Asifu wapinzani kutembelea
wananchi
Mwenyekiti wa CCM taifa Rais Jakaya Kikwete, amekiri kuwa CCM itaanguka
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kutokana na kukithiri kwa rushwa miongoni
mwa watendaji wa chama hicho.
Kikwete alisema kuwa kwa sasa chama hicho kikongwe kimepoteza
matumaini kwa watanzania kutokana na vitendo visivyo vya kiungwana vinavyofanywa
na watendaji ndani ya chama.
Alisema hata kama itatokea kwa chama hicho kushinda uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015 kama tabia walizonazo watumishi na viongozi hazitabadilika ni
wazi hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Rais Kikwete, alitoa onyo hilo juzi usiku, alipofunga mafunzo maalum ya
siku nne kwa makatibu wa mikoa, makatibu na wenyeviti wa wilaya wa
chama hicho nchini mkoani Dodoma.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa mwaka 2015 tutakuwa na
wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika Serikali basi
mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.
“Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi laki mbili za airtime
(muda wa mawasiliano). Jueni kwa mtindo huu hatutafika ama wengine watavuka na
wengine kukwama.” Alisema na kuongeza;
“Viongozi wa chama ndiyo mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata
aibu, nawaombeni tubadilike kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana
katika chaguzi mbalimbali nawaambieni,”alisema.
Mbali na hilo alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu
ambao wameanza kujipitisha katika viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili
ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama ubunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu
ambao wameisha anza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za
kugombea huku wakipenyeza rushwa jambo ambali linaendelea kukishushia adhi
chama hicho.
Akizungumzia chuki ndani ya chama alisema
watanzania kwa sasa wana akili zao na hawataki kudanganywa.
“Wapo badhi ya viongozi ndani ya chama
hawajui hata Ilani ya chama chao wakipanda kwenye majukwaa wanaanza kuzungumzia
ujenzi wa daraja la Mkapa ama lile la Malagarasi, watu hawataki kusikia hayo
mtu wa Ngara anataka kujua daraja lake limeishaje siyo la Mkapa” alisema
Hata hivyo alisema wazi kuwa kwa sasa
vyama vya upinzani vinafanya kazi kubwa zaidi ya kuwatembelea wananchi na
kusikiliza kero zao tofauti na ilivyo kwa chama cha mapinduzu kwani kwa sasa
CCM viongozi wake wapo mbali na wananchi.
“Nataka niwaambie vyama vya upinzani
vinafanya kazi kubwa na wanafika hatua ya kuaminika kwani wanapokwenda kwa
wananchi wanaambia kuwa CCM inafanya kazi za maendeleo kwa shinikizo la vyama
vya upinzani na wananchi wanaamini.
“Wananchi kwa sasa wanataka maendeleo na
kusikilizwa. Kwa sasa ukienda polisi umwambie RPC akuoneshe ratiba za mikutano
utaona orodha ndefu ya mikutano ni ya
vyama vya upinzani CCM hawapo mnafikiri hapo mtashinda.
“’Wapo watu ambao wanadai kuwa chama
kitafia mikononi mwangu nataka niseme kuwa chama hakifii mikononi mwangu
kitafia mikononi mwenu” alisisitiza Mwenyekiti wa chama hicho taifa.
Kikwete alisema kuwa siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na
siyo CCM peke yao.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali ambao wanaweza kufanya
kazi kwa uadilifu wa hali ya juu hivyo hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa
ambao watatupotezea sifa yetu kwa wananchi.
“Tukipoteza Urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.”
Katika hatua nyingine Kikwete aliwaonya
viongozi ambao wanajihusisha na uuzaji wa mali za chama kama vile viwanja na baadhi
yao kuingia mikataba yenye utata.
“Kuna watu wanapoingia mikataba sijui
wanakuwa wamelewa...kwanza unashindwa hata kuelewa...kwa mfano utakuta mtu
alipangishwa jengo la CCM kwa miaka 264 sasa unawaza huu mkataba wa aina gani
kwa sisi tuliopo hapa miaka 50 ijayo hakuna atakae kuwepo duniani sasa mmiliki
wa lile jengo atakuwa nani,?” alisema
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na
wenyeviti wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na kutafuta
wanachama wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali zijazo.
“Viongozi wengi hatuna tabia ya
kuwatembelea wanachama wetu na kuwatatulia kero zao hali ambayo inatugharimu
wakati wa uchaguzi kupata kura kidogo tofauti na idadi ya wanachama tulionao,”
alisema na kuongeza kuwa;
“Wenzenu wakiendelea kutembelea wanachama
na kutisha mikutano, nyie mnabakia kuimba wembe ni ule ule ushindi, shauri yenu
mtakatwa,”alisema.
Alisema wapinzani wanarikodi ya
kufanya vizuri kwa kufanya mikutano kuliko viongozi wa CCM.
Aidha, alisema iwapo hawatafanya kazi vizuri chama
hakitaweza kufanikiwa na kuwataka kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo
hayo kuhakikisha chama kinakuwa imara na chenye uwezo wa kuongoza.
"Lazima muendelee kuongeza wanachama
sio kupanda majukwaani na kuimba iyena iyena...Utendaji mpya wa kuongeza
wanachama na kuwatambua na kuwapa majukumu,"alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment