kitanzi’ vyombo vya habari na waandishi wa habari wanaodaiwa kuchapisha habari zenye uchochezi au uvunjifu wa amani.
Adhabu kwa vyombo vya habari na waandishi watakaobainika kutenda makosa hayo, itakuwa ni sh milioni tano au kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, alisoma muswada huo jana bungeni alipokuwa akiwasilisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali.
Werema alisema marekebisho hayo yanalenga kutekeleza Azimio la Bunge lililotaka serikali ipitie sheria zilizopo ili kuona kama zinatosheleza kuzuia lugha au kauli za uchochezi.
Alibainisha kuwa baada ya kupitia, serikali imebaini kuwa adhabu ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari za uchochezi au inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani ya sh 150,000 ni ndogo na sasa iwe sh milioni tano.
Alisema wamefikia hatua ya kupendekeza adhabu kubwa baada ya kulinganisha na madhara ya kosa husika kwa jamii.
Werema pia alisema wamependekeza yafanyike marekebisho ili adhabu ya kosa la kutoa matamshi katika mikusanyiko ya watu yanayoweza kusababisha vurugu au kuchochea uadui baina ya makundi mbalimbali ya jamii iwe faini isiyopungua sh laki tano au kifungo kisichopungua mwaka mmoja.
Alibainisha kuwa kosa hilo kabla ya kupitishwa sheria hiyo, adhabu yake ilikuwa ni sh 1,000.
Pia maekebisho mengine yaliyofanyika ni kanuni ya adhabu kwa kosa la kutumia lugha ya matusi, kupigana na vitisho vya kufanya vurugu ambapo sasa adhabu yake ni kifungo cha mwaka mmoja badala ya miezi sita iliyokuwapo awali.
Wapinzani wapinga
Akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, msemaji wake Tundu Lissu, alisema sheria ya magazeti ilitungwa kwa mara ya kwanza na dola ya kikoloni mwaka 1928 na haikuwa na vifungu vya jinai za kashfa na uchochezi.
Aliongeza kuwa vifungu hivyo viliingizwa katika sheria za Tanzania mwaka 1953 na vililenga kuwadhibiti wakosoaji na wapinzani wa sera na dola ya kikoloni waliokuwa wameanza kujitokeza katika miaka hiyo.
Alibainisha kuwa muathirika wa kwanza wa vifungu hivi alikuwa Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere, wakati huo akiwa rais wa chama cha siasa cha upinzani kiitwacho Tanganyika African National Union (TANU) na wenzake wawili.
Walishitakiwa kwa kuchapisha kauli ya Mwalimu Nyerere kwamba wakuu wa wilaya wa kikoloni waliokuwa wanazuia mikutano ya hadhara ya TANU walikuwa wapumbavu.
“Wakoloni walidai kwamba kauli hiyo ya Baba wa Taifa ilikuwa ya kichochezi na ya kashfa kwao, hivyo basi, wakoloni walimfungulia mashitaka ya jinai kwa kutumia kifungu hiki hiki ambacho leo, miaka 56 baadae, Bunge lako tukufu linaombwa kukirekebisha kwa kukiongezea adhabu,” alisema.
Alisema mwaka 1976 sheria ya magazeti ilianzishwa kwa lengo la kudhibiti na kuminya uhuru wa habari na haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari.
Aliongeza kuwa mwaka huo huo sheria ya Shirika la Habari Tanzania (Shihata) iliyokuwa na lengo la kudhibiti ukusanyaji, upokeaji na utoaji habari ndani na nje ya Tanzania ilitungwa.
Lissu alisema sheria hiyo ilipiga marufuku ukusanyaji, upokeaji na utoaji habari ambao haukufanywa na Shihata au chini yake au kwa mamlaka yake kwa kuyafanya kuwa makosa ya jinai yenye adhabu ya faini na/au kifungo.
Aliongeza kuwa sheria hiyo ilifutwa mwaka 2000, na Bunge lilitunga sheria nyingine ambayo ilitoa fursa kwa Idara ya Habari (Maelezo) kufanya kazi ya Shihata.
Alibainisha kuwa mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya magazeti hayana msingi kwa sababu hakuna ushahidi wa kuonyesha adhabu zilizoko zimeshindwa kudhibiti makosa ya uchochezi.
Kwa mujibu wa Lissu, serikali imejenga utamaduni wa kufungia magazeti na kutisha waandishi wa habari, na imefikisha marekebisho hayo bungeni kwa malengo ya kisiasa ya kudhibiti wakosoaji na wapinzani wa serikali na watawala na sio kuzuia makosa ya jinai.
“Badala ya kuwapeleka wakosaji wa aina hiyo mahakamani wakaadhibiwe kwa mujibu wa sheria hiyo, serikali hii ya CCM imejenga utamaduni wa kufungia magazeti na kutisha waandishi wa habari,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa kwa kipindi chote hicho, serikali hii ya CCM imekataa kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Nyalali. Badala yake Tanzania imegeuka kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya matendo ya watawala.
“Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti yanayofichua ufisadi, uchafu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa viongozi, watendaji na watumishi wa serikali hii ya CCM.
“Tanzania imegeuka, chini ya usimamizi wa wizara na serikali hii ya CCM kuwa taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na meno, kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua,” alisema Lissu.
Naye Mbunge Mbulu, Mustapha Akonay (CHADEMA), alisema kuwa kila taaluma ina kanuni na maadili yake, hivyo akashauri kuwa badala ya serikali kuwanyang’anya uhuru wanahabari na vyombo vya habari, kazi hiyo iachwe kwa Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Rajab Mbarouk wa CUF alipinga vikali adhabu hizo zinazopendekezwa, akidai ni kutaka kuvikomoa vyombo vya habari jambo ambalo ni hatari sana.
CCM washangilia
Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM), alisema anashangazwa na uamuzi wa serikali wa kuifanyia marekebisho sheria hiyo kila mara badala ya kupeleka muswada wa sheria ya kusimamia vyombo vya habari.
“Mnahofia nini? Si mlete muswada wa sheria ya magazeti ili tuiunde upya? Nina imani ikiletwa hapa itakuwa mkombozi mkubwa kwa tasnia ya habari,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Pindi Chana, alisema magazeti hivi sasa yanaandika kwa upendeleo na kuwaumiza watu wengine, jambo alilosema litasababisha uvunjifu wa amani.
Aliwatuhumu waandishi wa habari kutumiwa na wanasiasa mbalimbali kuwaharibia sifa wenzao, hivyo ni vema kukawepo na sheria ya kuwadhibiti.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), alisifu hatua hiyo ya serikali kuyabana magazeti, akidai wapinzani wanapinga kwa vile ndio wanayatumia kutoa kauli za kichochezi




No comments:

Post a Comment